Monday, October 27, 2008

Salamu za Mshikamano kuunga mkono Maandamano ya Wadau wa Habari

Salamu za Mshikamano kuunga mkono Maandamano ya Wadau wa Habari

Ndugu Wahariri

Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) tukiwa ni sehemu ya wadau wa sekta ya habari nchini, tunaunga mkono maandamano ya amani mliyoitisha ya kupinga hatua ya serikali kulifungia gazeti la MwahaHALISI.

Tunawapongeza wahariri kwa mshikamano wenu katika kipindi hiki cha majaribu; endeleeni kusimama pamoja, ni umoja wenu ndio utakaokuwa kinga ya pamoja dhidi mtu au chombo chombo chochote kinachoingilia uhuru wenu. Mshikamano wenu ni ishara ya kushindwa kwa mkakati wa ‘wagawe uwatawale’ na imani kwamba umoja ni nguvu. Wahariri wote hawapaswi kukaa kimya kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI kwa kuwa leo ni kwa gazeti hilo, kesho itakuwa kwa gazeti lingine; hivyo ni vyema kuungana pamoja kulinda uhuru, taaluma na sekta ya habari nchini.

Kwetu sisi hatua hiyo ya serikali tunaitafsiri zaidi ya kufungia gazeti la MwanaHALISI; ni hatua ya kufungia uhuru wa kusambaza habari na uhuru wa kupokea habari. Hivyo hatua hiyo ni kinyume cha haki za binadamu, kinyume cha utawala bora na ni kikwazo kwa demokrasia na maendeleo. Hakika serikali na viongozi wake wamevuka mstari wa kukubali kukosolewa na sasa wameamua kuanza kufungia uhuru wa fikra mbadala.

Hatua ya Waziri mwenye dhamana na sekta ya habari kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji ni mwelekeo mbovu wa kupuuza taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki. Uamuzi uliofanywa na serikali hauna tofauti na unaofanywa na raia wanaojichukulia sheria mikononi(mob justice). Kwa serikali inayoheshimu misingi ya asili ya haki, tulitarajia chombo chochote cha habari, kikivunja sheria ama kukiuka maadili dhidi ya serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka ama malalamiko yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari(MCT) ama Mahakama.

Hatua ya serikali kufungia gazeti la MwanaHALISI pamoja na kuwa imechukuliwa kwa mujibu wa sheria iliyopo, imekiuka misingi ya asili ya utawala wa sheria. Kwani kulikuwa na sheria nyingine nzuri ambazo serikali ingeweza kutumia kupitia mahakama lakini ikaamua kuchagua kutumia sheria mbaya kwa kutumia mamlaka ya Waziri. Itakumbukwa kwamba wadau wa sekta ya habari na hata serikali yenyewe imekuwa ikikiri kwamba Sheria hiyo iliyotumiwa ni sheria mbovu inayohitaji kufutwa ama kufanyiwa marekebisho makubwa ikiwemo kupunguza mamlaka makubwa ya viongozi wa serikali dhidi ya vyombo vya habari. Sheria yoyote inayotambulika kuwa mbovu katika jamii yoyote, inapoteza uhalali wa kihaki(legitimacy) miongoni mwa umma na hivyo kuendelea kuitumia ni kuteteresha misingi ya utawala wa sheria na kutoa mfano mbaya kwa vijana nchini na wananchi kwa ujumla. Hivyo, tunachukua fursa hii kuitaka serikali kuharakisha mchakato wa kupitisha sheria ya vyombo habari na sheria ya uhuru wa taarifa.

Aidha tumeshangazwa na uamuzi wa serikali kufanya maamuzi yake kwa ubaguzi kwa kulichukulia hatua gazeti la MwanaHALISI na kukwepa kuyachukulia hatua magazeti mengine ambayo yameandika habari inayoshabihiana na maudhui ya habari iliyoandikwa na gazeti hilo. Kwa muda mrefu sasa, habari za uwepo wa viongozi ama makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) yenye kupanga ‘kumng’oa’ Rais Jakaya Kikwete miongoni mwa wanaotarajiwa kugombea urais kupitia chama hicho mwaka 2010 zimeandikwa na magazeti mbalimbali. Hatua hii ya kibaguzi inaibua maswali kuhusu dhamira ya serikali kulifungia gazeti hilo wakati huu ambapo mchango wa gazeti hilo na mengine yaliyo mstari wa mbele kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za taifa unahitajika kwa kiasi kikubwa. Hata baada ya kulifungia gazeti la MwanaHALISI, habari za aina hiyo zimeendelea kuandikwa ikiwemo na vyombo vya habari vya nje; mathalani tarehe 24 Oktoba, 2008 kutoka Ufaransa gazeti la Africa Intelligence inayomtaja Rostam Aziz kukusanya fedha kwa ajili ya kufadhili kundi lake katika uchaguzi huo. Katika muktadha huo, serikali inapaswa kulifungia gazeti la MwanaHALISI mara moja, kama imeonyesha wazi kushindwa kuyachukulia hatua magazeti mengine.

Kadhalika kwa mtiririko wa matukio katika taifa letu, kuna mwelekeo wa Serikali na CCM kuminya maoni yenye kumkosoa au kumgusa Rais Kikwete. Mjadala wa Rais Kikwete ‘kung’olewa’ katika uchaguzi mwaka 2010 unaelekea kuichukiza kwa kiasi kikubwa Serikali na CCM. Gazeti la MwanaHALISI liliandika habari ya namna hiyo, likafungiwa na Serikali. Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa katika ‘Operesheni Sangara’, alitoa hoja hiyo na matokeo yake CCM ikaibuka na kujibu kwa vitisho na vioja. Vijana wa Tanzania wangependa kupata mfano uongozi bora wenye kukubali kukosolewa na kukubali mabadiliko badala ya uongozi legelege wenye kuendeleza udikitekta wa kimawazo na hivyo kuminya fikra huru. Si dhambi kwa CHADEMA ama mtu yoyote kutaka kuiondoa CCM ama kiongozi wake yoyote madarakani mwaka 2010 kupitia njia za kidemokrasia.

Mwisho, tunatoa mwito kwa watanzania wote kusoma alama za nyakati na kuunga mkono harakati hizi za wahariri na wadau wa sekta ya habari kutetea uhuru wa kweli katika taifa letu. Jamii itambue kwamba kitisho cha uhuru na haki kwa mtu Fulani au mahali Fulani ni tishio kwa watu wote na mahali pote. Yanayofanywa kwa vyombo vya habari, yanaweza pia kufanywa kwa watetezi wengine kwani hivi karibuni taifa limeshuhudia Asasi ya HAKIELIMU ikitishiwa kutokana na jitihada zake za kuhamasisha mabadiliko ya fikra katika sekta ya elimu na kupiga vita ufisadi unaoathiri sekta hiyo. Tuko katika kipindi cha majaribu; kuibuka kwa mijadala yenye kuchochea mgawanyiko/ubaguzi, kuongezeka kwa matabaka na malalamiko juu ya hali za maisha. Katika wakati huu ambapo misingi ya nchi yetu iliyopo katika Ngao ya Taifa ya Uhuru na Umoja inapotikiswa ni wakati wa kuunganisha “Nguvu ya Umma” kupinga aina zote za ufisadi na kutetea rasilimali za taifa kwa kuhamasisha maadili, fikra mbadala na mabadiliko ya kweli. Kuunga mkono maandamano ya wadau wa sekta ya habari ni sehemu ya azma hiyo. Mshikamano, daima; pamoja, tutashinda!

Wasalaam,

John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa
Mwanza, Tanzania-28/10/2008





4 comments:

Anonymous said...

Rekebisho:Inapaswa kulifungulia MwanaHALISI sio kulifungia

John Mnyika said...

Rekebisho: Isomeke- "Serikali inapaswa kulifungulia gazeti la MwanaHALISI haraka iwezekanavyo. Sio kulifungia"

JJ

erasto said...

Kaka nimesoma waraka wako na unasadifu mambo ambayo serikali hii inayafanya ambayo hayaendani kabisa na mipango endelevu, hii ni dhahiri kuwa serakali inafanya juu chini kunyamazisha kila jema ambalo watu wema wanajitahidi kuwafungua wacho wananchi. imefika wakati wa kuondokana na vitisho vya watu wachache na kusonga mbele bila kuogopa.

Protas said...

inaskitisha sana serikali kuhujumu uhuru wetu kupata habari zenye manufaa kwetu, imetuuma sana lakini napenda kuwatia moyo waandishi kutokata tamaa, huu ni wakati wa mabadiliko kwahiyo waandishi wa habari wasimame kidete na umoja wakutosha kusimamia vuguvugu hili.