Thursday, April 15, 2010

Mnyika: Uhamisho wa watumishi Mwananyamala ni wa kisiasa

Mnyika: Uhamisho wa watumishi Mwananyamala ni wa kisiasa

na Lucy Ngowi

MWENYEKITI wa Mkoa wa Kinondoni, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amesema suala la kuwahamisha watumishi 96 katika Hospitali ya Mwananyamala limefanywa kisiasa zaidi katika kipindi hiki kinachoelekea Uchaguzi Mkuu.

Mnyika alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa analiona suala hilo lipo kisiasa zaidi kwa kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa imechelewa, kwani wananchi na vyama vya siasa wamekuwa wakililalamikia tangu mwaka 2005.

Mnyika ambaye ni Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, alisema upunguzaji huo si suluhisho la kudumu, ila kiutawala ni hatua inayopunguza tatizo kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa Mnyika, hatua ambazo zilipaswa kuchukuliwa ni pamoja na kubadili mfumo mzima wa utoaji huduma katika hospitali za umma kwa kubadili uongozi na kuongeza masilahi ya watumishi wa sekta hiyo.

Mkurugenzi huyo wa vijana alisema kuwa hatua nyingine ni pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi, hususan upatikanaji wa dawa.

“Kuhamisha bila kushughulikia kero za msingi ni sawa na kiini macho. Serikali iweke wazi ripoti za tume na kamati zote zilizoundwa kuchunguza matukio yaliyokuwa yanajitokeza toka wakati huo, pamoja na kueleza gharama zilizotumiwa na tume ama kamati hizo bila mapendekezo kutekelezwa kwa ukamilifu,” alisema.

Mwanzoni mwa wiki hii, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, alisema kuwa, serikali imewahamisha watumishi 96 katika Hospitali ya Mwananyamala ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa kwa uzembe.

Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=14932