Sunday, December 30, 2012

Wakazi wa GOBA na KWEMBE: Msikose leo saa nane mikutano juu ya MAJI

Wakazi wa Kata ya GOBA:

Tume ya Haki za Binadamu imetangaza/imenukuliwa kwenye vyombo vya habari leo kuwa imeanza kuchunguza na kuchukua hatua juu ya mashtaka niliyowasilisha kuhusu mgogoro wa toka mwaka 2007 unaokwamisha huduma ya MAJI katika mtaa wa Goba. Kwa upande wa Mtaa wa Kulangwa-Kata ya Goba tenki limeshajengwa, ujenzi wa miundombinu mingine unakaribia kuanza ili wananchi wapate maji kupitia mradi wa Madale Kisauke. Ili kuwa na usimamizi bora kuanzia hatua za awali fikeni leo (Desemba 30, 2012) kuanzia saa nane mchana , Mahali: Shule ya Kulangwa kutoa maoni kuhusu Katiba ya Jumuiya ya watumiaji Maji.

Tume yachunguza kilio cha Maji Goba

Na Katuma Masamba

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini bado inafanyia kazi malalamiko yaliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) anayetaka kujua kiini cha wakazi wa Goba kutokupata maji.

Mnyika aliwasilisha barua yake yenye malalamiko kwenye Tume hiyo ili kujua tatizo linalosababisha kata ya Goba kukosa huduma ya maji tangu mwaka 2007.

Thursday, December 27, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.

Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.

Saturday, December 22, 2012

‘SUMATRA idhibiti nauli Kibamba’

na Betty Kangonga

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetakiwa kudhibiti nauli za daladala zinazofanya safari zake katika barabara ya Morogoro.

Inaelezwa kuwa daladala zinazokwenda Kata ya Kibamba zinatoza sh 650 na zile zinazokwenda Kiluvya zikitoza sh 900.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alisema jana kuwa katika kikao kilichoketi Oktoba 4, mwaka huu alimkumbusha mwakilishi wa Sumatra kushughulikia tatizo hilo, lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.

Wednesday, December 19, 2012

Mnyika ‘atema cheche’ gharama za umeme nchini

MBUNGE wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema John Mnyika, jana aliwaeleza wakazi wa Kijitonyama kwa Ali Maua ‘A’ Jijini Dar es Salaam kuwa nchi iko kwenye hali tete kutokana na kusudio la Serikali la kutaka kupandisha bei ya umeme.

Mnyika aliyasema hayo kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama hicho kwa nia ya kumpongeza Diwani wa Kata hiyo, Juma Uloleulole kufuatia ushindi alioupata wa kurudishiwa nafasi yake ya udiwani na Mahakama Kuu ya Tanzania wiki iliyopita.

Monday, December 10, 2012

ORODHA YA UFISADI NA UZEMBE TANESCO AWAMU YA KWANZA NA MWITO WA KUTOA MAONI KUHUSU KUSUDIO LA KUPANDISHA BEI YA UMEME KWA MARA NYINGINE


Shirika la Umeme (TANESCO) linakabiliwa na ufisadi na uzembe unaoongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa upande mmoja na uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine.  Ufisadi na uzembe huo unapunguza uwezo wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaongeza gharama na bei ya upatikanaji wa umeme hali inayoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kuchangia katika mfumuko wa bei na ongezeko la gharama za maisha. Mzigo wa ufisadi na uzembe katika TANESCO unajitokeza zaidi katika mikataba mibovu pamoja na ukiukwaji wa sheria za ununuzi wa umma, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 sehemu ya pili ya bunge (inayoundwa na wabunge) ndio chombo kikuu chenye madaraka na mamlaka kwa niaba ya wananchi ya kuisimamia serikali. Hata hivyo, katika kipindi cha kati mwaka 2008 mpaka 2012 maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo kuhusu umeme yamekuwa hayatekelezwi kwa wakati na kwa ukamilifu hali inayofanya tuhuma za ufisadi na uzembe kuendelea kujirudiarudia. Katika muktadha huo, ni muhimu kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi ibara ya 8 madaraka na mamlaka ni ya umma (serikali inafanya kazi kwa niaba tu) ipo haja ya kuanza kuunganisha ‘nguvu ya umma’ katika kushinikiza hatua kuchukuliwa kwa wahusika wa ufisadi na uzembe ili kuweka misingi bora ya uwajibikaji katika sekta ya nishati.

Ili umma uweze kuungana kuchukua hatua ni muhimu masuala yote ya ufisadi na uzembe yakaelezwa kwa uwazi kwa umma hivyo, katika mfululizo huu nitaweka hadharani orodha za watuhumiwa wa ufisadi na uzembe katika sekta ya nishati. Orodha hizi zinatolewa kwa awamu zikigusa kwa kuanzia mashirika na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati na Madini na baadaye Wizara yenyewe na hatimaye Serikali kwa ujumla. Aidha, orodha hizi zitatolewa kwa awamu masuala kwa masuala na matukio kwa matukio, ngazi kwa ngazi.

Katika orodha ya awamu ya kwanza nitaanza na TANESCO kuhusu masuala na matukio yaliyohusu kampuni ya M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED pamoja na kampuni ya M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED. Orodha nyingine zitafuata katika awamu ya baadaye iwapo vyombo na mamlaka husika hazitachukua hatua ikiwemo juu ya tuhuma za ufisadi na uzembe katika matumizi ya dola milioni 54 (zaidi ya bilioni 86) katika ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.


Nimetoa majina haya hadharani ili umma uunganishe nguvu kwa njia mbalimbali kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya ufisadi na uzembe ili kuhakikisha nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria na maadili katika utumishi wa umma.

Mamlaka zinazopaswa kuchukua hatua ni pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretariati ya Maadili ya Umma zote kila moja kwa nafasi yake zichunguze ukiukwaji wa sheria katika masuala yaliyo kwenye majukumu yao na kuchukua hatua za ziada kwa kuzingatia pia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo nimeitumia kama rejea kwenye baadhi ya masuala katika orodha hii.

Aidha, kwa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeitisha Mkutano wa Taftishi Juu ya Marekebisho ya Bei ya Umeme za TANESCO ambao inakusudiwa bei ya umeme kupandishwa tena, ni muhimu masuala ya ufisadi na uzembe ndani ya TANESCO yakajadiliwa kwa upana na umma, ili kupinga gharama zinazotokana na hali hiyo zisiingizwe katika mahesabu ya kukokotoa bei.

Ikumbukwe kwamba tarehe 9 Novemba 2011 EWURA ilipokea Ombi la Dharura toka TANESCO na kupandisha bei kwa wastani wa asilimia 155 kuanzia tarehe 1 Januari 2012 na niliunganisha umma kupinga na hatimaye EWURA ikapunguza asilimia hiyo na kuruhusu nyongeza ya wastani wa asilimia 40.29 ambayo ndiyo inayotumika hivi sasa.

Hivyo, nitumie nafasi hii kuhimiza pia umma kujitokeza tarehe 10 Disemba 2012 kuanzia saa 4 asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee Dar es salaam kwenda kutoa maoni kwa kuzingatia Taarifa ya Gharama za Huduma ya Umeme (Cost of Service Study) na zaidi kwa kupinga kuingizwa kwenye bei ya umeme gharama za uzembe na ufisadi ili kupunguza athari katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi miaka 51 baada ya Uhuru.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
09/12/2012

ORODHA YA AWAMU YA KWANZA: JUU YA MASUALA NA MATUKIO YA UFISADI NA UZEMBE YALIYOHUSU MIKATABA YA MAKAMPUNI YA M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED NA M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED.


Masuala na matukio ya ufisadi na uzembe yaliyohusu mikataba ya makampuni ya M/s Santa Clara Supplies Company Ltd na M/s McDonald Live Line Technology Limited ambayo yamefanyika kinyume na sheria mbalimbali.

Kwa ushahidi wa nyaraka baadhi ya sheria zilizokiukwa ni pamoja na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 na sheria nyinginezo. Aidha, masuala na matukio ya ufisadi na uzembe katika mikataba hiyo yamefanyika kinyume na kanuni, miongozo na maadili ya Shirika la Umeme (TANESCO). 

Ufisadi na uzembe umesababishwa na makosa mengine mbalimbali mathalani mgongano wa kimaslahi, utovu wa uaminifu, matumizi mabaya ya ofisi na makosa mengine yaliyo kinyume cha sheria na maadili ya viongozi na watumishi wa umma.

Orodha ya wanaotuhumiwa kuhusika katika ufisadi na/ama uzembe huo 18 ni kama ifuatavyo:

1.   Mhandisi WILLIAM GEOFREY MHANDO

Huyu alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na ndiye mtuhumiwa mkuu wa ufisadi unaohusu mikataba tajwa.

Akiwa mkurugenzi mkuu wa TANESCO aliingia mkataba na kampuni ya SANTA CLARA kwa tenda No PA/001/11/HQ/G/011 kuleta vifaa vya ofisini, kwa kipindi hicho kampuni hiyo tajwa hapo juu ilikuwa inamilikiwa na wanahisa ambao ni familia ya Mhando mwenyewe.

Mkataba huo ulisainiwa na mkewe kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo ya CLARA, kitendo hicho cha mkurugenzi kuipatia kampuni ya mkewe tenda ni kinyume na maadili ya Tanesco kifungu cha 2.2, ni kinyume na Sheria ya Ununuzi ya umma kifungu cha 33, 73(3) na 73 (5) pamoja na sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 6 (d), (e) kutokana na kuwa na mgongano wa maslahi na utovu wa uaminifu.

Aidha kusaini kwa mkataba huo yeye akiwa mkurugenzi wa TANESCO ni matumizi mabaya ya ofisi, kwa kutumia ofisi ya umma kujinufaisha yeye pamoja na familia yake na kushindwa kusimamia sheria zinazoongoza na kusimamia ununuzi wa umma.

Kwa upande mwingine, aliingia katika makubaliano na Donald George Mwakamele (mkurugenzi na mwanahisa katika kampuni ya McDONALD)  makubaliano ambayo hayaruhusiwi na yenye mgogoro ( Conflicting Joint Venture Agrement) kinyume na maadili ya TANESCO na sheria nyingine za nchi nilizozitaja awali.

Lakini pia akijifanya ni mfanya biashara alisaini na makubaliano na kampuni hiyo makubaliano ya pande mbili ya kutafuta tenda, kununua, kujenga, kufanya matengenezo na kufanya miradi yote inayohusika na umeme. Katika kuwezesha hilo Mhando alikuwa na jukumu la kutafuta miradi ya umeme na endapo ikikamilika pande hizi mbili zinagawana mapato na faida inayotokana na miradi hiyo wakati huo huo yeye akiwa mtumishi wa TANESCO.

Pamoja na kufukuzwa kazi, umma unapaswa kuunganisha nguvu kutaka Mhando achunguzwe kwa makosa ya kijinai kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomhusu na kufunguliwa mashtaka ya kukiuka sheria za nchi.

2.   Bw. HARUN MATTAMBO

Huyu ni Afisa ugavi wa shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) amefanya uzembe kwa kushindwa kuhakikisha manunuzi yote yanayofanywa na shirika yanazingatia  taratibu na kutimiza sheria za manunuzi ya umma.

Aliruhusu kufanyika kwa ufisadi na ukiukwaji wa sheria katika kupatikana kwa zabuni na. PA/001/11/HQ/G/011 na kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO).

Alipendekeza kampuni ya M/s Mc Donald ipewe mkataba pamoja na kuwa haikuwa imetimiza masharti ikiwemo kukwepa kuwasilisha mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa ya mwaka 2009 kama sheria ilivyohitaji.

Matokeo ya uzembe wake wa kuruhusu ufisadi ni kulisababishia hasara Shirika la Umeme (TANESCO) kwa kuwa kampuni hiyo ya Mc Donald ilipatikana bila kushindanishwa na makampuni mengine yaliyokuwa na unafuu na yaliyotimiza masharti.

Umma uungane kutaka Matambo afukuzwe kazi mara moja, na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za kufanya uzembe huo kwa lengo la kujinufaisha na kunufaisha washirika wake kwa ajili ya hatua za ziada za kisheria.
     

3.    Bw ROBERT SHEMHILU

Huyu aliwahi kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa TANESCO na anatuhumiwa kufanya uzembe ulioruhusu ufisadi.

Alifanya makosa ya kuruhusu malipo yaliyofanyika tarehe 5 Septemba 2011 kabla hata ya kusainiwa kwa mkataba na kuruhusu kuletwa kwa vifaa kabla hata ya kusainiwa kwa mkataba katika ya TANESCO na kampuni iliyopewa kinyemela zabuni ya kuleta vifaa.

Alifanya pia makosa ya kuilipa kampuni ya Mc Donald malipo ya juu ya asilimia 30 ya thamani ya mkataba wakati vifungu vya 26 na 54.1 vya mkataba huo (pamoja na kuingiwa kinyemela) vilielekeza malipo ya asilimia 15 tu.

Shemhilu pamoja na kusimamishwa  umma uunganishe nguvu kutaka, afukuzwe kazi mara moja na kuchunguzwa kwa ajili ya hatua za ziada.
      
4.   FRANCE MCHALANGE, NAFTARI KISIGA NA SOPHIA MSIDAI

Hawa walifanya uzembe wa kushindwa kusimamia Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na maadili kwa kupendekeza kwamba Kampuni ya SANTA CLARA ipewe zabuni ya kuuzia vifaa TANESCO pamoja na kufahamu kuwa kampuni tajwa ilikuwa haijatimiza masharti na kulikuwa na mgongano wa maslahi.

Umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka sheria ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuwajibika kutoa mapendekezo kwa kuzingatia sheria na maslahi ya umma.

5.   Mhandisi DECLAIN MHAIKI na Bw SUKE

Akiwa mtumishi wa umma alizembea na kukwepa kutoa taarifa  kuhusu kukiukwa kwa vigezo na masharti kuhusu zabuni na. PA/001/09/HQ/W/014 na kufanya kampuni ya McDonald Live Line Technology ipatiwe zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004.

Aidha alichangia kufanya kampuni hiyo kupewa zabuni pamoja na kuwa haikuwa na uwezo wa kifedha na kuiwezesha kupewa malipo ya asilimia ya ziada kinyume na mkataba. Huyu naye umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka sheria na mkataba.

6.   Mhandisi D. MHAIKI, S.NKONDOLA, N.NTIMBA.Mhandisi CHEGERE, MAKIA NA MWITA.

Wote kama timu walifanya maamuzi yaliyosababisha kutolewa kwa mkataba na. PA/001/HQ/W/14 wa tarehe 11 Machi 2010 kwa kampuni ya Ms. Donald Live Line Technology bila kuzingatia uwezo wa kitaalamu, kifedha na masharti mengine na hivyo kukiuka sheria ya ununuzi ya umma na kushindwa kulinda maslahi ya taifa.

Hawa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinadhamu ili kudhibiti maamuzi na mapendekezo ya wataalamu katika utumishi wa umma kuingiza mashirika ya umma na nchi katika mikataba mibovu ili kupanua wigo wa uwajibikaji.

7.   FATUMA CHUNGU, ATHANASIUS NANGALI, ELANGWA MGENI

Kundi hili limehusika katika majadiliano na kutoa mapendekezo yaliyowezesha kampuni ya McDonald kupewa mkataba kinyemela.

Iwapo kundi hili lisingefanya uzembe na kusababisha ukiukwaji wa sheria mchakato wa mkataba huo kati ya mwezi Machi mpaka Mei 2009 ungewezesha TANESCO kuingia mkataba na kampuni yenye uwezo na iliyotimiza masharti na kuepusha shirika hilo kupata hasara na kubeba gharama ambazo zingeweza kuepukika.

Ni muhimu wakachukuliwa hatua za kinadhamu ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa umakini na ueledi ili kuepusha TANESCO kuendelea kufanya majadiliano na kuingia mikataba mingine mibovu yenye kuongeza mzigo wa gharama kwa shirika na hatimaye ongezo la bei kwa wananchi.

8.   LUSEKELO KASSANGA (MKURUGENZI WA FEDHA)

Huyu alibariki ufisadi wa malipo yenye mkanganyiko katika TANESCO kwa kuilipa kampuni ya Santa Clara mapema kabla hata haijafanyiwa tathmini na kupatiwa zabuni.

Malipo yalifanyika kinyemela tarehe 5 Septemba 2011 wakati ambapo tathmini ya zabuni ilifanyika tarehe 23 Septemba 2011, maana yake ni kwamba malipo yalifanywa kabla hata kampuni husika haijapewa kazi kwa mleta vifaa asiye na uwezo na mwenye mgongano wa kimaslahi.

Kassanga anapaswa kufukuzwa kazi na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za ziada za kunufaika kutokana na baadhi ya malipo yaliyofanywa kwa makampuni mbalimbali wakati akiwa mkurugenzi wa fedha ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.

Sunday, December 9, 2012

Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru: Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa


Leo ni kumbukumbu ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), maadhimisho yanayoendelea yamenifanya nikumbuke, waraka niliouandika mwaka 2011 (“Uhuru na Mabadiliko”) wakati wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.

Kwamba “Ili uhuru wetu uweze kuwa wenye matokeo kwenye maisha yetu na ya taifa letu tunahitaji kuungana kufanya mabadiliko ya kweli. Changamoto kubwa ambayo nimeiona ni kwamba kuna udhaifu katika mifumo yetu ya kiserikali kwenye ngazi mbalimbali hali ambayo inakwaza hatua za haraka za kuleta mabadiliko.

Kwa pamoja tunapaswa kuendelea kulitoa taifa letu katika kufilisika kimaadili na kiitikadi na kukubaliana tunu za kitaifa zenye kuwezesha misingi ya uwajibikaji. Uhuru wa kweli wa kisiasa utakuja kwa kuwa na uongozi wenye maono (vision) na maadili (values) na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha kuanzia sasa na kuendelea kutuwezesha kunufaika na rasilimali zetu: iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu au maliasili za nchi yetu.”.


Mara baada ya maadhimisho yanayoendelea katika Uwanja wa Taifa, nitakuwa kwenye mitaa mbalimbali ya kata ya Ubungo kwenye mikutano na wananchi tukitafakari kuhusu nchi yetu na kuhamasisha umma kuunganisha nguvu kuchukua hatua dhidi ya ufisadi na uzembe katika muktadha wa kauli mbinu ya Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru iliyotolewa na Serikali mwaka huu wa 2012 ‘Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa’.

Lengo likiwa kuendelea kuunga mkono vuguvugu la mabadiliko kwa ajili ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Jimbo letu na Taifa letu kwa ujumla.

Nawatakia  upendo, furaha na mafanikio  katika kumbukumbu ya uhuru huku tukiweka mstari wa mbele ukweli, uadilifu, na uwajibikaji katika maisha yetu.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
09/12/2012

Thursday, December 6, 2012

Balozi Sefue na Yambesi watoe kauli iwapo Serikali imetoa waraka wa maagizo kwa watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano ya CCM kinyume cha maadili




Katibu Mkuu Mkuu Kiongozi (Ofisi ya Rais-Ikulu) Balozi Ombeni Sefue na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Yambesi watoe kauli kwa umma iwapo Serikali imetoa waraka mpya kwa watumishi wa umma kuhudhuria mikutano ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa taarifa kama sehemu ya kazi zao kama walivyotakiwa na chama hicho katika tamko lake la tarehe 2 Disemba 2012.

Kwa sasa utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma na. 8 ya mwaka 2002 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2007 pamoja na kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 na kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma za mwaka 2005.

Itakumbukwa kwamba awali utumishi wa umma Tanzania ulikuwa ukiongozwa na Sheria ya Utumishi Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kilimpa mamlaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi kutoa waraka kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa umma.

Chini ya Mamlaka hayo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Martem Y.C. Lumbanga tarehe 26 Juni, 2000 alitoa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma na. 1 wa mwaka 2000 wenye kumb. Na. SHC/C.180/2/113 uliohusu maadili ya Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Waraka huo unawataka watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao wa utumishi bila kufanya upendeleo wala ubaguzi wa chama chochote cha siasa. Waraka huo unawakataza watumishi wa umma kuzungumza na kutoa taarifa kwenye mikutano ya vyama vya siasa na haujatoa ruhusa kwa watumishi hao kuzungumza katika mikutano ya CCM pekee; hivyo Balozi Sefue na Yambesi wanapaswa kutoa kauli kwa umma iwapo Serikali imetoa waraka mwingine kwa siri wenye kuagiza watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano ya CCM.

Izingatiwe kwamba kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma hazielekezi watumishi wa umma kuwa na utii au kuwajibika kwa CCM bali zinaeleza kwamba watumishi wa umma watawajibika kwa umma na watakuwa na utii kwa Serikali na sio chama kinachotawala na zimeweka mipaka ya matumizi sahihi ya taarifa za kiserikali wanazowajibika kuzitoa kwa nafasi zao.

Izingatiwe kuwa mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 kuingia katika mfumo wa vyama vingi na marekebisho ya sheria yaliyofuata yameweka uhuru wa watumishi wa umma katika kujiunga na vyama vya siasa (isipokuwa watumishi wa kada maalum) na mipaka ya mahusiano kati ya kazi zao za kiserikali na shughuli za vyama vya siasa kikiwemo chama kinachotawala.

Hivyo maagizo au waraka wenye kuwalazimisha watumishi wa umma kuhudhuria mikutano ya CCM na kutoa kutoa taarifa ni kinyume cha uhuru wa kikatiba, sheria za nchi, kanuni za utumishi wa umma na misingi ya utawala bora.

Imetolewa na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
05/12/2012

MUHIMU: Rufaa ya kupinga ushindi wa Mnyika Ubungo kesho!


Kesho tarehe 7 Disemba 2012 kuanzia saa 3 asubuhi rufaa ya kupinga ushindi wetu wa Ubunge Jimbo la Ubungo itaanza kusikilizwa na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani. Kama tulivyotafuta kura pamoja, tukapanga mstari kupiga kura pamoja na tukakesha kuzilinda pamoja tujumuike pamoja kujua hatma ya kura zetu.

Kwa maelekezo au maelezo zaidi wasiliana na;
Aziz Himbuka (0784379542 au 0715379542)

Wednesday, December 5, 2012

TAARIFA KWA UMMA: Usafiri wa Treni Jijini Dar es Salaam

Baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuandika tarehe 3 Desemba 2012 kauli yangu kuwa usafiri wa treni katika jiji la Dar es salaam kwamba kwa sasa unaingiza hasara ya wastani wa shilingi milioni 10 kwa siku tano, wanahabari mbalimbali kupitia simu na baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wametaka nitoe ufafanuzi kuhusu madai hayo.

Ieleweke kwamba nilitoa kauli hiyo wakati nikijibu swali la mwananchi kwenye mkutano wa hadhara tarehe 1 Desemba 2012 katika mtaa wa Saranga Jimboni Ubungo ambaye alihoji kuhusu ufanisi wa usafiri wa treni jijini Dar es salaam na hatua nyingine ambazo Serikali inapaswa kuchukua kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es salaam; hivyo katika hotuba yangu nilizungumza masuala mengi na kueleza mapendekezo niliyotoa kwa nyakati mbalimbali ya kuboresha mfumo mzima wa usafiri.

Nilieleza kwamba naunga mkono usafiri wa treni kuwepo jijini Dar es salaam na kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ilikuwa ni moja ya masuala niliyoahidi wananchi kwamba nitayafuatilia, na wakati huo wa kampeni wapo walionipinga ikiwemo kwa kuzungumza katika mikutano yao ya kampeni na hata katika radio.

Tuesday, December 4, 2012

Kuchangia kukuza soka-Mburahati Queens


Mbunge wa jimbo la Ubungo, John Mnyika akikabidhi sehemu ya msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo, Shuka, Godoro na Chandarua pamoja na fedha taslimu kiasi cha sh. laki saba kwa Makamu Mwenyekiti wa timu ya soka ya Wanawake ya Mburahati Queens, Ridhwan Mkasa kwa ajili ya kuisaidi timu hiyo.

Monday, December 3, 2012

Ziara ndani ya Jimbo iliyofanyika Desemba 1, 2012: Kimara na Saranga

Ziara Jimboni: 
Kuzindua maofisi, kutoa mrejesho kuhusu kazi za maendeleo jimboni, kusikiliza hoja mbalimbali na masuala ya kuyawasilisha bungeni toka kwa wananchi na kuhamisha wananchi kwendan kutoa maoni ya katiba mpya. 

Maslahi ya Umma Kwanza!





























Sunday, December 2, 2012

Ufafanuzi kesi ya Dowans

Ufafanuzi kuhusu gharama za uendeshaji kesi ya Dowans. Juzi kwenye harambee ya M4C nilisema kwamba kabla ya kwenda Mwanza nilikuwa nafanya mahesabu ya kiwango cha gharama ambazo TANESCO imetumia na ina mwelekeo wa kutumia kwenye kesi ya Dowans pekee nikasema ni dola zaidi ya milioni 29 (ambayo ni bilioni takribani zaidi ya 40).