HATIMAYE Mkurugenzi wa Mambo ya Nchi za Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amepitishwa kuwania ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa kupata ushindi wa asilimia mia moja kwenye kura za maoni.
Kwa mujibu wa matokeo ya kura za maoni za CHADEMA katika Jimbo la Ubungo yaliyotolewa na Nassor Balozi, Mnyika aliyekuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo alipata kura za ndiyo 62 zilizopigwa na wajumbe wote 62 waliohudhuria mkutano mkuu wa jimbo hilo.
“Mkutano mkuu umepiga kura za ndiyo na hapana na kati ya wajumbe 62 wote wamepiga ndiyo, hakuna hapana, hakuna iliyoharibika. Hivyo John Mnyika amepitishwa na kura hizo za uteuzi kwa asilimia 100,” alisema Balozi.
Wajumbe wa mkutano huo walikuwa ni wenyeviti na makatibu wote wa CHADEMA Jimbo la Ubungo.
Aidha, mkutano huo pia ulishirikisha wageni waalikwa 60 ambao ni wawakilishi wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu vilivyomo ndani ya Jimbo la Ubungo pamoja na wawakilishi wa matawi ya chama hicho Jimbo la Ubungo.
Akizungumza baada ya matokeo hayo, Mnyika alisema alitarajiwa kupitishwa kugombea ubunge na mkutano huo lakini hakutegemea kupitishwa kwa asilimia 100 kama ilivyotokea na kuielezea hali hiyo kuwa ni kielelezo cha CHADEMA kuwa moja zaidi ndani ya jimbo hilo.
“Kwa matokeo hayo wamenipa changamoto kubwa, lakini pia ni changamoto kwao katika kuhakikisha wanaitekeleza imani yao kwangu kwa vitendo kwa kushiriki kikamilifu katika harakati zote za kutupatia ushindi,” alisema Mnyika.
Mnyika anayewania ubunge wa jimbo hilo kwa mara ya pili baada ya kudaiwa kushindwa kwa mizengwe katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alisema vipaumbele vyake ni kupigania ajira na maslahi ya wafanyakazi, miundombinu bora ya maji, barabara na makazi, kuchochea uwajibikaji wa watendaji wa serikali, idara na mamlaka zake pamoja na kufanikisha upatikanaji wa huduma bora za afya ndani ya jimbo hilo.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima-26/07/2010
No comments:
Post a Comment