Monday, March 28, 2011

Mbunge Awasilisha Hoja Binafsi Kuhusu Uvamizi wa viwanja vya Wazi

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amewasilisha hoja binafsi kuhusu uuzwaji/uvamizi wa viwanja vya umma maarufu kama viwanja vya wazi kwenye baadhi ya kata za jimbo hilo katika manispaa ya Kinondoni.

Mnyika amewasilisha hoja hiyo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Rafael Ndunguru tarehe 21 Machi 2011 kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano ujao wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni wabunge ni wajumbe wa mabaraza ya madiwani ya halmashauri wanazotoka, hivyo Mnyika kwa nafasi yake ya mbunge wa jimbo la Ubungo ni mjumbe wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Mnyika amewasilisha hoja binafsi hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 19 ya Kanuni za kudumu za Halmashauri na kanuni nyingine husika.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 mpaka 2010 pamekuwepo malalamiko mbalimbali ya wananchi kuhusu uvamizi ama uuzwaji wa viwanja vya umma maarufu kama viwanja vya wazi katika maeneo ya kata mbalimbali za jimbo la Ubungo.

Kutokana na malalamiko hayo Mnyika na viongozi wengine wamekuwa wakitoa shinikizo kwa serikali kuweza kuchukua hatua za haraka ikiwemo kwa kuweka hadharani baadhi ya taarifa za uuzwaji ama uvamizi wa viwanja vya umma.

Kutokana na msukumo huo wa umma tarehe 24 May 2010 Rais Jakaya Kikwete wakati akifanya majumuisho ya ziara ya kukagua hali ya maji katika mkoa wa Dar es Salaam alikiri kuwa yapo maeneo mengi ya wazi yaliyovamiwa na kuwa madiwani wanahusika na sakata hilo.

Kufuatia kauli hiyo ya Rais na malalamiko ya umma aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati huo William Lukuvi alitembelea Manispaa ya Kinondoni tarehe 15 Juni 2010 na kubaini mapungufu kadhaa ya kiutendaji kuhusiana na masuala ya ugawaji wa ardhi yakiwemo maeneo ya umma yaliyozoeleka kuitwa viwanja vya wazi.

Baada ya ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliunda kamati maalumu tarehe 18 Juni 2010 ya kuchunguza maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa katika mkoa wa Dar es Salaam.

Taarifa ya tume hiyo ilibaini kuwa Manispaa ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na maeneo mengi ya wazi yaliyovamiwa. Maeneo hayo yanahusisha pia viwanja vya wazi katika kata mbalimbali za jimbo la Ubungo ambalo lakini ripoti kamili haijawahi kuwekwa hadharani isipokuwa Mkuu wa Mkoa alitoa tu muktasari wa baadhi ya mambo katika ripoti hiyo; ripoti nzima kwa ujumla wake imefanywa kuwa siri mpaka hivi sasa.

Katika hoja yake Mbunge Mnyika ameelezea kwa kina aina ya uvamizi au uuzwaji wa viwanja vya wazi na kutaka hatua mahususi za kuchukuliwa ambazo ataziweka hadharani wakati wa kuwasilishwa kwa hoja hiyo.

Baadhi ya Viwanja ya wazi/umma ambavyo vimevamiwa au kuuzwa kinyemela katika kata za jimbo la Ubungo ni pamoja Kiwanja Na. 1022 Kitalu E Sinza; Eneo karibu na kiwanja Na. 636 Kitalu E Sinza; Kiwanja Na. 814, 818 Sinza Block D; Eneo jirani na viwanja Na. 75 na 77 Sinza Block D; Eneo lililopo mkabala na kiwanja Na. 475 Sinza B Eneo karibu na kiwanja Na. 23 Sinza C; Eneo karibu na kiwanja Na. 24 Sinza C; Eneo karibu Na. 765, 789, 790, na 797 Sinza C; Eneo la wazi lililozungukwa na viwanja Na. 21, 23, 25, 27, 29 Sinza B; Eneo la wazi lililozungukwa na viwanja Na.72-74.; Eneo la wazi linalozungukwa na viwanja Na. 1, 2, 89, 90, 141 na 142 Sinza E; Eneo la kiwanja cha michezo na Shule ya Msingi Sinza E; Eneo la wazi jirani na viwanja Na. 77, 79, 81, 151-154; Viwanja Na. 9 na 10 Sinza A; Kiwanja Na. 846 Sinza A. ; Jirani na viwanja Na. 18 na 19 Mtaa wa Malala Makurumla; Jirani na viwanja Na. 73, 78, 80, 82, 84 na 86 Mtaa wa Mengo Makurumla; Eneo la wazi lililopo Mtaa wa Kagera Makurumla ; Eneo la wazi nyuma ya Ubungo terminal (“buffer zone” ya reli); Eneo lipo jirani na kiwanja Na. 148; Nyuma ya jengo la RUBADA na viwanja vingine vya kata zingine za jimbo la Ubungo kwa kadiri ya ripoti ya Kamati/Tume iliyoundwa na Mkoa wa Dar es salaam na taarifa za nyingine.

Itakumbukwa kwamba Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alishiriki ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka na viongozi na watendaji wa mkoa wa Dar es salaam iliyofanyika tarehe 14 Disemba 2010.

Mnyika alishiriki ziara hiyo kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuhakikisha maeneo ya matumizi ya umma (ambayo yamezoeleka kuitwa viwanja vya wazi )yanalindwa na kuendelezwa.
Katika ziara hiyo Mnyika alimpongeza Waziri kwa kuamua kuanza kulifuatilia suala la viwanja vya umma vilivyovamiwa ama kuuzwa kinyemela kwa kuwa ni ajenda ambayo hata yeye kama mbunge wananchi wa jimbo lake la Ubungo walimtuma kuisimamia.

Mnyika alitoa mwito kwa Wizara husika na mamlaka za Mkoa wa Dar es salaam kuiweka wazi ripoti ya tume iliyoundwa mwaka huu kuchunguza kuhusu maeneo ya wazi (maarufu kama Tume ya Lukuvi) ambayo mpaka sasa imegongwa muhuri wa siri.

“Ripoti hiyo ikiwekwa wazi, hatua stahili zinaweza kuchukuliwa kwa haraka zaidi kurejesha maeneo husika kwa matumizi ya umma na kuchukua hatua kwa wote waliotoa vibali vya ujenzi kinyemela ama hati za viwanja kinyemela na kuuza viwanja husika katika mazingira yenye tuhuma za ufisadi”.

Aidha Mnyika alimuomba Waziri wa Ardhi kutembelea pia viwanja vya umma vilivyovamiwa katika jimbo la Ubungo kwenye kata ya Sinza, Makurumla pamoja na maeneo yenye migogoro ya ardhi ili hatua za haraka zaidi ziweze kuchukuliwa. Waziri alikubali ombi hilo na kuahidi kutembelea maeneo husika katika ziara zake za baadaye.

Siku hiyo hiyo ya tarehe 21 Machi 2011 wakati Mnyika akiwasilisha hoja binafsi kwa mkurugenzi kuhusu viwanja vya umma kwa upande mwingine Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka amemuomba Rais Jakaya Kikwete wakati alipotembelea Wizara yake kumkingia kifua katika kurejesha viwanja vilivyoporwa.

Saturday, March 26, 2011

MBUNGE AELEZWA CHANZO CHA WIZI KUIBUKA TENA KATIKA ENEO LA UBUNGO MATAA

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ameelezwa chanzo cha kuibuka tena kwa wimbi la wizi katika eneo la Ubungo mataa linalounganisha barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma.
Mnyika alielezwa hayo na Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob alipomuita ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo jana (24 Machi 2011) kueleza sababu za kuibuka tena kwa vibaka na waporaji kwenye eneo hilo katika siku za karibuni ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Awali Mnyika aliumueleza Diwani kuwa katika kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwezi Februari na mpaka mwezi Machi amepokea malalamiko toka kwa wananchi wenye magari na wanaotembea kwa miguu katika maeneo hayo kuporwa mali zao katika eneo hilo ambalo vitendo hivyo vilidhibitiwa mwanzoni mwa mwaka 2011 kutokana na ulinzi shirikishi.

Itakumbukwa kwamba katika kipindi cha miaka iliyopita palikuwa na wimbi kubwa la wizi katika eneo hilo ambavyo vilidhibitiwa kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010 na mwanzoni mwa mwaka 2011 baada ya kutokea kwa mabadiliko katika kimkakati katika jeshi la polisi na kiungozi wa kisiasa na hivyo kufanya suala la usalama katika eneo hilo kupewa kipaumbele cha ziada.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi Kamanda wa Kanda Maalum wa Mkoa wa Dar es salaam Seleman Kova na Kamanda mpya wa polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela waliweka mkazo kwenye ulinzi shiriki ukiungwa mkono na Diwani mpya wa kata ya Ubungo Boniface Jacob na mbunge wa jimbo hilo.

Kama sehemu ya hatua zilizochukuliwa paliundwa kikundi cha vijana wa ulinzi shirikishi ambacho kilipatiwa vifaa na wadau na kuanza kazi ya kushirikiana na jeshi la polisi na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya wizi katika eneo hilo hususani katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Februari 2011.

Diwani Boniface Jacob alimueleza mbunge kwamba chanzo cha kuibuka kwa hali hiyo ni vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari polisi wasiowaaminifu ambao kwa miaka kadhaa walikuwa wakishirikiana na wezi kuanza tena kuuhujumu mfumo wa ulinzi shirikishi uliowekwa kwa kuwakamata vijana ambao walikuwa wakifanya ulinzi katika eneo hilo na hivyo kuwaacha vibaka na waporaji kurejea katika eneo hilo kwa kuwa wanahongwa mgawo.

Mnyika alimuelekeza Diwani kukutana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela kumweleza kwa kina suala hilo hili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa na jeshi hilo kuhakikisha usalama wa raia katika eneo hilo hususani nyakati za jioni.

“ Kwa kuwa sasa niko katika jukumu la kuwawakilisha wananchi kwenye vikao vya kamati ya nishati na madini ya bunge vinavyoendelea hivi sasa, niwakilishe katika kukutana na uongozi wa jeshi la polisi. Na usisite kuwataja kwa majina askari wanaotuhumiwa kushirikiana na wezi toka maeneo ya nje ya kata ya Ubungo kuja kufanya wizi katika eneo letu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kulinda usalama wa wananchi na mali zao”, Alisema Mnyika.

Tuesday, March 22, 2011

Wananchi kuandamana kuhusu bomoa bomoa Ubungo

LICHA ya Rais Jakaya Kikwete kuwaonya viongozi wa Chadema kwa kuandaa maandamano na kupandikiza kile alichoita mbegu mbaya za chuki dhidi ya serikali, Chama hicho kipo katika harakati za kuongoza maandamano mengine, jijini Dar es Salaam.Hayo yatakuwa maandamano ya tatu kufanywa na Chadema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba Mwaka jana.

Maandamano ya kwanza yalifanyika mkoani Arusha kupinga uchaguzi wa Meya wa jiji hilo na maandamano mengine yakafanyika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.Maandamano ya Dar es Salaam ambayo Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Chadema) amethibitisha kuyaongoza, yatafanywa na wananchi wanaoishi kando ya barabara ya Morogoro, kuanzia eneo la Ubungo mpaka Kimara ambao nyumba zao zipo katika mpango wa kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo.

“Mmesema mmemwandikia barua Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Ujenzi, Mkurugenzi wa jiji na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni kuomba msaada na kukutana nao lakini hamjajibiwa lolote,” alisema MnyikaAliongeza, “Kama ni hivyo pitisheni azimio ili serikali itoe ufafanuzi wa sakata hili. Wapeni siku saba ili wawajibu, wakishindwa kufanya hivyo, itabidi mwende kwa Waziri Mkuu mkamweleze matatizo haya, mtaniambia tu ni lini, mimi pia nitashiriki.

”Mnyika alisema kama mwakilishi wa wananchi bungeni na kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63 (2), kama sakata hilo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi, atalipeleka bungeni ili lijadiliwe.“Kwanza naweza kuliuliza kama swali la papo kwa papo, ikishindikana nitalichangia katika hoja mbalimbali, pia hiyo ikishindikana nitalipeleka suala hili kama hoja binafsi,”alisema Mnyika.Aliongeza, “Ila njia nzuri kwangu ni kulipeleka suala hili kama ombi, tena sio langu bali ni ombi la wananchi. Hili litakwenda bungeni kama hoja ya wananchi.

”Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya waathirika wa bomoa bomoa hiyo ambao wamepewa siku 60 wawe wameondoka maeneo hayo, Naomi Alimanoti alipitisha azimio hilo na kuongeza kuwa wanaipa serikali siku saba zinazoanzia kesho.“Tutakutana Jumamosi ijayo, pale pale katika eneo letu la siku zote ili kuona kama tumejibiwa ama laa. Kama tutakuwa hatutajibiwa tutaandamana hilo halina mjadala. Hapa mpaka kieleweke, hatuwezi kuvunjiwa nyumba zetu wakati tuna hati halali na sheria inatulinda,” alisema Alimanoti.

Awali Mnyika alisema kuwa propaganda zinazoenezwa kwamba Chadema wanapinga mikakati mbalimbali ya maendeleo si za kweli bali maendeleo hayo yanatakiwa kufanywa bila kukiuka sheria na haki.“Iweje mwaka 1973 katika ubomoaji wa nyumba katika barabara hii watu walipwe, lakini hivi sasa watu hawa waambiwe kuwa wamevamia eneo la hifadhi ya barabara,” alihoji Mnyika.Kwa mujibu wa Mnyika, katika eneo hilo kuna nyumba ambazo zitaathirika kutokana na mradi wa mabasi yaendayo kasi (DAT) hivyo akatoa wito kwa serikali kumjibu kimaandishi juu ya miradi yote ya barabara katika eneo hilo kwa kuwa inawezekana wanaobomolewa nyumba zao wakati eneo lenyewe halihusiki na mradi wowote.

“Kwa tafsiri ya serikali, wananchi walioko katika eneo la barabara hii hawatalipwa fidia, mwaka 1997 mpaka 2001 watu walivunjiwa na hawakulipwa kwa maelezo kwamba wote walilipwa mwaka 1973,” alisema Mnyika.Alifafanua kuwa serikali inatakiwa kutorudia makosa ya mwaka 1997, ambapo wakimbizi wa Tanzania walihifadhiwa ndani ya nchi yao wenyewe.

“Waliovunjiwa kipindi hicho walihifadhiwa katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, serikali isipokuwa makini itatengeneza mazingira ya mwaka 1997. Katika hili hauwezi kukaa kimya, tena bomoa bomoa hii si Kimara ni karibu mikoa yote nchini,”alisema Mnyika.

Mnyika aliwataka wananchi hao kujiorodhesha ikiwa ni pamoja na kuwa na vielelezo vyao vyote kwa kuwa kati yao wapo waliovamia na wapo walio na umiliki halali wa maeneo hayo.Alisema wanatakiwa kuwa na jopo la mawakili watakaowasimamia katika kesi ambayo wataifungua kama hatua zote watakazozichukua zitagonga mwamba pamoja na kuandaa utaratibu wa kufanya uthamini wa nyumba zao kabla hazijavunjwa.

Mnyika aliendelea kueleza kuwa jambo lolote linapotokea kabla ya kuanza kulizungumza, inatakiwa ufanyike uchunguzi na kusisitiza kuwa ilitakiwa uchunguzwe uhalali wa wananchi wa Kimara kudai haki zao kwanza kuliko kuanza kuwashutumu kuwa wanapinga maendeleo.“Huu si wakati wa serikali kuendeshwa kwa shinikizo.

Ni wakati wa kuchunguza na kujua ukweli. Hatua yoyote itakayochukuliwa na wananchi hawa itakuwa ya kidemokrasia,”alisema Mnyika.Mmoja wa wananchi hao, Charles Mwandembwa alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete anatakiwa kuwa makini, kwa kuwa wanaomwangusha ni watendaji wake ambao wamekuwa waking’ang’ania kuwaondoa wananchi wa Kimara ili wao wamiliki ardhi.

Naye Joshua Mlekani alisema wanatakiwa kuweka kutafuta zuio la Mahakama ili ubomoaji wa nyumba katika eneo hilo, usitishwe kwa muda ili wapate nafasi ya kufuatilia haki zao.Mwisho


Chanzo: Mwananchi-6/3/2011

Serikali itoe kauli katika wiki ya maji

Tarehe 22 Machi 2011 ni kilele cha wiki ya taifa ya maji ambayo pia ni siku ya kimataifa ya maji ambapo ujumbe wa mwaka huu ni “Maji kwa ajili ya Miji: Kukabiliana na changamoto mbalimbali mijini”.

Maadhimisho ya mwaka huu kwa ngazi ya Mkoa wa Dar es salaam yatafanyika katika kata ya Mburahati ndani ya Jimbo la Ubungo katika Manispaa ya Kinondoni.
Pamoja na kushiriki katika uzinduzi wa miradi ya maji, nitatumia siku hiyo kuendelea kufanya ufuatiliaji na kuisimamia serikali ili kuweza kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya sekta husika.

Nakubaliana na uamuzi wa serikali uliofanyika mwezi Machi wa kuweka programu maalumu ya kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi na maji taka katika mkoa wa Dar es salaam kama moja ya vipaumbele katika muongozo wa bajeti ya mwaka 2011/12 kuwa kuwa umeendana na mwito ambao tuliutoa katika Kongamano la Maji Jimbo la Ubungo lililofanyika tarehe 31 Januari 2011.

Aidha nakubaliana na uamuzi wa serikali wa kutaka kutenga bilioni 654 kwa ajili ya kuteleza mpango husika huku asilimia 80 za fedha hizo zikipangwa kutoka kwenye vyanzo vya ndani; hata hivyo uamuzi huo utakuwa wa maana ukianza kutekelezwa kwa ukamilifu kuanzia mwaka huu wa fedha. Uchimbaji wa Visima virefu Kimbiji na Mpera na ujenzi wa bwawa la Kidunda pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Ruvu juu na Ruvu chini ni mipango inayopaswa kuungwa mkono na kufuatiliwa kwa karibu na kila mpenda maendeleo.
Hatahivyo, siridhishwi na viwango na kasi ya utekelezaji wa mipango husika. Kati ya mwaka 2005 mpaka 2010 kiwango cha fedha ambacho kimetumiwa na DAWASA/DAWASCO na mamlaka zingine kutokana na fedha za umma ikiwemo mikopo toka kwa washirika wa kimaendeleo hakilingani na ubora wa miundombinu na huduma inayopatikana; hivyo mifumo thabiti ya usimamizi na ukaguzi inahitajika ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
Natoa mwito kwa mamlaka mbalimbali za kiserikali kutumia kilele cha siku ya maji kutoa taarifa za kina zaidi kwa umma kuhusu utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi wa mkoa wa Dar es salaam hususani wa jimbo la Ubungo.

Mathalani akihutubia Bunge mwezi Juni mwaka 2010 wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka wa fedha 2010/11 Waziri Mark Mwandosya aliahidi kwamba usanifu wa bwawa la Kidunda linatarajiwa kutoa mchango mkubwa wa utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi wa Ubungo ungekamilika mwezi Septemba mwaka huo wa 2010; lakini mwezi Machi mwaka huu Waziri ametoa kauli tofauti kuwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bwawa hilo utakamilika mwezi Juni mwaka 2011 na ujenzi mwaka 2013. Natoa mwito kwa Waziri Mwandosya kueleza wananchi wa Ubungo na watanzania kwa ujumla sababu za kuchelewa kwa mpango huo na mikakati iliyopo ya kuhakikisha bwawa husika linajengwa mapema zaidi ya muda uliotangazwa.

Aidha wakati hatua hizi za muda mrefu zinaendelea kutekelezwa ni muhimu kwa DAWASA, DAWASCO, Manispaa na Wizara husika kuongeza kasi ya kuchukua hatua za muda mfupi za kupunguza kero ya maji kwa kutimiza wajibu ipasavyo.

Mfano mwezi Mei mwaka 2010 Rais Jakaya Kikwete alifanya ziara katika jimbo la Ubungo kata za Mburahati na Kimara eneo la Mavurunza na kuahidi idadi maalum ya visima ambavyo serikali imengevichimba lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatimizwa kwa ukamilifu wake katika muda ambao uliahidiwa. Hivyo, kupitia siku hii ya maji ni muhimu kwa Rais Kikwete au wasaidizi wake kutoa kauli kuhusu utekelezaji wa ahadi husika ama sivyo itabidi tuunganishe nguvu ya umma katika kuchukua hatua za ziada kukabiliana na kero husika ambayo inawasumbua wananchi miaka 50 baada ya uhuru wa nchi yetu.

Kadhalika, upungufu wa maji unachangiwa pia na upotevu wa maji uliopo sasa wa karibu asimilia hamsini (50%) ambao unaambatana na hujuma mbalimbali katika ratiba za mgawo wa maji katika baadhi ya maeneo. Katika kikao cha saba tarehe 18 Februari 2011 niliuliza Swali la Nyongeza kutokana na majibu ya Swali namba 85 kwa Wizara ya Maji. Kwenye swali langu la Nyongeza kuwa pamoja na uwekezaji wa fedha za miradi ya maji za Benki ya Dunia na Wadau wengine wa maendeleo kwenye Ruvu Juu na Ruvu chini ikiwemo kuweka mtandao mpya wa mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya wachina; bado maji kwenye kata za Kwembe, Kibamba, Msigani, Mbezi, Saranga, Kimara nk maji hayatoki kwa pamoja na mambo mengine upotevu wa maji na wafanyabiashara wanauza maji bei juu kujiunganishia kinyemela; je Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa? Naibu Waziri alijibu kwa kunipongeza kwa kuweka kipaumbele cha kwanza suala la maji katika kazi zangu na kuahidi kutembelea miundombinu husika. Hata hivyo, ziara ya kutembelea miundombinu husika katika maeneo ambayo wananchi wametoa tuhuma mbalimbali bado haijafanyika. Natoa mwito kwa Wizara husika ambayo ofisi zake zipo ndani ya Jimbo la Ubungo, DAWASCO au Kamati husika ya Bunge kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya maji ambao ujumbe wake mwaka huu ni muhususi kwa mijini kutembelea maeneo husika na kuchukua hatua ili maadhimisho ya mwaka huu yaweze kuchukua sura tofauti kwa kushughulikia kero za msingi za wananchi katika sekta ya maji badala ya hotuba za viongozi pekee.

Imetolewa tarehe 20 Machi 2011 na:

John Mnyika
Mbunge wa Ubungo

Friday, March 11, 2011

MNYIKA AANDAA BONANZA LA SOKA KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ameandaa bonanza la soka kwa wanawake katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.

Bonanza hilo la siku mbili litafanyika katika Uwanja wa Santos Barafu kuanzia tarehe 8 Machi mpaka 9 Machi mwaka 2011.

Bonanza hilo litashirikisha jumla ya timu nne za wanawake; tatu za wanawake katika jimbo la Ubungo za Mlimani, Mburahati na Uzuri pamoja na timu mwalikwa ya Tanzanite toka jimbo la Kinondoni.

Wabunge wanawake wa viti maalum wa CCM na CHADEMA toka manispaa ya Kinondoni na madiwani wa viti maalum jimbo la Ubungo wamealikwa kuwa wageni rasmi kwenye mechi za ufunguzi wa Bonanza hilo wakati mbunge wa Jimbo hilo, John Mnyika atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha bonanza hilo.

Izingatiwe kuwa tarehe 8 Machi ni siku ya Wanawake Duniani ambayo kwa mwaka huu ujumbe wake kimataifa ni “Fursa sawa ya elimu na teknolojia ni njia ya ajira bora kwa wanawake”.

Ni muhimu kwa vijana wa kike, wanawake na mashabiki wengine wa soka kujitokeza katika bonanza hilo ambalo halitakuwa na kiingilio chochote ambalo litafanyika kwenye uwanja huo wa wazi uliopo katika kata ya mburahati.

Mechi za Bonanza hilo zitatoa fursa ya kufikisha ujumbe kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa wanawake hasa katika wakati huu ambao dunia inaadhimisha miaka mia moja toka kuanza kwa siku hiyo ya wanawake mnamo mwaka 1911.

Thursday, March 3, 2011

TAMKO LA AWALI KUHUSU KUBOMOLEWA KWA SOKO LA URAFIKI

Tarehe 2 Machi 2011 nikiwa mkoani Kagera kwenye maandamano ya kitaifa ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha, kupanda kwa bei na mgawo wa umeme, , kutaka uchaguzi wa Meya wa Arusha, kutaka waziri wa ulinzi awajibike kutokana na milipuko na mabomu ya Gongo la Mboto na kupinga malipo ya fidia kwa kampuni ya Dowans yenye mitambo yake katika jimbo la Ubungo- masuala ambayo yanagusa maisha ya watanzania wakiwemo wakazi wenzangu wa jimbo la Ubungo; nimepokea taarifa za kuvunjwa kwa Soko la Wafanyabiashara wa mitumba Urafiki maarufu kama “Big Brother” usiku wa kati ya saa 6 na 7 wa kuamkia siku hiyo.

Awali ya yote ieleweke wazi kuwa kwa nafasi ya yangu ya ubunge wa Ubungo naunga mkono uamuzi wa upanuzi wa Barabara ya Morogoro kwa ajili ya njia ya mabasi ya haraka mkoani Dar es salaam (DART) kwa kuwa ni kati ya masuala ambayo niliyaweka mstari wa mbele kwenye miundombinu na kwa miaka kadhaa nimekuwa nikiilaumu serikali kwa uzembe wa kuchelewesha utekelezaji wa mradi husika.

Hata hivyo, nalaani hatua ya serikali kutokuwa makini katika utendaji wake kwenye utekelezaji wa miradi na hatimaye kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima na madhara katika mali za watu kama ilivyokuwa kwenye uvunjaji wa soko la mitumba la Urafiki maarufu kama Big Brother.

Ni muhimu umma wa watanzania ukafahamu kuwa wafanyabiashara wa eneo la Urafiki Big Brother hawakuvamia eneo husika bali walihamishiwa na manispaa ya Kinondoni toka eneo la Manzese Darajani na kutengewa eneo husika kwa ajili ya mabanda yao ya biashara ya mitumba. Hivyo, uamuzi wowote wa kuwahamisha ulipaswa kuambatana na maandalizi thabiti ya eneo mbadala la kufanyia biashara zao ama sivyo serikali inakuwa imeingia katika kashfa ya kuondoa watu wake kwa ajira zao bila sababu za msingi.

Pia, serikali makini inapaswa kutoa taarifa za ukweli na kwa wakati kwa wananchi wake katika hatua zote za utekelezaji wa miradi katika masuala yanayowagusa wananchi. Kimsingi, katika suala la uvunjaji wa soko la Mitumba la Urafiki maarufu kama Big Brother serikali imeshiriki kutoa taarifa za uongo kwa wananchi na pia waliotumwa kutekeleza zoezi husika wanatuhumiwa kufanya wizi. Pia, hatua za kuwaondoa kwa notisi ya siku chache ni kuweka mazingira ya hasara na kuwakosesha ajira na hivyo kuchangia katika kuongeza umasikini hususani kwa wanawake na vijana.

Ni muhimu wananchi wakafahamu kwamba tarehe 1 Februari mwaka 2011 tulifanya ziara ya kukagua miradi ya Barabara mkoani Dar es salaam na kati ya miradi ambayo tuliikagua ni ya Barabara hiyo ya Morogoro kuhusiana na mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) na kati ya maeneo tuliyotembelea ni hilo la soko la mitumba Urafiki maarufu kama Big Brother.

Tukiwa kwenye eneo hilo mbele ya baadhi ya wafanyabiashara hao ndogondogo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Soko hilo Iddi Toatoa maofisa wa mradi wa mabasi ya haraka (DART) waliulizwa kwa mujibu wa mipango ya mradi wao ni jambo gani linahitajika kufanyika katika eneo hilo ili mradi utekelezwe kwa haraka. Ilielezwa kwamba kinachohitajika ni kusogezwa kwa nguzo moja ya umeme ambayo itahusishwa kuondolewa kwa muda kwa vibanda vichache kuwezesha nguzo hiyo kuhamishwa na kwamba biashara ya mitumba katika eneo hilo ingeendelea kama kawaida.

Maelezo hayo yalitolewa mbele ya Afisa Tawala wa Manispaa ya Kinondoni Ndugu Benard ambaye alikuwa akimwakilisha mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana na mbele yangu pamoja na maofisa wengine wa mamlaka mbalimbali wakiwakilisha manispaa, wakala wa barabara (TANROADS).

Katika mazungumzo hayo ilielezwa kwamba Afisa Tawala Manispaa ya Kinondoni atatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya na pia Mkurugenzi wa Manispaa ili hatimaye manispaa ambayo ndiyo wameingia makubaliano na wafanyabiashara wa eneo husika kuweza kufanya taratibu ili kazi husika iweze kufanyika.

Taarifa hiyo ya ukaguzi wa miradi ikiwemo kuhusu eneo husika ilitolewa kwenye kikao cha bodi ya barabara cha tarehe 2 Februari 2011 ambacho mimi ni mjumbe. Katika vikao hivyo, hakukutolewa maelezo ya kwamba soko zima litavunjwa badala yake kilichoelezwa ni uhamishaji wa nguzo. Na wakati wote manispaa imekuwa ikisisiza kwamba kwa wafanyabiashara wataothirika watapatiwa maeneo mbadala ya kufanyia biashara zao.

Toka tarehe hiyo, serikali haikutangaza kwa umma hatua mbadala na kuwezesha wafanyabiashara hao kwenda maeneo mbadala mpaka nilipotaarifiwa siku ya tarehe 2 Machi 2011 baada ya kuvunjiwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni alitoa ilani yenye tarehe 14 Februari 2011 iliyosainiwa kwa niaba yake na L.B.KIMOI kuwataarifu watu wote waliojenga mabanda yao yaliyopo ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro kwenye soko la mitumba la Urafiki kuwa wabomoe na kuondoa mali zao kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe ya ilani tajwa; kwa wengi wa wafanyabiashara hao ilani hiyo ilifika ikiwa imechelewa. Nimeelezwa kwamba kutokana na kuchelewa huko wafanyabiashara hao waliuandikia barua mkurugenzi wa manispaa ya tarehe 1 Machi 2011 wakiomba kupatiwa maeneo mbadala ili waweze kuhamia huko.

Wakati hatua hizo zikiendelea usiku wa siku hiyo hiyo ndipo uvunjaji ukafanyika ambapo wafanyabiashara wanatuhumu kuharibiwa na kuibiwa mali zao na mgambo wa manispaa ambao ndio waliotumwa kutekeleza zoezi husika.

Kutokana na hali hiyo kupitia taarifa hii ya awali natoa matamko yafuatayo:
Mosi; Serikali ikutane na wafanyabiashara hao walioathirika kubaini athari walizozipata na kuwapatia eneo mbadala la biashara kwa kushughulikia mapendekezo yaliyoko kwenye barua yao ya tarehe 1 Machi 2011 ambayo baadhi yake yako ndani kabisa ya uwezo wa manispaa.

Pili; Manispaa ifanye uchunguzi kuhusu vitendo vya uwizi vinavyoelezwa kufanywa na mgambo waliotuma kufanya zoezi husika na kueleza sababu za zoezi hilo kufanyika usiku. Serikali inastahili kuchukua hatua na kutoa fidia ya uwizi huo.

Nne; tarehe 2 Machi 2011 baada ya tukio hilo nilimtuma Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob kufanya mazungumzo ya awali na wafanyabiashara husika pamoja na kuhamasisha utulivu wakati hatua zikiendelea kuchukuliwa, kati ya mambo ambayo yalijitokeza katika mazungumzo yao ni hoja ya wafanyabiashara kutaka kufanya maandamano na haja ya kuchukua hatua za kisheria. Nimepokea mapendekezo hayo na tutafanya maamuzi ya pamoja nikirejea.

Tatu; Katika muktadha huo naitisha Mkutano na wafanyabiashara husika pamoja na watanzania wengine ambao wanatarajiwa kuathiriwa na upanuzi wa barabara ya Morogoro kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) ili kupeana taarifa na kukubaliana kuchukua hatua mbalimbali. Mkutano huo utafanyika eneo la Kimara Baruti uwanja wa Central kuanzia saa 4 asubuhi mpaka saa 7 Mchana siku ya jumamosi ya tarehe 5 Machi 2011 ambapo nitakuwa nimerejea jimboni Ubungo. Tamko langu kamili nitalitoa baada ya mkutano huo.

Iwapo Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni hawatatoa taarifa ya kujitosheleza kuhusu suala husika ikiwemo kukutana na waathirika wa bomoa bomoa hiyo kabla au kupitia mkutano huo basi tutajibika kupeleka suala husika kwa mamlaka ya juu zaidi katika hatua ya sasa ikiwa ni kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye pia ni msimamizi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuunganisha nguvu ya umma ili suluhisho la mapema liweze kupatikana.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika
Mbunge-Jimbo la Ubungo
03/03/2011-Kagera

Tuesday, March 1, 2011

Taarifa ya Mkutano wa Mbunge na Wananchi Goba

TAARIFA YA MKUTANO WA MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO NA WANANCHI W A KATA YA GOBA TAREHE 27/02/2011.

Utangulizi
Mnamo tarehe 07/02/2011 Mbunge wa Jimbo la uchaguzi Ubungo aliziandikia mamlaka za kiserikali barua yenye kumb: OMU/UW/002/2011 kutoa taarifa kuwa atakuwa na mkutano wa hadhara wa kiserikali katika kata ya Goba eneo la Mwembemadole tarehe 27/02/2011 kuanzia saa tisa alasiri hadi saa kumi na mbili jioni.

Lengo la mkutano tajwa lilikuwa kuzungumza na wananchi kuhusu mambo mabalimbali ya kimaendeleo hususani sekta za Maji, Ardhi, Umeme, Barabara pamoja na ulinzi na usalama.

Mkutano huo ulifanyika kama ulivyokuwa umepangwa na kuhudhuriwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Goba, Diwani wa Kata ya Goba, Diwani wa viti maalumu wa Kata ya Goba pamoja na mwenyekiti wa mtaa wa Goba.

Ufunguzi
Afisa Mtendaji wa Kata ya Goba alifungua mkutano saa 9:25 alasiri na kumkaribisha Diwani wa Kata hiyo Mh. Kisoki ili aweze kutoa nasaha na maelezo kwa ufupi kabla ya kumkaribisha Mbunge. Diwani alitoa maelezo ya awali kama ifuatavyo;
Diwani alimshukuru Mbunge wa kuitisha Mkutano na wananchi ambao ndio mkutano wa kwanza kufanyika kwenye kata ya Goba toka uchaguzi wa mwaka 2010 na kutumia fursa hiyo kumshukuru wananchi kwa kumchagua yeye pamoja na mbunge.
Usafiri; alisema lipo daraja la kuunganisha Goba na Makongo ambapo tayari mkandarasi DEL MONTE amekwisha kuteuliwa ili ujenzi uanze.
Ulinzi na Usalama; wamewasiliana na polisi ili kuwe na uwezekano wa kujenga kituo cha polisi na wakapewa kazi ya kutafuta eneo ili kituo kijengwe. Eneo limepatikana ingawaje nusu ya shamba hilo lina kesi na wanafanya utaratibu wa kuanza kutumia sehemu ambayo haina kesi ili kuanza ujenzi. Alisema pia wanafanya mchakato wa kujenga vituo vidogovidogo ili kuweza kuboresha ulinzi kulingana na jiografia ya eneo la Goba ambayo ni kubwa mno.

Ardhi; alimuomba Mbunge kubeba swala la fidia kwa wananchi kwa wale ambao maeneo yao yanapitiwa na miradi hasa ya barabara kwa sababu swala hilo lineleta migogoro baina ya wananchi na mamlaka za kiserikali. Na pia alimuomba Mbunge kusemea barabara ya Mbezi Luis Tangi Bovu kupitia Goba ijengwe kwa kiwango cha lami. Pia Kata ya Goba ina mapori mengi sana na pindi wananchi wanapotaka kuyatumia wanaambiwa kuwa yanamilikiwa. Hivyo Diwani alimuomba Mbunge kufuatilia hilo ili pale inapowezekana wananchi wajue ni maeneo gani ambayo wanaweza kuyatumia.

Maji; Diwani alitoa taarifa kuwa Kata ya Goba miradi ya maji mitatu na tayari mradi wa Goba-Kisauke umekamilika kwa kuwa tank limeshajengwa na maji yataanza kuingia usiku wa siku hiyo na tatizo lililopo sasa ni miundombinu kwa ajili ya usambazaji. Mradi wa maji Goba alisema wenyewe unaendelea kuhudumia wananchi. Lakini kamati iliyokuwepo ilishamaliza muda wake na ilishindikana kuivunja kutokana na uchaguzi na pia zipo kazi ambazo zilikua hazijakamilika. Alisema kuwa tayari walishawatangazia wananchi kuwa wateue wawakilishi wawili kila mtaa ili waweze kuingia kwenye kamati ya maji kwenye kikao cha tarehe 06/03/2011.

Baada ya maelezo/ taarifa hiyo Diwani alimkaribisha Mbunge, lakini baada ya kuwasalimia wananchi aliomba kwanza isomwe risala ya wananchi ndipo ataweza kuhutubia wananchi katika mkutano huo.

Risala ya wananchi

Risala ya wananchi ilisomwa na Bw. Dickson mbele ya Mbunge, viongozi wengine pamoja na wananchi . Pamoja na mambo mengine risala hiyo ilijikita kwenye kero sugu ya maji ambayo lawama kubwa ilipelekwa kwa kamati ya muda ya mwaka 2007.

Malalamiko ya wananchi kupitia risala yao ni kama ifuatavyo;

Kwamba kuna unyanyasaji katika upatikanaji wa maji kwa kuwa kuna ubaguzi katika mgawanyo wa huduma hii pale inapopatikana na kwa ujumla kuna upendeleo kwa kuwa kuna wafanyabiashara wa matofali wanapata maji ya kumwagilia matofali huku wananchi wakiendelea kutaabika.

Kuhoji utendaji wa kamati ni kikwazo kwa wananchi, hii inatokea pale baadhi ya wananchi kusingiziwa tuhuma za kuweka sumu kwenye maji ya mradi pale wanapojaribu kuhoji utendaji wa kamati ya maji au wanapoikosoa.
Pia wananchi walisema kuwa kamati ya maji iliyopo sio halali kwa kuwa ilikuwa ni kamati ya muda ilipoundwa mwaka 2007 na kuamriwa kutoa ripoti yake kwa wananchi lakini kamati hiyo haikufanya hivyo toka kipindi hicho mpaka leo.

Pia kuna njama kati ya Dawasco na watendaji wa kamati iliyopo katika kudanganya kiwango cha maji ya kinachotumika swala ambalo linafanya kiwango cha maji kinachotumika kwa mujibu wa mita za Dawasco kuwa tofauti na hali halisi ya maji yanayowafikia wananchi na maji wanayotumia.

Pia kamati hii haina akaunti maalumu ya mradi huu kitu ambacho kinafanya Mwenyekiti na Katibu wa mradi huu kuwa na akaunti ya pamoja ambayo siyo ya mradi. Na wananchi wana mashaka na utendaji wa watu hawa.
Mambo mengine yaliyozungumzwa na wananchi katika risala yao ni pamoja na haja ya kuwa na barabara ya kiwango cha lami pamoja na barabara za mitaa na pia walidokeza kuwa swala la salama linahitaji kupewa uzito wa uwajibikaji kwa kuwa katika kayo kuna changamoto nyingi sana za kiusalama.

Pendekezo : Msomaji wa risala alimalizia kwa kusema kuwa umma uliopo katika mkutano huo ndo uamua kuhusu mapendekezo.

Baadhi ya wananchi walitoa maoni yao baada ya risala hiyo kama ifuatavyo;

i. Wananchi wa Goba wawe kitu kimoja katika kutetea maswala mbalimbali ya kimaendeleo na kuzingatia kwa umakini yale yaliyoainishwa kwenye risala hiyo ya wananchi.

ii. Walimuomba Mbunge kushirikiana na wananchi awaongoze ili kuivunja kamati ya maji ya mradi wa maji Goba na kupata kamati nyingine.


iii. Kusiwe na itikadi za kisiasa katika maendeleo ya watu.

iv. Wajumbe wa kamati ya maji wasichaguliwe kwa mfumo diwani amependekeza kwa kuwa tayari wananchi hawana imani, jambo hilo limetamkwa baada ya mbunge kuitisha mkutano na wananchi kabla ya hapo hakukuwa na dhamira hiyo.


v. Mradi wa maji usiwe ni mali ya watu wachache kwa kuwa ulikuwa ni msaada kutoka shirika la Japan la JICA kwa hiyo inabidi watu wote bila kujali itikadi wanufaike nao.

vi. Kamati ya uchunguzi iundwe ili kubaini ukweli wa tuhuma za kamati ya maji iliyopo ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake. Aidha chombo chochote kitakachoundwa kutekeleza mradi kiwe na chombo kingine juu yake kama bodi kwa ajili ya usimamizi.


Hotuba ya Mbunge
Mbunge aliwashukuru wananchi kwa umoja wao kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao katika Bunge na pia aliwashukuru kwa kuitikia mwito na kuhudhuria katika mkutano huo muhimu.

Pili alimshukuru Diwani pamoja na viongozi wa kiserikali kushiriki katika mkutano huo na akawaahidi ushirikiano wake wa karibu kwao katika mambo mbalimbali ya kiutumishi.
Alianza kwa kugusia mambo mbalimbali kama ifuatavyo;

Barabara; alisema kuwa amejenga hoja katika kikao cha bodi ya barabara ili barabara ya Mbezi Luis kupitia Goba itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuendana na mradi wa mabasi yaendayo kasi ili kuinusuru barabara ya Morogoro na foleni. Alisema kwamba upembuzi yakinifu wa barabara hiyo umekwishanyika isipokuwa tathmini ya fidia bado haijafanywa. Aliomba uongozi wa kiserikali kutoa ushirikiano kwa maafisa watakaofika maeneo yao kutathmini mali za wananchi zitakaoathiriwa na ujenzi wa barabara hiyo. Kuhusu barabara zinazounganisha mitaa Mbunge alimshauri Diwani kuliongelea hilo kwenye vikao vya WDC ili baadae iende Manispaa na akaahidi kuchangia pale atakaombwa kufanya hivyo.

Kituo cha Polisi; alisema kuwa RPC wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni alikubali kuhusu ujenzi wa kituo cha polisi akaagiza litafutwe eneo. Na kwa kuwa Diwani amesema eneo limepatikana aliahidi kuwa baada ya kupata specifications atajitahidi kulifuatilia ili kazi ujenzi ianze haraka.

Umeme; kuhusu mtaa wa Matosa ambao bado hakuna umeme alisema kuwa amewasiliana na Waziri wa Nishati na madini na alimuahidi kuwa kwenye mwaka wa wa fedha ujao fedha zitatengwa kwa ajili ya kusambaza umeme katika mtaa huo.

Maji; alijikita sana kwenye swala la maji kwa kuwa alipokea malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi na mengi yaligusa mradi wa maji Goba yaani GOBA WATER USERS ASSOCIATION. Na kwa maana hiyo alishauri kuwa mjadala unahitajika ili kufikia maazimio kuhusu mapungufu ya mradi huo kama ulivyoibuliwa na katika risala ya wananchi pamoja na wananchi wengine waliotoa maoni katika mkutano huo. Kwa miradi mingine alishauri wananchi kuishughulikia kwa karibu ili kuelewa mienendo yake kwa manufaa ya watu wote.

Kuhusu kuvunja kamati ya maji; alisema yafuatayo;
Kuwa kimamlaka yeye hana uwezo wa kuvunja kamati, uwezo huo upo kwa wananchi wenyewe wakiamua kufanya hivyo.

Alitoa angalizo kuwa binafsi hapendi kufanya mambo kwa haraka na akashauri kuwa swala hilo lisiwe kwa haraka ili kuwe na ufanisi wa kupata kamati mpya.

Pia alishauri kuwa mapendekezo ya ripoti ya ukaguzi ya mradi wa maji ya 2007 (ambayo aliigawa siku hiyo kwa wananchi) yazingatiwe.

Uamuzi wa kuvunja kamati iliyokuwepo tarehe 06/03/2011 ulipingwa na wananchi katika mkutano huo, na mbunge alifafanua kuwa kimsingi uhalali wa kamati ya mwanzo ulishapotea toka awali (ab initio) kwa kuwa ilipewa muda maalumu ambao ulishapita toka mwaka 2007

Pia aliasa kuwa swala la maji katika Kata hiyo lisipotafutiwa ufumbuzi linaweza kuhatarisha amani na utulivu katika maeneo hayo. Hivyo inatakiwa ufumbuzi wa haraka kuhusu utatuzi wa swala hilo na la kudumu.

Alishauri pia iundwe kamati ndogo ya wajumbe wanne na kila mtaa utoe mjumbe mmoja. Na baada ya hapo kamati hiyo ndogo itashirikiana na Afisa Mtendaji ili kuandaa mkutano wa tarehe sita ili kupata wajumbe wengine wane na pia kujadili ripoti ya kamati iliyokuwepo. Mbunge ameahidi kuhudhuria katika mkutano huo.



Maazimio
Baada ya hotuba ya mbunge mkutano huo kwa pamoja ulifikia maazimio kama ifuatavyo;

i. Kuwa kamati ya maji iliyopo ivunjwe na wananchi wenyewe.

ii. Wajumbe wanne wachaguliwe ili kuandaa mkutano wa tarehe 06/03/2011 kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Goba ili kupata kamati kamili.


iii. Kuwa iundwe timu ya uchunguzi ili kuchunguza tuhuma za kamati iliyokuwepo ili kubaini ukweli wa mambo na hatimaye hatua za kisheria zichukuliwe.

iv. Kamati iliyomaliza muda wake ilete ripoti yake iletwe kwenye mkutano wa tarehe 06/03/2011 na ijadiliwe siku hiyo na wananchi.


v. Wajumbe waliochaguliwa ni wafuatao;

a. Monica Modestus Kimario- Mtaa wa Goba

b. Leonard Haule- Mtaa wa Matosa


c. Dickson Luyela- Mtaa wa Kinzudi

d. Nickson Mbando-Mtaa wa Kulangwa

Hadibu za rejea

Kamati ndogo iliyoundwa ilitakiwa kufanya yafuatayo;

i. Kamati ishirikiane na Afisa mtendaji wa Kata ili kuandaa mkutano wa tarehe 06/03/2011.

ii. Kamati hii iandae ripoti yake na itajadiliwa katika mkutano ujao.

iii. Mkutano huo wa tarehe 06/03/2011 uwe na ajenda ya kupokea taarifa kutoka kamati iliyomaliza muda wake.




Mwisho
Mbunge wa Jimbo la Ubungo aliwakaribisha Afisa Mtendaji, Diwani, na Diwani wa viti maalumu kuongea maneno machache kwa ajili ya kufunga mkutano.
Mwisho kabisa Mbunge aliwashukuru wananchi kwa kuhudhuria katika mkutano huo na aliwaomba tena kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa tarehe 06/02/2011 ili kupata kamati kamili ya maji.