Ngawaiya: Nguvu ya Umma ilishinda yote Tarime
Na John Mnyika
Makala ya mtizamo wa Thomas Ngawaiya aliyejitambulisha kama Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (CEGODETA) ya 21 Oktoba, 2008 si ya kupitwa bila kutolewa mtizamo mbadala.
Kwa mtizamo wake, Bwana Ngawaiya amejenga hoja za ‘vioja’ kadhaa: Mosi, amepotosha umma kuwa CHADEMA ilishikilia halmashauri ya Tarime kuanzia mwaka 2005. Pili, amepotosha zaidi umma kuwa viongozi wa CHADEMA wanakataza wananchi wasilipe kodi. Tatu, amedanganya umma kuwa kutokana na kukataza huko, Tarime imekosa maendeleo na kwamba miradi ya shule katika wilaya hiyo imeshindwa kutekelezwa na sasa shule hizo zimekuwa magofu. Nne, ameibua kioja kingine kwa hoja yake kuwa viongozi wa CHADEMA wanasera ya kutaka biashara zipitie njia za panya. Tano, ametoa mtazamo wake kuwa mapigano ya koo Tarime yanaletwa na mababa wa vita(war lords) kwa lengo la kujipatia fedha. Mwisho, ameibua uzushi wa kuhusisha CHADEMA na hoja ya wananchi kuhusu mbolea ya ruzuku tani 6,000 iliyopelekwa msimu uliopita kutowafikia walengwa.
Nitaacha kwa muda mjadala wa viti maalum, niliouchangia kwa wiki kadhaa sasa ili nipate fursa ya kuzijibu hoja hizi za Bwana Ngawaiya. Awali ya yote, ni vyema ikazingatiwa kuwa mwandishi wa mtazamo huu, amewahi kuwa Mbunge na kwa maana nyingine amewahi pia kuwa diwani; hivyo anaelewa utendaji wa halmashauri na pia wa serikali kwa ujumla wake kupitia uwajibikaji ambao unafanyika bungeni.
Hivyo, naamini upotoshaji huo wa hoja sita hapo juu, kama nitavyoeleza ameufanya si kwa kutokujua-bali kwa kudhamiria, kwa lengo la kuendeleza kile ambacho niliwahi kukiita; propaganda chafu!
Huko nyuma, niliwahi kuandika kwamba katika sanaa na sayansi ya siasa na maendeleo, kuna aina tatu za propaganda; propaganda nyeupe, huu ni ukweli ambao mimi hupenda kuuita propaganda safi, ni mfumo wa kusambaza ukweli kwa lengo la kujenga imani na kukubalika. Aina ya pili ni propaganda za kijivu, ambapo mwenezi au msambazaji huchanganya ukweli na uwongo katika sura ambayo kwa uchambuzi wa kawaida si rahisi kujulikana. Aina ya tatu, ni propaganda nyeusi ambayo huhusisha mahubiri ya uwongo. Unaotolewa kishujaa na kwa uwazi, katika hali ambayo, kama mtu haufahamu ukweli basi huweza kuamini uwongo kuwa ukweli na ukweli ukageuzwa kuwa uwongo.
Naandika makala haya, nikiwa nimerejea toka Tarime ambapo nimepata wasaa wa kuzunguka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na kuzungumza na wananchi. Kama ilivyoada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo, iliendeleza zile zile mbinu zake za zamani za kutumia maadui, ujinga, umasikini, maradhi na ufisadi katika kutafuta madaraka kwa nguvu!
Nimeshuhudia, CCM ikijaribu kutumia umasikini wa watanzania kwa kufanya uchaguzi kuwa gulio la kura- kwa kugawa fedha taslimu wazi wazi, kununua kadi za kura, kugawa mavazi ili kutafuta ridhaa ya kuongoza. Nimeshuhudia, CCM ikitumia ujinga, kutafuta madaraka, ikijaribu kumwaga propaganda chafu badala ya sera safi ili kutafuta madaraka. Hakika mkakati huu, ulihusisha makada wa upotoshaji, mmojawao akiwa Bwana Thomas Ngawaiya. Katika mikutano yake, alikuwa akihubiri hizo hoja sita hapo juu, akijaribu kupotosha kila hali mtizamo na hatimaye msimamo wa wananchi wa Tarime. Katika kundi hilo, wapo pia makada wengine ambao kampeni zao hazikuwa na lingine zaidi ya kusingizia, mimi na viongozi wengine katika CHADEMA pamoja na watu wengine wa pembeni- kwamba tumemuua kwa ‘kumchoma na kisu na kumpiga na nyundo kichwani’ hayati Chacha Zakayo Wangwe(Apumzike kwa Amani). Nimeshuhudia, CCM wakijaribu kutumia maradhi ikiwemo kufadhili na kutuma vikundi vya kiharamia vyenye silaha kuwazuru wananchi ili kujenga mazingira ya hofu na vitisho kwa lengo la kupata madaraka. Katika kundi hili, nilishuhudia pia Askari polisi, waliotumwa kufanya operesheni demokrasia wakiwa wa kwanza kuanzisha ghasia ili kupata sababu ya kuwapiga wananchi, kutukamata na wakati huo huo kufanya vitendo vya uwizi na unyang’anyi. Nilishuhudia CCM, ikiwatumia maadui hawa watatu-ujinga, umasikini na maradhi kwa kumtumia vizuri adui namba nne aliyetangazwa na Mwalimu Nyerere-adui ufisadi! Haya ndiyo niliyoyashuhudia Tarime, chama kinachotawala, kikitumia kila aina ya ufisadi, kikifadhiliwa na fedha za mafisadi ili kushinda uchaguzi. Moyoni, nikasema wakishinda hawa, hakuna uadilifu utakaokuwepo zaidi ya kuendeleza ufisadi Tarime, kwa ari, nguvu na kasi mpya. Hivyo, Tarime ilikuwa mpambano kati ya mafisadi na umma.
Katikati ya mazingira hayo hayo ya kukatisha tamaa, nikashuhudia Tumaini Jipya. Nikashiriki katika kampeni ambazo ziliongozwa na maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Nikashuhudia falsafa ya CHADEMA, ya Nguvu ya Umma ikiwa katika maneno na vitendo-katika uhalisia kwenye maisha ya wananchi. Nikashuhudia: uwongo ukikabiliwa kwa ukweli; vitisho vikikutana na msimamo wenye amani. Wananchi wakasimamia haki na maendeleo kwa nguvu ya umma. Hakuna mabomu ya machozi, vipigo, risasi, rumande, mapanga ya maharamia yaliyoweza kuzima dhamira ya kuchagua viongozi wao na nguvu ya umma iliyohamasishwa miongoni mwa wananchi wa Tarime. Hakuna uwongo na propaganda chafu ulioweza kuushinda ukweli; hakika, wapiga kura waliufahamu ukweli na ukweli ukawapa uhuru wa kuchagua viongozi waliowataka. Kuna mengi niliyoyashuhudia Tarime, ambayo pekee yanaweza kuandikiwa mfululizo wa makala kadhaa, hususani hatua kwa hatua yaliyotokea tulipokamatwa na taathira yake katika siku zilizofuatia. Kwa ujumla kampeni zile zilijaa huzuni na furaha, huku vijana wakiwa mstari wa mbele kuandika historia. Vituko vya kampeni zile, navyo vinaweza kujaza kurasa.
Ukweli uliposambaa na kukabiliana na uwongo, hata CCM iliamua kuiga mikakati ya kampeni za kisayansi ikiwemo kutumia helikopta; kile chama kilichokuwa kikibeza matumizi ya helikopta kuwa ni anasa, nacho kikaleta helikopta mbili. Hata hivyo, kwa nguvu ya ukweli, wale wananchi waliokuwa wakibezwa kuwa ni ‘wahuni’ wanaokwenda kwenye mikutano ya Mbowe ‘kushangaa helikopta’ wakawazomea wao na helikopta yao! Helikopta za CCM zikawa karaha badala ya raha.
Bila kujiuliza ni kwanini yote haya yanayokea, CCM ikaendeleza kampeni za kuwatumia makada wake kusambaza propaganda chafu ikiwemo hizo sita hapo juu zilizokuwa zikipigiwa upatu na Bwana Thomas Ngawaiya.
Ukweli katika vichwa vya wananchi ulikuwa ukizijibu hoja hizo sita moja baada ya nyingine, na hukumu ya hoja hizo za uwongo ikiwa ni katika sanduku la kura. Sasa naona wameanza kuhamishia hoja hizo kwenye makala za magazeti ili kuwapotosha watanzania wa maeneo mengine ya nchi.
Wakati Ngawaiya na wenzake wakisema kuwa CHADEMA imeshikilia halmashauri toka mwaka 2005, wananchi walikuwa wakiwapuuza kwa kuwa wanajua ukweli kuwa mwaka 2005 CHADEMA ilishinda Ubunge na udiwani katika maeneo kata kadhaa; halmashauri ilikuwa chini ya CCM. Kwa taarifa ya Bwana Ngawaiya na wenzake, CHADEMA ilipata halmashuri ya Tarime mwaka 2007 baada ya Halmashauri ya awali kugawanywa kuwa mbili za Rorya na Tarime.
Wakati Bwana Ngawaiya na wenzake wasema kwamba viongozi wa CHADEMA wamewakataza wananchi kulipa kodi na hivyo kukwamisha maendeleo, wananchi wa Tarime walikuwa wanawapuuza. Kwa kuwa wanajua ukweli kuwa hakuna kiongozi aliyekataza wananchi wasilipe kodi. Wananchi wanaelewa wazi hoja ya Wabunge wa CHADEMA akiwemo marehemu Chacha Wangwe ilikuwa ni nini. Lakini inasikitisha kwamba Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo na Utawala Bora katika mtizamo wake gazetini anashindwa kabisa kuelewa tofauti kati ya michango na kodi. Kwa taarifa ya Bwana Ngawaiya, hakuna kiongozi wa CHADEMA aliyekataza wananchi wasilipe kodi. Kodi ni lazima, na kukataza mtu kulipa kodi ama kuzuia kodi kukusanywa ni kosa la jinai. Kwa hiyo Bwana Ngawaiya anataka kusema kuwa viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakivunja sheria na serikali ya CCM chini ya Amiri Jeshi Mkuu Rais wa nchi ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho amekuwa akikaa kimya wakati wote? Wananchi wa Tarime wanajua kuwa wanalipa kodi kila wanaponunua bidhaa kama sukari na nyinginezo. Wanajua kabisa kuwa wote wanalipa kodi, tena kodi nyingi sana. Viongozi wa CHADEMA wametoa somo kuhusu kodi mpaka kimeeeleweka. Wafanyakazi Tarime wanajua kuwa wanalipa kodi. Suala la msingi kule, ni je, kodi zetu zinatumikaje, na nini mgawo unaobaki kwenye halmashauri kutokana na kodi hizo ikiwemo kodi zinazolipwa na Makampuni ya madini yaliyopo katika halmashauri hiyo? Je, haziwanufaishi mafisadi na tabaka la matajiri wachache? Na hapo ndipo inapozaliwa hoja ya michango, ambayo pengine ndiyo ambayo Ngawaiya alitaka kuizungumzia. Ni kweli, viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakikataza wananchi kulipa michango, bila kwanza kuelezwa na kuridhika kwamba kodi wanazolipa hazitoshelezi kufanya maendeleo. Na pili, kupewa taarifa za mapato na matumizi ya michango iliyotangulia. Na tatu; wamewakataza wananchi kukataa kulipa michango kama michango hiyo inakusanywa kwa njia ambazo zinavunja haki za binadamu ikiwemo kupora mali za raia. Sasa kwa CCM na makada wake, ambao wamekubali serikali yao ilee ufisadi, itumie kodi za wananchi katika matumizi makubwa ya anasa; somo hili ni mwiba mchungu hususani katika uchaguzi!
Na hapo ndipo wanapozua vioja vingine, kwamba eti kutokana na uamuzi huo Tarime imekosa maendeleo. Ngawaiya na wenzake, wanashindwa kujua kabisa kuwa kwa miaka zaidi ya arobaini toka uhuru wa Tanzania, halmashuri ya Tarime imekuwa chini ya CCM ikikusanya kodi na kutoza michango lukuki bila maendeleo yanayokusudiwa. Wanajua kuwa Halmashauri zilizotangulia kuchukuliwa na CHADEMA kama Karatu zilionyesha njia kwa kufuta michango ya manyanyaso lakini bado zikaweza kuleta maendeleo kwenye sekta za maji, elimu nk. Bahati nzuri, wananchi wa Tarime katika uchaguzi ule, walikuwa na rekodi za kulinganisha. Tuweke pembeni rekodi ya utawala wa giza wa CCM wa zaidi ya miaka 40 toka uhuru, wananchi walikuwa na fursa ya kulinganisha mwaka mmoja na nusu toka CCM ichukue halmashuri hiyo mwaka 2005 na mwaka mmoja toka CHADEMA ikuchukue halmashuri hiyo mwaka 2007. Na tofauti ilikuwa bayana. Wakati CCM kwa muda mrefu ikiwa inapokea mamilioni ya kodi toka kwenye migodi iliyomo kwenye halmashuri hiyo na mamilioni hayo kuishia kutumika kifisadi na mengine kutumika kwenye matumizi ya anasa ya posho za wakubwa katika halmashauri;CHADEMA ilifanya tofauti. Kwa muda mchache wa uongozi wa CHADEMA, Charles Mwera akiwa Mwenyekiti wa Halmashuri; CHADEMA ilipiisha utaratibu wa kwamba katika milioni 260 zinazopatikana toka migodini, milioni 140 zitumike kulipia elimu ya watoto wa Tarime kwa wastani wa milioni saba kwa kila kata. Hii ni sera ya CHADEMA ambayo imeanza kutekelezwa katika kata zote zenye madiwani wa CHADEMA, huko watoto wote waliopata nafasi ya kusoma Tarime wanasomeshwa bure na halmashauri yao. Kwa bahati mbaya, katika kata chache za madiwani wa CCM, wamekataa utaratibu huu na hivyo kukwamisha maendeleo ya vijana na watoto katika kata hizo! Hawa ndio wakina Ngawaiya wanaoamini kwamba ili tuendelee ni lazima wananchi wachangishwe kwa wingi zaidi na ni lazima kwenda kuomba omba nje ya nchi. Huu ndio utawala bora na maendeleo wanayohubiri.
Bwana Ngawaiya inaelekea haielewi hali halisi ya Tarime, inaelekea aliishia kwenye majukwaa ya kisiasa alipokuwa kule na hakupata fursa ya kutembelea shule zilizojengwa Tarime toka mwaka 2005 mpaka sasa ndio maana amezuka na kioja kuwa ‘shule zimetelekezwa na kuwa magofu’! Badala ya kuinyooshea kidole Tarime, ambayo imeonyesha mfano wa kuwa halmashuri pekee nchini ambayo wanafunzi wanasomeshwa bure, azitazame halmashuri zilizo chini ya chama chake CCM katika mkoa huo huo wa Mara. Aende Bunda akaone shule ambazo hazina vyoo, binafsi nafahamu shule sita katika wilaya hiyo ambazo hazina huduma hiyo muhimu kwa mwanadamu. Aende Wilaya ya Mugumu chini ya utawala wa miaka zaidi ya arobaini ya CCM hakuna barabara ya Lami, halafu alinganishe na Tarime iliyochini ya CHADEMA. Halafu apitie mahesabu ya halmashuri hizo kwenye taarifa za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG), aione zilivyojaa hati chafu. Halafu arudi Tarime, akatazame; baada ya miaka mingi ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma yaliyopelekea hati chafu katika wilaya hiyo, wananchi wakaamua kuichagua CHADEMA kuongoza halmashauri. Na katika kipindi kifupi, cha kuwa chini ya CHADEMA, halmashauri ikaongozwa kwa uadilifu na kupata hati safi. Ngawaiya na wenzake wafahamu kuwa rangi nyeupe katika bendera ya CHADEMA haipo kama urembo, ni nembo ya kwamba chama hicho kinasimami uwazi, ukweli na uadilifu katika uongozi wake kwa kupinga aina zote za ufisadi na kutetea rasilimali za taifa.
Katika mtizamo wake Bwana Ngawaiya anasema kwamba viongozi wa CHADEMA wanatetea biashara huria na kutaka biashara zipitie njia za panya. Hapa ndipo sanaa na sayansi ya propaganda majivu inapotumika kupotosha umma. Wananchi wa Tarime na watanzania, wanajua kabisa kuwa ni kweli CHADEMA chini ya itiakadi yake ya mrengo wa kati inaungana mkono soko huria bila kupora mamlaka ya umma katika sekta nyeti. Lakini CHADEMA imetamka bayana katika katiba yake kuwa haiungi mkono soko holela. Na wakati wote, nimekuwa nikisema kwamba serikali ya CCM inayoamini katika ujamaa wa dola kumiliki njia za uzalishaji mali, imerukia sera ya soko huria bila kuwa na misingi ya utekelezaji wake kupitia yale Maamuzi ya Zanzibar yaliyozika Azimio la Arusha. Matokeo yake, wameipeleka nchi katika soko holela! Ieleweke wazi, chini ya mfumo wa chama cha kina Ngawaiya, ambacho kinadhodhi mamlaka ya mambo mengi katika serikali kuu tofauti na mfumo wa majimbo ambao CHADEMA inaupigia upatu, udhaifu katika mipaka ya Tarime unafanywa na serikali ya CCM na si halmashauri ya wilaya ya Tarime iliyoko chini ya CHADEMA. Ikumbukwe kwamba, uhamiaji na askari walioko mipakani, wanapokea maagizo na maelekezo toka serikali kuu ambayo kwa sasa iko chini ya CCM. Matokeo ya mifumo mibovu ya serikali hiyo, ni kufanya mipaka kuwa na njia chache za kiserikali hali inayopelekea wananchi kutengeneza njia nyingine za panya. Serikali ya CCM inashindwa kusimamia mipaka ya nchi, na hata katika njia rasmi kama za Sirari katika wilaya ya Tarime, napo kuna udhaifu mkubwa! Lilipojitokeza suala la uhaba wa mchele nchini Kenya, ambapo wafanyabishara walikuwa wakipitisha na kuuza katika nchi hiyo kwa bei ya juu kupitia njia za panya; serikali ya CCM badala ya kukabiliana na chanzo cha tatizo, ikaanza kukimbizana na matokeo. Ikaamua kuweka kizuizi cha barabarani katika eneo la Kirumi; mpakani mwa wilaya ya Musoma na Tarime. Matokeo yake, ili kudhibiti mchele kwenda Kenya serikali ikaamua kudhibiti mchele kwenda Tarime!. Watanzania wakaanza kunyimwa haki ya kula wali kwa uhuru kwa sababu ya wakenya. Hapo ndipo Marehemu Wangwe, akiwa mbunge anayewakilisha sauti ya tabaka la chini, akaibua suala hilo bungeni. Serikali ya CCM badala ya kushughulika na mzizi wa tatizo, wameendelea na utamaduni wao wa kushughulikia matunda; sasa wamehamishia kizuizi hicho eneo la Rubana, mpakani mwa Bunda na Mwanza.
Bwana Ngawaiya ameenda mbele zaidi kwa kuwaita viongozi wa koo zinazokinzana huko Tarime kuwa ni mababa wa vita(war lords) wanapogiana kutafuta fedha. Ni hoja za kutokujua historia ya migogoro ya koo kama hizo ndizo zilizofanya makada wa CCM wakina Ngawaiya, Makamba na wengineo kunyimwa kura katika maeneo hayo. Bahati nzuri, Mbunge Mteule Charles Mwera, katika ilani yake ya uchaguzi akigombea ubunge mwaka huu, ameeleza bayana asili ya matatizo ya koo hizo kuwa ni migogoro ya ardhi. Na ameweka wazi dhamira yake na ya chama anachotoka ya kuhakikisha kwamba panakuwa na mipaka na upatanisho. Ni muhimu sasa akapewa ushirikiamo na asasi zote za haki za binadamu na za utawala bora kutekeleza azima hiyo.
Bwana Ngawaiya amemalizia mtazamo wake kwa kuibua uzushi wa kuhusisha CHADEMA na hoja ya wananchi kuhusu mbolea ya ruzuku tani 6,000 iliyopelekwa msimu uliopita kutowafikia walengwa. Bila kujijua ameibua kashfa kwa chama chake na serikali yake. Lakini pia, ameibua mjadala mkubwa zaidi kwa kuwa huko Kilimanjaro, kwa miaka kadhaa kati ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitajwa tajwa katika kashfa za ruzuku za wakulima yeye ni mmoja wao. Bahati nzuri, wananchi wa wilaya ya Tarime na watanzania wa maeneo mengi wanafahamu kwamba makala wa kusambaza mbolea hizi wanateuliwa kutoka serikali kuu moja kwa moja. Matokeo ya serikali kuu kuhodhi mamlaka hayo, ni kuwepo kwa tuhuma za ufisadi katika uteuzi wa baadhi ya mawakala ambao wengine wameshindwa kufikisha mbolea hizo kwa wananchi na wengine wamepandisha bei tofauti ya dhamira ya mpango wa mbolea ya ruzuku. Halmashauri za CHADEMA, na wabunge wake, wamekwisha anza harakati za kufichua ufisadi na/ama matumizi mabaya ya madaraka katika eneo hilo mpaka kieleweke! Bwana Ngawaiya ameyasema yote hayo, kujenga hoja kwamba Tarime hawakufanya chaguo bora; hii ni baada ya wananchi wa huko kudhihirisha kuwa ‘sauti ya watu ni sauti ya Mungu’. Nguvu ya umma ilishinda yote Tarime.