Wednesday, March 10, 2010

Maandalizi ya Uandikishaji wa Wapiga Kura Mkoa wa Dar es salaam yaanza na kasoroTAARIFA KWA UMMA: Serikali izingatie Katiba, Sheria na maelekezo katika maandalizi ya uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la Kudumu la wapiga kura katika Mkoa wa Dar salaam. Tarehe 9 Machi 2010 Vyombo vya Habari hususani gazeti la Tanzania Daima vimemnukuu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam William Lukuvi akifungua semina ya uboreshaji wa daftari katika mkoa husika. Aidha katika semina hiyo Lukuvi alitangaza kwamba zoezi la uandikishaji litafanyika katika mkoa wa Dar es salaam kwa ufanisi mkubwa.

CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam tunaungana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam katika kuwahimiza wananchi wote wenye miaka 18 na kuendelea ama ambao watakuwa wamefikisha miaka 18 mwezi Oktoba na wale waliohama makazi yao kujitokeza kujiandikisha wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura utakaofanyika katika mkoa wa Dar es salaam kuanzia tarehe 22 mpaka 27 Machi, 2010.

Hata hivyo CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam hatukubaliani na kauli ya Mkuu wa Mkoa kwamba zoezi hilo litaendeshwa kwa ufanisi kwani tayari ofisi yake imeanza kufanya kasoro katika hatua za mwanzo ambazo kama hazitarekebeshwa kwa haraka zitavuruga zoezi hili muhimu kwa ustawi wa demokrasia katika mkoa wa Dar es salaam na taifa kwa ujumla.

CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalumu Dar es salaam tumeshangazwa na hatua ya uongozi wa Mkoa kuendesha mafunzo ya waandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura bila kuwashirikisha kikamilifu wadau katika maandalizi ya awali kama katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na maelekezo ya uandaaji wa daftari la wapiga kura yanavyoitaka serikali kufuata.

Tunamtaka Mkuu wa Mkoa azingatie kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 74 vifungu vya 14 na 15; maofisa waandikishaji, maofisa waandikishaji wasaidizi na waratibu wa mikoa hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.

Ili kuweza kuzingatia msingi huu wa katiba ya nchi ambayo viongozi walioko madarakani wameapa kuilinda maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu kipengele cha 2.2 na 2.4 yanataka vyama vya siasa vipewe fursa ya kutoa maoni kuhusu waandikishaji kabla ya kuanza kazi yao rasmi ili kuweza kuwawekea mapingamizi wale ambao wamekiuka masharti hayo ya katiba ya nchi.

Kitendo cha Mkuu wa Mkoa William Lukuvi kufungua semina ya mafunzo ya waandikishaji ambao vyama havijapewa fursa ya kuwatolea maoni na kuwawekea mapingamizi kama katiba, sheria na maelekezo yanavyohitaji kinaweza kutafsiriwa kuwa ni kutoa mwanya kwa makada wa chama tawala kuratibu zoezi la uandikishaji jambo ambalo linaweza kuruhusu hujuma za kiuchaguzi wakati wa uandikishaji kama zile zilizojitokeza Visiwani Zanzibar.

Hivyo, tunamtaka Mkuu wa Mkoa William Lukuvi kuwasilisha majina ya waratibu wa uandikishaji wa wapiga wa Mkoa na waandikishaji katika Manispaa/Wilaya mbalimbali kwa vyama vya siasa ili kuweza kuwatolea maoni na mapingamizi kama itahitajika.

Aidha tunamtaka azielekeze Halmashauri za Wilaya za mkoa wa Dar es salaam kufanya vikao rasmi na vyama vya siasa kujadili maandalizi ya mchakato wa uandikishaji kama kipengele cha 7.1 cha Maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi kinavyoeleza. Pia awatake wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwasilisha majina ya waandikishaji wasaidizi ili kuweza kuwatolea maoni na mapingamizi kama itabainika wamekiuka Katiba ya Nchi ibara ya 74(14) na (15).

“Mkuu wa Mkoa Lukuvi azingatie kuwa Tume ya Uchaguzi imetoa maelekezo rasmi kwake ambayo kifungu cha 7.2 kinaelekeza kuwa vyama vya siasa vyote vyenye usajili wa kudumu vina haki na wajibu katika mchakato mzima wa uandikishaji wa wapiga kura ikiwemo kuwahamasisha raia wenye sifa kujiandikisha, kusahihisha taarifa na kukagua daftari husika. Hivyo, tunamtaka Mkuu wa Mkoa azingatie Katiba, Sheria, Maelekezo na misingi ya kidemokrasia kama kweli anataka zoezi liwe huru na lenye ufanisi”.

Imetolewa tarehe 10 Machi, 2010:John Mnyika-0754694553; mnyika@chadema.or.tz
Mwenyekiti wa Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum (CHADEMA)
Na Mwakilishi wa wenyeviti wa mikoa ya Kinondoni, Temeke na Ilala- Kanda Maalum ya Kichama Dar es salaam.


No comments: