Friday, April 22, 2011

Barabara Bonyokwa na Daraja Ubungo Msewe

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametaka hatua za haraka kuchukuliwa kufanya matengenezo ya Barabara ya Kimara Bonyokwa na daraja la Ubungo Msewe kutokana na uharibifu uliochangiwa na mvua zinazoendelea.

Mnyika aliyasema hayo katika kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi cha Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kilichofanyika mapema wiki hii (19/04/2011) katika ukumbi wa Manispaa hiyo.

“ Nimetembelea barabara ya Bonyokwa ambayo ukarabati wake ulipaswa kufanyika mwaka huu wa fedha; hali ni mbaya, magari yanashindwa kupishana na mawasiliano yanaelekea kukatika. Daraja la Msewe linalounganisha kata ya Ubungo na Chuo Kikuu cha Dar es salaam nalo limezolewa kutokana na mvua zinazoendelea. Hivyo, hatua za dharura zinahitajika kuchukuliwa na Halmashauri. Na kutoa mwito kwa mkurugenzi hususani kupitia idara ya ujenzi kwenda katika maeneo husika na kuchukua hatua za haraka”, Alisema Mnyika.

Kutokana na mwito huo, Mkuu wa Idara ya Ujenzi ya Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Uriyo Athanas aliahidi kufuatilia kwa ajili ya hatua stahiki kuchukuliwa.

Mnyika alisema kwamba ujenzi wa Barabara ya Bonyokwa ni kati ya ahadi za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa mwezi Mei mwaka 2010 wakati alipotembelea kata ya Kimara na kuitaka Manispaa kufuatilia kwa wakala wa Barabara (TANROADS) ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa wakati.

“Katika kipindi hiki ambacho tunasubiria ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, matengenezo ya dharura kwa kuweka kifusi yanapaswa kufanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kuwa ndiyo yenye wajibu huo”, Alisisitiza Mnyika.

Kwa upande mwingine, Mnyika alisema kwamba ukarabati wa daraja la Msewe ambalo limezolewa na maji ni suala la dharura katika kupunguza foleni katika barabara ya Morogoro kwa kuwa njia hiyo imekuwa ikiwezesha sehemu ya magari kupitia njia ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Hatahivyo, Mhandisi Uriyo alieleza kuwa hatua hizo za haraka zinapaswa pia kusubiri kupungua kwa mvua ili kuepusha matengenezo yatayofanyika kuathiriwa na mvua za masika zinazoendelea.

Chanzo: Ofisi ya Mbunge Ubungo

Ps: TANROADS wamekubali kufanya matengenezo kwenye daraja husika kwa haraka

Thursday, April 21, 2011

Mbunge atoa rambirambi vifo vya watoto

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watoto watano vilivyotokea jana tarehe 19 Aprili na leo tarehe 20 Aprili 2011 kutokana na ajali ya kuangukiwa na ukuta katika eneo la Matosa Kimara B, Dar es salaam.

Marehemu hao walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Chekechea ya Nia na walifikwa na mauti hayo kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba jirani na shule yao; watoto wanne walifariki papo hapo jana wakati mmoja amefia hospitali leo.

Mbunge Mnyika ametoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu wote na kuwatakia moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Aidha kufuatia msiba huo, Mnyika ameahirisha kushiriki katika vikao vya Kamati za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni vinavyoendelea leo kwa ajili ya kushiriki maziko ya watoto hao.

Mnyika ameomba taasisi za masuala ya haki za watoto na wadau wengine kujumuika na familia za marehemu kuwafariji katika majonzi.

Kwa upande mwingine, ametoa mwito kwa serikali kufanya uchunguzi wa mazingira ya ajali na kuchukua hatua zinazostahili.

Chanzo: Ofisi ya Mbunge Ubungo

Thursday, April 7, 2011

Serikali itoe kauli ya kina kuhusu ufisadi wa Kagoda

Katika mkutano wa tatu wa Bunge kikao cha kwanza leo tarehe 5 Aprili 2011 niliuliza swali la nyongeza kutokana na swali la msingi namba 4 kwa ofisi ya Rais Wizara ya utawala bora.

Katika swali hilo niliiuliza serikali itoe kauli kuhusu hatua zilizochukuliwa kuhusiana na Kampuni ya Kagoda Agricultural Limited na kukumbusha kwamba serikali imekuwa ikitoa kauli za mara kwa mara bungeni kuwa uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na vyombo vya kimataifa; niliuliza ni lini uchunguzi huo utakamilika.

Katika majibu yake serikali ilitoa kauli kwamba uchunguzi bado unaendelea. Pamoja na kuwa sikuridhishwa na jibu hilo la serikali, hakukuwa na fursa kwa mujibu wa kanuni kuuliza swali lingine.

Hivyo natoa kauli ya kuitaka serikali itoe tamko la kina kuhusu uchunguzi huo kwa kuwa miaka takribani mitatu imepita toka uchunguzi huo uanze.

Itakumbukwa kwamba Kagoda inatuhumiwa kuchota jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) mwaka 2005.
Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu ufisadi wa Kagoda mathalani tarehe 15 Septemba 2006 Waziri wa Fedha wa wakati huo Zakhia Meghji aliandika barua kwa wakaguzi wa mahesabu wa kampuni ya Deloitte& Touche ya Afrika Kusini kuwa fedha za Kagoda zilitumika kwa kazi ya usalama wa taifa na kutaka usiri na busara katika ukaguzi wa mahesabu ya kampuni hiyo. Baadaye Waziri Meghji alifuta barua hiyo.

Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba cheti cha usajili wa Kagoda kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA) kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005.

Mpaka sasa siri za ufisadi wa Kampuni hiyo na wa kampuni zingine zilizohusika kwa wizi wa Kagoda zimebaki kwa Rais Jakaya Kikwete na wajumbe watatu wa timu uliyoiunda wakati huo ikiwemo idadi na majina ya watuhumiwa wanaodaiwa kurejesha sehemu ya fedha.
Wakati serikali imekuwa ikieleza kwamba haiwajui wamiliki wa Kagoda; taarifa mbalimbali zimekuwa zikimtaja Rostam Aziz (Mb) na wengine.

Baadhi ya vyombo vya habari vimewahi kuandika kwamba Wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi (Malegesi Law Chambers) ya Dar es Salaam katika maelezo yake kwa Kamati ya Rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) alikiri kwamba alishuhudia mkataba wa Kagoda na mikataba mingine iliyohusu ufisadi huo.

Wakili huyo alieleza kwamba mkataba huo ulishuhudiwa na Caspian Construction Limited (inayomilikiwa na Rostam Aziz) iliyopo Dar es salaam na kwamba alielezwa kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiwezesha CCM kugharamia uchaguzi na kwamba maelekezo hayo yalitolewa kwa aliyekuwa gavana wakati huo (marehemu Daudi Balali) na Rais wakati huo Benjamin Mkapa.
Hata hivyo, pamoja na serikali kwa wakati wote kuendelea kusisitiza kutowajua wamiliki wa Kagoda; Taarifa za hivi karibuni zimemtaja mfanyabiashara Yusuph Manji kupitia kampuni ya familia yake ya Quality Finance Corporation Limited (QFCL) anadaiwa na serikali kurejesha fedha za Kagoda.

Katika mazingira haya ya utata ndio maana natoa kauli ya kuitaka serikali kutoa tamko la kina kuhusu kashfa hii ya Kagoda.

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
05/04/2011

Tuesday, April 5, 2011

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MSIBA WA MWANAHABARI ADAM LUSEKELELO NA MHADHIRI DR JUSTINE KATUNZI

Nikiwa safarini kwenda Dodoma naomba kueleza masikitiko yangu kwa vifo vya wakazi wawili wa Jimbo la Ubungo ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwa taifa letu kwa namna mbalimbali.

Mosi, ni kifo cha mwanahabari mwandamizi Adam Lusekelo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupitia kalamu yake kuhamasisha uwajibikaji katika taifa letu. Marehemu Lusekelo amekuwa akiandika kwa kutumia mfumo wa sitiari (satire) kupitia safu maarufu za “In A Light Touch”, “Eye Spy” nk kadhaa vya habari. Natoa mwito kwa wadau wa sekta husika kumuenzi marehemu Lusekelo kwa kukusanya makala zake na kuziweka pamoja katika kitabu kwa jina lake ili maudhui yake ya ukombozi yaendelee kukumbukwa na vizazi vijavyo.

Pili, ni kifo cha mhadhiri katika Chuo Cha Biashara cha Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDBS) Dr Justine Katunzi ambaye ametoa mchango katika fani ya utawala na usimamizi wa rasilimali kwa kutoa mafunzo na machapisho mbalimbali.

Natuma salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wawe na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Wasalaam,

John Mnyika (Mb)
04/04/2011

Sunday, April 3, 2011

Kauli juu ya Hotuba ya Rais kuhusu umeme

Aprili Mosi 2011 Rais Jakaya Kikwete alilihutubia taifa na kuzungumzia masuala matatu: shughuli ya kutembelea Wizara na Idara za serikali, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Katiba Mpya.

Katika hotuba hiyo Rais Kikwete alizungumzia kuhusu hali ya umeme nchini na gharama za kuunganisha umeme kama sehemu ya mambo aliyoyatolea maelekezo wakati wa ziara yake katika Wizara ya Nishati na Madini.

Katika hotuba hiyo Rais Kikwete amekiri kwamba serikali yake haina suluhisho lolote la umeme wa dharura kwa ajili ya kupunguza mgawo wa umeme katika kipindi cha sasa mpaka Julai zaidi ya kutegemea kudra ya mvua kuendelea kunyesha. Katika hali hiyo Rais alipaswa kuwawajibisha wote waliochelewesha maandalizi ya kukabiliana na dharura ambayo yalijulikana toka mwaka 2008 na Rais Kikwete amekuwa akiyatolea maelezo na maelekezo toka wakati huo bila kusimamia kikamilifu utekelezaji.

Aidha kauli ya Rais Kikwete kwamba mchakato wa kukodi mitambo ya kufua umeme wa megawati 260 uko kwenye hatua ya zabuni kutangazwa imedhihirisha uzembe kwa upande wa serikali kwa kuwa toka mwezi Februari kauli hiyo hiyo imekuwa ikijirudia hali ambayo inaashiria kwamba mpango huo hautakamilika mwezi Julai mwaka 2011 kama inavyodaiwa. Uamuzi wa kukodi mitambo hiyo ulifikiwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 15 Februari 2011 ambacho Rais Kikwete alikuwa mwenyekiti wake, Rais baada ya kikao hicho alipaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maazimio husika badala ya kusubiri mpaka kutoa maagizo mengine kwenye ziara ya wizarani mwezi Machi mwishoni. Hali hii itapelekea taifa kulipia baadaye mitambo ambayo haitatumika kikamilifu katika kipindi chote cha dharura kama ilivyotokea katika kashfa ya Richmond/Dowans.

Kadhalika kauli ya Rais Kikwete imedhihirisha kuwa serikali yake imeshikilia msimamo wa kukodi mitambo ambayo itatumika kwa kipindi cha miezi sita pekee kwa gharama za zaidi ya bilioni 400 badala ya kuweka mkazo katika kununua mitambo kama ambavyo imeshauriwa na wadau mbalimbali. Ni muhimu kwa Wizara husika kuueleza umma kiwango cha fedha ambacho kitatumika katika mpango huu ambacho kimsingi kitazidi kuongeza mzigo wa madeni kwa TANESCO.

Pia, serikali ieleze maandalizi ambayo yamekwishafanyika mpaka hivi sasa kukabiliana na tatizo la upatikanaji, usafirishaji na uhifadhi wa mafuta mazito (HFO) ambayo yatahitajika kwa kiwango kikubwa katika kuendesha mitambo hiyo katika mikoa itakayowekwa mitambo hiyo. Jambo hili ni muhimu kwa kuwa katika mazingira ya sasa serikali inashindwa kukabiliana vya kutosha na mahitaji ya mafuta mazito kwa mitambo ya megawati 100 ya IPTL iliyopo Dar es salaam ambayo hutumia takribani bilioni 15 kwa mwezi kwa mafuta pekee.

Kwa upande mwingine, naunga mkono kauli ya Rais ya kuwataka TANESCO kuangalia kwa haraka namna ya kupunguza gharama kubwa za kuwaunganishia umeme wateja jambo ambalo nimekuwa nikitoa mwito kwa serikali kulifanya toka mwaka 2010. Natambua kwa Rais Kikwete amekubaliana na pendekezo la kuwaunganishia watu umeme na kuingiza gharama hizo katika bili ya umeme kidogo kidogo hata hivyo ni muhimu pendekezo hilo likaambatana pia na utaratibu ambapo wananchi wanapogharamia wenyewe vifaa kama nguzo za umeme basi gharama hizo warejeshewe kupitia punguzo katika malipo ya bili zao kama umeme uliolipiwa kabla kwa kuwa miundombinu hiyo hubaki kuwa mali ya TANESCO.

Hatahivyo, pamoja na kutoa kauli kwa TANESCO Rais Kikwete alipaswa kuwaeleza watanzania namna serikali yake ilivyojipanga kuipunguzia mzigo wa madeni TANESCO kutokana na madeni ambayo serikali inadaiwa na pia mzigo mkubwa ambao TANESCO inaubeba kutokana na mikataba mibovu ya kifisadi ambayo serikali iliingia. Kuwepo kwa gharama kubwa ya kuunganisha umeme na bei ya umeme wenyewe ni matokeo ya mzigo wa madeni na ufisadi katika mikataba kubebeshwa wateja waliopo. Sekta ikiwemo umeme imegubikwa na rushwa na ufisadi mkubwa ukihusisha viongozi wa juu wa Serikali tangu mwaka 1991, wakati wa IPTL ambayo inaendelea kuitafuna nchi hadi leo. Pamoja na kashfa ya Dowans/Richmond mwaka 2006 serikali iliingia mkataba na Alstom Power Rentals kuzalisha umeme wa dharura Mkoani Mwanza na kampuni hiyo kulipwa bilioni takribani 40 bili kuzalisha umeme wowote. Hivyo natoa mwito kwa Serikali kupitia upya haraka mikataba ya umeme hapa nchini ambayo imeliingiza taifa katika fedheha na hasara kubwa, ikiwemo mikataba ya IPTL na Songas,Artimas,Tanpower Resources /Kiwira, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kishera na kinidhamu patakapobainika uzembe au ufisadi wowote kwa wote wanaohusika, kwa mikataba iliyoisha lakini ambayo iliingiza nchi katika hasara kubwa kama sehemu ya mkakati wa kupunguza gharama za umeme nchini Tanzania.

Nilitarajia pia Rais Kikwete angetumia hotuba hiyo kueleza kwa umma maelekezo ambayo ameyatoa kwa Wizara ya Nishati na Madini kuhusu sekta ndogo ya mafuta hususani yanayohusiana na ubora na bei ya mafuta ikiwemo mkakati wa kupunguza tozo na kodi ili kupunguza gharama ambazo zinaongeza ugumu mkubwa wa wananchi hivi sasa. Kwa ujumla, maagizo ambayo Rais Kikwete ameyatoa mengi ni yale yale ambayo amekuwa akiyatoa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2006 mpaka 2010, hivyo wakati umefika sasa kwa Rais kusimamia kikamilifu utekelezaji wa masuala ambayo baraza la mawaziri ambalo yeye ni mwenyekiti wake ndicho chombo cha haraka zaidi kinachopaswa kuongeza ufanisi. Mfumo wa utawala unaotumiwa na Rais Kikwete wa kuzunguka (Management By Walking Around-MBWA) hauwezi kuleta tija ya kutosha ikiwa Rais Kikwete hataweka mkazo katika mifumo ya kiutawala inayozingatia malengo na matokeo (Management by Objectives and Results).

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli-Nishati na Madini
02/04/2011

Friday, April 1, 2011

TAMKO LA AWALI KUHUSU MUSWADA WA MABADILIKO YA KATIBA

Nimeshtushwa na maudhui ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011 (The Constitutional Review Act 2011) uliochapwa katika gazeti la serikali toleo No. 1 Vol. 92 la tarehe 11 Machi 2011. (Muswada unapatikana hapa: http://www.policyforum-tz.org/node/7806)

Maudhui ya muswada huu yamedhihirisha tahadhari niliyotoa mara kadhaa kwamba serikali haina dhamira ya kweli ya kuhakikisha panakuwepo na mchakato mzuri wa kuwa na katiba mpya.

Muswada huo umelenga kuhalalisha yote ambayo yalitangazwa kufanywa na Rais kuhusu mchakato wa katiba mpya na kupingwa na wadau mbalimbali; sasa yanataka kupewa uhalali kwa sheria inayotaka kutungwa na bunge kupitia muswada huo.

Muswada huo unataka kumpa mamlaka Rais ya kuunda tume ya kuongoza mchakato mzima wa katiba bila kuhusisha bunge ama wadau wengine wa msingi. Muswada huo pia utaka kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa tume husika bila kushauriana na mtu yoyote isipokuwa Rais wa Zanzibar. Muswada huo unaelekeza kuwa katika kuteua wajumbe Rais atazingatia uwakilishi wa makundi ya kijamii, lakini makundi husika hayatajwi hata kwa ujumla wake na hivyo kuacha mamlaka yote ya kuamua uwakilishi kubaki kwa Rais.

Muswada huo unataka kumpa Rais mamlaka ya kutengeneza hadidu rejea za Tume jambo ambalo lilipaswa kufanywa Bunge kwa kuwa sehemu ya sheria husika ama kufanywa na mkutano mkuu wa kikatiba. Kwa kutoa mamlaka ya kuunda hadidu rejea kwa Rais mwanya umetolewa kwa mtu mmoja kuweka mipaka ya nini kinastahili kufanywa na tume wakati wa mchakato wa katiba mpya na hivyo kuminya wigo wa mabadiliko.

Muswada huo unataka Tume iwasilishe ripoti yake kwa Rais ambaye atampa nakala Rais wa Zanzibar na baadae kumwelekeza waziri mwenye dhamana kupeleka yale atayoamua Rais bungeni. Muswada huu kwa kuwa na kifungu hiki utaendeleza yaliyofanywa na marais waliopita kuhusu ripoti na mapendekezo ya tume zingine na hivyo kukwamisha mabadiliko ya kweli.

Muswada huo unataka kutoa mamlaka kwa tume itayoundwa kuitisha jukwaa (fora) ambalo litaundwa kwa ajili ya kupata maoni pekee (ad hoc) badala ya kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa Katiba (National Conference/congress) kama wadau walivyohitaji. Aidha uwakilishi katika jukwaa hilo umejwa tu kuwa ni wa kijografia na kimakundi bila kuweka bayana mnyumbuliko wa uwakilishi. Muswada huo unataka kutoa mamlaka finyu kwa jukwaa hilo kuwa ni kutoa ushauri kuhusiana na muswada; tofauti na mkutano mkuu wa kikatiba ambao ungekuwa na mamlaka zaidi katika mchakato husika.

Muswada huo unataka kutoa mamlaka kwa Rais kuitisha bunge la katiba (constituent assembly) ikiwemo kuteua wajumbe wa bunge husika. Muswada huo unataka kutoa mamlaka makubwa kwa Rais kuteua wawakilishi wa chombo kikuu zaidi katika mchakato wa katiba bila kushauriana na kundi lolote ama wananchi kuhusika katika uteuzi ama kuwa na wawakilishi walioteuliwa na makundi yenyewe mathalani vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama wa wakulima, vyama vya wanafunzi, vyama wa wafanyakazi nk. Muswada huo unataka Rais ashauriane na Rais wa Zanzibar na mwanasheria mkuu wa serikali pekee. Muswada huo unatoa mamlaka makubwa zaidi ya Rais kuamua hata kufanya bunge la kawaida kuwa ndilo bunge la katiba, jambo ambalo linaweza kurejesha udhaifu uliofanywa katika mchakato wa katiba inayotumika sasa ambapo umma uliporwa wajibu na mamlaka yake ya kushiriki moja kwa moja katika kupitisha katiba.

Muswada huo kwa ujumla haujaeleza muda wa mchakato wa katiba na vipindi vitavyotumiwa na vyombo mbalimbali katika hatua mbalimbali za mchakato wa katiba; ama kutoa mamlaka ya kuwekwa kwa muda huo kwa chombo chenye uwakilishi mpana wa umma kama mkutano wa katiba au bunge na hivyo kutoa mwanya kwa mchakato mzima kucheleweshwa.

Haya ni baadhi ya maudhui ndani ya muswada husika ambayo yamenishtusha na kunifanya nitoe tamko hili la awali wakati nikiendelea kufanya uchambuzi wa kina ambao nitautolea kauli katika hatua za baadaye.

Lengo la kutoa tamko hili la awali ni kutoa mwito kwa vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari, taasisi za dini na watanzania kwa ujumla wakiwemo wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo kufuatilia kupata nakala ya muswada huo ama maudhui yake kwa ajili ya kuujadili kwa dharura na kutoa matamko. Aidha kwa katika kauli hii ya awali naitaka serikali itoe taarifa kwa umma namna ambavyo wananchi wanaweza kupata nakala za muswada huo nyeti na sababu za serikali kupuuza maoni mengi ya wadau yaliyotolewa kabla ya kuandaliwa kwa muswada huo kuhusu mchakato unaofaa kuongoza mabadiliko ya katiba katika taifa letu.
Ikumbukwe kuwa tarehe 9 Februari 2011 nilitoa tamko kuwa nilipokea kwa tahadhari uamuzi wa Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kubadili misimamo ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kuamua kukubaliana na mwito wa kutaka mchakato husika uanzie bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika kama nilivyokuwa nikitoa mwito kwa nyakati mbalimbali.

Nilieleza kwamba nilipokea kwa tahadhari kwa kuwa bado kauli za serikali kuhusu mchakato husika zina utata kwa kuwa hotuba ya Rais Kikwete ya tarehe 5 Februari 2011 pamoja na kutaja kuwa katiba mpya itapitishwa kwa kura za maoni, haikueleza iwapo Mkutano Mkuu wa Kikatiba utaitishwa katika hatua za awali za mchakato husika. Utata huu unaongezeka zaidi kwa kuwa Waziri Mkuu Pinda akilihutubia bunge tarehe 8 Februari 2011 pamoja na kueleza kwamba muswada kuhusu mchakato husika utawasilishwa kwenye mkutano wa tatu wa bunge mwezi Aprili, ameelezea kuwa sheria husika itahusu kuundwa kwa tume.

Katika muktadha huo nilitoa kauli ya kuitaka serikali iwapo muswada unaopelekwa bungeni mwezi Aprili iwapo utaweka utaratibu wa kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba kuanzia hatua za awali pamoja na mwishowe kupigwa kwa kura kwa kura za maoni. Ni muhimu kwa tume ya mchakato wa katiba kuandaliwa hadidu rejea zake na kuundwa na mkutano wa kikatiba ambao utaweka tunu/misingi muhimu kabla ya kuanza kwa mchakato, ili tume ikusanye maoni, ipeleke rasimu kwa mkutano mwingine wa kikatiba na hatimaye katiba ithibitishwe kwa kura ya maoni. Nilitoa mwito pia kwa serikali kutoa ufafanuzi iwapo sheria husika inayokusudiwa kutungwa itagusa marekebisho ya katiba ibara ya 98 ili kutoa uhalali kwa katiba mpya kupitishwa na umma kupitia mkutano wa kikatiba na kura za maoni badala ya bunge pekee ambalo kwa sasa ndicho chombo chenye mamlaka ya mabadiliko ya katiba.

Ikumbukwe kwamba msimamo wa awali wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu mabadiliko ya katiba alioutoa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari tarehe 17 Disemba 2010 ulikuwa na kumshauri Rais aunde jopo shirikishi ili kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Kutokana na msimamo huo tarehe 19 Disemba 2010 nilifanya Mkutano na waandishi wa habari na kupinga msimamo huo na kueleza kwamba ni muhimu kwa mchakato wa katiba mpya kuanzia bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika badala ya kuundwa kwa jopo shirikishi la wataalamu kama alivyotaka Waziri Mkuu. Aidha katika mkutano huo nilipingana na azma ya Waziri Mkuu Pinda ya kutaka marekebisho ya katiba badala yake nikaitaka serikali itangaze rasmi kuanzisha mchakato wa katiba mpya. Katika Mkutano huo na waandishi wa habari nilidokeza kuwa kutokana na serikali kutoa msimamo wa kutokupeleka hoja au muswada wa serikali bungeni wa kuratibu na kusimamia mchakato husika nitalazimika kupeleka hoja binafsi bungeni ili bunge litipishe maazimio ya kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya ili hatimaye kuwezesha kutungwa kwa sheria ya kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Tarehe 27 Disemba 2010 nilitekeleza azma hiyo kwa kuwasilisha taarifa ya hoja kwa katibu wa bunge ya kutaka kuwasilisha hoja ili bunge lipitishe azimio la kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya na kupitisha utaratibu wa kisheria wa kuratibu na kusimamia mchakato mzima. Katika Mkutano wangu na waandishi wa habari siku hiyo nilieleza kwamba baadhi ya mambo ya msingi yatayozingatiwa katika hoja binafsi ni pamoja na kuhakikisha kwamba kunatungwa sheria ya kuwezesha kuitishwa kwa mkutano mkuu wa taifa wa kikatiba, tunatunga sheria ya kuwezesha tume ya kuratibu mchakato husika kuundwa kwa sheria ya bunge badala ya kuteuliwa na Rais, kutoa kwa mujibu wa sheria elimu ya uraia kwa umma kuhusu maudhui na mchakato husika na kuweka utaratibu wa kisheria wa kuwezesha kufanyika kwa kura za maoni.

Tarehe 31 Disemba 2010 Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa akatangaza kukubaliana na suala la kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya na kutangaza dhamira yake kuwa ya kuunda tume ya kusimamia mchakato husika na hatimaye vyombo vya kikatiba kufanya mabadiliko husika.
Tarehe 2 Januari 2011 nilitoa kauli yangu kwa umma ya kuitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu kauli ya Rais Kikwete na kueleza bayana iwapo serikali inakubaliana na hoja ya kupeleka suala husika ili mchakato uratibiwe na kusimamia kwa sheria itayotungwa na bunge itayaozingatia kufanyika kwa mkutano wa kitaifa wa katiba, kuundwa kwa tume kwa mujibu wa sheria badala ya uteuzi wa Rais na hatimaye kufanyika kwa kura za maoni; na nikaeleza bayana kwamba wakati nasubiria ufafanuzi wa serikali taarifa yangu ya hoja binafsi kuhusu katiba inaendelea.

Tarehe 7 Januari 2011 badala ya kutoa ufafanuzi na kueleza azma ya serikali kupeleka suala husika bungeni Rais Jakaya Kikwete akarudia tena mbele ya mabalozi kwenye hafla ya mwaka mpya kuwa anakusudia kuunda moja kwa moja tume ya kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa maoni bila kuhusisha bunge katika hatua za msingi.

Kutokana na serikali kuendeleza msimamo huo tarehe 9 Januari 2011 nilitoa tamko kwa umma la kupinga utaratibu wa Rais kuunda moja kwa moja tume ambapo ni kuendeleza hodhi ya serikali na kusababisha mapitio (review) ya katiba na hivyo kuendeleza kasoro za msingi kama zilivyojitokeza katika vipindi vilivyopita. Katika tamko langu hilo nilieleza wazi kuwa kama serikali itaendelea na msimamo wake wa kutaka kuunda tume ya Rais badala ya mchakato husika kuanzia bungeni hali hiyo itadhihirisha serikali kutokuwa na dhamira ya kuandikwa kwa katiba mpya na umma wenyewe. Kutokana na hali hiyo nilitoa tamko ya kuendelea na uamuzi wangu wa kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili mchakato husika uanzishwe kwa maazimio ya bunge na kusimamia kwa sheria itayotungwa na bunge.

Siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa bunge (ambao ulianza tarehe 8 Februari 2011 ) hatimaye serikali kupitia Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilieleza dhamira ya kulipeleka suala la mchakato wa katiba mpya bungeni kupitia kuwasilisha muswada wa serikali na hivyo kubadili msimamo wa awali wa kutaka kuunda moja kwa moja tume ya Rais na kukubaliana na sehemu ya hoja yangu ya kutaka mchakato husika kuanzishwa na kusimamiwa kwa sheria iliyotungwa na bunge.

Wakati wote nimekuwa nikisisitiza kuwa ipo haja ya suala hili la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Rais Jakaya Kikwete akihutubia Mkutano wa CCM tarehe 5 Februari 2011 alitoa kauli kuwa Kiserikali matayarisho yanaendelea ya kupeleka Bungeni Mswada wa Sheria wa kuanzisha mchakato wa katiba mpya ikijumuisha kuundwa kwa Tume ya kuongoza mchakato huo. Aidha katika Mkutano huo Rais Kikwete aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni na katika kupiga kura ya maoni itakayoidhinisha katiba hiyo.

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisoma tamko la serikali bungeni tarehe 8 Februari 2011 alisema kwamba serikali katika kuitikia mwito wa wananchi kuundwa kwa katiba mpya imetangaza kuwa itawasilisha bungeni muswada wa kuundwa kwa tume itayoratibu mchakato wa katiba mpya katika mkutano wa tatu wa bunge la kumi Aprili mwaka 2011.
Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
30/03/2011