Thursday, March 26, 2015

Kufuatia Kumbukizi UDSM Tutangaze #AjaliBarabaraniJangalaTaifa Tuwajibike kuzipunguza










Kumbukizi maalum ya tarehe 20 Machi 2015 ya wanafunzi watano wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani imetukumbusha msiba mkubwa wa watu 50 katika ajali moja ya basi na lori ya tarehe 11 Machi 2015.

Wakati tukiendelea kuwaombea marehemu na majeruhi na kutoa pole kwa wafiwa na wahanga wakati umefika sasa tutangaze #AjaliBarabaraniJangalaTaifa tuwajibike kuzipunguza.

Kumbukizi katika ukumbi wa Nkurumah ilihusisha ibada, nyimbo maalum na kusomwa kwa wasifu wa wanafunzi walioaga dunia wakiwa wadogo familia zao na taifa likiwahitaji na hatimaye salamu kutoka makundi mbalimbali.

Niliguswa na salamu za Chuo cha Fani za Jamii zilizosomwa na Mkuu wa Chuo cha Fani za Jamii aliyeeleza kwamba mabasi sasa yanaua kuliko magonjwa mengi. Alipendekeza utafiti ufanyike UDSM kuchangia kupunguza hali hiyo kwa kuzingatia kwamba Chuo Kikuu hicho kina fani mbalimbali (multi disciplinary).

Alieleza kwamba kwa upande wa uhandisi waangalie iwapo teknolojia ya mabasi yenye spidi inawiana na barabara zetu kuu ambazo nyingi ni za njia moja. Huku fani ya jamii iangalie masuala ya maadili kufanya madereva wa mabasi kujifunza kwamba wanabeba binadamu sio wanyama.

Nakubali kwamba kuna umuhimu wa kuendelea na utafiti lakini tujiulize ni wananchi wangapi wataendelea kupoteza maisha wakati tukisubiri matokeo ya utafiti mpya.

Hivyo, kuna haja ya UDSM kuitisha Kongamano Maalum kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili matokeo ya tafiti zilizofanyika tayari yajadiliwe na mapendekezo ya hatua za dharura yatolewe.

Pamoja na tafiti zilizofanywa na wasomi, Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta awasilishe matokeo ya Ripoti ya kamati iliyoundwa kutathmini na kutoa mapendekezo ya hatua ya kuchukua ili kupunguza ajali za barabarani ambayo ripoti yake ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison Mwakyembe Novemba 2014.

 

UDSM iende mbele zaidi ya kufanya utafiti kwa kuzingatia dhima iwezeshe msukumo wa kisomi na kimkakati katika huduma kwa umma.

Natambua pia katika salamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar Es Salaam (DUCE) zilizosomwa kwa niaba ya Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Fani na Sayansi Jamii (DUCE) Serikali iliombwa kuongeza juhudi za kupunguza ajali.

Lakini maombi pekee hayatoshi kuna haja ya kutaka utekelezaji na uwajibikaji na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salam isibaki nyuma katika kukabiliana na  #AjaliBarabaraniJangalaTaifa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amenukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba chanzo cha ajali ya basi la Majinja Express na lori ni ubovu wa barabara katika eneo la ajali na mwendo kasi.

 

Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha kulikuwepo na shimo kubwa la muda mrefu katika barabara kuu. Lakini pamoja na hali hiyo hakuna kiongozi yoyote wa Wakala wa Barabara (TANROADS) au mamlaka zingine zinazohusika aliyewajibika au kuwajibishwa mpaka hivi sasa.

 

Baada ya Ikulu kusambaza taarifa ya salamu za rambirambi za Rais ni vyema sasa ikasambaza tena taarifa nyingine ya kueleza umma hatua ambazo Rais ameelekeza kuchukuliwa kwa waliosababisha hali hiyo.

 

Aidha, Waziri wa Uchukuzi atakiwe kuwasilisha kupitia Mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea hivi sasa kauli ya Serikali kuhusu mkakati wa kushughulikia kukithiri kwa ajali za barabarani nchini.

 

John Mnyika (Mb)

25 Machi 2015

Sunday, March 22, 2015

World Water Day na Wiki ya Maji: #MajinaMabadilikokwaMaendeleo #WaterIs #MaMaMa



Leo ni siku ya maji duniani ( #WorldWaterDay )na kwa Tanzania ni kilele cha wiki ya maji. #MajiNi maisha, #MajiNi maendeleo  ( #WaterIs Life, #WaterIs Development ). Shiriki na Umoja wa Mataifa katika maadhimisho kwa kutembelea http://www.unwater.org/worldwaterday na kushiriki kupiga picha za #WaterIs ( #MajiNi ) na kuweka katika mitandao ya kijamii.
Ujumbe wa wiki ya maji kitaifa ni “maji kwa maendeleo endelevu” na maadhimisho yanafanyika Musoma ambao Rais anatarajiwa kuhutubia. Kwa kuwa maadhimisho haya ni ya mwisho kwa utawala wake, anapaswa kulieleza taifa ni kwa nini ameonyesha udhaifu wa kushindwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati akizindua Bunge mwaka 2005 ya kwamba anatambua kuwa maji ni kero ‘nambari wani’ na kwamba Serikali yake ingeandaa mpango kabambe wa kuhakikisha matatizo ya maji yanakuwa historia.
Ameonyesha udhaifu 2005-2010 na ameendeleza udhaifu huo mwaka 2010-2015 hivyo aelekeze Waziri Mkuu atekeleze ahadi iliyotolewa na Waziri Mwandosya kwa niaba yake ya Serikali kuwasilisha katika kila Mkutano wa Bunge Taarifa ya Mpango wa dharura kwa kuwasilisha katika Mkutano huu wa 19 wa Bunge taarifa hiyo.
Aidha, nabashiri kwamba Rais atatumia maadhimisho ya Musoma kwenye uzinduzi wa miradi kueleza ‘mafanikio’ makubwa yaliyopatikana kutokana na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (MMS)- Big Results Now BRN.
Hata hivyo, Rais azingatie kwamba MMS/BRN kwenye Sekta ya Maji haijaweza kushughulikia kwa ukamilifu matatizo niliyoyaeleza kwenye hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni kuhusu Hatua za Haraka za Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na Ushughulikiaji wa Maji Taka Jijini na Nchini (Rejea: http://mnyika.blogspot.com/2013/02/maelezo-na-hoja-binafsi-ya-kupendekeza.html ). Ilani ya CCM ya mwaka 2005 iliahidi ifikapo 2010 maji yangepatikana mijini ikiwemo Jijini Dar Es Salaam kwa asilimia 90 na vijijini kwa asilimia 75 ahadi ambayo haijatekelezwa.
Ili Rais asiendelee kuonekana dhaifu zaidi walau kupitia siku hii ya maji awaagize watendaji katika ofisi yake watekeleze agizo alilowapa la kuitisha kikao cha kazi Ikulu kuhusu matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam mwezi Machi 2013 kama alivyoahidi ( rejea: http://gkitalima.blogspot.com/2013/03/jakaya-kikwete-kukutana-na-mnyika.html na http://www.matukiotz.co.tz/2013/03/mnyika-aitwa-ikulu.html ).
Namshukuru Rais kwamba kuna hatua katika upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa miradi ya Ruvu Chini na Ruvu Juu na pia miradi mingine ya visima vya dharura ikiwemo katika Jimbo la Ubungo ikiwemo mradi wa Mpiji Magohe ambao tumeuzindua siku chache zilizopita kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maji; hata hivyo kasi, nguvu na ari ya mpaka sasa hailingani na ahadi za kufanya tatizo la maji kuwa historia 2010, 2011, 2012, 2013, 2014 na hata 2015.
Zipo hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa iwapo tukikutana  na kujadili udhaifu uliopo katika utekelezaji wa Mpango Maalum wa maji Dar es Salaam; hivyo kwa kuwa nimeshamkumbusha yeye mwenyewe na wasaidizi wake mara kadhaa bila kikao hicho kuitishwa ni wakati sasa wa wananchi wa Dar Es Salaam kushiriki kumkumbusha kwa njia mtakazoona zinafaa.
Kwa kuzingatia hali hii kwa wote wenye kutaka kushiriki ujumbe wetu kwake na kwa wengine kitaifa unapaswa kuwa #MajiNaMabadilikoKwaMaendeleo ( #MaMaMa ) ili tuitumie siku hii na zijazo kuhamasisha mabadiliko yenye kuwezesha kupatikana kwa maji kwa maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla. ( #WaterIs #MaMaMa ).
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
22 Machi 2015

Saturday, March 21, 2015

MUSWADA BINAFSI WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA KUJADILIWA BUNGENI TAREHE 31 MACHI 2015


MUSWADA BINAFSI WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA KUJADILIWA BUNGENI TAREHE 31 MACHI 2015
Nashukuru wote ambao mmekuwa mkifuatilia hatma ya muswada binafsi wa Baraza la Vijana la Taifa niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.
Vijana na wadau wa maendeleo ya vijana mzingatie kwamba muswada huo hatimaye umepangwa kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa Bungeni Jumanne tarehe 31 Machi 2015 katika Mkutano wa 19 wa Bunge.
Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21 Disemba 2013. Maoni kutoka kwa wadau yalikusanywa Oktoba 2014 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii.
Baraza la Vijana la Taifa pamoja na malengo mengine litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Aidha, Baraza hilo litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana ikiwemo kuhusu ajira, elimu na sekta zingine katika Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa maendeleo.
Pia, Muswada huo utawezeshwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kulipa jukumu Baraza la Vijana kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; kuhakikisha kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Kujadiliwa kwa muswada huo ni hatua ya pekee katika historia ya harakati za vijana nchini kwa kuzingatia kuwa Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa  Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.
Hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa kwa wakati pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini.

Natambua mchango wa vijana na taasisi zote za vijana mlioshiriki katika maandalizi ya muswada huu, unaitwa binafsi kwa sababu tu ndio neno linalopaswa kutumika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge lakini ukweli ni kwamba huu ni muswada wenu; mimi ni mwakilishi.

John Mnyika (Mb)
Machi 2015

Kuupitia muswada utakaojadiliwa ingia hapa: