Wednesday, May 22, 2013

Maoni na Mapendekezo ya CHADEMA juu ya Rasimu Muongozo uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi yenye mlengo yanayofanana


1.0. UTANGULIZI 

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (kifungu cha 18 (3)) imetoa wajibu kwa tume wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume.

Kifungu cha 17 (8) kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utatumika kila upande wa Muungano. 

Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba kwa kueleza kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. 

Ikumbukwe kwamba Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 7 Januari 2013 kuwasilisha maoni ya CHADEMA kuhusu katiba mpya kama ilivyoalikwa lakini pia kutumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na maboresho yanayohitajika kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata katiba bora. 

Tarehe 31 Januari 2013 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa kwamba imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa) na Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu). 

CHADEMA baada ya kupitia muongozo huo na kwa kuzingatia kuwa tayari tume ilishafanya uamuzi kuwa mabaraza ya katiba yatakuwa ya wilaya, tarehe 14 Februari 2013 kiliwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu uteuzi wa wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika mchakato mzima wa uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya. 

Kufuatia hali hiyo katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2013: 

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014

(Inatolewa chini ya kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)


A: UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010.

Mheshimiwa Spika, Katika kujadili Mapitio ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014 naomba tuyatafakari maandiko ya katika muktadha wa uongozi wetu wa leo na hatma ya sekta hizi mbili muhimu za nishati na madini.

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE katika ukurasa wa pili tutafakari kwamba, naomba kumnukuu ‘ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa.Ukiniona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nitalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa.


Mheshimiwa Spika, Tuendelee kutafakari maandiko ya Nyerere kwamba ‘Wakati mwingine, mtu tunayempinga huwa anamakosa kweli, lakini hoja tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nilifikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha.Ni kweli mbili mara tatu ni sita;lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu ,au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana, Huu ni mfano wa upuuzi; lakini mara nyingi hoja tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda,au kukubali mawazo yetu, huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayojadili’.

Sunday, May 19, 2013

Waraka kuhusu muswada wa Baraza la Vijana la Taifa wa Mwaka 2013

Vijana wenzangu na wote wenye dhamira ya kuwezesha maendeleo ya vijana nchini, salaam! 

Mtakumbuka kwamba mwezi Januari 2013 nilitoa taarifa kwa umma ya kueleza kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge Muswada Binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa na kuomba hatua za ziada toka ofisi ya Bunge kwa kuzingatia Kanuni ya 21 na Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. 

Toka wakati huo muswada huo mpaka sasa Mei 2013 haujachapwa katika gazeti la Serikali na nimepokea barua toka kwa ofisi ya Bunge kwamba wamepokea ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa muswada huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi. 

Sababu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri huo ni kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana. 

Kwa maoni yangu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo bila kuzingatia kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.