Friday, October 23, 2009

Uchaguzi Mitaa: Kampeni mwisho Oktoba 24; Kupiga kura tarehe 25-Mambo Mawili!

Leo tarehe 24 Oktoba ni Siku ya Umoja wa Mataifa lakini pia kwa hapa nchini ni siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Upigaji kura ni tarehe 25 Oktoba, 2009.

Kama nilivyobashiri kwenye mfululizo wa makala zangu kuhusu uchaguzi huu kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu(Makala hizo zinapatikana kwenye blogu http://mnyika.blogspot.com); pamekuwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu za uchaguzi. Uchaguzi si upigaji kura tu na utangazaji wa matokeo; uchaguzi ni mchakato wenye hatua mbalimbali.

Kati ya hatua muhimu za uchaguzi ni pamoja uandikishaji wa wapiga kura; uteuzi wa wagombea; kampeni; elimu ya uraia; upigaji kura na utangazaji wa matokeo- lakini roho ya uchaguzi ni hatua ya ‘usimamizi wa uchaguzi’. Hatua hii huanza mwanzo mpaka mwisho wa uchaguzi. Usimamizi wa uchaguzi ndio kimsingi huamua kama uchaguzi utakuwa huru na haki ama ni uchafuzi tu wa demokrasia na maendeleo.

Nimesikiliza kauli za hivi karibuni za viongozi waandamizi wa CCM na serikali yake; kauli ambazo ni bezo kwa utawala bora.

Alianza Rais Kikwete kwa kusemwa kwamba anatoa mwito kwa wote watakaoshindwa kukubali matokeo badala ya kwenda mahakamani kwa kuwa uchaguzi unaigharimu serikali. Kikwete anayesema hayo akijua kabisa jinsi Wizara ya TAMISEMI(Chini ya Waziri Mkuu Pinda, na Waziri wa Nchi Kombani) imeacha mwanya wa hujuma kwa wagombea kwa kuwatumia watendaji wa kiserikali kama nilivyowahi kubashiri. Kabla kauli ya Kikwete haijakauka, ndani ya Kata yake mwenyewe ya Lugoba; ufa uliotokana na kura za maoni za chama chake, ulisababisha wanavitongoji na vijiji kuhakama CCM kwa wingi na wananchi kuamua kuunga mkono CHADEMA. Kuona hivyo, watendaji wakaamua kuwaengua wagombea waliopitia CHADEMA kwa sababu zisizo na msingi. Wapo walioenguliwa kwa maelezo kuwa hawana kipato kinachowawezesha kuishi; wakulima wa kawaida wanaojulikana kijijini; wengine wakiwa ni wafanyabiashara pale Lugoba miaka nenda miaka rudi. Mmoja baada ya kuleta leseni na risiti za michango ambayo amekuwa akitoa kutokana na biashara yake, bado akaenguliwa kwa kigezo kwamba hana TIN namba! Mgombea wa Uenyekiti wa Kijiji cha Lugoba yeye akaenguliwa kwa maelezo kwamba amedhaminiwa na ngazi ya kata ya chama; jambo ambalo kwa miaka nenda rudi halikuwa na utata miaka nenda miaka rudi kwani kanuni zinaeleza tu kuwa kinachotakiwa ni mgombea kudhaminiwa na chama; kuhusu ngazi gani ni uamuzi wa chama chenyewe. Ya Lugoba ni mfano tu wa jinsi wagombea walivyoenguliwa kwa maelfu katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani vijijini. Lakini hata hapa DSM katika uso wa Kikwete mambo hayo hayo yamefanyika; mfano Mgombea wa Uenyekiti hapa Sinza D ameendolewa kwa maelezo kwamba amedhaminiwa na Kata; wakati wagombea wengine wote wameachwa na kimsingi jimbo zima la Ubungo wagombea wamedhaminiwa na kata katika mitaa mbalimbali. Huyu ameondolewa kwa sababu tu Diwani wa Sinza-Mwaking’inda akishirikiana na Meya Londa; swahiba wake mkubwa katika tuhuma zote za Halmashauri ya Kinondoni; wameweza kufanya shinikizo. Ikumbukwe Kamati ya Rufaa ina wajumbe wawili tu wenye kura; mwenyekiti akiwa na Afisa Tawala, katibu wake akiwa ni Afisa ndani ya ofisi yake. Maamuzi hayo, mgombea wetu amepatiwa jana mchana; huku tayari alishaanza kampeni toka tarehe 18 Oktoba. Kamati ya Rufaa ilipaswa kufanya kazi yake mpaka tarehe 18 Oktoba na kutoa taarifa kwa wahusika; lakini kwa kuwa Ofisi ya Afisa Tawala; chini ya Bwana M. Mkapa; inafanya kazi kwa shinikizo, ndio maana haya yanatokea!.

Baadaye Waziri Mkuu Pinda akajitokeza akisikitika kwamba watu wengi hawajajitokeza kujiandikisha na akaja na hoja kuwa sasa serikali inafikiria kuunganisha uchaguzi huu na wa madiwani ili kuongeza mvuto. Watu wakaona Pinda amekuja na wazo jipya, kumbe ukweli ni kuwa hii imekuwa ni hoja ambayo wadau wamekuwa wakiitaja na kutaka serikali ibadili sheria toka mwaka 2004. Lakini Pinda alisahau kuwa kitendo cha ofisi yake kuhodhi mamlaka ya kutoa elimu ya Uraia na mpiga kura kwenye uchaguzi huu kimepunguza nguvu ya wadau wengine kufanya hivyo. Mathalani hapa Kinondoni, ziara zangu za mikutano ya hadhara zilizuiwa na Kamanda wa Polisi kwa maelekezo kwamba vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya mikutano ya aina hiyo. Pinda anajua ni ofisi yake ndiyo iliyokiuka kanuni kuhusu uandikishaji; tarehe 25 Julai ilichapa magazeti ratiba sahihi kuwa uandikishaji ungefanyika tarehe 4 mpaka 24 Septemba; hii ingekuwa kwa siku 21, na mchakato ungekamilika siku 21 kabla ya uchaguzi. Lakini baadaye pamoja na kuwa kanuni zinataka ratiba itolewa siku 90 kabla ya uchaguzi; Ofisi yake ikatoa ratiba nyingine mwezi Septemba kuwa uandikishaji ufanyike tarehe 4 mpaka 10 Oktoba; kwa siku 7 tu; na hivyo umekamilika chini ya siku 21 kama kanuni inavyotaka. Lakini anajua kuwa kwa kufanya hivyo, ofisi yake imechanganganya ratiba hiyo na uboreshaji wa Daftari la Kudumu(DKWK) ambao unaendelea. Kwa mfano katika Jimbo lake yeye mwenyewe la Mpanda Kati; kabla ya kuanza kuandikishwa daftari la mitaa; lilianza la Kudumu; hivyo wananchi wengi walijua kwamba wameshajiandisha tayari hawawajibiki kujiandikisha tena.


Kama Kikwete alijua, kauli yake ikafuatiwa na ile ya Makamba ya kutangaza kwamba CCM imepita bila kupingwa. Siku Makamba anatoa kauli hii alikuwa anajua kabisa kule nyumbani kwake Tanga; watendaji walichelewesha fomu na kujifisha ili wagombea wa upinzani wasipate; na pia mamia ya wagombea waliofanikiwa kuchukua fomu baada ya nguvu kubwa wakaenguliwa na watendaji kwa sababu zisizo na uzito wowote; jamii ya hizo hapo juu.

Hata hivyo, ndondondo si chururu; pamoja na hujuma zote hizo, bado idadi ya wagombea wa upinzani imeongezeka hali inayoashiria kupanuka kwa upinzani na vuguvugu la mabadiliko. Makamba anasema CCM imepita bila kupingwa vijiji takribani elfu 3; hii ni dalili njema kwani kwa tafsiri yake ni kwamba zaidi ya vijiji elfu 10 kuna wagombea wa upinzani; kwa upande wa vitongiji anasema elfu 20 wamepita bila kupinga; hii tafsiri yake ni kwamba zaidi ya vitongoji elfu 80; CCM imepata wapinzani. Hili ni ongezeko ukilinganisha na mwaka 2004; ambapo CCM ilipita bila kupingwa vitongoji vingi zaidi na hatimaye ikashinda kwa ujumla kwa asilimia 96 huku vyama vya upinzani vikigawana asilimia 4; hali ya mambo inaonyesha kuwa pamoja na hujuma zote matokeo ya 2009 yatakuwa tofauti sana na yaliyopita. Yapo maeneo ambayo CHADEMA kwa mfano haikuwa na mtandao mpana wa kichama mwaka 2004 lakini sasa imepanuka kuanzia ngazi ya chini; mathalani Jimbo la Ubungo mwaka 2004, CHADEMA ilikuwa na Mgombea 1 tu wa uenyekiti wa Mtaa; Sasa inawagombea kwenye Mitaa 54; wataalamu wa hesabu wanaweza kukukotoa ni ongezeko la Asilimia ngapi, hii ni ishara njema tunapoelekea uchaguzi wa mwaka 2010.

Hata hivyo, tunapoelekea uchaguzi wa kesho Oktoba 25; kuna mambo mawili lazima yatolewe ufafanuzi kwa umma haraka; mambo haya niliwaeleza TAMISEMI ana kwa ana tarehe 8 Oktoba, wakaahidi kuyafanyia ngazi; ukimya wao unaacha maswali mengi. Hata yanahusu mchakato wa upigaji kura hiyo kesho.

Mosi, TAMISEMI haikuwa imepanga utaratibu wa kuwa na wino usiofutika kama ilivyo kawaida; matokeo yake ni kwamba mianya ya watu kupiga kura zaidi ya mara moja imeachwa wazi. Walijieleza kwamba muda hautoshi kwa mujibu wa sheria ya ununuzi kuagiza wino toka nje ya nchi; niliwaeleza njia mbadala ni kutumia wino hata wa ndani. Kama wameweza kuwa na masanduku ya kura ya kawaida na karatasi za kura za kawaida; kwa nini kila halmashauri isipewe maelekezo ya kutafuta wino wake kama zilivyopewa mamlaka ya kutengeneza makaratasi ya kura?

Pili; uchaguzi wa mwaka huu karatasi za kura hazitakuwa na picha za wagombea, wala majina yao wala ya vyama vyao; Mpiga kura atapewa kura iliyowazi ataandika mwenyewe majina ya anaowachagua. Kwa miezi wadau mbalimbali tumekuwa tukihimiza umuhimu wa kuwa na majina na nembo katika karatasi lakini msimamo wa serikali umekuwa ni kukataa kwa sababu mbalimbali. Lakini hivi karibuni, niliwapa pendekezo mbadala ya kwamba majina ya wagombea yasibandikwe nje pekee kama kanuni zinavyoelekeza bali Ofisi ya Waziri Mkuu itoe maelekezo kwa wasimamizi wote majina yabandikwe pia ndani karibu na eneo ambalo mpiga kura atasimama kuandika majina yake.

Haiingii akilini kwa uchaguzi ambao; kwa upande wa mijini ambapo nafasi zinazogombewa ni saba; Mwenyekiti wa Mtaa na Serikali yake yenye wajumbe Sita; eti mpiga kura aingie ndani akiwa amekumbuka majina kamili ya wagombea wote akayaandike mwenyewe kwa ukamilifu wake; na kwamba makosa yanafanya kura inakuwa imeharibika.

Kichekecho zaidi ni vijiji ambapo pamoja na Mwenyekiti, Halmashauri za Vijiji huwa na wajumbe kati ya 15 mpaka hata 25; Je, unaweza kukariri majina kamili ya watu wote hao halafu akapewa karatasi tu ndani ukayaandike? Mfumo huu wa kura; unafanyika katika nchi ambayo asilimia kubwa ya wananchi hawajui kusoma na kuandika!

Hivyo ndiyo vituko vya uchaguzi huu; na kwa kweli matokeo ya uchaguzi hayawezi kuwa kiashiria kamili cha matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambayo mfumo na utaratibu wake ni tofauti kabisa. Tufuatilie tuone!

Tuesday, October 20, 2009

Maandamano

Oktoba 14, niliongoza maandamano ya kumbukumbu ya Nyerere. Wapo waliunga mkono, wapo waliokosoa. Kwa wakosoaji, hoja mbili kubwa ziliibuliwa; mosi, kwa viongozi wa CHADEMA kumuenzi Mwalimu, na kwamba kumuenzi huko ni utamaduni ule ule wa kusifu na kuabudu viongozi. Ulikuwepo pia mtazamo kwamba kumuenzi kwa maandamano badala ya kufanya shughuli nyingine ni kupoteza muda. Katika kundi hilo, wapo waliopendekeza kwamba tulipaswa kumuenzi kwa njia nyingine mathalani kusafisha mazingira nk!.
Tuliamua kufanya 'maandamano'(sio matembezi) kufikisha ujumbe mahususi wa mabadiliko. Kati ya mambo ambayo tulikuwa na ubishani na polisi ni kuomba kibali cha maandamano badala ya matembezi. Nashukuru kwamba polisi walitupa kibali, hata hivyo, nilieleza masikitiko yangu kuwa baada ya kutoa kibali na taarifa kuanza kusambaa; polisi hao hao wakaaandika barua nyingine ya kufuta kibali. Maelezo ya kikao nao ni kwamba maandamano yangepunguza 'attention' kwa hotuba ya rais Butiama, na pia ya kwamba siku ya Nyerere ni ya maombolezo ya kifo; hivyo si vyema kufanya maandamano. Tulikuwa na mjadala wa zaidi ya masaa kadhaa mpaka usiku. Nampongeza kamanda wa polisi mkoa, kwa kuwa hatimaye baadaye aliacha kutupatia barua ya kufuta maandamano. Nashukuru kwamba alitambua kwamba uamuzi wa kufuta maandamano yale ulikuwa kinyume cha katiba, na hakukuwa na sheria yoyote ambayo ilimpa mamlaka hayo(sheria inazungumza sababu za kiusalama).
Tulifanya maandamano kwa lengo la kufikisha ujumbe, kwamba Nyerere anaenziwa kinafiki na watawala, na chama chao. Njia za kupitia maandamano hayo tulizipanga kwa sababu maalumu; maandamano hayo yalianzia Uwanja wa Tanganyika packers; pembeni ya magofu ya kiwanda ambao kilibeba maadhui ya sera za mwalimu za kuweka kipaumbele uzalishaji wa ndani. Magofu ya kiwanda kile, ni ishara ya sera mbovu za CCM ya sasa, za kutanguliza ubinafsi kwa kisingizio cha ubinafsishaji kuuza viwanda kwa bei chee. Na kugeuza nchi kuwa soko holela!.Tulipotoka hapo, tulipita Msasani/Mikocheni kwa Mwalimu, pale tulisimama kwa dakika moja kumkumbuka; pembeni yetu kikiwepo kiwanja cha wazi ambacho bila nguvu ya umma, tayari kilishatekwa kinyemela karibu kabisa na macho ya Nyerere!Tukaelekea mpaka Kinondoni; tukipita katika maeneo yanayowakilisha kuongezeka kwa pengo baina ya matajiri na masikini katika nchi yetu. Tukapita makao makuu ya chama, ilikuwa Dr Slaa atusalimu, lakini baada ya kuwa ameshasikia hotuba ya Kikwete na namna ambavyo aligeuza maadhimisho ya Nyerere ya kitaifa kuwa ya CCM, Dr Slaa akaamua kujiunga nasi kuendelea na maandamano ili kutoa ujumbe maalum.Tukafika ofisi ya Mkoa wa kichama wa Kinondoni ya CHADEMA, pale Dr Slaa akahutubia(Mwenye audio ya Hotuba yake atuwekee maana alisema maneno mazito sana kuhusu polisi, Kikwete na mwelekeo wa taifa)
Kwa sababu mbalimbali, tulikatishia maandamano hapo; lakini itakumbukwa kwamba kwa mujibu wa ratiba niliyoisambaza awali; maandamano yalikuwa yaendelee kupitia Magomeni, Mburahati, Makurumla, Manzese mpaka Ubungo.Pale Magomeni, ilikuwa tusimame kwenye nyumba ya kwanza kabisa aliyoishi Mwalimu ambayo alipangishiwa na wazee wa Dar es es salaam wakati wa harakati za kudai uhuru. Ilikuwa tuwe na ujumbe maalumu pale, kuhusu mchango wa wazee wa Magomeni, Kinondoni na DSM kwa ujumla katika harakati za kudai uhuru. Na wajibu wao wakati huu katika kuleta mabadiliko baada ya misingi ya taifa hili kutikiswa na maadili kutekelezwa. Hata nyumba hii ambayo imebeba kumbukumbu ya historia kwa bahati mbaya nayo imeshavunjwa.
Pale Urafiki, ilikuwa tusimame tena katika kukumbuka mchango wa Mwalimu; katika kujenga viwanda vyenye muunganiko wa mbele na nyuma(foward and backward) na sekta zetu za kiuchumi. Kiwanda cha nguo cha urafiki, sasa uzalishaji umepungua, mitambo mingine imeuzwa kama vyuma chakavu, nyumba za wafanyakazi zimeuzwa kinyemela; wafanyakazi wanateseka kwa maslahi duni; maghorofa yale yanakodishwa kwa watu tofauti kibiashara badala ya makusudio ya awali. Ilikuwa tusimame kituo cha mabasi Ubungo, pale ilikuwa tuweke bayana ufisadi wa pale na ukikukwaji wa sheria katika zabuni. CAG tayari alishakamilisha ripoti ya ukaguzi mpaka leo Waziri Mkuu Pinda ameikalia. Lakini nilidokeza nikiwa pale Kinondoni, UBT ni mfano wa namna ambavyo makada wa CCM wanaojigamba kumuenzi Mwalimu walivyomsaliti; mradi ule uko chini ya familia ya Kingunge Ngombare Mwiru; mwenye kujiita mjamaa, kumbe ni kiwakilishi cha tamaa za viongozi hao. Matokeo ya Maamuzi ya Zanzibar yaliyofukia miiko ya uongozi.
Ilikuwa tutoke pale, tusonge mbele tukipita makao makuu ya msururu wa Majenereta ya umeme kuanzia Songas, Dowans nk; jirani kabisa na Makao Makuu ya TANESCO. Kiwakilishi cha CCM ya leo, wakati wa mwalimu aliona mbali na kuwekeza katika miradi ya muda mrefu ya nishati; CCM ya leo, inaendesha nchi kwa dharura; lakini pia njia ile ni ishara ya namna wananchi wanavyonywa katika sekta ya nishati ya umeme kupitia mikataba ya kifisadi kwa barakoa ya capacity charges nk. Pale ilkuwa turudie tena mwito wetu wa miaka kadhaa nyuma, wa kutaka mitambo ile ya Dowans itaifishwe; wakati huo huo taifa lichague uongozi na sera mbadala zitakazosimamia uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya nishati wa taifa letu.
Naandika ujumbe huu leo; kwa sababu bado naamani, maandamano yale yanapaswa kuendelea; kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere haipaswi kuwa ya siku moja, ni suala endelevu kwa vitendo. Naandika ujumbe huu kuuliza kama kuna ambao wako tayari kuunga mkono maandamano haya ya safari ya pili kufikisha ujumbe huu.
Naandika ujumbe huu mgao wa umeme ukiwa unaendelea; naandika ujumbe huu ikiwa Zitto na viongozi wengine wamerudia tena mwito wa kutaka mitambo ile itaifishwe. Naandika ujumbe huu nikijua kwamba tunahitaji masuluhisho ya muda mfupi ya dharura, lakini pia tunahitaji kufikiria masuluhisho ya muda mrefu. Kuna ambaye yupo tayari kuandamana? Iwe kwa yeye mwenyewe au kuwezesha watanzania wengine kuandamana? Tafadhali tuwasiliane kupitia 0784222222 au mnyika@yahoo.com.
Tunaweza tukatoa matamko kwenye vyombo vya habari, tunaweza tukajenga hoja bungeni, tunaweza tujadili kwenye makongamano. lakini tukumbuke pia, tunawajibu wa kuunganisha nguvu ya umma. Maandamano ni njia mojawapo ya kufikia azma hiyo. Iwe ni maandamano ya kulaani ama kutoa ujumbe mbadala. Iwe ni kuonyesha hasira ya kutopata tunachostahili kupata ama ni kushinikiza kupata tunachopaswa kupata. Tukubali kuwa mawakala wa mabadiliko tunayotarajia kuyaona. Pamoja tunaweza!

Thursday, October 15, 2009

Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-2

Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-2

Na John Mnyika

Septemba 2009

Katika makala iliyopita nilianza kutafakari iwapo masuala kwenye makubaliano ya wadau yameingizwa katika kanuni na taratibu zilizotolewa na Waziri Mkuu Pinda kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 304 ya tarehe 21 Agosti 2009. Makala hii inaendeleza mjadala wa wadau kuhakikisha kwamba marekebisho ya msingi walau yanayogusa mambo ambayo serikali ilishakubaliana na vyama vya siasa na asasi za kiraia yanafanyika kabla ya uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa ambao umetangazwa kufanyika tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka 2009.

Izingatiwe kuwa chini ya sheria zetu, kanuni za chaguzi hizo hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI). Na kwa mujibu wa muundo wa sasa wa utawala wa Tanzania pamoja na kuwa na waziri wa nchi anayehusika na TAMISEMI, mwisho wa siku mwenye dhamana kamili ya “Wizara” hii ni Waziri Mkuu, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Mizengo Pinda.

Waziri Mkuu Pinda amepindisha kanuni na taratibu kuhusiana na uandikishaji wa Orodha ya wapiga kura. Kwa mujibu wa Kanuni, Waziri Mkuu alipaswa kutoa tangazo kwa umma kupitia magazeti yanayosambazwa nchi nzima ya kiingereza na Kiswahili si chini ya siku tisini kabla ya uchaguzi ili umma uweze kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi. Kama sehemu ya kutekeleza kifungu hicho cha kanuni, Waziri Mkuu Pinda alitangaza ratiba ya uchaguzi na shughuli zinazohusika kupitia Tangazo ambalo alilichapa katika baadhi ya magazeti Julai 25 mwaka 2009. Katika tangazo hilo pamoja na mambo mengine ratiba ya uchaguzi ilieleza kuwa uandikishaji wa wapiga kura ungefanyika kwa jumla ya siku 21 kuanzia tarehe 4 mpaka 24 Septemba, 2009.

Hata hivyo, takribani mwezi mmoja baadaye Waziri Mkuu Pinda akaamua kupindisha Kanuni na Taratibu kwa kutoa maelekezo ya uchaguzi yenye kuelekeza kuwa uandikishaji utafanyika tarehe 4 mpaka 10 mwezi Oktoba. Ikifuatiwa na uhakiki na hatimaye Orodha ya mwisho ya wapiga kura imepangwa kubandikwa kati ya tarehe 23 na 25 Oktoba 2009. Tafsiri ya maamuzi haya ni kwamba siku za uandikishaji wa wapiga kura, zimepunguzwa kutoka ishirini na moja(21) mpaka siku saba(7) tu; na pia orodha haitaandaliwa siku ishirini na moja(21) kabla ya uchaguzi kama makubaliano ya wadau na kanuni zinavyohitaji. Hiki ni chanzo kingine cha vurugu, kwani wasimamizi wamepewa mamlaka ya kuendelea kubandika orodha za wapiga kura mpaka siku yenyewe ya uchaguzi!. Suala hili ni nyeti kwa uzoefu katika chaguzi mbalimbali unakumbusha kuwa orodha ya wapiga kura ni moja ya zana inayotumika kuhujumu uchaguzi ama kwa kufanya wapiga kura wa upinzani majina yao yasionekane kwenye orodha za nje ya vituo au kwa kupenyeza wapiga kura wa nyongeza.

Waziri Mkuu Pinda pia amepindisha makubaliano ya wadau kwa kutoa kanuni zinazoeleza kwamba Kamati ya Rufaa itakuwa na wajumbe watatu, kati yao mmoja hatakuwa kura. Hii ni sawa na kuwa na kamati ya watu wawili, ambayo maamuzi ya kutumia kura ambao kura zitakuwa zinagongana na hakuna kifungu kinachompa yoyote kura ya turufu. Kanuni na maelekezo havitoi fursa kwa vyama kuweza kufahamishwa majina ya wajumbe wa kamati ya rufaa na kuwaweka pingamizi kama itahitajika. Marekebisho ya haraka yanastahili kufanyika kuongeza idadi ya wajumbe wa kamati ya rufaa lakini pia kutoa ratiba yenye kutoa fursa kwa vyama kuweza kufahamishwa kwa majina wajumbe wa Kamati ya rufaa na kuwawekea pingamizi kama vyama vitahitaji.

Kwa upande mwingine, yapo maeneo ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu imekiri mnamo 11 Septemba 2009 kupitia barua yenye kumbukumbu Na. HB.114/126/01 kwamba maelekezo ambayo imeyatoa yamepindisha kanuni. Mathalani, Wakati Kanuni zinasema kwamba siku ya kura watu wawe mita 300 kutoka kituo cha kupiga kura, maelekezo yanasema mita 200. Kwa upande mwingine, unaweza kujiuliza dhamira ya Waziri Mkuu Pinda na jopo lake wakati wanapanga umbali mrefu kiasi hicho hasa ikizingatiwa kuwa katika uchaguzi mkuu umbali kwa mujibu wa sheria ni mita 100 tu!. Pengine uzoefu wa chaguzi ndogo za Tarime, Busanda, Biharamulo na kwingineko umeisukuma serikali kutaka watu wasiosogee kabisa karibu na vituo baada ya kupiga kura; hali ambayo inaacha maswali mengi kuhusu dhamira ya serikali ya kuzuia watu kushuhudia kinachoendelea kama sehemu ya uwazi wa mchakato wa uchaguzi. Uamuzi wa Waziri Mkuu Pinda kuweka umbali mrefu kiasi hicho unaweza kuzua mivutano baina ya raia na vyombo vya dola kwa kuwa uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa unafanyika kwenye ngazi ya chini sana na vituo vya kura viko karibu na makazi ya wananchi; swali la kujiuliza, ni je wananchi itabidi waondolewe umbali huo wa mita 300 ili wasije wakakamatwa kwa kukiuka kanuni, na je watakubali bila kuwa na hisia kwamba wanaondolewa ili wakae mbali kuruhusu mianya ya hujuma za kiuchaguzi?

Hata hivyo, kifungu husika pia kina utata kwa kuwa hakitamki kuhusu ‘kusimama’ kama ilivyo katika sheria ya uchaguzi inayohusu uchaguzi mkuu, bali kinazungumzia kukataza kuvaa sare au kuonyesha ishara za chama ndani ya umbali huo. Hivyo, ufafanuzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliotolewa kwa barua yake ya Septemba 11, 2009 kuhusu suala hilo ni batili kwa kuwa unarejea maelekezo ambayo kanuni hazijayatoa. Kama tutasoma na kuzifuata kanuni mstari kwa mstari basi ukweli ni kuwa wananchi hawajakatazwa kusimama karibu na vituo ili mradi wasiwe wamevaa sare za chama chochote cha siasa!.

Pia maelekezo ya uchaguzi yaliyotolewa na Waziri Mkuu Pinda yanapingana na kanuni ambazo ofisi yake imezitoa kuhusiana na dhamana ya wagombea. Kanuni zitaka mgombea awe amedhaminiwa na chama cha siasa. Hata hivyo, katika maelekezo Ofisi ya Waziri Mkuu imekwenda mbali zaidi kwa kuongeza maneno mengine ambayo hayapo kabisa kwenye kanuni ya kwamba mgombea lazima awe amedhaminiwa na ‘ngazi ya chini kabisa ya chama chake’. Mathalani katika CHADEMA ngazi ya chini kabisa ya chama ni msingi, ambayo ikifuatiwa na ngazi ya Tawi. Kwa upande wa CCM ngazi yao ya chini ni mashina halafu ndio matawi yanafuata. Kwa maelekezo hayo ya Ofisi ya waziri mkuu, dhamana ya mgombea ikiwa ni ngazi ya chini maana yake ni kuwa mgombea anapaswa adhaminiwe na msingi kwa CHADEMA na shina kwa CCM. Maelekezo hayo yanapingana kabisa na katiba za vyama shiriki ambazo zimeeleza bayana ni ngazi zipi zenye mamlaka ya kudhamini wagombea. Maelekezo hayo yanafunga pia milango kwa ngazi za juu za chama mathalani kata na kuendelea kudhamini wagombea kama ikibidi. Hivyo kwa ujumla, maelekezo hayo yanapaswa kubatilishwa mara moja kwa kuwa yanapingana na kanuni na katiba za vyama na yanatoa mianya kwa wagombea kuwekewa mapingamizi kutokana na utata kuhusu udhamini wao.

Yapo maneno muhimu ambayo yametumiwa kwenye kanuni na maelekezo ambayo hayajapatiwa tafsiri ya kuridhisha kuzuia mianya ya kupindishwa kwa kanuni na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao. Maneno hayo ni “Mkazi” na “Kipato halali”. Neno “Mkazi” limetafsiriwa kuwa ni raia wa Tanzania ambaye kwa kawaida anaishi katika kaya au taasisi iliyopo katika eneo husika. Tafsiri hii inaacha maswali mengi, kwa kuwa bila tafsiri kamili mpiga kura ama hata mgombea anaweza kuwekewa pingamizi kuwa hastahili kupiga kura au kugombea katika eneo Fulani. Maswali ya kujiuliza ni nini maana ya mkazi wa kawaida? Je mtu aliyehamia siku ya kujiandisha katika eneo Fulani anaweza kuhesabika moja kwa moja kuwa mkazi wa eneo hilo? Je, mtu aliyeishi miaka mingi katika eneo hilo akahama kwenda kwingine, akirejea kujiandikisha je bado anaweza kutambulika kuwa mkazi wa eneo husika? Nani mipaka ya vitongoji, vijiji na mitaa inatambulika kikamilifu na wananchi? Maana mtu anaweza kuwekewa pingamizi kwa kuambiwa tu kuwa kaya au taasisi anayoishi haiko ndani ya mipaka ya mtaa aliotaka kujiandikisha au aliojiandikisha. Jambo hili nalo linaweza kuwa chanzo cha mivutano hasa ukizingatia mambo yanayoendelea Zanzibar katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, ambao vitambulisho vya ukazi vinatumika kama kigezo cha kuamua nani aandikishwe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Kwa upande mwingine, kanuni zimetaja sifa mojawapo ya mgombea kwamba awe “ana kipato halali kinachomwezesha kuishi”. Hata hivyo, hakuna mahali popote, hata kifungu cha tafsiri ambapo maneno ‘kipato halali kinachomwezesha kuishi’ yamefafanuliwa. Jambo hili linaweza kutazamwa juu juu, lakini katika taifa ambao sehemu kubwa ya wananchi wamejiajiri katika sekta isiyo rasmi, na katika mazingira ya hujuma za kiuchaguzi; mgombea anaweza kuwekewa pingamizi kwa kuelezwa kuwa hana kipato halali kinachomwezesha kuishi. Mgombea ambaye amejiajiri kwenye ngazi ya chini kabisha hana kitambulisho cha kazi yake, anategemea hisani ya viongozi wa kiserikali kumuandikia barua za kumtambulisha hali ambayo ina mianya ya hujuma. Utata huu wa kukosekana kwa tafsiri unaweza kutoa mwanya kwa wasimamizi kukubaliana na mapingamizi yasiyokuwa na msingi wowote na kuwaengua wagombea, katika mazingira ambayo uchaguzi unasimamiwa na watumishi wa umma ambao hushinikizwa kuegemea matakwa ya chama tawala. Hivyo, ni lazima ufafanuzi utolewe ambao utahitaji mzigo wa kutoa ushahidi (burden of proof) uwe kwa anayeweka pingamizi badala ya anayewekewa pingamizi. Ielezwe wazi kuwa ni jukumu la mweka pingamizi kuonyesha kwamba Fulani hana kipato halali, ama ana kipato haramu au hana kipato kabisa. Ama sivyo, ufinyu wa tafsiri uliopo unatoa mwanya wa kupindishwa kwa kanuni na kuchochea mivutano katika mchakato wa uteuzi.

Kwa ujumla, kama kuna eneo ambao Waziri Mkuu Pinda amepindisha kanuni za msingi za uchaguzi huru na haki basi ni kuhusu uteuzi wa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi. Kwa mujibu wa kanuni, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa, wilaya ama afisa mwingine wa umma atayeteuliwa kwa ajili hiyo. Hata hivyo, si kanuni hazielezi mchakato wa uteuzi ambao ungetoa fursa kwa vyama kuweza kuweka pingamizi kama havikubaliani na uteuzi wa msimamizi wa uchaguzi. Kinachoshangaza zaidi ni kuwa maelekezo yaliyotolewa yamechukulia moja kwa moja tu tayari wakurugenzi ndio wasimamizi na moja kwa moja wamepewa mamlaka ya kuteua wasimamizi wasaidizi.

Kwa upande wa wasimamizi wasaidizi kanuni zimetaja kuwa ni maofisa watendaji wa vitongoji, vijiji, mitaa ama maofisa wengine watakaoteuliwa kwa ajili hiyo; kwa upande wao pia mchakato wa uteuzi haujatoa fursa ya kuwawekea pingamizi. Hii imeondoa uhuru wa mchakato mzima kwa kuwa uchaguzi unaposimamiwa na msimamizi au msimamizi msaidizi ambaye wadau hawamkubali tayari uhalali wa mchakato mzima unakuwa mashakani kwa kuruhusu mianya ya hujuma. Lakini pia, kuruhusu watendaji ambao kwa mujibu wa kanuni hizo hizo ni wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Kamati za Mitaa kusimamia uchaguzi ni kinyume kabisa na utawala bora. Katika maeneo mbalimbali ya nchi, watendaji hao ndio ambao wameshirikiana na wenyeviti kufanya ufisadi ama kutumia madaraka vibaya, kanuni zilizotungwa na Waziri Mkuu Pinda zinawapa mamlaka watu hao hao kusimamia uchaguzi. Inakuwaje pale wenyeviti waliokuwa madarakani, ambao kimsingi ndio ‘mabosi’ wao na washirika wao wa karibu katika kipindi chote walichoongoza? Hali hii inatoa fursa ya kuvurugika kwa uchaguzi. Lakini hata baada ya uchaguzi, kwa mujibu wa kanuni ni watendaji hao hao ndio ambao kwa nafasi yao ni makatibu wa Halmashauri za Vijiji na Kamati za Mitaa; unategemea kweli utawala bora baada ya heka heka za ama kupendeleana au kukomoana wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi? Kama ilikuwa ni lazima kutumia watendaji wa vitongoji, vijiji na mitaa; basi walau wangefanya kazi hiyo katika maeneo ya jirani yao badala ya kufanya kazi hizo kwenye maeneo yao. Ingewezekana kabisa kwa Waziri Mkuu Pinda kuweza kutunga kanuni ambazo zingetumia watumishi wengine wa umma pekee; nje ya watendaji wa mitaa ili kuweka uwanja sawa wa kisiasa na kuzingatia misingi ya utawala bora.

Izingatiwe kuwa mfumo wa utawala wa nchi yetu unaanzia katika vitongoji, vijiji na mitaa ambayo ina mamlaka kadhaa ya kiutendaji na kimaamuzi. Kuruhusu uchaguzi huu kuvurugika ama kuleta viongozi wabovu, kama taifa tutakuwa tumeweka msingi legelege wa utawala na demokrasia na athari zake zitaonekana katika kukwama kwa jitihada za kimaendeleo. Awali kabla ya kanuni kutoka niliweka bayana kwamba njia kuu ya kuzuia upindishaji wa kanuni, ni kuwashirikisha wadau kupitia rasimu ya kanuni kabla ya kuchapwa kwenye gazeti la serikali ili kuhakikisha kwamba makubaliano yote yamezingatiwa. Lakini Waziri Mkuu Pinda ametunga kanuni moja kwa moja bila walau kuitoa rasimu kwa vyama ndio maana udhaifu huu haukuweza kurekebishwa mapema. Katika muktadha huo, jibu la swali langu ni kuwa Waziri Mizengo amefanya ‘mizengwe’ na kupindisha kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Ameweka uwanja usio sawa wa kisiasa hivyo ni wajibu wa wadau wote kuingilia kati kwa haraka kurekebisha hali hii ili tusije kuwa uchafuzi wa amani na demokrasia. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha nchi yetu inakuwa na uchaguzi huru na haki kuanzia kwenye vitongoji, vijiji na mitaa. Bado kuna fursa ya kurekebisha kanuni, bado Waziri Mkuu Pinda anaweza kurekebisha hali ya mambo na kutoa ufafanuzi na maelekezo mbadala.


Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@yahoo.com na http://mnyika.blogspot.com



Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-1



Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-1

Na John Mnyika

Septemba 2009

Mwishoni mwa mwezi Julai niliandika makala kuhusu uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa yenye kuchokoza mjadala kuhusu kanuni za uchaguzi husika. Makala hiyo ilibeba kichwa na maudhui yenye kuulizwa swali: Pinda kupindisha kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa? Niliandika makala hiyo, kabla ya kutolewa kwa kanuni za uchaguzi husika kwa lengo la kuibua mjadala wa wadau kuhakikisha kwamba kanuni za uchaguzi na taratibu zake zinatolewa kwa kuzingatia makubaliano yaliyotiwa saini kwa pamoja kati ya ofisi yake, vyama vya siasa na asasi za kiraia mnamo mwezi Februari 20 mwaka 2009 kuhusu masuala yanayopaswa kuzingatiwa katika kanuni na taratibu za uchaguzi husika.

Izingatiwe kuwa chini ya sheria zetu, kanuni za chaguzi hizo hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Na kwa mujibu wa muundo wa sasa wa utawala wa Tanzania pamoja na kuwa na waziri wa nchi anayehusika na TAMISEMI, mwisho wa siku mwenye dhamana kamili ya “Wizara” hii ni Waziri Mkuu, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Mizengo Pinda. Katikati ya mwezi Agosti baada ya kimya cha muda mrefu, kilichoambatana na shinikizo toka kwa wadau kutokana na serikali kuchelewesha kutoa kanuni tofauti na ahadi yake, hatimaye Waziri Mkuu Pinda alitoa kanuni na maelekezo kuhusu taratibu za uchaguzi husika yaliyotolewa kwa nyakati mbalimbali. Sasa ni wakati muafaka kutoa jibu la swali nililolitoa kwa wadau kuibua mjadala.

Ikumbukwe kwamba mwanya huu wa kisheria wa Waziri kutunga kanuni ulitumiwa vibaya mwaka 2004 na kufanya kanuni hizo kutungwa kupendelea chama kinachotawala kwa kuweka mianya ya hujuma za kiuchaguzi. Matokeo yake ni uchaguzi uliopita wa vitongoji, vijiji na mitaa kutokuwa huru na haki kutokana na mapungufu mengi ambayo hata serikali yenyewe iliyakiri.

Mathalani upigaji kura haukuwa wa siri, fujo katika mikutano ya uchaguzi, matayarisho kuwa hafifu, kuingiliwa na maafisa na watendaji wa kata na vijiji ambao walifikia hatua ya kuwatisha wananchi na kutotoa taarifa za muhimu za uchaguzi, kukosekana kwa daftari la wapiga kura na uchaguzi kusimamiwa na chombo kisicho huru cha kiserikali moja kwa moja(Wizara ya TAMISEMI).

Kutokana na mapungufu hayo CCM ilishinda kwa asilimia 96 na kupata mtaji haramu wa kisiasa ambao ilianza nao kama hujuma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kufanya uwanja wa ushindani wa kisiasa usiwe sawa. Na hivyo, CCM ikashinda kwa takribani asilimia 80 katika uchaguzi mkuu mwaka mmoja baadaye.



Ilitarajiwa kwamba marekebisho ya haraka yangefanyika, hata hivyo hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kati ya mwaka 2005 mpaka 2008. Kesi iliyofunguliwa na vyama vya upinzani mwaka 2004 kuhusu kanuni na taratibu za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa mpaka sasa bado ni kizungumkuti. Kwa upande mwingine, Serikali ilikuwa ikiitisha mikutano na vyama na kuiahirisha bila maamuzi ya msingi kufikiwa kuhusu marekebisho yanayostahili kufanywa katika sheria na kanuni zinazosimamia chaguzi husika.


Mwaka 2009, mwezi Februari ndipo serikali imesaini makubaliano na wadau kuhusu uchaguzi huu. Kwa kisingizio cha ufinyu wa muda, masuala ya msingi yaliyopaswa kufanyiwa marekebisho mengi hayapo kama sehemu ya makubaliano hayo. Kwa mara nyingine tena, serikali imechelewesha muda na baadaye kutumia kisingizio cha muda kukwepa kufanya mabadiliko ya msingi ya kisheria ya kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki.

Kama ilivyotarajiwa kutokana na makubaliano hayo, yafuatayo iliamuliwe yasifanyiwe marekebisho kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na serikali ikiwemo ufinyu wa muda. Kuhusu kilio cha miaka mingi cha wadau cha kutaka uchaguzi usimamiwe na Tume ya uchaguzi kama ilivyo katika baadhi ya nchi nyingine duniani; makubaliano yameweka bayana kuwa uchaguzi utaendelea kusimamiwa na serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa. Ndio maana kanuni zimeendelea kutungwa na waziri badala ya chombo huru. Katika kanuni hizo umri wa kugombea; umebaki kuwa miaka 21 badala ya kushuka mpaka 18. Wagombea binafsi; hawajaruhusiwa.

Mwito wa Vyama vya siasa kutaka viwezeshwe kutoa elimu ya uraia nao haujazingatiwa. Serikali imeendelea kuweka msimamo kupitia maelekezo ya taratibu za uchaguzi husika kuwa jukumu la kutoa elimu ya uraia litaendelea kuwa la serikali. Hoja ya kutaka uchaguzi wa madiwani uende sambamba na chaguzi zingine za mitaa nayo haipo katika kanuni zilizotolewa na Waziri Mkuu Pinda. Uchaguzi wa madiwani utaendelea kuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2010; hii ni kwa sababu suala hili linahitaji marekebisho ya kisheria na serikali ilishatamka wazi kwamba muda umeshakwisha wa kufanya marekebisho husika.

Haya ni masuala nyeti ambayo wadau wengi walipenda yafanyiwe marekebisho lakini hakuna mabadiliko yoyote ambayo Serikali imeyafanya kuhusu masuala hayo katika kanuni zilizotungwa ambazo Waziri Mkuu Pinda ameshazitangaza. Shabaha ya makala hii si kuyajadili masuala hayo ambayo hayakuwemo katika makubaliano ya wadau ya mwezi Februari 2009; masuala haya yanapaswa kutafakariwa na taifa kwa ajili ya marekebisho ya muda mrefu ili kuhakikisha yanazingatiwa katika uchaguzi unaofuata wa vitongoji, vijiji na mitaa wa mwaka 2014. Safari hii, wadau wasikubali serikali itoe visingizio vya ufinyu wa muda kwa kuwa kuna muda wa kutosha kuanzia sasa mpaka wakati huo kuweza kufanya mabadiliko yanayokusudiwa.


Dhima ya makala hii ni kutafakari iwapo masuala kwenye makubaliano ya wadau yameingizwa katika kanuni na taratibu zilizotolewa na Waziri Mkuu Pinda kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 304 ya tarehe 21 Agosti 2009. Tafakari hii inaendeleza mjadala wa wadau kuhakikisha kwamba marekebisho ya msingi walau yanayogusa mambo ambayo serikali ilishakubaliana na vyama vya siasa na asasi za kiraia yanafanyika kabla ya uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa ambao umetangazwa kufanyika tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka 2009.

Waziri Mkuu Pinda ameweza kuingiza baadhi ya masuala kwenye kanuni na taratibu alizozitoa kama makubaliano ya wadau yalivyohitaji. Mathalani kanuni zimeelekeza kwamba kutakuwa na karatasi maalum za kura zenye nembo ya halmashauri husika; karatasi hazitakuwa na majina ya wagombea, majina yatabandikwa sehemu ya wazi baada ya uteuzi. Maelekezo ya taratibu yanaeleza kuwa uteuzi wa wagombea ni tarehe 5 Oktoba 2009; hivyo wagombea wanaweza kuchukua fomu za kiserikali kuanzia tarehe 28 Septemba mpaka 4 Oktoba, 2009.

Kwa mujibu wa Kanuni Uchaguzi utafanyika kwenye majengo ya umma, kama hakuna msimamizi atashirikiana na vyama kupata sehemu muafaka. Kanuni zimeelekeza kuwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri za Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji utafanyika katika kitongoji ili kuwafanya wapiga kura wengi kuweza kufika na kupiga kura zao; suala hili limewezakana baada ya Bunge kubadili sheria husika katika mkutano wake uliomalizika hivi karibuni. Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za Mitaa utafanyika katika mitaa husika, vituo vitakuwa zaidi ya kimoja kulingana na wakazi wa mtaa.

Kwa mujibu wa kanuni Kampeni zitafanyika kwa muda wa siku saba kama ilivyo kwa kanuni za 2004; na maelekezo ya taratibu yameweka bayana kuwa ni kuanzia tarehe 6 mpaka 24 Oktoba 2009.

Orodha ya wapiga kura(Local Voter register) itaandaliwa siku 21 kabla ya uchaguzi ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kukagua orodha na kuweka pingamizi. Orodha itaandaliwa na watumishi wa umma lakini wasiwe watendaji wa vijiji, mitaa au kata. Uthibitisho wa mpiga kura utatokana na jina lake kuwepo katika orodha ya wapiga kura, vitambulisho vitavyotumika kumtambulisha chochote kati ya vifuatavyo- kadi ya mpiga kura, kitambulisho cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha chuo/shule, leseni ya uderava au wakazi kama mpiga kura hana kitambulisho chochote.

Kanuni zina kifungu cha kamati ya rufaa kama ilivyohitajiwa na wadau, wajumbe wake wanatajwa kuwa ni Katibu Tawala wa wilaya, afisa yoyote kutoka Taasisi ya Umma aliyoko katika wilaya husika na afisa yoyote wa umma anayefanya kazi katika ofisi ya katibu tawala wa wilaya ambaye atakuwa katibu na hatakuwa na haki ya kupiga kura. Kanuni pia zimeweka bayana kuwa wafuatao hawatateuliwa kuwa wajumbe wa kamati ya rufaa; afisa anayehusika na uteuzi wa wagombea, msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, kiongozi wa ngazi yoyote wa chama cha siasa na mtumishi wa halmashauri.




Hata hivyo, kwa upande mwingine Waziri Mkuu Pinda na ofisi yake wamepindisha Kanuni na taratibu za uchaguzi wa vitongoji na mitaa na kinyume na misingi ya chaguzi huru na haki ambayo ni mhimili wa utawala bora. Ama kwa hakika mambo haya yanahitaji kutazamwa kwa kina na kwa haraka na wadau wowote ili kuepuka uchaguzi huu kugubikwa na vurugu zenye kutishia amani na demokrasia.

Tayari vyama mbalimbali vimeshaanza michakato ya uteuzi na uchukuaji wa fomu za ndani ya vyama. Katika hali inayoibua maswali mengi, CCM ilianza mchakato wa uteuzi ndani ya chama chao kabla hata ya kanuni za uchaguzi kutolewa na Waziri Mkuu Pinda. Hali hiyo imeelezewa na wachambuzi mbalimbali kuwa ni ishara ya kuwa chama hicho kilipewa kanuni husika mlango wa nyuma na serikali kukipa fursa ya kujiandaa mapema kabla ya kanuni kutolewa kwa vyama vingine. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba kura za maoni katika chama hicho vimetawaliwa na rushwa na vurugu katika maeneo mbalimbali, hali ambayo mpaka sasa imesababisha kifo cha mtu mmoja huko wilayani Serengeti. Kwa upande wa CHADEMA, fomu hizo za uteuzi wa ndani ya chama zimeanza kutolewa kuanzia Agosti 25 na michakato ya uteuzi inaendelea mpaka Oktoba Mosi, 2009 kutegemea na ratiba ya ndani ya mamlaka zinazotoa fomu katika ngazi mbalimbali za chama.

Kama ilivyodokezwa awali, kanuni zimeelekeza kwamba karatasi za kura hazitakuwa na majina ya wagombea na kwamba mpiga kura atalazimika kuandika mwenyewe. Hali inaweza kuchochea kuchelewa ama kuvurugika kwa mchakato wa upigaji na uhesabuji wa kura. Katika nchi ambayo zaidi ya nusu ya wananchi wake hawajui kusoma na kuandika na sehemu kubwa ya wanaojua bado si kwa kiwango kizuri, uamuzi wa kutunga kanuni ambazo zinalazimisha kwamba wapiga kura waandike wenyewe majina kamili ya wagombea umetoa mianya ya kuvurugika kwa uchaguzi.

Waziri Mkuu Pinda pia amepindisha kanuni katika kifungu cha 20(8) ambapo inatamkwa kwamba mpiga kura atapatiwa kura nne; wakati ambapo uchaguzi huo unahusisha mafungu ya nafasi tatu: Mwenyekiti, wajumbe wa ujumla na wajumbe wa viti maalum wanawake. Hivyo, kwa vyovyote vile marekebisho yanapaswa kufanyika ili Oktoba 25 mpiga kura apatiwe kura tatu; hali hii ikiachwa bila ufafanuzi inaweza kuzua mzozo siku ya kupiga kura.

Kwa upande mwingine, yapo maeneo ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu imekiri mnamo 11 Septemba 2009 kupitia barua yenye kumbukumbu Na. HB.114/126/01 kwamba maelekezo ambayo imeyatoa yamepindisha kanuni. Mathalani, maelekezo yanasema wajumbe wa Halmashauri ya vijiji wanawake wa viti maalum watakuwa si chini ya 25%. Wakati ambapo Sheria Na. 19 ya mwaka 2009 inatamka kwamba idadi ya wanawake viti maalum katika halmashauri ya kijiji inatakiwa kuwa si chi ya theluthi moja ya wajumbe ambayo kwa vyovyote vile sio chini ya wanawake nane(8). Wakati kanuni zinazungumza kwamba ukomo wa utumishi wa wenyeviti na wajumbe wao walioko madarakani hivi sasa ni siku tatu kabla ya uteuzi ambayo ni tarehe 02 Oktoba 2009; tayari ofisi ya Waziri Mkuu ilishatoa maelekezo kwamba utumishi wao ulikoma toka tarehe 2 mwezi Septemba 2009. Kitendo cha Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi tarehe 11 Septemba kubatilisha maelekezo ambayo waliyatoa kabla kinaacha maswali mengi kuhusu uhalali wa wenyeviti wa mitaa na wajumbe walioko madarakani hivi sasa ambao walishatangazwa kujiuzulu nyadhifa zao toka mwanzoni mwa mwezi Septemba. Katika makala inayofuata nitaeleza hoja zaidi zinazodhirisha mapungufu zaidi yaliyopo kwenye kanani na maelekezo na hatua zinazohitaji kuchukuliwa na wadau kwa haraka ili kuhakikisha uchaguzi husika unakuwa huru na haki.


Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@yahoo.com na http://mnyika.blogspot.com