Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa nyakati mbalimbali kati ya tarehe 28 Februari na 2 Machi 2013 kupitia baadhi ya vyombo vya habari wametoa majibu yasiyokuwa ya kweli juu ya mgawo wa dharura wa umeme uliotokea mwezi wa Februari.
Katibu Mkuu wa Wizara Eliackim Maswi na Afisa Habari wa TANESCO Badra Masoud wote wameeleza kwamba hakukuwa na mgawo wa umeme bali kilichotokea ni matatizo madogo madogo ya mitambo na kwamba matengenezo yanaendelea.
Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ninazo taarifa kwamba ukweli ni kuwa umetokea mgawo wa umeme wa dharura kutokana na upungufu zaidi wa kina cha maji katika mabwawa ya kufua umeme, upungufu wa fedha za kununua mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kufua umeme wa dharura na upungufu wa gesi asili ya kuendeshea mitambo ya kufua ya umeme.
Hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kuingilia kati kuwaeleza ukweli wananchi ikiwemo hatua zilizochukuliwa kuhakikisha kwamba hali hiyo haiendelei mwezi Machi kinyume na ahadi iliyotolewa bungeni tarehe 28 Julai 2012 kwamba mgawo wa umeme ungekuwa historia.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
02 Machi 2013
No comments:
Post a Comment