Sunday, June 24, 2012

Waraka wa kwanza mwaka 2012 wa Mbunge kwa Wananchi- “Ukweli ni Uhuru”


Waheshimiwa Wananchi wenzangu,
Amani iwe kwenu,
Kwa kipindi cha wiki nzima kumekuwepo na mjadala mkali bungeni, kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na katika taifa kwa ujumla juu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13 sanjari na yaliyojiri kutokana na kauli niliyotoa bungeni juu ya udhaifu wa Rais katika usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti pamoja na mipango muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.
Aidha, kupitishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 bila marekebisho yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa kumedhihirisha kile nilicho tahadharisha tangu awali kwamba; kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na uendeshaji wa nchi, udhaifu wa Rais una athiri maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Katika mazingira haya, udhaifu wa rais na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na serikali kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea pia migomo baridi ya watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kutokana pia na madai yao ya muda mrefu kutokuzingatiwa kwenye bajeti. Ukweli ni Uhuru!.
Kadhalika udhaifu wa kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia tu mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Pia, katiba imempa mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge likikataa bajeti ya serikali kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja bunge suala ambalo huwapa hofu wabunge wengi hususani wa chama kinachotawala na kuwafanya wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika. Hivyo, udhaifu wa bunge unachangiwa na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais katika kuvunja bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo wabunge hawana uwezo wa kubadilisha na wakati huo huo wakikataa bunge linavunjwa, katika mazingira haya udhaifu wa Rais wa kushindwa kutumia nguvu hizo za kikatiba una madhara makubwa sana kwa nchi na maisha ya wananchi.  Ukweli ni Uhuru!.
Kwa mantiki hiyo, katika mchakato wa katiba mpya ni muhimu kwa wananchi kutoa maoni ya kuwezesha ukuu na uhuru wa bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. Wakati katiba mpya ikisubiriwa, ni muhimu kwa marekebisho ya haraka kufanyika katika kanuni za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka kanuni ya 107 ili kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa. Katika muktadha huo, nimeanza kufanya uchambuzi  ili kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Hata hivyo, hata kwa kanuni zilizopo sasa udhaifu wa bunge unaongezeka kutokana na maamuzi ya kizembe mathalani ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge, mfano Kanuni ya 94 inalitaka bunge ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano wake wa mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, kanuni ambayo toka niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa wakati hata mara moja pamoja na kuwakumbusha wanaohusika kusimamia kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Mwaka huu udhaifu umekuwa mkubwa zaidi kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sanjari na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni 2012 hali ambayo imechangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilfu mpango wa taifa wa miaka mitano. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru kwamba Spika wa Bunge Anna Makinda amekiri bungeni tarehe 20 Juni 2012 kwamba kulikuwa na udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge kukamilisha kazi ya kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha serikali kuongeza vyanzo vya mapato kama wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na pendekezo hilo kurudiwa tena na kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni 2012. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa iwapo sheria ya fedha ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012 kama ilivyokuwa imepangwa awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia sehemu kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye bunge na waziri. Hivyo, michango na mapendekezo ya wabunge bila Rais mwenyewe kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa mapato kwa kuwa kwa kuwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) udhaifu wa bunge ni pamoja na kukatazwa kutoza kodi au kuongeza kodi. Ukweli ni Uhuru!.

Hivyo, Kamati ya Fedha na Uchumi itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3) kurejea maoni yake, ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne wa Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 na kufanya marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri Waziri. Ukweli ni Uhuru!.

Aidha, ili kuondoa udhaifu uliopo Rais Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu rasmi za bunge (Hansard) za tarehe 18 Juni mpaka 22 Juni 2012 na kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha Waziri wa Fedha ya 86 (10)  kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika bidhaa zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa ufupi nilichosema bungeni na nilichotarajia kusema na kuahidi kwamba nitatoa tamko kamili baadaye; baada ya kujipa muda wa kutafakari nimefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati bunge litakapoelekea kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013; ambapo pamoja na masuala mengine nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa kwa watanzania kuweza kutekelezwa na serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa sasa niwashukuru wananchi wa Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na watanzania kwa ujumla walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni yao kwenye mitandao ya kijamii, simu za mkononi na katika vyombo vya habari. Nawashukuru pia viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya taifa.  Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru pia kwa mchango wa walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli niliyotoa juu ya udhaifu wa Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana na jazba na wengine wameeleza kuwa ningetumia lugha ya diplomasia kufikisha ujumbe ili kutodhalilisha taasisi ya urais na kwa kuzingatia utamaduni wetu wa heshima kwa wakubwa na wapo wachache waliosema kwamba ni matusi kutamka ‘udhaifu wa Rais’. Ukweli ni Uhuru!.
Wakati mjadala huu ukiendelea ni rai yangu kwamba rejea ifanyike katika mchango wangu wa tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili pia ifanyike kwenye mchango wangu wa tarehe 19 Juni 201; na ieleweke kwamba naheshimu taasisi ya urais na umri, naamini katika matumizi ya lugha ya kidiplomasia, hata hivyo nilitafakari na kuamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka zote zinazohusika na wauchukulie kwa uzito tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita. Ukweli ni uhuru!.
Niliamini, naamini na nitaendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka; hata hivyo kwa kuwa pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa chanzo cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni wa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa; nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli ni uhuru!.
Katiba ya Nchi ambayo niliapishwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”. Toka nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010 kwa nyakati na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wa kawaida wakilalamika kuhusu udhaifu wa Rais na kutaka atumie nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti serikali kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayolikabili taifa; niliamua kuendelea kusema bungeni kwa mara nyingine ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Tarehe 19 Juni 2012 nilieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti na tarehe 22 Juni 2012 nilipiga kura ya hapana ya kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa ajili ya miradi ya barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais Kikwete na kuingizwa kwenye jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande wa miradi ya maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika bajeti ya 2012/2013. Ukweli ni Uhuru!.
Pamoja na utetezi uliotolewa na Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri kati ya kiingereza na Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua kuikataa bajeti kwa kuwa ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao uliwasilishwa na Rais Kikwete na ukapitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo kama zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli ni Uhuru!.
Naamini Rais Kikwete anayofursa ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake katika muswada wa sheria ya fedha kupanua wigo wa mapato na hatimaye kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 107 mapendekezo ya matumizi ya nyongeza ya fedha za serikali yenye kulenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo. Kwa upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam, serikali kwenye bajeti ya nyongeza inayopaswa kuwasilishwa iongeze fedha za miradi ya Maji kwa upande wa Ruvu Juu ikiwemo kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa Bwawa la Kidunda, kwa upande wa Barabara iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za pembezoni za mchujo na za mzunguko za kupunguza msongamano wa magari, na fidia ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la Mloganzila. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa Wasemaji wa CCM waliodai kwamba nimetoa lugha ya matusi dhidi ya Rais na mwenyekiti wa chama chao wasome Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania cha mmoja wa waasisi wa TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere  ambapo wakati huo taifa likiwa katika mtanziko alimueleza Rais wa wakati huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’ katika ukurasa wa 50 na kuendelea kusema katika Ukurasa wa 51 na namnukuu “Kwa sababu ya minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake salama” . Ukweli ni Uhuru!
Naamini Mwalimu Nyerere hakumtukana Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu nimetukana ni kumtuhumu pia Marehemu Baba wa Taifa; narudia tena kusisitiza kuwa udhaifu uliojitokeza ni kutokana na Rais kutokutumia kwa uthabiti nguvu na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ibara za 33, 34, 35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji wa serikali na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni Uhuru!.
Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “ Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa.  Na msingi wa woga ni ubinafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho wa kunukuu:   Ukweli ni uhuru.

Wenu katika utumishi wa umma, 

John Mnyika
22 Juni 2012
Bungeni-Dodoma






27 comments:

Anonymous said...

Huna jipya tatizo unafikiri watanzania wote ni wajinga. Kama kweli una uchungu na nchi yako mbona mpaka leo unapokea posho ulizogomea awali pia kiongozi wako kapokea gari la kifahari japo mwanzo alikataa mtabaki kupiga kelele ili kujitengenezea mwanya kupata kura uendelee kula maisha kama hautendewi haki jing'atue 2kuone shujaa.

Anonymous said...

Usamehewe hujui uliandikalo, badala ya kumuunga mkono Mh !nyika unaanza kuleta fitiza zako hapa?
Wewe tunajua haki zetu.
Funguka ww.

Anonymous said...

Ndiyo nimefunguka hivyo,jibu hoja kama anaona hatendewi haki aondoke na vp posho hapokei, mbowe gari hajachukua sasa kelele za nn. 2nahitaji kiongozi ambaye yuko kwa maslai ye2 kwisha. Yeye kaungana na hao wanao2mia mali za uma vibaya alafu huku nje anapiga kelele. If u can't fight them join them ndicho wanachofanya alafu nakuomba utafute manifesto ya CHADEMA uisome na ujue ilianzia wapi na kwa lengo gani then uje kutoa commet

mruta Julius said...

ukweli hauna umri wala hauna taaluma na wala hauna jinsia, uzembe wa mawazo kujipendekeza na kuomba hisani za watawala kumeviza mawazo ya watu. kwa misingi hii tumetoka kwenye kutengeneza jamii jasiri na yenye maadili na kutengeneza jamii ya watu waoga, wanafiki na wanaojipendekeza ili kupata hisani za watawala. Katika ulimwengu wazi na kweli hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia ukweli kwa gharama yeyote hata kama anajeshi na vifaru vya namna gani." Kuna vitu kamwe Huwezi kuvificha hapa Duniani navyo ni Ukweli,mwezi na Jua" Confucius mwanafarsa wa china.

Anonymous said...

ANONYM WA KWANZA U MUST HAVE A MENTAL DISORDER, HAMA KUSOMA HUWEZI HATA PICHA HUWEZI ONA, KAMA NAJUA WEWE NI MTUMWA WA MAGAMBA AND AM TELLING U, U WILL KEEP ON KISSING ASS UNTIL U DIE, CHAMA CHA MAPINDUZI NDIO KILICHOIFIKISHA TANZANIA HAPA ILIPO, USIFIKIRI IPO SIKU KITAKUWA NA UWEZO WA KUTUTOA HAPA NA KUTUPATIA MAISHA BORA. MNYIKA KEEP IT UP, MIMI NI MPIGA KURA WAKO NIPO KIMARA TEMBONI.

Elias Charles said...

Well said Hon. JJ Mnyika. Nakubaliana nawe katika hoja nyingi ulizoweka bayana bila hila. Kujua tatizo ni Mwanzo wa suluhisho la tatizo lenyewe. Swali langu ni Kuwa; Nini kifanyike ili kuinusuru Tanzania na Tanganyika yetu.

Anonymous said...

Woga ni dhambi,ulisema kweli na kweli hiyo imekuweka huru!Ni vizuri hata kubaki peke yako lakini ukasimamia kweli,huo ndio uongozi.
Baya ni lipi kusema Rais ni dhaifu au kuendelea kuwa kimya?

Mungi said...

Mchangiaji wa kwanza lazima atakuwa Mwigulu Nchemba

Anonymous said...

Ukweli ni uhuru

Anonymous said...

Mnyika u right kaka, endelea kupigania usisikilize mafisadi wa ccm, huyo anayeponda kwa waraka wenye evidence kama huu na kuja na mada ambayo haiajajadiliwa ni mjinga namba moja, tunajua kuwa ccm ina tabaka la watu wa aina mbili, walioshiba (mafisadi) na wale wajinga sana wasiojua kitu. huyu anaweza akawa katika kundi la pili, ana jaziba zisizoluwa na msingi, pia aelewe kwamba no development without revolution/change, tumezaliwa tukaikuta ccm lakini hadi leo jipya haina, ongeza juhudi kaka mwisho wao hao 2015.

Anonymous said...

Anonymous wa kwanza kama sio Lukuvi basi atakuwa ni Job Ndugai

Deusdedit Jovin Kahangwa said...

Mh Mnyika, maneno yafuatayo ni sahihi: "kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka." Naunga mkono nia yako ya kuliomba bunge lifanye marekebisho katika kanuni za kudumu za 2007 ili kifungu cha 64 kikarabatiwe ipasavyo kwa kuzingatia mtazamo wako. Kifungu hiki kinakataza matusi, lugha ya kuudhi, n.k. Lakini hakuna ufafanuzi wa kitaalam kuhusu maana za maneno haya. Ninachoona ni kwamba kanuni hii ya 64 ilidurufu kimakosa maudhui ya kanuni za maadili za CCM za mwaka 2002. Nikipata muda nitaonyesha vizuri jambo hili.

Anonymous said...

Mh Mnyika kwanza pole kwa misukosuko kiasi iliyokupata kutokana na nia yako thabiti kwa kushambuliwa na watu wanao ona mbele Yao lakini sio Mbali!
Kila mtu ikumbukwe Ana udhaifu na Uimara wake, Rais ni binadamu wa kawaida ingawa ni senior citizen ambapo ni lazima ana madhaifu na mazuri, na kwa Hali hii ni lazima pia watu hususani wazalendo halisia Kama Mnyika lazima washiriki katika kumkosoa pale yanapojitokeza madhaifu ya wazi wazi na ya kiuzembe ambao unaweza kuonekana hata kwa vihiyo!
Hivi Leo hii nani asiyejua kwamba Rais na Waziri Mkuu wapo kimya tu wakitazama mambo ya ajabu yakiendelea Kama vile wizi wa wanyama kupelekwa nje! Wizi wa madini na ndege za wazungu kule kahama na Kakola, na mengine mengi! Je angekuwa Sokoine na Nyerere udhaifu huo ungekuwepo?
Jamani Tujifunzeni UTAMADUNI wa Hayati Edward Moringe Sokoine! Hakuonea aibu kipele cha cancer kilichokuwa kinamea mwilini maana aliamini asipokitibu mapema madhara yake ni kukata kiungo hicho cha mwili!Mnyika Kama haupati usingizi basi uanze kuupata brother! Kwani wanaokutuhumu wasifikirie kila siku ni sherehe tu kwa Rais kushangiliwa na kupigiwa makofi! La khasha siku zingine misukosuko lazima akutane nayo.

Anonymous said...

Ingekuwa enzi za mwalimu tungeshakusahau ungefia jela Mheshimiwa!Kuwa makini na kauli zako utapoteza some of ur valuable supporters, hata kama kuna udhaifu find a good way to say it, not in a childish way!Na unapokosea kusema sorry ni ustaarabu wa kawaida tu kukataa kusema sorry unatangazia umma kuwa ww ni mtu wa namna gani no ustaarabu

Anonymous said...

Ushasema enzi za mwalimu, we ngadu nini. Sasa tupo enzi za ukweli na uwazi. Hata mwanao usipomwambia ukweli hatajirekebisha. Kwani nini maana ya UDHAIFU au kwa sababu limetamkwa kwa kiswahili. Mbona hata kwenye interview tunaambiwa tell us your strength and weaknesses hatulalamiki kama tumetukanwa. Tatizo la sisi watanzania tuna nidhamu ya uwoga. Kwani Raisi ni mungu hakosei. Na kwa taarifa yako Mnyika ndo kapata umaarafu zaidi sasa. Hawa ndo viongozi tunaowataka "wanathubutu" na sio kuchekacheka tu. Ukweli ni Uhuru.

Anonymous said...

Nimeona jengo moja ambalo ni la mmoja wa viongozi wa chadema sasa sijui kama kweli mko na mpango wa kutukomboa wananchi ama mnataka nafasi na nyie ya kula pesa kama hawa mafisadi ..sidhani kama wafuasi wote watabaki kama wafuasi kama mkiendelea kujilimbikizia mali hivi

Anonymous said...

Inavyoonekana mchangiaji wa kwanza ametumwa na walewale au amejituma mwenyewe kwa kujipendekeza ili dhaifu wenzake wamuone.

Anonymous said...

@ Anonymous June 24, 2012 10:02 PM

Childish way?What was the best way to say truth?Funguka!

Anonymous said...

Kaka mnyika nimekukubali yote uliyoyaandika yanaukweli ndani yake,Na mimi naomba kadi ya uanachama kwasababu chama tawala hakina jipya,japokuwa nilikuwa mpigakura na mfuasi wa chadema sasa nataka kuwa mwanachama nipo Kilombero-Ifakara

Anonymous said...

Tungeyajua wapi yote haya,wakati hiyo katiba itumikayo sasa tumeanza kuwa kuisoma juzi tu baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza.Hivyo kama tunapenda wa-TZ tuendelea mbele tusipuuze michango ya wanaitwa vyama vya upinzani japo sio wapinzani wa maendeleo.Wapinzani wa maendeleo ni hao wanaopitisha bajeti mbovu ili mradi haiathiri maslahi yao binafsi.Hivyo Mh.Mnyika na wapenda maendeleo wengine kazi uzi mabadiliko sio kitu rahisi mtatishwa,mtatukanwa matusi lakini mjue sio ninyi mnaotukanwa bali wananchi waliowachagua.Kuambiwa udhaifu mtu haijarishi ni nani sio tusi ni kukusaidia kujichunguza zaidi.UDHAIFU utabaki kuitwa udhaifu tu hata tungeupaka na rangi za kijani au njano.

Anonymous said...

Tanzania hii tutaikomboa wenyewe,mafisadi watatusumbua kama tutaendekeza udhaifu.mabadiliko yanawezekana, kwani Chadema ilikua na wabunge wangapi b4,vp leo wapo wangapi?hebu tuyaruhusu haya mabadiliko then tuone kama hapatakua na maendeleo.Hongera Mnyika.

Anonymous said...

Ndugu zangu Watanzania,mimi naungana na Mbunge wangu Mh.Mnyika katika mabadiliko ya kikatiba kuhusu Nguvu za Raisi na Nguvu ya Bunge, nilikuwa sifahamu eti Wabunge wakikataa Bajeti eti Bunge linavunjika huu ni udhaifu mkubwa si tu udhaifu wa Raisi bali ni udhaifu wa katiba.Hatuhitaji katiba ya namna hiyo.Hii inamaanisha kwamba Bajeti ata ikiwa ya sh.10,000/= tuikubali tuu kisa eti Bunge litavunjwa.sijawai ona mambo kama haya.Mimi nimeona wazi kumbe Watanzania tunakwamishwa kutokana na mambo kama haya.Nchi haina vipaumbele yaaani tunakwenda twenda tu hatuna mwelekeo.Hivi jamani tujiulize kama unataka kwenda Mbezi shamba toka Ubungo stendi ya mkoa,utaenda kituo cha Ubungo Darajani kupanda gari za Temeke au Mwenge? tunapotea njia Watanzania.ni wakati wa kujua tunaenda wapi sasa la sivyo tunapotea Ndugu Zangu.Mwalimu alisema KIONGOZI ni kama TOCHI anaongoza njia watu wamfuate kama kiongozi anatupoteza huyo ni DHAIFU,tunahitaji watu wanaojua njia watuongoze washike na kuangalia Ramani tunaenda wapi.Mimi sijakata tamaa mimi ni kijana na natumaini nitasaidia Wenzangu tuone tunaenda wapi.Mh.Mnyika tuko pamoja nakuunga mkono Katika mabadiliko ya Kimaendeleo hasa tunahitaji katiba ya Ukweli na Huru.

Unknown said...

Sure, Truth shall set you free!

Anonymous said...

Ndugu yangu Mnyika kweli ulikosea, hatuwezi kuwakosea adabu wakubwa tusiige vitu na kusema ndiyo demokrasia. Leo kwake kesho kwako.

Anonymous said...

kutaja jina la mkuu kwa kukosoa bungeni ni kosa ila kwa kusifia sio kosa!! huu ni unafiki na wale wote wanaoshabikia unafiki huu mwisho wao unakaribia!! wameishiwa na mawazo!! ni hao wanaotengeneza barabara wakati wa mwenge wa uhuru tu!!

Anonymous said...

I believe truth is truth whether you save face or not. The fact is if the president and Kikwete in particular is weak, he is weak. I don't agree with presidency being weak. It's a president who can be weak. So I don't see a problem in context. Those who found it a problem they may agree with me that it is because of "wording"

Anonymous said...

Hoja za Mnyika kumkosea heshima hazifai. Watanzania tunachohitaji ni maendeleo kama Kikwete ni dhaifu, na of course tunajua ni dhaifu, basi ni dhaifu acha wamwambie.
Hatuchagui rais kwa sababu ni mzee au ni mkubwa tunamchagua atatue changamoto zinazolikabili taifa letu. Urais wake kama Kikwetwe na heshima inayoambatana na cheo chake itatokana na jinsi alivyotumikia umma. Mnataka tumuheshimu nduli Iddi Amini kwa sababu alikuwa rais? Tumuheshimu Hiltler kwa sababu alikuwa rais? Kikwete acha udhaifu utumikie taifa letu kama huwezi achia ngazi