Tuesday, August 28, 2012

DAWASCO NA DAWASA WASHUGHULIKIE MATATIZO YA MAJI MBEZI


Nimefuatilia Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na kujulishwa kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa kuhusu matatizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya kata za Mbezi Luis na Msigani kwa takribani wiki tatu kufuatia ratiba ya mgawo wa maji kuathiriwa na kuhamishwa kwa huduma ya maji kutoka katika bomba la maji la inch 24 mpaka la inch 30. Hali hiyo imeathiri zaidi maeneo ya Magari Saba, Kibanda cha Mkaa, Kwa Msuguri, Temboni na maeneo mengineyo. 


Aidha, kuhusu maghati ya umma na maeneo ya pembezoni ambayo yalikuwa na matatizo makubwa ya maji kabla hata ya kipindi husika ikiwemo maeneo ya Bwaloni na Msingwa, nimeiandikia barua Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kuwaalika kufanya nao ziara ya kikazi mapema iwezekanavyo katika maeneo husika kwa ajili ya kutoa maelezo ya kiutendaji kuhusu hali iliyopo na kueleza mipango inayopaswa kutekelezwa ya kupata ufumbuzi wa haraka.

Natoa taarifa hii kwa kuzingatia kuwa tarehe 25 Agosti 2012 nilipokutana na wananchi katika eneo la Mbezi kwa Msuguri wakati nikiwa katika kazi ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika sensa, kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya na kupata mapendekezo yao kuhusu masuala ya kuyapa kipaumbele baada ya kurejea kutoka katika mkutano wa nane wa Bunge nilielezwa kuhusu matatizo ya maji katika maeneo tajwa.

Kufuatia maswali yaliyoulizwa na masuala yaliyoelezwa nilitoa majibu ya ujumla kwamba: Mosi, kuhusu matatizo yaliyojitokeza nilieleza kuwa chanzo chake ni marekebisho yaliyokuwa yakiendelea ya kuondoa baadhi ya watu waliokuwa wamejiunganisha maji kinyemela katika mabomba makuu pia kuhamisha huduma kwa wananchi wa maeneo tajwa kutoka bomba la inch 24 mpaka la inch 30, hata hivyo kwa kuwa matatizo hayo yameendelea niliahidi kuwasiliana na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na kutoa majibu ya hatua za kuharakisha huduma ya maji kurejea katika hali ya kawaida.

Pili, kuhusu maeneo ambayo yalikuwa hayatoki maji hata kabla ya wiki tatu ikiwemo baadhi ya maghati ya umma na maeneo ya pembezoni nilieleza chanzo cha hali hiyo kwa kadiri ya majibu niliyoelezwa na DAWASCO nilipofanya nao ziara katika kata ya Msigani tarehe 1 Machi 2012 na kwa kuwa matatizo katika maeneo hayo yanahitaji hatua kubwa zaidi niliahidi kwamba nitawaalika Watendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) ili kufanya nao ziara ya kikazi karibuni kuweza kutafuta ufumbuzi.

Izingatiwe kwamba kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali na vyombo vyake kuwezesha maendeleo, na katika muktadha huo Machi Mosi 2012 niliungana  pamoja na DAWASCO kwenye kata za Sinza, Makurumla, Mburahati, Msigani, Mabibo, Saranga, Kwembe na Makuburi kufuatilia kazi za kuboresha upatikanaji wa maji katika Jimbo la Ubungo.

Kupitia ushirikiano huo tuliona bayana kwamba mtandao wa biashara haramu ya maji unaohusisha kujiunganisha mabomba ya maji kinyemela nao unachangia katika matatizo ya maji katika baadhi ya maeneo, mathalani tuliona mota za biashara hizo katika  maeneo ya kata ya Makurumla hususani mtaa wa Kagera, Makuburi kwenye nyumba yenye matanki yaliyounganishwa chini chini kwa ajili ya biashara ya maji na Kata ya Saranga eneo la Kimara B ambapo mtandao wa maji ulitolewa toka kwenye maeneo ya wananchi na kupelekwa nje ya makazi ya watu kwenye mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa maji. Mitandao hiyo ilianza kukatwa na majalada yalifunguliwa polisi kwa ajili ya wahusika kuchukuliwa hatua za kijinai.

Hali hiyo ilishamiri kutokana pia na vishoka na tulikubaliana kwamba kuanzia wakati huo yoyote anayekwenda kugusa bomba la DAWASA lazima kwamba aripoti kwenye serikali za mitaa na pia popote anapofanya kazi hizo lazima awe na kitambulisho cha DAWASCO na pia kadi ya kazi (job card) yenye saini ya meneja wa eneo ya kueleza aina ya kazi na ruhusa iliyotolewa kuifanya. Nachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua dhidi ya yoyote anayekwenda kinyume na makubaliano hayo kama ilivyo kwa wahalifu wengine wanaokiuka sheria.

Katika kazi tulizofanya Machi Mosi 2012, ilionekana bayana kwamba bado yapo maeneo ambayo mtandao wa mabomba ya wachina hautoi maji kutokana na msukumo mdogo na matatizo ya mfumo mzima, kama ilivyo katika majimbo yote ya Dar es salaam, Kwa upande wa Jimbo la Ubungo hali hii imeathiri maeneo ya Malambamawili, kwa Msuguri, Makoka na mengine. Aidha, yapo maeneo ambayo hayakufikiwa kabisa kwenye awamu ya kwanza ya utandazaji wa mabomba husika mathalani ya Msingwa, Mbezi Msumi na mengineyo katika jiji la Dar es salaam.

Haya ni masuala yanayohusu mwenye mali na miundombinu ambaye ni Serikali kupitia Wizara ya Maji na DAWASA, zaidi ya DAWASCO ambayo pamoja na kuwa nalo ni shirika la umma ni mwendeshaji tu. (Maji DSM ni kama duka, kuna mwenye bidhaa ambaye anawajibika kujaza duka lake ili wateja wasikose-DAWASA na muuza duka ambaye ana kazi ya kuuza duka lenye bidhaa chache-DAWASCO malalamiko mengi ya wateja yanamuangikia yeye).

Kufuatia hali hiyo niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge hoja Binafsi kwenye mkutano wa nane wa Bunge uliomalizika kutaka bunge lipitishe maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam; hata hivyo hoja hiyo haikupangiwa kujadiliwa bungeni kutokana na ufinyu wa muda baada ya ratiba ya bunge kufanyiwa marekebisho na kipengele cha hoja za wabunge kuondolewa. Kutokana na hali hiyo, wakati nikisubiri mkutano tisa wa bunge unaofuata niendelee na kazi zingine ikiwemo kuwaandikia DAWASA ili wafike jimboni Ubungo na kuchukua hatua kwa masuala ya maendeleo yaliyo ndani ya uwezo wao.

Wenu katika uwakilishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
27 Agosti 2012




Monday, August 27, 2012

Msimamo wangu vurugu,risasi,kujeruhi na “kuua” Morogoro!



Niliwahi kutahadharisha baada ya tukio la Dkt Stephen Ulimboka kuwa serikali imeanza kutumia mbinu haramu kudhibiti fikra mbadala, CCM imeanza kuongoza serikali kiimla na ipo siku umma utafikia hatua ya kukiona kama chama cha mauaji. Raia watatu wasio na hatia wamefyatuliwa risasi na mmoja amefariki. Haya yamefanyika kwenye maandamano ya amani ya wananchi kuwapokea viongozi wa CHADEMA kuelekea kwenye mkutano. Vurugu zimeanzishwa na polisi kwa mujibu wa mashuhuda wa ushahidi wa video. Vyanzo vyangu vinaniambia sasa wameagiza gari tatu za FFU na gari za kuwasha toka Dar Es Salaam. Tuombe MUNGU wasiamue kuvuruga mkutano wa hadhara ambao wananchi wamekusanyika kwa wingi hivi sasa. States captured by grand corruption of the ruling party cronies for so many years resorts to bullets as a way of stopping M4C through the ballot. Maisha ya wachache yako mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.

John John MNYIKA,
27 Agosti, 2012

Nape amezidi kuibua vioja!!


Leo Nape Nnauye amekwepa kujibu hoja ameibua vioja. Kwa kuwa amekataa kuomba radhi, CHADEMA kitamburuza mahakamani kwani madai yake ya uongo kwa CHADEMA imepata mabilioni toka nje hayawezi kuwa na ushahidi wa ukweli. Nape na CCM wajibu hoja kwa kuwa Dr. Slaa alitaja mpaka namba ya silaha, CCM ilipaswa kueleza iliingiaje nchini na suala ambalo Nape hajui kwa hiyo tunasubiri jibu la Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete. CCM huwa wanatoa madai ya uongo dhidi ya CHADEMA ushahidi ni hukumu ya kesi ya Igunga ambapo ilithibitika Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alizusha kuwa CHADEMA imeingiza magaidi toka nje ya nchi. Kati ya CHADEMA na CCM ni chama kipi kimepoteza mvuto jibu wanatoa wananchi wanavyounga mkono vuguvugu la mabadiliko (M4C) kwa hali na mali kwa kiwango cha CCM kufanya siasa chafu.

Baada ya Dr.Slaa kufichua silaha za CCM, leo wametumia za polisi Morogoro. Umma umeweka hofu pembeni, mkutano umejaa name naelekea huko tukawavue magamba. Peopleeee……..ss!!!

John John Mnyika
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
27 Agosti, 2012

Tunapaswa kuendelea kushiriki vuguvugu la mabadiliko!


Nimetoka kwenye kikao cha RCC. Itachukua muda  kwa uozo aliouanika kwenye UDA, kituo cha mabasi Ubungo, soko la Karikoo, fidia ya wahanga wa mabomu Gongo la Mboto, EAMTCO kushughulikiwa!

Nchi hii ina uozo sehemu nyingi hali inayohitaji mabadiliko ya utawala ili kuharakisha maendeleo. Kadiri tunavyojifungia DSM na kuleta maendeleo kidogo mjini, huku vijijini wakididimia kwenye umaskini ndivyo watu wengi hukimbilia DSM na vijana kukosa ajira na miundo mbinu ya maji, barabara na mengine mengi kuzidiwa DSM. Hatimaye DSM nayo itaendelea kuwa jiji lenye kero. Kwa hiyo, tunao wajibu pamoja na kuisimamia serikali kwa maendeleo ya DSM, tuna wajibu pia wa kuunganisha nguvu kuwezesha vuguvugu la mabadiliko vijijini. Leo naelekea Morogoro, kesho nitakuwa Iringa na kesho kutwa nitarejea DSM kuendelea na kazi za maendeleo jimboni Ubungo kwa mwezi mzima wa Septemba.

Maslahi ya Umma Kwanza.

John John Mnyika
Jimboni Ubungo
27 Agosti, 2012

Chadema Kimemtaka Katibu Mwenezi wa CCM Nape Nnauye Kukiomba Radhi Chama Hicho ndani ya Siku Saba na Kulipa Fidia


Chadema imeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nape Nnauye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kufuatia madai ya uzushi na uongo aliyoyatoa tarehe 12 Agosti 2012

Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari leo asubuhi.Picha na Francis Dande
---
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nape Nnauye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kufuatia madai ya uzushi na uongo aliyoyatoa tarehe 12 Agosti 2012 kuwa anao ushahidi kwamba CHADEMA kimekuwa kikiwahadaa wananchi kwa kuwachangisha fedha huku kikipokea mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili kutoka nje.
Izingatiwe kuwa matamshi yake yalitangazwa na vyombo vya habari vya kielekroniki ikiwemo vituo vya televisheni, radio na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii tarehe 12 Agosti 2012 na katika kurasa za mbele za magazeti mbalimbali tarehe 13 Agosti 2012.
Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA iliagiza wanasheria wamwandikie barua ya kumtaka kukiomba radhi Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kwa kutumia njia ile ile aliyotumia kufanya propaganda chafu za kuikashifu na kuifitisha CHADEMA kwa umma wa watanzania ikiwemo kuzusha kuwa upo uwezekano wa CHADEMA kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani.
Tayari ameshaandikiwa barua ya kisheria tarehe 24 Agosti 2012 ya kumtaka aombe radhi na kulipa fidia ya bilioni tatu kwa matamshi hayo ya uzushi na uongo yenye maana ya kuwapotosha waliyoyasikia na kuyasoma kuwa CHADEMA kinawalaghai wananchi, kina viongozi wasio waaminifu na kwamba kiko tayari kuuza nchi wa uroho wa madaraka.
Kipaumbele cha CHADEMA katika suala hili ni kuombwa radhi hata hivyo kiwango cha fidia ya fedha kwa fedheha kilichotakiwa ni fundisho kuwa uzushi na uongo unagharimu.
Ikumbukwe kwamba tarehe 12 Agosti 2012 nilitoa kauli ya awali baada ya mkutano Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine nilieleza kwamba tutatoa tamko la kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa kamili aliyoitoa.
Katika kauli hiyo nilitoa mwito kwa Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete kueleza watanzania iwapo propaganda hizo chafu zina baraka zake; hivyo ukimya wake mpaka sasa kuhusu matamshi hayo inakifanya CHADEMA kuwa na imani yenye shaka (benefit of doubt) kwamba Nape hakutumwa na chama chake kutoa matamshi aliyoyatoa.
CHADEMA inachukua fursa hii kuutaarifu umma kwamba asipotekeleza matakwa hayo ndani ya siku saba kuanzia tarehe hiyo aliyopokea barua hatua nyingine ya kumfikisha mahakama kuu zitaanzishwa ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi.
Pamoja na kuchukua hatua za kisheria, CHADEMA kinaendelea kutimiza dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania kwa pamoja na mikakati mingine kutekeleza operesheni ya vuguvugu la mabadiliko nchini (M4C) na tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kuunganisha nguvu ya umma kwa hali na mali katika maeneo mbalimbali nchini.
Imetolewa tarehe 26 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

Sunday, August 26, 2012

Mrejesho wa ufuatiliaji wa hali duni ya barabara jimboni Ubungo


Nimeziandikia mamlaka husika za Serikali kutoka ofisini na kwenda kukagua wa ubovu wa barabara za Kimara-Mavurunza-Bonyokwa, Ubungo Maziwa-Kisiwani Darajani- Mabibo External, Makuburi-Kibangu-Makoka ili kuweza kufanya maamuzi ya matengenezo ya haraka.

Nimechukua hatua hiyo baada ya kuona hali halisi ya barabara hizo nilipozitembelea kati ya tarehe 24 na 25 Agosti 2012 na pia kutokana na maoni ya wananchi niliokutana nao katika tarehe hizo kwenye kata za Kimara, Mabibo na Makuburi.

Kwa upande wa Barabara ya Kimara-Mavurunza-Bonyokwa ambayo tayari Wizara ya Ujenzi imekubali kuihudumia, leo tarehe 27 Agosti 2012 nitapeleka barua kwa meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es salaam kutaka hatua zake kwa hali mbovu ya barabara hiyo pamoja na kuwa kero wa wananchi inamwaibisha Rais Kikwete mbele ya wakazi husika kwa kuwa alitembelea mwaka 2010 na kuahidi itajengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, mwaka 2011 ilifanyiwa matengenezo ya kawaida lakini kwa sasa imeharibika tena kufuatia mvua zilizonyesha, hali mbovu ya barabara hiyo inaathiri pia hatua za kupunguza msongamano kwenye barabara ya Morogoro wakati huu ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) unapoendelea kwa kuwa barabara hiyo hutumika kama njia mbadala kutoka Manispaa ya Kinondoni mpaka Manispaa ya Ilala.

Kuhusu barabara Ubungo Maziwa-Kisiwani Darajani-Mabibo External leo nitamkumbusha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya barabara kwa mkoa afuatilie kutoka mfuko wa barabara fedha za ujenzi wa daraja kwa dharura kwa kuwa kwa hali ya sasa na uzito wa magari yanayopita daraja linaweza kuvunjika na kusababisha maafa. Aidha, asimamie pia utekelezaji wa upande wa TANROADS kwa kuwa fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo zilishatengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na nyingine katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013.

Kwa upande wa barabara ya Makuburi-Kibangu-Makoka mpaka sasa matengenezo yanasubiri malipo yafanyike ya fidia ya nyumba chache zilizobaki kiasi cha shilingi milioni 64, suala ambalo Manispaa ya Kinondoni inapaswa kulitolea kauli kwa kuwa lilipaswa kukamilika katika mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe 30 Juni 2012, leo nimemuagiza katibu msaidizi wa mbunge kufuatilia suala hilo katika ofisi za Manispaa. Mpaka kufikia tarehe 3 Mei 2012 jumla ya shilingi milioni 122 zilikuwa zimeshalipwa kama fidia, hivyo Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Manispaa ya Kinondoni kuharakisha malipo ili kuepusha gharama za fidia kuongezeka kwa kuzingitia kuwa iwapo malipo yangefanyika kwa wakati mwaka 2010 gharama za fidia zingekuwa milioni 80 tu lakini sasa zimeongezeka mpaka kufikia zaidi ya milioni 180.

Wakati hatua za haraka za serikali zikisubiriwa kuwezesha matengenezo makubwa nitawaeleza karibuni utaratibu kwa kushirikiana na madiwani kwa ajili ya kuunganisha wananchi wa maeneo husika na wadau wengine ili kufanya matengenezo madogo kupunguza kero.

Izingatiwe kuwa tarehe 24 na 25 Agosti 2012 nimekwenda mitaa mbalimbali ya kata 12 kati ya 14 za Jimbo la Ubungo kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye sensa ya watu na makazi na kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya.

Aidha wananchi niliokutana nao wamepata fursa ya kuuliza maswali kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na mrejesho kuhusu mkutano wa nane wa bunge ambapo pamoja na kupata majibu nimepokea pia mapendekezo ya masuala ya kuyapa kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia jimboni katika kipindi cha mwezi Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa bunge na pia kuhusu maandalizi ya mwaka 2013.

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
27/08/2012

Tuesday, August 21, 2012

Taarifa Fupi kuhusu Kazi za Maendeleo Jimboni Ubungo (AMUA)


UTANGULIZI:
Kwa nyakati mbalimbali kumekuwepo na mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu utendaji kazi wangu katika kuwezesha maendeleo Jimboni Ubungo. Mijadala hiyo imeshika kasi jana tarehe 20 Agosti 2012 siku nzima baada ya habari kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la Tanzania Daima “Mnyika kinara bungeni” ambayo imerejea rekodi za bunge na kuniweka katika orodha ya wachangiaji wa mara kwa mara bungeni.

Napokea kwa unyenyekevu pongezi zilizotolewa na wachangiaji mbalimbali lakini izingatiwe kuwa michango yangu bungeni ni matokeo ya heshima mliyonipa ya kuwawakilisha. Aidha yapo maoni machache ambayo yametoa tafsiri tenge kuhusu kazi ya mbunge na wengine mmetaka nieleze nimefanya kazi gani za maendeleo jimboni Ubungo.

Tarehe kama ya leo 21 Agosti 2005 nilianza mchakato wa kuwa kugombea ubunge nikiwa kwenye chakula na watoto yatima, tarehe kama hiyo mwaka 2010 nilianza kampeni za uchaguzi mitaani Ubungo, tarehe hii hii kwa mwaka huu wa 2012 naomba niitumie kutoa taarifa fupi ya utekelezaji kwa masuala ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe 30 Juni 2012; taarifa ya kina ya utekelezaji nitaitoa nitakapotimiza miaka miwili ya utendaji.

AHADI NILIZOTOA WAKATI WA UCHAGUZI WA MWAKA 2010
Kabla ya kueleza kazi nilizofanya katika kutimiza majukumu ya kibunge katika kuwezesha maendeleo jimboni ni muhimu nikawapa rejea ya ahadi nilizotoa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 ili kupata msingi  wa kupima utekelezaji.

Wakati wa kampeni nilitoa ahadi chache na kuelekea mwishoni mwa kampeni niliorodhesha ahadi zote na kuziweka kwenye maandishi ikiwa ni mkataba kati ya mbunge na wananchi wa kutumika kama rejea katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi 2010 mpaka 2015.

Ahadi hizo ziko katika kipeperushi cha AMUA ambacho tulikisambaza kwenye kaya mbalimbali jimboni wakati wa kampeni, ahadi hizo nilizirudia mara baada ya kuchaguliwa na zinapatikana hapa:  http://mnyika.blogspot.com/2010/11/ujumbe-wa-mbunge-shukrani-twende-kazi.html

UTEKELEZAJI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA NA NUSU
Toka kuapishwa mwezi Novemba 2010 mpaka mwezi Juni 2012 ni takribani mwaka mmoja na na miezi tisa  ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo kwa nafasi niliyochaguliwa ya mbunge wa Ubungo; hizi ni baadhi katika orodha ya za maendeleo ambazo nimeshiriki jimboni:

ELIMU:
Akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Katika muktadha huo katika kipindi husika nimesimamia yafuatayo kuwezesha elimu bora:

Mbunge amefuatilia kupitia vikao vya manispaa ya Kinondoni na kupitia ziara jimboni, maswali bungeni ili kuhakikisha ruzuku ya bajeti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, inafika na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya elimu na huduma zingine za muhimu katika Jimbo la Ubungo, katika mwaka 2012/2013 nitafuatilia kwa karibu zaidi kasoro zilizobainika katika mwaka 2011/2012 .

Katika kipindi husika mbunge ameendelea kutetea haki na maslahi ya walimu na wanafunzi wakiwemo wa elimu ya juu wa Jimbo la Ubungo. Aidha, nimeshiriki katika kuwezesha uamuzi wa kuhamisha fedha katika mafungu mengine yasiyokuwa ya lazima kuelekeza katika matengenezo ya madawati kwa shule za msingi na sekondari ambapo zaidi ya madawati 7,000 yamesambazwa katika Jimbo la Ubungo kutoka Manispaa ya Kinondoni, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) na kutoka Sekta Binafsi. Kwa ushirikiano na madiwani tumefuatilia kuhakikisha mgawo wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari katika kata mbalimbali kutoka katika Manispaa ya Kinondoni na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF), orodha ya shule na viwango vya fedha vilivyotumika inaweza kupatikana katika Ofisi ya Mbunge. 

Mbunge amependekeza sehemu ya fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDCF) kutumika kutoa elimu maalum ya kuwawezesha wananchi kujua haki zao, fursa zilizopo na namna ya kujiendeleza,   haswa kwa akina mama, vijana na walemavu. Mfano; haki za mirathi kwa wajane na kukuza vipaji kwa vijana. Hata hivyo, utekelezaji wa kazi hii haukuwezekana kwa kutumia CDCF kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kutokana na utata kuhusu tafsiri ya shughuli za kuchochea maendeleo zinazoweza kutengewa fedha kutoka kwenye mfuko, hivyo shughuli hiyo itazingatiwa kwa ukamilifu kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 baada ya kibali kupatikana.

Ili kuziba pengo nje ya CDCF katika mwaka 2011/2012 kupitia ofisi ya mbunge Ubungo na Asasi ya Maendeleo Ubungo (UDI) tumefanya programu ya “Toa Kitabu Kisomwe” na pia kuunganisha vijana na wanawake na elimu maalum kupitia taasisi zingine.

Mbunge amechangia asilimia 20 (20%) ya mshahara wake kwa mwezi kwenye masuala mbalimbali ya elimu, orodha ya baadhi ya michango kwa shughuli za elimu kwa wanafunzi na walimu wa msingi, sekondari na vyuo inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge (majina ya waliopewa michango yamehifadhiwa kulinda faragha).

Kazi hizi zitapanuliwa zaidi katika mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia Mfuko wa Elimu Ubungo tutakaouzindua karibuni.

AJIRA: 
Katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake kuweza kujiajiri mbunge alifanikiwa kushawishi Manispaa ya Kinondoni kuongeza fedha za mikopo kwa vikundi vya kina mama na vijana ambapo awali zilikuwa zikitengwa milioni 20 tu, na hivyo milioni zaidi ya 200.

Orodha ya vikundi vilivyopatiwa mikopo na mitaji mpaka sasa katika Jimbo la Ubungo inapatikana kwenye Ofisi ya Mbunge. Aidha, mbunge ametetea wafanyabiashara wadogo kuendelea kutengewa maeneo ya biashara na katika mwaka 2011/2012 amewezesha kamati maalum inayohusisha wafanyabiashara na Manispaa kuundwa kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wa Ubungo kupatiwa maeneo katika masoko yaliyotengwa. Katika mwaka 2012/2013 hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo ambao hawajapata maeneo mpaka sasa.

Mbunge amefanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha nguo cha Urafiki ili kuzungumza na wafanyakazi na menejimenti katika kuisimamia serikali kushughulikia matatizo yaliyojitokeza katika kiwanda na kuathiri ajira na ujira bora. Matokeo ya ziara ya mbunge na ufuatiliaji bungeni yamefanya kiwanda hicho kutembelewa pia na kamati ya bunge na mawaziri husika ambapo hatua zimeanza kuchukuliwa, katika mwaka wa fedha 2012/2013. Mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu matatizo yanayoendelea kuhusu ufisadi na uwekezaji katika kiwanda husika.

Aidha, mbunge amefuatilia pia masuala ya ajira katika viwanda vilivyofunguliwa kwenye maeneo ya uwekezaji wa kiuchumi (EPZ/SEZ) yaliyopo katika jimbo la Ubungo ikiwemo kutaka kutengwa kwa maeneo maalum ya wawekezaji wadogo.

Katika kupanua wigo wa ajira mbunge amefuatilia pia kuhusu viwanda vingine vilivyobinafsishwa au kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo la Ubungo mathalani Ubungo Garments;  Ubungo Spinning Mill;  Polysacks Ltd; Tanzania Sewing Thread; Coastal Diaries (Maziwa) na  Kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI); na hatimaye serikali imemjibu kuwa waraka utawasilishwa kwenye baraza la mawaziri ili kurejesha viwanda vilivyodidimizwa kinyume cha masharti ya mikataba. Katika utekelezaji wa hatua hiyo, mbunge amependekeza kuwa miongoni mwa maeneo ya viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa ajili ya wenye viwanda vidogo vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana katika mwaka wa fedha 2012/2013.

Mbunge ameunga mkono jimboni na ndani ya bunge madai ya ujira bora na stahili za wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi kama walimu, madaktari/manesi, polisi, madereva nk. Hata baada ya nyongeza ndogo ya mishahara iliyopatikana kufuatia shinikizo la migomo kutoka vyama vya wafanyakazi, mbunge ataendelea kuungana na wafanyakazi na wabunge wengine katika kutaka kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi na mazingira ya utoaji huduma hususan katika sekta za elimu, afya, usalama na mahakama. Katika ya masuala ambayo aliyapata kipaumbele katika mwaka wa fedha 2011/2012 ni nyongeza ya posho ya lishe (rationing allowance) kwa askari polisi kutoka laki moja mpaka laki moja unusu suala ambalo serikali imelitekeleza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013.

MIUNDO MBINU:
Msimamo wangu katika kipindi chote umekuwa kwamba pamoja kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake iliyotengewa zaidi ya bilioni 240 inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2015 au zaidi. Hivyo ili kupunguza msongamano katika barabara kuu ya Morogoro, pamoja na mbinu zingine mbunge amekuwa mstari wa mbele kutaka barabara za pembezoni zijengwe kwa haraka; hatimaye baada ya ufuatiliaji wa mara kwa mara kupitia ziara jimboni, vikao vya manispaa, vikao vya bodi ya barabara, ziara jimboni, mawasiliano kwa barua na mamlaka husika na kuhoji bungeni Serikali imekubaliana na mapendekezo tuliyowasilisha hivyo maamuzi yamefikiwa kuwa barabara husika zihudumiwe na Serikali kuu (TANROADS) badala ya Manispaa.

Jumla ya shilingi bilioni 10.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zifuatazo:  Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Ubungo Maziwa-External, Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mbunge ataendelea kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi na pia kuboresha usafiri wa maeneo ya pembezoni kwa kuwa baadhi ya barabara hizo zilitengenezwa kwa kiwango cha changarawe kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 lakini zimeharibika tena baada ya mvua zilizonyesha katika jiji la Dar es salaam.

Katika mwaka wa fedha 2011/2012 tumefuatilia madaraja mbalimbali kujengwa ikiwemo Daraja Golani, Msewe, Matosa nk pia kupitia mfuko wa maendeleo ya Jimbo (CDCF) vivuko kwa watembea kwa miguu vimejengwa Makurumla na Msigani; orodha zaidi ya matengenezo ya barabara yaliyofanyika inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge.

Kufuatia ufuatiliaji wa karibu kwa njia mbalimbali hatua imechukuliwa ya kupeleka umeme katika eneo la Goba Matosa (hata hivyo bado kuna malalamiko ya eneo lilirukwa la Mgeni Chongo) ambalo tunaendelea kufuatilia.

Aidha, miradi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ya kupeleka umeme katika miradi ya maji ya King’ongo na Kilungule inaendelea kutekelezwa kwa haraka zaidi. Mbunge amefuatilia mara kwa mara ahadi ya Rais ya kupunguzwa kwa gharama za umeme na hatimaye ahadi imetolewa ya utekelezaji kuanza kuanzia Januari 2013, pia kanuni za Februari 2011 zimetungwa kuhusu kurejeshwa kwa gharama kwa wateja wanaolazimika kuvuta umeme zaidi ya umbali wa kawaida.

Katika mwaka 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kurekebisha kanuni hizo kwa kuwa zina vifungu visivyotekelezeka na kutaka pia gharama za nguzo na nyinginezo ziwekwe kwenye bili ya mteja kama umeme uliolipiwa kabla. Orodha ya maeneo mengine katika Jimbo la Ubungo ambayo ufuatiliaji umefanyika kuhusu kusambaziwa umeme inapatikana katika Ofisi ya Mbunge.

MAJI:
Katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji katika Jimbo la Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi.

Hatua nyingine zote nilizochukua baada ya hapo zilikuwa ni za ufuatiliaji kuwezesha utekelezaji wa haraka. Nikiri kwamba katika hatua za awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji.

Pia, wakati wa hatua hizo nimewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao. Hata hivyo, udhaifu wa kimfumo uliopo ni mkubwa kuliko hatua ambazo zimeweza kuchukuliwa mpaka sasa. Katika mazingira hayo nilianza pia kutaka hatua za DAWASA na tayari nao nimefanya nao ziara ya kikazi kwenye vyanzo vya maji pamoja na matenki ya maji, na kutaka hatua za haraka za ushirikiano kati ya DAWASA na DAWASCO.

Kwa maana ya miradi ya muda mrefu ya mwaka 2013/2014 kumetengwa fedha kuanzia mwaka 2012/2013 zaidi ya bilioni 200 kutokana na fedha za MCC na Mkopo wa India kwa ajili ya upanuzi wa vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa mabomba mengine miradi ambayo itagusa wananchi wa Ubungo. Hata hivyo, hatua hizi za muda mrefu hazileti matumaini bila hatua za haraka ambazo zilipaswa kuchukuliwa katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Katika kuwezesha hatua za haraka kwa mwaka wa fedha 2011/2012 nilifuatilia ratiba ya mgawo wa maji kuweza kutolewa kwa mbunge na kwa ngazi za kata na mitaa na kufuatiliwa ili mgawo uwezeshe kuheshimiwa bila ya upendeleo wa baadhi ya maeneo au hujuma kwa ajili ya kuwezesha biashara haramu ya maji. Ofisi ya mbunge wakati wote imetaka kupatiwa taarifa pale mamlaka husika au ngazi tajwa zinaposhindwa kufuatilia ratiba husika ili kuweza kuingilia kati. Kuanza kuweka miundombinu ya maji katika maeneo yaliyorukwa kwenye awamu ya kwanza ya uwekaji wa mabomba, tayari utekelezaji umeshaanza katika maeneo ya Mbezi na maeneo mengine utafanyika kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2013 kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa na DAWASCO/DAWASA kwa mbunge.

Katika kutekeleza ahadi ya kuhamasisha ujenzi wa visima kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na mtandao wa maji ya bomba kama suluhisho la muda, huku tukifuatilia ufumbuzi wa kudumu katika maeneo hayo, mbunge amefuatilia uchimbaji wa visima uliokuwa umesimama katika maeneo ya Mavurunza/Bonyokwa, Kilungule na King’ongo kwa kwenda maeneo husika, kuziandikia mamlaka zinazohusika na kuhoji kwenye vikao vya manispaa, bungeni na kufanya ziara za ukaguzi wa maendeleo ya miradi.

Uzinduzi kwa miradi ya Mburahati ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 2011 na hatimaye sasa uzinduzi wa maeneo yaliyotajwa utafanyika katika mwaka huu wa 2012 kwa kuratibiwa na DAWASA na Wizara ya Maji.

Aidha, uchimbaji wa visima kama hivyo unaendelea katika maeneo ya Saranga na Malambamawili. Aidha, kupitia miradi ya Manispaa ikiwemo mradi unaofadhiliwa na benki ya dunia mbunge amefuatilia uchimbaji katika maeneo ya Mpiji Magohe, Msakuzi, Makoka na Msumi ambao unasuasua kutokana na udhaifu wa kiutendaji.

Mbunge ameunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba na amewasiliana na DAWASA/DAWASCO kwa ajili ya hatua za kusaidia miradi husika na TANESCO kwa upande wa kuweka transfoma yenye uwezo mkubwa zaidi ili kuwezesha pampu za maji kwenye maeneo husika ziweze kufungwa. Orodha ya maeneo mengine yaliyochimbwa visima vidogo ipo katika Ofisi ya Mbunge.

Mbunge amefanikiwa kufanya suala la maji kuwa moja ya masuala yanayojadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya Manispaa ya Kinondoni hali ambayo haikuwepo kabla. Aidha alipendeza na hatimaye ukafanyika ufuatiliaji wa miradi iliyo chini ya jamii au mamlaka za ngazi ya chini iliyokwama kwa muda mrefu na hivyo kukosesha wananchi maji katika maeneo mbalimbali ambayo hayapewi huduma ya moja kwa moja na DAWASA/DAWASCO. Kati ya miradi hiyo baadhi imefufuliwa kama wa Msewe Golani na mingi inaendelea kusuasua ikiwemo ya kata ya Goba. Mbunge amependekeza kwa DAWASA kwamba maeneo ambayo hayakuwa yakihudumiwa na DAWASCO ikiwemo ya kata ya Goba yachukuliwe moja kwa moja na mamlaka husika kwa kuwa kutokana na ongezeko la watu maeneo hayo hayawezi kuhudumiwa kwa ufanisi na kamati za maji kama ilivyokuwa miaka ya zamani.

Mbunge amefuatilia pia masuala ya bei na ubora wa maji na kuitaka bei ya maji inayotozwa kwenye Viosk inaendana na viwango vilivyopangwa na mamlaka husika (EWURA), kufuatia hatua hizo operesheni zimefanyika katika maeneo ambayo yanatoza maji kinyume na bei iliyotangazwa na DAWASCO imeingia mikataba na waendeshaji wa vioski husika kuhusu bei elekezi. Hata hivyo, changamoto imeendelea kuwa ni usimamizi wa utawala wa sheria katika kuhakikisha bei inayotozwa ni ile inayopaswa kutoswa kwa mujibu wa maagizo ya EWURA. Katika kipindi husika mbunge ametaka pia EWURA itoe bei elekezi kwa upande wa maji katika jiji la Dar es salaam kwa upande wa sekta binafsi ili kudhibiti pia biashara holela ya maji ya kwenye malori. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 EWURA iliahidi kutoa kanuni za kudhibiti biashara husika hatua ambayo mpaka sasa haijachukuliwa, suala ambalo mbunge atalifuatilia katika mwaka wa fedha 2012/2013.

UWAJIBIKAJI:
Mbunge amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha ngazi mbalimbali ili kuchangia katika  kuhakikisha fedha nyingi zinazopatikana kila mwaka zinatumika kuwahudumia wananchi, ikiwemo kwa kutaka kushughulikiwa kwa mapungufu yaliyoanishwa na wakaguzi wa hesabu katika vipindi vilivyopita. Mathalani mbunge amefuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Ukaguzi Maalum (Special Audit) ya Kituo cha Mabasi cha Ubungo uliofanyika mwaka 2009 lakini utekelezaji wa matokeo ulikuwa ukisuasua. Alifanya hivyo kupitia bungeni na katika vikao vya halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na hatimaye baadhi ya mapendekezo yametekelezwa ikiwemo kumwondoa mkandarasi aliyekuwa akikusanya mapato chini ya kiwango; aidha mbunge ataendelea kufuatilia mapendekezo mengine kuhusu mikataba mibovu iliyoingiwa katika kituo husika.

Mbunge amefanya hivyo vile vile kuhusu vitega uchumi vingine vya Jiji la Dar es salaam ikiwemo Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA). Aidha, kwa kushirikiana na madiwani amefuatilia pia miradi hewa au ya chini ya kiwango iliyofanyika katika miundombinu, elimu na maji na hatua mbalimbali zimechukuliwa kama zinavyoelezwa katika Taarifa za Ofisi ya Mbunge.

Mbunge kupitia uwakilishi bungeni na kupitia hatua zingine nje ya bunge amezifuatilia mamlaka za serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi wa Ubungo, mathalani EWURA katika nishati/mafuta, SUMATRA katika usafiri na TANESCO katika umeme.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge atafanya ziara za kikazi pamoja na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali yenye kero ili kuziwezesha kuendelea kuchukua hatua zaidi kuhusu maeneo hayo kwa ajili ya kuchangia katika maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Mbunge amefanya mikutano na wananchi katika kata zote 14 za Jimbo la Ubungo kwenye maeneo mbalimbali ya kiserikali na ya kichama kwa ajili ya kutimiza wajibu wa uwakilishi kabla na baada ya vikao vya bunge.

Aidha mbunge ameshiriki katika mikutano ya wakazi ya masuala ya maendeleo jimboni kama ambavyo imetajwa katika Taarifa ya Utendaji. Mbunge amewezesha ofisi ya mbunge kuwa vitendea kazi pamoja na wasaidizi wawili wakati wote baada ya kukwama kupata vifaa kutoka kwenye mfumo wa kawaida wa kiserikali.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2011/2012 maombi ya mbunge kupata ofisi ya kutumia jimboni kutoka kwenye majengo ya manispaa au ya wilaya yalikataliwa na katika mwaka 2012/2013 mbunge ataweka mkazo katika kufuatilia eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mbunge.

Aidha, mbunge amewajibika katika kuisimamia serikali bungeni na kushiriki katika kutunga sheria. Rejea katika ofisi ya Mbunge kuhusu kazi za mbunge bungeni inaeleza masuala ambayo mbunge ameisimamia serikali bungeni, hatua zilizochukuliwa na serikali kupitia mchango wake na pia sheria ambazo amewasilisha majedwali ya marekebisho katika vifungu mbalimbali vilivyokubaliwa na vilivyokataliwa.

USALAMA:
Mbunge amechangia katika harambee ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Mavurunza ambapo vifaa vya awali vilichangiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) lakini pia fedha taslimu zilichangwa na mbunge kutoka mfuko wake binafsi. Aidha, kupitia CDCF mbunge amechangia pia kwenye ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi Golani Msewe na pia kituo cha Polisi Kata ya Sinza.

Pia, mbunge ameanza ufuatiliaji wa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kimara katika eneo lenye nafasi tofauti na eneo la sasa la barabarani la Mbezi kwa Yusuph; kufuatia ufuatiliaji wa mbunge tayari Wizara ya Mambo ya Ndani imeiandikia barua Manispaa ya Kinondoni kuomba eneo.

Kadhalika, mbunge amefuatilia kuhusu eneo la ujenzi wa kituo cha Polisi kata ya Goba ambapo kwa mujibu wa taarifa toka ngazi ya kata eneo limekwishapatikana. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataweka kipaumbele katika kazi ambazo zilianza kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 ili ziweze kukamilika.

Mbunge ameshirikiana na polisi na viongozi wa kata/mitaa kufanya harambee kuhakikisha doria inakuwepo ili kupunguza vitendo vya wizi, ukabaji na ujambazi hususani kwenye maeneo yenye vitendo vingi vya uhalifu mathalani ya Kimara B kupitia ulinzi shirikishi na polisi jamii.

Aidha, ili kuwe na mfumo endelevu wa kuhudumia vikundi vya ulinzi shirikishi mbunge alipendekeza kwamba masuala ya ulinzi na usalama kuwa sehemu ya vipaumbele vya maendeleo katika mapato ya ndani ya Manispaa kama ilivyo kwa sekta za elimu, afya, barabara nk. Kwa usimamizi wa Meya pendekezo hilo liliingizwa kwenye baraza la madawani na kutakiwa kutekelezwa kupitia fedha zinazobaki katika kata kutokana na ufanisi katika makusanyo ya ndani ili kuimarisha ulinzi na usalama.

AFYA:
Mbunge aliguswa na kasi ya kupungua kwa fedha za wahisani katika bajeti ya afya kwa masuala ya matibabu kwa wanaoishi na UKIMWI/VVU, Wazee, Walemavu na wagonjwa wa kifua kikuu, hivyo pamoja na kuhoji bungeni na kutaka nyongeza ya bajeti kwenye Wizara ya Afya amechukua hatua jimboni kwenye ngazi ya Manispaa kwa kupendekeza kiwango cha fedha toka vyanzo vya ndani kuongezwa hatua ambayo imeanza kuchukuliwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2012/2013.

Kwa ajili ya afya mazingira mbunge alipendekeza kwamba tathmini ifanyike kuhusu mfumo mzima wa uzoaji taka katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla kutokana na kukithiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali. Kufuatia pendekezo hilo Meya alifanya mkutano na wenyeviti wa mitaa na watendaji wengine ambapo maazimio ya hatua mbalimbali yalifikiwa ambayo yameboresha uzoaji taka katika maeneo machache. Hata hivyo, matatizo ya uchafu yameendelea katika maeneo mengi, hivyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kuu na serikali za mitaa katika kuchukua hatua kubwa zaidi kuhusu udhaifu wa kimfumo ambao ulishababainishwa tayari unaochangia kasi ndogo ya uzoaji taka ngumu na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

ARDHI:
Mbunge amefuatilia kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa eneo la Ubungo Maziwa wanapewa fidia stahiki. Aidha, mbunge amefuatilia na hatimaye fidia imeanza kulipwa kwa wananchi eneo la Riverside wanaopaswa kubomolewa kupisha njia mbadala ya kwenda Kibangu.

Hata hivyo, suala la fidia ya ardhi kwa upande wa wananchi wa Kwembe kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu eneo la Mlongazila limekwama kwa Serikali kuchukua msimamo wa kutoa fidia ya maendelezo/mali pekee. Mbunge anaendelea kufuatilia suala hilo katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kushirikiana na wananchi waliofungua kesi mahakamani wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea. Kwa upande mwingine, kiasi cha shilingi bilioni 10 kimeweza kutengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Ubungo walio karibu na mitambo ya umeme ambao walikuwa wanadai fidia toka mwaka 2004.

Mbunge amesisitiza kupitia vikao vya Mkoa, halmashauri ya Jiji, Manispaa na bunge kuhusu haja ya serikali kuweka kipaumbele katika kusimamia mpangilio mzuri wa makazi na kuhamasisha upimaji wa viwanja ili wananchi wapate hati na leseni za makazi kwa urahisi na kwa bei nafuu kutokana na matatizo ya gharama kubwa na ucheleweshaji yaliyoko hivi sasa. Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi amemjibu mbunge kuwa wizara itawekwa mfumo ili hati iwe inatolewa kwa haraka katika muda usiozidi miezi sita. Mbunge amefuatilia mradi wa urasimishaji unaofanywa na Ofisi ya Rais (MKURABITA) katika eneo la Kimara Baruti, aidha mbunge ametaka elimu kutolewa kwa wananchi na madiwani na watendaji wengine kuhusu namna fursa za upimaji na urasimamishaji zinavyoweza kutumiwa katika maeneo yao.

Mbunge amefuatilia vile vile taarifa kuhusu mji wa kiungani (Sattellite town) ya Luguruni na maeneo jirani ya mji huo na kubaini kasoro kama zinavyoelezwa katika Taarifa ya Utendaji, aidha Wizara imeahidi kwamba muendelezaji mwenza wa mji huo amepatikana na kwamba kasoro zinazoendelea zitarekebishwa.

Mbunge amefuatilia kupitia hoja binafsi na maswali katika manispaa na bungeni kuhakikisha viwanja vya umma vilivyouzwa kinyume na taratibu na viwanja vya wazi vilivyovamiwa, vinarejeshwa. Mfano: viwanja vya Makurumla, Sinza, Ubungo, Makuburi, Mbezi nk. Kufuatia hatua hizo, sehemu ya viwanja hivyo imejadiliwa kwenye baraza la madiwani la manispaa ya Kinondoni na pia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ametembelea kata ya Sinza na kuweka mabango kwa ajili ya wahusika kubomoa. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu ili ubomoaji uanze.

HITIMISHO:
Nihitimishe kwa kurejea msimamo wangu kuhusu kazi za mbunge ambao nimekuwa nao miaka mingi kabla ya kuingia kwenye siasa na niliurudia mwanzoni mwaka 2010 wakati natangaza nia ya kugombea Ubunge:
“Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu) katika kuwezesha maendeleo Jimboni kwake na kwa taifa kwa ujumla:

Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.

Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.

Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.

Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”
, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html

Hivyo, ufanisi wa ubunge wangu upimwe kwa kuzingatia msimamo huo ambao niliwaeleza wananchi wakati wa uchaguzi hivyo nilichaguliwa ikifahamika wazi kuwa huo ndio wajibu ambao nitautekeleza katika kipindi cha miaka mitano.

Bado naendelea kuamini kwamba jimbo la Ubungo na taifa kwa ujumla tutapiga hatua ya haraka zaidi ya maendeleo kupitia mabadiliko katika mifumo yetu ya mgawanyo wa rasilimali na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na pia kwa kuweka mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji wa sekta binafsi.

Tuliyoyafanya mpaka sasa ni sehemu tu katika mahitaji makubwa ya maendeleo kutokana na pengo la miaka 50 ukilinganisha na fursa ambazo taifa letu linazo; hata hivyo naamini miaka mitatu iliyobaki itafanya miaka mitano ya kuisimamia Serikali iliyopo madarakani hivi sasa pamoja na udhaifu wote uliokuwepo kuleta tofauti katika maendeleo majimboni. Ni katika muktadha huo wakati mwingine tunazimika kuwakilisha na kuwasilisha matakwa ya wananchi namna hii: http://www.youtube.com/watch?v=ES4OMOD_xME tukiamini kwamba watawala wenye dhamana kwa sasa ya kukusanya kodi watasikiliza na kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya wananchi.

Aidha, baada ya kazi mkutano wa nane wa bunge naomba kutumia fursa mjadala utakaofuatia taarifa hii kupata maoni yenu kuhusu masuala ninayopaswa kuyapa kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia jimboni katika kipindi cha mwezi Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa bunge na pia kuhusu maandalizi ya mwaka 2013. Kero nyingi zinazoendelea kuwepo kwa sasa ni neema iliyojificha (blessing in disguise) ili tuendelee kuunganisha nguvu ya umma kuendeleza wimbi la mabadiliko. 

Narudia tena kuwakumbusha kuwa nguvu ile ile tuliyoitumia kwenye kutafuta kura na kulinda kura ndio naiomba toka kwenu katika hatua hii ya kufanya kazi za kuwezesha maendeleo kwa kutimiza wajibu kila mmoja wetu kwa nafasi yake, kuisimamia serikali na kuunganisha rasilimali za wadau wengine; 

Maslahi ya Umma Kwanza.

Nimeandika taarifa hii leo tarehe 21 Agosti 2012 siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Jimboni-Ubungo





Sunday, August 12, 2012

Kauli ya awali kufuatia madai ya kizushi na kijinga ya CCM kuwa CHADEMA imepewa mabilioni na nchi za nje

Katika mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini. Nitatoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo:


Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu. Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.

CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.

Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.

Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli.

Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.

Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.

CCM ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.

Ikumbukwe kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani.

Itakumbukwa kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua zaidi na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.

Nimeelezwa kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani.

Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.

CCM inatoa madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuichagua CHADEMA.

CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya madini na tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.

Hivyo, badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya mabadiliko ya kweli.

Hivi karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko ya kweli.

CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na badala yake kimejikita katika propaganda chafu.

CHADEMA tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM.

CHADEMA kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa.

CCM imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA. Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi.

Hivi karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu, madaktari na mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.

Mikakati yote hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.

John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

12/08/2012- Dodoma