Friday, June 2, 2017

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHESHIMIWA JOHN JOHN MNYIKA (MB), KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2016/2017 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/ 2018

(Inatolewa chini ya 99(9) ya kanuni za Bunge, Toleo la Mwaka, 2016)
  1. A. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Awali ya yote niungane na wenye mapenzi mema katika kuomba ulinzi wa mwenyezi Mungu wakati wa kutimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuishauri na kuisimamia Serikali kwa Wizara ya Nishati na Madini juu ya bajeti ya mwaka 2016/2017 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, nitumie fursa hii kuwatakia waislamu wote mfungo mwema katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, Nitambue mchango Mheshimiwa John Heche, Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini alioutoa katika maandalizi ya hotuba hii. Aidha tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona na kurejea katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa familia ya marehemu Mzee Philemon Ndesamburo, wanachama wa CHADEMA kote nchini, wananchi wa Moshi Mjini, wabunge na watanzania wote walioguswa na msiba huu. Marehemu atakumbukwa kwa mchango wake kama mmoja wa waasisi wa chama chetu, Mbunge Mstaafu na Mfanyabiashara Mashuhuri. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema.

  1. B. MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA MADINI, MAFUTA NA GESI ASILIA

Mheshimiwa Spika, Novemba 4, 2016 Mheshimiwa Rais alipokuwa akizungumza na watanzania kupitia vyombo vya habari, ikulu jijini Dar es salaam alinukuliwa akisema hakuwahi kuzungumzia katiba mpya wakati wa kampeni zake, kwa hiyo siyo kipaumbele chake na kwamba anachotaka kwanza ni kunyoosha nchi.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali hii ya awamu ya tano ikisema swala la katiba mpya kama siyo kipaumbele chake, watanzania walitoa mapendekezo ya kuwepo kwa vifungu kwenye katiba mpya vinavyohusika na madini, mafuta na gesi asilia ili kuondoa migogoro ambayo inayohusu rasilimali na kuwezesha nchi na wananchi kunufaika na maliasili ambazo Mwenyezi Mungu amelijalia taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo na matakwa ya wananchi kuhitaji katiba mpya kuwa na vifungu vinavyohusika na madini, mafuta na gesi asilia, yalitokana na ukweli kwamba katiba ya sasa ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania hususan ibara ya 27 haijaweka misingi bora ya umiliki, usimamizi na ushughulikiaji  wa masuala yanayohusu rasilimali za nchi. 

  1. 1. Uzoefu wa nchi nyingine kuhusu katiba na mustakabali wa madini, mafuta na gesi asilia

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kutoa mifano michache juu ya uzoefu wa nchi nyingine ili kuionesha Serikali ni nini hasa kilitokea kwa wenzetu, ambao nao pia walikuwa na tatizo kama la kwetu. Nchi ya Norway ilianza uchimbaji wa mafuta na gesi asilia mwaka 1971 na kwa sasa Norway ni mojawapo ya nchi zilizofanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kuboresha uchumi na maisha ya wananchi wake kutokana na sekta ya mafuta na gesi asilia. Mafanikio ya Norway yalipatikana baada ya kubadili sera zilizokuwa zinatoa upendeleo  kwa makampuni binafsi na kuweka sera zilizokuwa zinatoa kipaumbele kwa maslahi ya nchi na wananchi. Pamaja na hayo, Norway iliweka mafuta na gesi asilia katika katiba yake, ibara ya 110b na msimamo huo ukafafanuliwa zaidi na sheria ya mafuta. Huu ni mfano wa katiba na sheria kuwekwa kipaumbele na kutumika kama nyenzo ya kunyoosha nchi.
Mheshimiwa Spika, Nchi ya Bolivia ni mfano wa pili ambao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia inapenda kuutoa kwa nia na malengo yaleyale. Nchi hiyo ni miongoni mwa nchi ambazo zimejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi. Pamoja na utajiri huo, wananchi wa Bolivia kwa kipindi kirefu walikuwa na malalamiko kuwa mafuta na gesi asilia haziwanufaishi. Bolivia ilifanya mabadiliko ya sera zake lakini tofauti na Norway, mabadiliko ya Bolivia yalisababishwa na malalamiko na vurugu za wananchi waliokuwa wanataka mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, kuanzia miaka ya 2000, nchi ya Bolivia ilishuhudia vurugu na maandamano zilizosababishwa na kile kilichoitwa vita vya maji kutokana na kupinga kubinafisishwa kwa maji na baadaye vurugu hizo zilihamia katika gesi asilia na mafuta. Aidha mwaka 2003 vurugu na maandamano makubwa dhidi ya sera mbovu zilisababisha aliyekuwa Rais wa Bolivia  Gonzalo Sanchez de Lozada “Goni” kujiuzulu na kukimbilia Marekani. Hata hivyo alirithiwa na makamu wa Rais ambaye pia alilazimishwa kujiuzulu mwaka 2005 kwa maandamano kama mtangulizi wake.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2006 Evo Morales alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo na aliongoza nchi hiyo kupata katiba mpya mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine ilihakikisha kuwa mafuta na gesi asilia yananufaisha wananchi wa Bolivia.
Mheshimiwa Spika, Tanzania pia inayo madini, mafuta na gesi asilia kama zilivyo nchi ambazo mifano yake imeelezwa hapo juu. Ikumbukwe kwamba mwaka 2013  Tanzania ilishuhudia vurugu  na umwagaji wa damu kwa wananchi wasiokuwa na hatia mkoani Mtwara zilisababishwa na mgogoro wa gesi ambao kiini chake ni madai ya wananchi kutokunufaika na rasilimali. Mchakato wa mabadiliko ya katiba ulibeba matumaini ya watanzania kwamba pamoja na mambo mengine nchi ingeweka misingi ya wananchi kunufaika na rasilimali ikiwemo madini, mafuta na gesi asili. Hata hivyo mchakato huo ulikwama na kupunguza matumaini ya wananchi. Serikali hii inayoongozwa na CCM inataka mpaka wananchi waanzishe migomo na maandamano ndio itambue kwamba katiba mpya ni kipaumbele cha wananchi katika masuala mengi ikiwemo juu ya rasilimali za nchi? Hivi ni lini Rais atatambua kwamba katiba na sheria ni zana muhimu za kunyoosha nchi? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kuwa mstari wa mbele kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha mchakato wa mabadiliko ya katiba unaendelezwa na masuala ya madini, mafuta na gesi yanapewa kipaumbele katika katiba mpya.

  1. 2. Ushauri wa kufanya katika kipindi hiki ambacho katiba mpya haijapatikana

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Tanzania tunakabiliwa na changamoto katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inapendekeza kwamba, Serikali ilete mbele ya Bunge lako tukufu marekebisho ya sheria ambayo yataweka misingi ifuatayo;
  • Serikali isimamie shughuli za uvunaji wa madini katika mfululizo wake wote (entire production chain) kuanzia kwenye uchimbaji ili kuhakikisha kuwa madini yanatoa mchango katika maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.
  • Kuwepo kwa utaratibu wa kutoa leseni kwa njia ya zabuni ya wazi badala ya utaratibu wa mikataba kati ya Serikali na mwekezaji.
  • Serikali iwe na makampuni yake yanayoweza kuingia katika ubia na makampuni au taasisi zingine au mjumuiko wa kampuni katika shughuli za uvunaji wa madini, mafuta na gesi asili Tanzania. Serikali pia imiliki hisa kutokana na thamani ya rasilimali zetu.
  • Ili kupunguza mianya ya rushwa na kuongezeka kwa uwajibikaji katika mikataba, iwepo sheria inayotaka bunge kuridhia mikataba yote utafutaji na uvunaji wa Madini, Mafuta na gesi asilia.
  • Serikali ihakikishe kwa niaba ya wananchi, Tanzania inanufaika na uvunaji wa madini, mafuta na gesi asilia, na usiwepo mkataba wowote unaokiuka misingi hii.
  • Uvunaji wa madini, mafuta na gesi asilia uhakikishe unachangia kuboresha maisha ya jamii, ajira na kulinda mazingira, kuhakikisha pia maslahi ya Serikali kuu, halmashauri za wilaya, vijiji na waathirika wa uwekezaji mkubwa wananufaika na miradi iliyopo.
  • Wananchi ambako uwekezaji utafanyika washirikishwe kuhusu maamuzi yeyote yanayohusu utafutaji, na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia na halmashauri zao zihusike katika umiliki kupitia hisa.

  1. 3. Makinikia ama “Mchanga wa Dhahabu” na Hatma ya Sekta ya Madini Nchini

Mheshimiwa Spika, Tarehe 24 Mei 2017 Mheshimiwa Rais Dr John  Magufuli  alipokea ripoti ya Kamati ya Kwanza ya Rais juu ya kusafirishwa nje kwa makinikia ya dhahabu/shaba. (Maarufu kama “Mchanga wa Dhahabu”). Aidha, wakati wa tukio la kukabidhi ripoti hiyo Mwenyekiti wa Kamati tajwa Prof Abdulkarim Mruma alieleza muhuktasari wa matokeo ya ripoti hiyo na Rais alitoa kauli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Ni vyema ikafahamika kwamba makinikia haya yanahusu migodi miwili ya Bulyankulu na Buzwagi chini ya kampuni moja ya Acacia. Makinikia haya yanahusu takribani asilimia 30 ya dhahabu inayozalishwa katika migodi hiyo ambayo kwa sheria mbovu na mikataba mibovu ni mali ya mwekezaji. Huku stahili ya nchi ikiwa mrabaha wa asilimia nne (4%) tu. Ripoti hiyo ya makinikia ama ‘mchanga wa dhahabu’ haihusu mapato ya taifa na maslahi ya nchi katika asilimia 70 ya dhahabu inayopatikana katika migodi ya Bulyankulu na Buzwagi wala haihusu asilimia 100 ya dhahabu na madini mengine yanayopatikana katika migodi mingine nchini.

Mheshimiwa Spika, Rais makini kabla ya kufikiria makinikia angefikiria kuhusu madini yanayochimbwa na kuchenjuliwa kwa ukamilifu hapa nchini lakini nchi haipati mapato yanayostahili. Hivyo, taarifa ya kamati ya Prof Mruma na kauli za Rais zimeiingiza nchi na wananchi katika mjadala mdogo wa makinikia ama mchanga badala ya mjadala mkubwa madini na matatizo makubwa yaliyopo katika mfumo wetu.

Mheshimiwa Spika, katika muktadha kabla ya kutoa maoni kuhusu makinikia ama mchanga Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa Bunge na wananchi kujadili matatizo makuu ya sekta ya madini katika taifa letu. Matatizo makubwa katika sekta ya madini katika nchi yetu yamesababishwa na sera na sheria mbovu zilizotungwa chini ya Serikali inayoongozwa na CCM na mikataba mibovu iliyoingiwa katika awamu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tunapojadili mathalani kukosa mapato kutoka mgodi wa Bulyankulu ni vyema tukakumbuka kuwa katika kipindi cha mwisho cha Rais Ali Hassan Mwinyi makampuni ya kigeni yaliongezeka kuingia katika nchi yetu. Kati ya makampuni hayo ni pamoja Kampuni ya Sutton Resources ya Vancouver, Canada, iliyopatiwa leseni kwa ajili ya eneo la Bulyanhulu/Butobela mwaka 1994. Leseni hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Jakaya Kikwete alipokuwa  Waziri wa Maji, Nishati na Madini. Mara baada ya Rais Benjamin Mkapa kuapishwa mwaka 1995 iliandikwa fax baada ya Rais kuapishwa iliyokuwa na maneno “our man has been sworn into office, now Bulyankulu file will move”. Na kweli Mwaka 1996, wachimbaji wadogo wadogo walihamishwa kwa nguvu huku mengine wakidaiwa kufukiwa katika mashimo na kampuni ya Sutton Resources wakakabidhiwa eneo hilo. Yaliyofanywa Bulyankulu yalifanywa pia kwa namna nyingine katika maeneo mengine kwa nyakati tofauti tofauti ikiwemo Nyamongo, Mererani, Geita na Buzwagi.
Mheshimiwa Spika, ili kuyawekea makampuni hayo mazingira halali ya kisheria ya ‘kunyonya rasilimali nchi’ Mwaka 1997, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilitengeneza matatizo kwa kutunga sheria mbili mbovu kwa siku moja chini ya hati ya dharura. Kati ya sheria hizo ni Sheria ya Marekebisho mbali mbali ya Sheria za Fedha (Financial Laws Miscellaneous Amendments Act, 1997) ambayo ilifanya marekebisho makubwa katika sheria mbali mbali za kodi ambayo yalifuta kwa kiasi kikubwa kodi, tozo na ushuru mbali mbali kwa makampuni ya madini. Matokeo ya sheria hii ni miaka mingi ya kukosa mapato ya kutosha katika madini. Sheria nyingine ni ile ya Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Act, 1997) ambayo iliyapa makampuni ya nje kinga za kisheria za mambo ambayo mengine yanalalamikiwa kuhusu makampuni hayo mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, udhaifu katika mfumo mzima wa madini katika nchi yetu ukataasisishwa mwaka 1998 kwa Bunge kutunga Sheria ya Madini (Mining Act, 1998). Sheria hii kimsingi iliweka bayana kwamba madini yanayopatikana na fedha za mauzo yake ni mali ya mwenye leseni. Sheria iliruhusu makinikia ama mchanga kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya usafishaji. Nchi yetu kupitia Sheria hii ilipaswa kulipwa mrabaha wa asilimia 3, sheria ya mwaka 2010 imeongeza tu kiwango kuwa asilimia 4. 

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine sheria zetu zinatoa wajibu wa makampuni hayo kulipa kodi ya mapato ya asilimia 30, hata hivyo ni baada ya kupata ‘mapato yenye kuweza kutozwa kodi’ (taxable income); yaani baada ya kupata faida. Sheria hizo mbovu zimeyaruhusu kwa muda mrefu makampuni ya madini kuondoa gharama zote za uzalishaji kabla ya kutangaza mapato ya kikodi. Makampuni hayo yametumia mianya hiyo na udhaifu wa taasisi za nchi yetu mathalani TMAA na TRA kuweka gharama zisizostahili na hivyo kutangaza kupata hasara na kutolipa kodi au kutangaza faida ndogo na kulipa kodi kiduchu. Rais makini alipaswa kabla ya kuzuia makinikia ama mchanga kudhibiti mianya kama hii ya upotevu mkubwa wa mapato katika madini. Mfumo huu wa ‘kuepuka kodi’ (tax avoidance) na ‘kupanga kodi’ (tax planning) ambao umeikosesha nchi mapato kwa muda mrefu umehalalishwa na sheria mbovu za nchi yetu. 

Mheshimiwa Spika, matokeo ya kuwa na sera bomu na sheria mbovu ni mikataba mibovu ambapo kwa upande wa Mikataba ya Uendelezaji wa Madini (MDAs) kati ya Serikali na makampuni makubwa, mikataba hiyo imeweka misamaha ya kodi na kuachia pia mianya  ya uepukaji wa kodi. Mikataba hiyo mibovu imetoa misamaha ambayo mingine hata haipo katika sheria tajwa kwa mfano kwa halmashauri zilizo na migodi ya madini makampuni yameruhusiwa kutoa kiwango cha ujumla cha dola laki mbili kwa ajili ya tozo ya huduma badala ya asilimia kati ya 0.14 na 0.3 ya mapato ya mwaka ya kampuni (annual turn over) ambayo yangekuwa malipo makubwa zaidi. Kwa nyakati mbalimbali tumeomba mikataba iletwe Bungeni ili ijadiliwe na kupitiwa upya hata hivyo Serikali imekuwa ikigoma. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuileta mikataba hiyo Bungeni na kuwezesha majadiliano ya marekebisho (renegotiation) kati ya Serikali na wawekezaji ili nchi na wananchi waweze kunufaika ipasavyo na rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amelijalia taifa letu.

Mheshimiwa Spika, masuala haya hayakuzungumzwa na Mwenyekiti wa ‘kamati ya makinikia’ wala Mheshimiwa Rais wakati akipokea ‘ripoti ya mchanga’. Badala yake ilitolewa taarifa yenye kuonyesha kuwa katika makontena 277 yaliyopo bandari ya Dar Es Salaam kiwango cha dhahabu katika makontena yote ambacho ni cha mwezi mmoja tu wa uzalishaji kimetajwa kuwa tani 7.8 (au wakia 250,000). Kwa mahesabu rahisi tu ya kuzidisha kiwango hicho kwa kufanya makadirio ya mwaka na kujumlisha na uzalishaji mwingine wa migodi hiyo miwili ya Bulyankulu na Buzwagi tu kunaifanya Tanzania kuwa mzalishaji namba tatu wa dhahabu duniani!. 
Mheshimiwa Spika, hapa kuna mwelekeo wa udanganyifu wa kitakwimu. Taswira hasi imeanza kujengeka kimataifa ambapo tarehe 25 May 2017 jarida la Mining Journal lilichapisha makala “Trouble in Tanzania” ambayo ilimalizia kwa mwito wa kufanyika kwa ‘World Risk Survey’. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwasilisha Bungeni taarifa kamili ya kamati hiyo ikiwemo metholojia iliyotumika kutathmini sampuli ijadiliwe na Bunge liweze kuazimia uchunguzi huru uweze kufanyika.
Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa Serikali iliwahi kuunda tume ambayo ilijulikana kama, tume ya Mheshimiwa Jaji Mark Bomani, ambayo ilipewa kazi ya kuishauri Serikali kuhusu usimamizi wa sekta ya madini. Aidha tume hiyo iligusia kipengele cha uchenjuaji na usafishaji wa Madini. Katika ukurasa 157 wa taarifa ya kamati ya Rais ya kuishauri Serikali kuhusu usimamizi wa sekta ya Madini ya mwaka 2008 kamati ilisema na nina nukuu “Kamati imechambua hali halisi ya shughuli za uchenjuaji na usafishaji (smelting and refinery) wa madini hapa nchini…na kuona kuwa shughuli hizi hazifanyiki katika kiwango cha kuridhisha. Aidha hakuna miundombinu hasa umeme na reli ya kuwezesha kuanzishwa kwa shughuli hizo. Hali hii imetokana na kutokuwepo kwa mkakati wa kisera wa kuhamasisha uwekezaji katika uchenjuaji na usafishaji wa madini hapa nchini

Mheshimiwa Spika, Taarifa hiyo inaendelea kuwa “kamati ilibaini kuwa kukosekana kwa shughuli hizi hapa nchini kunazifanya kampuni kama vile Bulyankulu Gold Mine Limited kusafirisha mchanga (Copper Concetrate) kwenda Japan na China ili kuchenjuliwa. Hali hii isiporekebishwa, italazimisha mgodi wa Kabanga Nickel unaotarajiwa kuanzishwa kupeleka mchanga nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjuliwa. Hii itaifanya Serikali kutokuwa na uhakika wa kiasi na aina ya madini yaliyomo katika mchango huo na inaweza kuathiri mapato ya Serikali”. Kamati katika mapendekezo yake kwa Serikali, kuhusu kipengele hiki, ilipendekeza “Serikali iweke mikakati katika sera ya madini na kutunga au kurekebisha sheria ya madini ili kuingiza vipengele vitakavyowezesha uanzishwaji na uimarishwaji wa viwanda vya uchenjuaji na usafishaji wa madini hapa nchini”. Rais Magufuli alikuwa mjumbe wa baraza la mawiziri wakati taarifa hii inawasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete. Aidha, Rais Magufuli alikuwa na muda toka alipoingia madarakani kuweza kushughulikia jambo hili katika hali yenye kuepusha migogoro isiyo ya lazima. Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa Bunge kuingilia kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mustakabali mwema wa sekta ya madini nchini.

  1. C. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA 2016/2017
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara ya Nishati na Madini iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,122,583,517,000 na kati fedha hizo, shilingi 1,056,354,669,000 zilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Aidha hadi kufikia tarehe 13 Machi, 2017 fedha zilizokuwa zimetolewa na hazina kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ni shilingi 372,877,980,724 tu sawa na 35% ya fedha zote za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu zilizooneshwa hapo utabaini kwamba, miradi ya maendeleo ilitekelezwa kwa 35% tu. Miradi iliyokwama ni pamoja na ya umeme vijijini. Aidha Miradi hii inatekelezwa kwa kiwango hicho pamoja na sababu nyingine ni kutokana na Taifa hili kukosa fedha za wafadhili kwenye miradi ya umeme ikiwemo miradi ambayo ingepata ufadhili wa MCC. Kwa maneno mengine watanzania wameshindwa kunufaika na miradi ya maendeleo kutoka kwa wafadhili kutokana na kukosekana kwa utawala bora, kuvurugwa kwa uchaguzi wa Zanzibar na uvinjifu wa haki za Binadamu. 

Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali iliwaaminisha watanzania kuwa miradi itatekelezwa kwa gharama za fedha za ndani katika kipindi cha Bajeti cha mwaka wa fedha 2016/2017.  Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata majibu ya kina, kuhusu sababu zilizopelekea Serikali kushindwa kutekeleza bajeti yake, huku ikijinadi ndani ya Bunge hili tukufu kwamba fedha za MCC hazina madhara na Taifa litatekeleza miradi kwa fedha zake! Je, kwa mwendo huu ni lini Taifa litafikia malengo tuliyojiwekea kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa?
  
  1. D. SEKTA YA NISHATI
    1. 1. Shirika la umeme Tanzania – TANESCO
      1. i. Usimamizi wa kampuni Binafsi za uzalishaji umeme na gharama za kuiuzia TANESCO

Mheshimiwa Spika, Shirika la umeme Tanzania, TANESCO katika jitihada za kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika wa umeme nchini, shirika liliingia mikataba na makampuni binafsi yanayozalisha umeme kwa lengo la kuiuzia TANESCO. Aidha taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba, TANESCO inanunua umeme kwa bei ya wastani wa shilingi 544.65 kwa kila “unit” na kuuza kwa shilingi 279.35 na hivyo kulifanya shirika kupata hasara ya shilingi 265.3 kwa kila unit.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kusitishwa kwa mkataba na kampuni ya Symbion, TANESCO ilikuwa inalipa jumla ya dola za Marekani milioni 16.36 kama capacity charge kwa makampuni yanayozalisha umeme wa dharura. Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inazo zinaonesha kwamba Kwa sasa, Shirika linatumia Dola za Marekani milioni 9.75 kwa mwezi kununua umeme kutoka Aggreko, Songas na IPTL na gharama za umeme zinazolipwa na TANESCO kwa mwezi ni Dola za Marekani milioni 9.75. 
Mheshimiwa Spika, Bei za nishati ya umeme inayotozwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinadhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kila robo mwaka baada ya mapitio ya gharama halisi za uzalishaji.  Aidha kwa mujibu wa tarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kuwa mapitio ya kila robo mwaka ya bei ya nishati ya umeme hayahusishi madeni yaliyojitokeza kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu wa mapitio ya bei ya umeme ya robo mwaka. Hivyo, utaratibu huu Mheshimiwa Spika, hauiwezeshi TANESCO kulipa madeni yote inayodaiwa. 
Mheshimiwa Spika, bei ya umeme inayopitishwa na EWURA haionyeshi gharama halisi zilizotumiwa na TANESCO jambo linaloathiri uwezo wa TANESCO katika kulipa madeni yanayolikabili Shirika. Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inaishauri Serikali kupitia EWURA kuzipitia kwa umakini gharama za umeme ili kuhakikisha kuwa gharama zote za uzalishaji wa umeme zinahusishwa, ili hatimaye, kusaidia upatikanaji wa faida baada ya uwekezaji wenye lengo la kuboresha huduma na kuongeza matokeo chanya kwa TANESCO.
Mheshimiwa Spika, shughuli za TANESCO zinahusisha pia utekelezaji wa mikataba mbalimbali ikiwemo iliyoridhiwa kipindi cha Serikali za awamu zilizotangulia. Miongoni mwa mikataba hiyo ni ile iliyopigiwa kelele na watanzania kuwa ina harufu ya ufisadi na baadhi ikidaiwa kutokuwa na maslahi kwa Taifa. Mikataba hii inayohusu ununuzi wa umeme ni ghali kwa unit kiasi cha kuipa wakati mgumu TANESCO kupata fedha za kujiendesha na wakati huo huo kuwauzia umeme watanzania kwa bei juu, hivyo inapaswa kupitiwa upya. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kulieleza Bunge hili tukufu pamoja na watanzania, ni lini TANESCO itapitia mikataba yote mibovu ya shirika hilo na ikibidi TANESCO kuachana na mikataba ile inayoongeza mzigo na gharama za uendeshaji wa shirika hilo? 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inaishauri Serikali mambo ya nyongeza yafuatayo:
      1. i. Bei za umeme zinazopitishwa na EWURA zizingatie gharama halisi zinazotumiwa na TANESCO kuzalisha umeme au kununua toka kwa makampuni binafsi ya uzalishaji umeme kuliko hali ilivyo kwa sasa kwa kuwa shirika linaonekana kuendeshwa kwa kuficha ukweli kuliko uhalisia ambao hauwekwi wazi.
      2. ii. Kwa kuwa miongoni mwa majukumu ya shirika hili ni pamoja na kufua na kuimarisha mitambo ya umeme ya shirika, kununua kutoka kwa wazalishaji binafsi na nchi za jirani, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha manunuzi ya umeme toka kwenye makampuni binafsi ya uzalishaji umeme yanafanyika kwa uwazi na ushindani kama inavyotakiwa na sheria ya manunuzi ili kuiweesha TANESCO kununua umeme kwa bei nafuu.
      3. iii. Ili kuhakikisha shirika linatimiza jukumu lake la kuwekeza kwenye miradi mipya ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na kufanya tafiti za vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme kama vile nguvu za maji (hydropower), gesi asilia, makaa ya mawe (coal), jua na upepo; Serikali iliwezeshe shirika la umeme nchini (TANESCO) ili iweze kuwekeza kwenye uzalishaji umeme wa bei nafuu hivyo kusaidia kuepukana na utaratibu wa kununua toka vyanzo vya gharama kubwa. 

      1. ii. TANESCO kushindwa Kukusanya Madeni
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Rais alikaririwa akisema TANESCO wanapaswa kukusanya madeni wanayodai na akaenda mbali zaidi na kusema hata kama Ikulu inadaiwa TANESCO ikate tu umeme. Aidha katika hali ya kawaida kauli hiyo ilitarajiwa iende sambamba na vitendo kwa Serikali pamoja na taasisi zake kulipa madeni ya shirika hilo kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Spika, Kwa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kuwa TANESCO inadai fedha nyingi ambazo hazijakusanywa na hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016 jumla ya deni la umeme kwa Serikali na taasisi zake zilifika Shilingi bilioni 144.854, sawa na asilimia 67.4 ya deni lote la umeme. Deni lililobaki kwa wateja binafsi ni Shilingi bilioni 70.063 sawa na asilimia 33. Ni wazi kuwa, kutokulipwa kwa madeni ya umeme na taasisi za umma na binafsi kunaathiri uwezo wa TANESCO kujiendesha kwa ufanisi na kulipa madeni kwa wadaiwa  wake. 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kupitia wizara hii, kuliambia Taifa ni lini Serikali ilitoa maelekezo kwa taasisi zake kulipa madeni ya umeme kwa wakati na ni lini hasa deni hili la shilingi bilioni 144.8 litalipwa kwa TANESCO ili kauli ya Rais ionekene ni ya uhalisia na siyo matamko ya kufurahisha tu?

      1. iii. Wizara ya Nishati na Madini Kutolipa Deni la Kodi ya Pango kwa TANESCO
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaelewa kwamba Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini iliingia makubaliano na TANESCO ya kupanga jengo kwa muda wa miaka 10 kwa ajili ya matumizi ya ofisi kwenye jengo la TANESCO lililopo barabara ya Samora, jijini Dar es Salaam. Aidha muda rasmi wa kuanza makubaliano hayo ilikuwa tarehe 1 Januari, 2013 kwa kodi ya Shilingi milioni 26.60 kwa mwezi. Hata hivyo, Kwa taarifa zilizopo Wizara haijalipa kiasi chochote tangu mkataba uliposainiwa, kiasi ambacho hakijalipwa kimefikia Shilingi bilioni 1.12. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza ni lini Serikali itailipa Tanesco fedha hizo za pango? 
Mheshimiwa Spika, Wizara imetenga fedha hizi kwenye fungu lipi kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kulipia deni la shilingi bilioni 1.12? Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza, Serikali inapata wapi uthubutu wa kuiagiza TANESCO kuwakatia umeme wateja wake inaowadai wakati Wizara mama yake inadaiwa na TANESCO fedha nyingi kama hizo?
      1. iv. Miradi ya kuzalisha umeme kwa njia ya Maji na Jotoardhi

Mheshimiwa Spika, miradi ya kufua umeme wa maji inakadiriwa kuwa miongoni mwa miradi ambayo umeme wake ni wa bei ya chini ikilinganishwa na uzalishaji wa umeme kwa kutumia mitambo inayozalisha umeme kwa kutumia nishati ya Mafuta. Pamoja na miradi ya kufua umeme ya Kakono- MW 87, mradi wa Malagarasi MW 45 na Mradi wa Rusumo – MW 80, lakini bado kuna miradi mingi ambayo Serikali haionyeshi jitihada zozote za kuikamilisha kwa wakati pamoja na kwamba miradi hiyo ilishatumia fedha za walipa kodi katika hatua za awali za utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika,  kwa mujibu wa Mpango wa pili wa Maendeleo wa Miaka mitano ni kwamba Serikali ilitarajiwa kuendeleza mradi wa kuzalisha 200MW wa Geothermal wa Ngozi- Mbeya. Takwimu zinaonesha kuwa gharama za mradi huo ni shilingi bilioni 204.72 na kila mwaka hadi 2020/21 zilitakiwa kutengwa shilingi bilioni 40.94.

Mheshimiwa Spika, kama inavyojulikana kuwa mipango bila kuwa na bajeti ya utekelezaji ni sawa na hadithi tu. Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge, je kuna umuhimu kwa waheshimiwa wabunge kuendelea kurejea miradi ya umeme kama ilivyoorodheshwa kwenye kitabu cha Mpango wa awamu ya pili wa maendeleo ya miaka mitano huku Serikali ikiwa haitengi fedha kwa ajili ya utekelezaji?

      1. v.   Ununuzi wa Transfoma kutoka nje ya Nchi

Mheshimiwa Spika, TANESCO kwa kipindi kirefu wamekuwa wakinunua transfoma kutoka nje ya nchi wakati hapa nchini kuna kiwanda cha TANALEC kinachotengeneza transfoma hizo. Kwa mujibu wa Mkurungenzi wa kiwanda, Transfoma zao zina ubora wa Kimataifa na kwa sasa na wana matarajio ya kutengeneza Transforma ambazo hazitumii mafuta ili kuepukana na wizi wa mafuta kwenye Transforma wa mara kwa mara. Aidha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikaririwa akiliagiza Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kuacha kununua Transfomer kutoka nje ya nchi na badala yake wanunue zinazotengenezwa nchini.

Mheshimiwa Spika, Katika ziara yake kwenye kiwanda cha utengenezaji transfoma cha TANALEC mkoani Arusha Waziri alionesha kushangazwa na kauli ya watendaji wa TANESCO kuwa transfoma zinazotumika nchini ni kutoka nje ya nchi. Aidha TANESCO kupitia kwa Meneja mauzo na masoko Kanda ya Kaskazini ilikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba hali hiyo inasababishwa na sheria ya ununuzi kuwabana.

Mheshimiwa Spika, wakati TANESCO wakilalamikia sheria ya ununuzi kuwabana, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini alipotembelea kiwanda cha Kutengeneza Transforma cha TANALEC alipingana vikali na kauli ya watendaji wa TANESCO kuwa sheria ya manunuzi ndio inawakataza kununua Transiforma hizo. Aidha Waziri aliagiza TANESCO kununua Transforma hizo ambazo wao wana hisa na kuhusu sheria za manunuzi kukataza kununua bidhaa zao wenyewe ni mbinu na rushwa zilizojaa katika zabuni za manunuzi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu, inashangazwa na kitendo cha Serikali kwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini kupingana na TANESCO kuhusu sheria ya manunuzi, wakati TANESCO wakisema kinachowafanya kununua transfoma kutoka nje ya nchi ni sheria ya ununuzi, Serikali kwa upande wao wanasema hizo ni mbinu za rushwa zilizojaa katika zabuni za manunuzi. Kwa kuwa Serikali inakiri kuwepo kwa mbinu za rushwa katika zabuni za manunuzi, na kwa kuwa Serikali hii inasema ni Serikali ya viwanda lakini, Serikali yenyewe ikiwa hainunui bidhaa zinazotokana na viwanda vya ndani ya nchi; je ni lini Serikali itaacha maigizo haya na kuja na suluhisho la tatizo hili kwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji iliosema wanaendekeza mbinu hizo za rushwa?

    1. 2. Wakala wa nishati vijijini- (REA)

Mheshimiwa Spika, lengo la uanzishwaji wa REA lilikiwa ni kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa wakala huyu bado Serikali haijaonesha kwa vitendo kuwa ina nia ya kusaidia wakala huyu ili aweze kuimiza majukumu yake kikamilifu na hasa linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Serikali imekuwa haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA fedha kama zinavyotengwa na kuidhinishwa na Bunge hili, kwa mfano mwaka 2008/2009 zilipitishwa shilingi bilioni 20.00 lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 12.06 sawa na 60%. Mwaka 2009/2010, fedha zilizopitishwa ni shilingi bilioni 39.55 na kiwango cha fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 22.14 sawa na 56%. Mwaka 2010/2011 kiasi cha fedha kilichotengwa ni shilingi bilioni 58.883 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 14.652 sawa na 25%, mwaka 2011/2012 kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 71.044 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 56.748 sawa na 80%, mwaka 2012/2013 kiasi cha fedha kilichotengwa ni shilingi bilioni 53.158 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 6.757 sawa na 13%.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeamua kutoa takwimu hizo ili kuonesha kwamba tatizo la Serikali kutopeleka fedha kwa Wakala huyu pamoja na kwamba sasa fedha hizi zinatokana na fedha za wananchi kupitia ongezeko la shilingi 100 kwenye kila lita moja ya mafuta ya petroli kwa ajili ya nishati vijijini lakini bado fedha hazipelekwi kwenye miradi hiyo. Ni vyema sasa Serikali iwaambie watanzania sababu zinazosababisha kushindwa kupelekwa kwa fedha hizi kwa wakala huyu wakati wananchi wameshatoa fedha kwa ajili ya lengo hilo.

Mheshimiwa Spika, uzoefu kutoka kwenye awamu mbili zilizotangulia zinaonesha kwamba, Serikali imekuwa ikishindwa kupeleka fedha kwa ajili ya miradi ya REA kwa wakati na pale ambapo imekuwa ikipelekwa basi fedha hizo zimekuwa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya mradi husika, hali inayosababisha miradi kushindwa kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kucheleweshwa kupelekwa kwa fedha za miradi kunasababisha miradi pia kuchelewa kukamilika na kuchelewa kukamilika kwa miradi kwa wakati kunasababisha kuongezeka kwa gharama za miradi husika. 

Mheshimiwa Spika, taarifa ya wakala iliyotolewa Januari, 2017 takwimu zake zinaonyesha kuwa jumla ya miradi 13 inayoendelea kutekelezwa yenye thamani ya shilingi 1,210,050,878,902 kama mikataba yake ilivyosainiwa, hadi sasa fedha zilizotolewa na Serikali ni shilingi 1,019,957,110,048.20 na kiasi kilicho baki ni shilingi 190,093,768,854. Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha, na ni miradi iliyoingiwa mikataba tu, lakini REA ina miradi mingi kwa kulingana na bajeti zilizopitishwa na Bunge pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha kuorodhesha miradi kumi na tatu tu inayoendelea kutekelezwa, maana yake ni kutaka kupimwa kwa kigezo kidogo na sehemu kubwa inayolingana na bajeti inayotengwa na miradi iliyopangwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa isipimwe kwa kiwango cha fedha kilichotakiwa kutengwa.

    1. i. Mapungufu katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kwa awamu ya pili:
Mheshimiwa Spika, kuna malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza kutokana na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika awamu ya pili ambayo Serikali imeeleza kuwa imekamilika. Baadhi ya mifano ya mapungufu kutoka maeneo mblimbali ni pamoja na mkoani Mara, mkandarasi kuweka transfoma zenye 50 kVA na ufungaji wake kutokamilika, badala ya transfoma yenye 100 kVA; Mkoani Morogoro kulikuwa na utekelezaji mdogo wa mradi ambapo ni 15.6% ya wateja wa umeme wa njia tatu waliunganishiwa umeme, huku kwa wateja wa njia moja waliounganishiwa umeme ni 29%. Aidha wakati utendaji wa mkandarasi huyu ukiwa hivi, mkandarasi inadaiwa alikuwa ameshalipwa karibia 69.6% ya fedha zote. Mapungufu mengine ni pamoja na kuongezwa kwa wigo kazi na mkandarasi bila idhini ya wakala wa umeme vijijini, transfoma 21 badala ya transfoma 10 ziliwekwa ambayo ni kinyume na mkataba.
Mheshimiwa Spika, Huko Babati baadhi ya vijiji vilikosa umeme kutokana na TANESCO kushindwa kuidhinisha ombi la kutumika kwa nguzo zake za umeme; kasoro za kiufundi huko Arumeru; mgogoro wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro unaohusu ardhi inayodaiwa kuwa mali ya mamlaka ya viwanja vya ndege na hivyo kuathiri upatikanaji wa umeme kwa baadhi ya vijiji.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali, kutoa kauli juu ya hatua ilizochukua ili kurekebisha kasoro ambazo zilijitokeza katika utekelezaji wa REA awamu ya pili.
    1. ii. Utekelezaji wa REA awamu ya Tatu
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni wakala wa umeme vijijini REA umezindua mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu, baada ya kukamilika kwa awamu mbili zilizotangulia, taarifa iliyotolewa kwa umma inaonesha kwamba mradi huu utajumuisha vijiji 7,873 katika mikoa yote na wilaya za Tanzania bara kwa utekelezaji wa kipindi cha miaka mitano. 

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na REA kupitia tovuti yake, wakala wa Nishati vijijini REA, ulikamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu. REA kupitia taarifa hiyo uliwajulisha wakandarasi walioshinda kwamba hatua iliyokuwa inafuata ni kuwapatia barua za tuzo (Award Letters) na kusaini mikataba.
Mheshimiwa Spika, zabuni hizo zilihusu mradi wa REA awamu ya tatu, zinalenga kufikisha umeme wa gridi kwenye vijijini 3559 katika mikoa 25 ya Tanzania bara, kwa thamani ya zaidi ya Bilioni 900.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba mradi huu unagharimu fedha nyingi za walipa kodi, takribani bilioni 900 lakini tayari kuna madhaifu mengi yameshajitokeza katika michakato ya dhabuni hizo. Taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imezipata kuhusu mapungufu katika mchakato wa zabuni za tenda ni pamoja na baadhi ya kampuni kupewa zabuni wakati hazijasajiliwa katika bodi ya usajili wa makandarasi;  kampuni ambazo hazikusajiliwa na bodi ya wakandarasi lakini wakashirikiana na wabia ambao ni wa madaraja ya chini na hawakustahili kupewa zabuni kubwa;  baadhi ya makampuni yenye sifa sawa na makampuni yaliyopata zabuni kukosa zabuni hizo; baadhi ya makampuni kupewa zabuni wakati makampuni hayo hayana sifa za kupewa zabuni hizo na baadhi ya makampuni kupewa zabuni wakati makampuni hayo yalikosa sifa za uzoefu katika kazi hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa zabuni zilizotangazwa makampuni yenye sifa za moja kwa moja kwenye zabuni hizi ni makampuni yenye sifa za daraja la kwanza. Makampuni yenye sifa za daraja la kwanza hayana ukomo wa kiasi cha fedha zinazopaswa kulipwa kwenye kila kifungu. Daraja la pili kikomo cha fedha ni shilingi bilioni 2, daraja la tatu, shilingi bilioni 1.2, daraja la IV shilingi milioni 600, Daraja la V shilingi milioni 300 na Daraja la VI shilingi milioni 150.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepata zinaonesha kwamba, yapo makampuni yanayodaiwa kupatiwa zabuni katika mazingira yenye utata na hivyo, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inaitaka Serikali kufanya uchunguzi juu ya makampuni hayo ili kuhakikisha fedha hizi za mradi wa REA III hazitumiki kwa makampuni yasiyo na uwezo wa kutekeleza miradi hiyo.  
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Radi Service Limited ambayo iliingia ubia na kampuni za Njarita Contractor Ltd pamoja na kampuni ya Agwila Electrical Contractors Ltd, na walipata mafungu ya zabuni ya dola 991,971 za kimarekani na shilingi bilioni 7.393. Aidha wabia hao pia walishinda lot nyingine yenye thamani ya dola milioni 3.787 na shilingi bilioni 25.61. Pamoja na ushindi wa kampuni hizi, zenye ubia, taarifa za Bodi ya Usajili wa wakandarasi (CRB) zinaonesha kwamba, kampuni ya Radi ni ya daraja la II na III, kampuni ya Agwila kwa mujibu wa taarifa za CRB ni ya daraja la V, na kampuni ya Njarita Contractor, usajili wake ni wa daraja la V. Pale inapotokea kampuni zote wabia ikawa hakuna kampuni yenye daraja la I, lakini zikawa zimeungana, zinaruhusiwa kuandika barua CRB ili zipatiwe kibali kabla ya kuomba zabuni. Kampuni zote hizi, pamoja na kuwa wabia hazikuwahi kuandika barua na kupewa kibali. Lakini pia pamoja na kwamba, kampuni hizi hazikusajiliwa kwa daraja la I, walipewa kazi ya mabilioni ya shilingi kwenye lots zote mbili zilizooneshwa hapo juu, kinyume na taratibu.
Mheshimiwa Spika, Kampuni nyingine ya whitecity International Contractor Limited iliingia ubia na kampuni ya Guangdong Jianneng Electric Power Engerneering na kupewa zabuni ya lot yenye thamani ya dola milioni 2.9 za Marekani na shilingi bilioni 22. Wakati wabia hawa wakishinda zabuni hiyo, taarifa za Bodi ya Usajili wa Makandarasi zinaonesha kwamba, kampuni ya Whitecity International Contractor Limited imesajiliwa kwa kazi umeme daraja la IV, Majengo daraja la II, Civil daraja la IV na civil specialist daraja la II. Mbia mwenza, kampuni ya Guangdong Jianneng Electrical Power Engineering, kwa taarifa zilizopo hana usajili wowote kutoka bodi ya usajili wa makandarasi. 

Mheshimiwa Spika, Zabuni nyingine yenye utata, ilitolewa kwa kampuni ya MF Electrical Engineering Limited ambayo iliingia ubia na kampuni ya GESAP Engineering Group Limited. Kampuni hizi kwenye lot ya kwanza wanalipwa dola milioni 5 pamoja na bilioni 23.748, lot ya pili walishinda zabuni yenye thamani ya dola milioni 3.852 za marekani na pia bilioni 19.899. Aidha taarifa kutoka bodi ya usajili wa makandarasi zinaonesha kwamba MF Electrical Engineering Limited usajili wake ni wa daraja la V,na kampuni ya GESAP Engineering Group Limited usajili wake kwenye maswala ya umeme ni wa daraja la II.

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Joe’s Electrical Ltd iliingia ubia na kampuni ya AT & C Pty na L’S Solution Ltd, kampuni zote hizi hadi zinakabidhiwa barua za kusudio la kuwapa zabuni hazikuwa na usajili kutoka bodi ya usajili wa makandarasi, lakini pamoja na upungufu huo, REA waliweza kuwapatia lots mbili, lot ya kwanza ina thamani ya dola za kimarekani milioni 1.5 na shilingi bilioni 15.695 na huku lot ya pili ikiwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 1.915 pamoja na shilingi bilioni 17.958. Ikumbukwe kwamba, ikiwa kampuni ya kigeni kama hii ya Joe’s hata kama ina daraja la I, lakini akishakuwa na mbia mtanzania ambaye hana usajili, basi wanakosa sifa ya kupewa zabuni lakini, kama ambavyo inaonekana hapa, kampuni hii ilipewa zabuni ya ushindi wa lots mbili.

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Nipo Group Limited inausajili bodi ya usajili wa wakandarasi wa Daraja la V, kampuni hii haina mbia lakini ilipewa zabuni yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2.011 na kiasi kingine cha sh bilioni 15.545. Kampuni hii ilipewa zabuni hii ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya kazi za kiwango cha gridi na hivyo kama zilivyo kampuni nyingine pia  uwezo wake unatiliwa mashaka.

Mheshimiwa Spika, ni vyema ikaeleweka kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani haipingi wazawa wala wageni kupewa zabuni za ujenzi, tunachotaka kuona ni taratibu zote zinazingatiwa. Hivyo, kutokana na uchunguzi huo makampuni yakayobainika kuwa yalipewa zabuni bila viwango ni vyema vigogo wote walio nyuma ya makampuni hayo wakajulikana na hatua zaidi zikachukuliwa.

    1. E. SEKTA YA GESI- NCHINI:
    2. 1. Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
Mheshimiwa Spika, Bomba la kusafirisha Gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam lilijengwa na Kampuni ya China Petroleum and Technology Development Company (CPTDC) kwa gharama ya takriban Dola za Kimarekani takriban bilioni 1.283 ambapo kati ya hizo, dola za Kimarekani bilioni 1.225 zilipatikana kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China. Marejesho ya mkopo huo yalitegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara. 
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kwamba bomba la gesi lilijengwa kabla ya kutafuta wateja na kusainiana mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wateja lengwa wa gesi asilia. Aidha mapungufu haya kwa vyovyote ile yanaathiri malipo ya mkopo kwa vile mauzo halisi ya gesi asilia yatakuwa chini ya kiwango cha makadirio ya awali cha futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku (mmscfd). 
Mheshimwa Spika, taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepata zinaonyesha kwamba, kwa sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndilo mteja mkuu wa gesi asilia; ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku, sawa na asilimia sita (6%) tu ya ujazo wa bomba; ambapo, kiasi hicho ni pungufu futi za ujazo milioni 737.39 kwa siku ili kujaza bomba. Matumizi haya ni tofauti na makubaliano ya awali ambayo ilikua TANESCO liweze kutumia takribani futi za ujazo milioni 80 kwa siku kama ilivyokuwa kwenye makubaliano ya mkataba wa mauziano ya gesi asilia (GA). 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inapenda kupata ufafanuzi kutoka Serikali kuhusu jitihada ambazo Serikali imechukua ili kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa Serikali. 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya TPDC na TANESCO uko wazi kwamba TANESCO itatumia gesi asilia kwenye mitambo yake sita (6) ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II, Tegeta na Symbion kwa kima cha chini cha matumizi cha futi za ujazo milioni 80 kwa siku na futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku kama kiwango cha juu. Hata hivyo, hadi sasa mtambo wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I ndio pekee unaotumia gesi asilia kuzalisha umeme; na unatumia kiwango asilimia thelathini na nne (34%) ya kiasi cha gesi yote iliyolengwa kutumiwa na TANESCO. 
Mheshimiwa Spika, Mitambo mingine mitano iliyokuwa imekadiriwa kutumia kiasi cha (66%) bado haijaanza kutumika; na haijulikani ni lini mitambo hiyo itaanza kutumia gesi asilia. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba, TANESCO bado ina mikataba ya muda mrefu na wazalishaji wakubwa wa umeme ambao ni kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Songas; ambapo mikataba yao inaisha mwaka 2022 kwa ule wa IPTL na mwaka 2023 kwa Songas. Hii inaiongezea TPDC na TANESCO ugumu kwenye kutimiza vifungu walivyokubaliana kwenye mkataba wa mauziano gesi asilia (GA). 
Mheshimiwa Spika, ni ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, mikataba ya makampuni yaliyotajwa hapo juu haina maslahi kwa taifa na hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazitaka TPDC, TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini wajadiliane ni kwa namna gani mitambo ya uzalishaji umeme ya TANESCO itaweza kumalizika kwa haraka ili bomba la gesi litumike kwa ufanisi na kuweza kulipa mkopo wa bomba la gesi kutoka Benki ya Exim ya China kwa wakati. 
Pia, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuliambia Bunge lako tukufu, Ni jitihada gani Serikali imefanya kutafuta wateja zaidi wa gesi asilia ili kuongeza mapato ya gesi na kuiwezesha TPDC kutimiza wajibu wa kulipa madeni? 
    1. 2. TANESCO kudaiwa na TPDC Ankara za Mauzo kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 61.35 
Mheshimiwa Spika, taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba mnamo tarehe 31 Oktoba 2013, TPDC na TANESCO walisainiana mkataba wa TPDC kuiuzia gesi asilia TANESCO. Katika mkataba huo pia, kulikuwa na makubaliano kwamba Serikali iweke dhamana benki kiasi kinachoweza kulipa mauzo ya gesi kwa miezi mitatu au zaidi kwa ajili ya TPDC huku dhamana hiyo ikitakiwa kuwapo hadi pale madeni yote ya TANESCO yanayohusiana na kuuziana gesi asilia yatakapolipwa. 
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijafahamu, Serikali haikuweka dhamana hiyo kinyume na makubaliano hayo. Aidha, hadi kufikia mwezi Desemba 2016, jumla ya deni la mauzo ya gesi asilia kiasi cha dola za kimarekani milioni 61.35, sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 133.4, kimelimbikizwa bila kulipwa na TANESCO. 
Mheshimiwa Spika,hali ya TANESCO kuchelewa kuilipa TPDC, inasababisha TPDC kuchelewa kuyalipa makampuni yanazouza gesi. Na hivyo kuongeza hali ya sintofahamu kwenye ulipaji wa mkopo kutoka benki ya Exim ya China. Kuchelewa huku kwa malipo kunaweza kusababisha gharama zaidi za riba ambayo itatakiwa kulipwa na TPDC kwa wadai wake. 
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kufahamu nini mpango wa Serikali kupitia TPDC wa kuhakikisha inalipa madeni kutoka kwa wauzaji wa gesi na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China ili kuepuka kulipa riba kubwa hapo baadaye.
    1. 3. Kuzuiliwa kuingia kwa Gesi ya Tanzania nchini Kenya
Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni, Serikali ya Kenya imepiga marufuku uingizwaji nchini humo wa gesi ya kupikia kutoka Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya, Kenya ilipiga marufuku uingizwaji wa gesi kutoka Tanzania ndani ya siku saba kuanzia tarehe 24 Apri, 2017. Uamuzi wa Kenya ni kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania na Kenya ni wanachama. Aidha kwa mujibu wa itifaki ya soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, bidhaa kutoka nchi wanachama zinaruhusiwa kusambaa ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya hii.
Mheshimiwa Spika, Uamuzi wa Kenya kuzuia Gesi kutoka Tanzania ni uamuzi ambao kwa vyovyote vile unalenga kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika mashariki na kuwazuia watanzania wanaofanya bishara hii nchini Kenya, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu, inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi ndani ya Bunge lako tukufu kuhusu 
    1. i. Hatua ambazo imechukua kwa kuhusisha Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wizara ya Viwanda na Biashara ili kuwanusuru watanzania wanaofanya biashara hii nchini Kenya na kuhakikisha mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na pamoja na itifaki ya Masoko ya pamoja havivunjwi?
    2. ii. Ikiwa Kenya inafanya hivyo kwa kulinda Bandari yao ya Mombasa, bidhaa zake za ndani pamoja na wafanya biashara wake, na kwa kuwa kwa kufanya hivyo Kenya imevunja mkataba na itifaki za soko la pamoja, je Serikali inachukua hatua gani za kisheria dhidi ya kitendo cha Kenya kuzuia bidhaa kutoka Tanzania na nini hatma ya bidhaa za Kenya zilizo kwenye soko la Tanzania?

    1. F. KIGUGUMIZI CHA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KURUHUSU UWEKEZAJI KATIKA UZALISHAJI WA UMEME KWA KUTUMIA NISHATI JADIDIFU (RENEWABLE ENERGY) KATIKA TEKNOLOJIA ZA UPEPO NA JUA (WIND &SOLAR ENERGY)

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa la uwekezaji katika uzalishaji wa nishati jadidifu kwa kutumia teknolojia ya jua na upepo, licha ya nchi yetu kuwa na rasilimali jua na upepo wa kutosha. Kutokana na uwepo wa rasilimali hizo, wapo wawekezaji ambao wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika uzalishaji wa nishati hiyo, lakini Wizara ya Nishati na Madini imekuwa haitoi ushirikiano kwa wawekezaji hao, jambo ambalo linairudisha nyuma sekta ya nishati nchini.

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa umeme kwa kutumia teknolojia ya jua na upepo, unaweza  kutoa mchango mkubwa wa umeme katika gridi ya taifa kwani tunazo rasilimali  jua na upepo  za kutosha  kuliko hata majirani zetu. Nchi yetu  inayo sera na sheria za kuendesha teknolojia hizi, lakini  tunajiuliza kwa nini wizara inazuia sekta hii kuendelea?

Mheshimiwa Spika, EWURA wamefanya kazi iliyogharimu taifa ya kutengeneza kanuni za uzalishaji wa nishati jadidifu kwa wazalishaji wadogo (Small Power Producers – SPP Regulations) ambazo  zilizokwisha kukamilika tangu July, 2016. Kanuni hizo zinaitwa “the Second Generation Small Power Producers Regulations”  Regulation hizi zimeainisha uzalishaji wa umeme katika teknolojia za upepo na jua katika makundi makuu matatu:

    1. i. Kiwango cha  0 – mpaka Mega Watt 1 (0 – 1MW)
    2. ii. Kiwango cha  kuanzia  Mega Watt 1 – mpaka Megawatt 10 (1  – 10 MW)
    3. iii. Kiwango cha kuanzia  MegaWatt  10 na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, hizi kanuni za Second Generation Small Power Producers’ ziliyofanyiwa kazi na EWURA zinaelekeza  makundi yote matatu yaliyotajwa hapo juu kuzalisha umeme kwa kutumia  teknolojia hizi na kuuza kwenye grid ya taifa kwa taratibu zilizoelekezwa kwenye sheria ya Umeme Sura 131 kama ifuatavyo:

Kundi la 1: (0 – 1 MW)  litatumia “Feed-in Tarrif inayopangwa na EWURA kwa kuzingatia ukokotoaji uliozingatia gharama za uzalishaji kwa teknolojia hizi ambazo ni chini kuliko teknolojia zingine zinazotumiwa na TANESCO kwa sasa isipokuwa teknolojia ya maji (hydro) ambayo imeathiriwa sana na hali ya “ tabianchi”(climate change). Kwa kiasi kikubwa aina hii haina matatizo mengi kwa sababu inashughulikiwa na EWURA na TANESCO bila kulazimisha urasimu wa Wizara.

Kundi la 2: (1 MW – 10 MW) ambayo ndio inategemewa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza renewable energy kwenye grid ya taifa, sheria hii inaelekeza kufuata utaratibu wa “Competetive bidding”). Sheria hii itaipa Serikali/Tanesco kuchagua kwa kupitia zabuni za wazi, mwekezaji mwenye uwezo kiteknolojia, kifedha na mwenye kuahidi kuuza umeme kwenye gridi ya taifa kwa bei yenye maslahi kwa taifa kupitia SPPA (Small Power Purchasing Agreement). 

Mheshimiwa Spika, Utaratibu huu ulishatangazwa na EWURA kwa wawekezaji wa teknolojia hizi wa ndani na nje kwa takribani Zaidi ya mwaka mzima sasa. Wawekezaji hawa hadi sasa wamekwisha kutumia gharama nyingi  za kufanya maandalizi yaliyoelekezwa na EWURA kujiandaa kwa zabuni hizi; ikiwa ni pamoja na kufanya makubaliano ya Ardhi kubwa inayohitajika kwa miradi ya aina hii, na gharama nyingine nyingi zinazoambatana na uwekezaji wa miradi ya aina hii.

Mheshimiwa Spika, EWURA/na TANESCO wamekamilisha kazi yao na kukabidhi shughuli hii kwa wizara ya Nishati na Madini ambayo kila wawekezaji wakiwafuata kuulizia kinachoendelea wanajibiwa wasubiri. Hali hii inawakatisha tamaa wawekezaji wa teknolojia hizi, ambazo tunaamini zitaongeza umeme ulio rafiki kwa mazingira yetu kwenye gridi ya taifa, na umeme ulio na gharama nafuu ukilinganisha na wa kutumia mafuta. Miradi hii ndio inaweza kuwa upgraded kwa jinsi grid yetu ya taifa inavyokua na hatimae kufikia Megawatt 50 – 100 na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa na kitendo cha Serikali kuweka mkazo pekee kwenye miradi mikubwa ya upepo ya Singida na Makambako ambayo kiuhalisia haitakamilika hivi karibuni. Tafiti zinaonyesha kuwa hata wenzetu waliobobea katika teknolojia hizi walianza na miradi midogo midogo mingi ya 10 MW na ikawa upgraded taratibu hadi kufikia giant wind farms and solar farms.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Wizara ya Nishati na Madini iharakishe zabuni ya ushindani( Competetive bidding process) ya teknolojia hizi kama sheria ya EWURA inavyoelekeza ili kuwezesha kupatikana kwa teknolojia hizi tunazozihitaji  kwa ukombozi wa wananchi wetu kwenye sekta hii ya umeme usioharibu mazingira. 
Kundi la  3: Kwa mujibu wa  sheria  ya EWURA, EWURA haina udhibiti mkubwa.  Mwekezaji ameachiwa uhuru wa  kufanya majadiliano na TANESCO kuhusu PPA (Power Purchasing Agreement).Lakini sheria inawataka wakishakubaliana wakasajili PPA hiyo EWURA. Uzoefu unaonyesha miradi hii itatuchukua nchi hii miaka mingi kufanikiwa. Na mfano rahisi ni miradi mikubwa ya umeme wa upepo ya Singida na Makambako ambayo imegubikwa na migogoro mikubwa ya ardhi.

Mheshimiwa Spia, kwa kuzingatia taratibu za uzalishaji katika makundi yote matatu, wataalamu wengi wanashauri kuwa kipaumbele cha nishati jadidifu katika gridi yetu ya taifa  kwa kutumia upepo na jua ni katika Kundi la 2, ambalo linaruhusu wawekezaji kuomba kufanya uzalishaji kwa kutumia zabuni za wazi – competitive bidding.

    1. G. SEKTA YA MADINI

Mheshimiwa Spika, sekta ya madini inahusu utafutaji na uchimbaji wa madini. Nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini, lakini mchango wa sekta kwenye uchumi hauridhishi.  Pamoja na maoni ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tumeyatoa kupitia hotuba hii kwenye kipengele kuhusu makinikia ama ‘mchanga wa dhahabu’ yapo masuala ya ziada ambayo ni vyema Wizara ya Nishati na Madini ikayatolea majibu kama ifuatavyo.

    1. 1. Mapungufu katika Mikataba ya uchimbaji Madini 
Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi kirefu yamekuwepo malalamiko yanayohusu mikataba ya uchimbaji madini ambayo Serikali iliingia na wawekezaji wa makampuni ya uchimbaji wa madini.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba baadhi ya mikataba ya madini iliyoingiwa kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania na makampuni ya madini ni pamoja na mikataba kati ya kampuni ya Geita Gold Mining (GGM) inayoendesha mgodi wa dhahabu wa Geita, na Kampuni ya ACACIA inayoendesha migodi ya Buzwagi, Bulyanhulu na Mara Kaskazini. 
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba, mikataba ya madini mingi ina vifungu visivyolinda maslahi ya umma, vifungu hivyo ni pamoja na vile vinavyoweka masharti yasiyoridhisha katika kuongeza mikataba, vifungu vinavyozuia mabadiliko ya sheria kuathiri mikataba husika, sera zisizoridhisha kwenye fedha za kigeni na forodha, motisha za kodi zilizozidi, kwenye taratibu za kihasibu katika kutambua na kukokotoa  matumizi ya mitaji. 
Mheshimiwa Spika, Kutokana na mapungufu hayo yaliyoko kwenye mikataba ya uchimbaji wa madini, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali;
    1. i. Kuacha kulalamika na badala yake itumie kifungu kinachoruhusu kurejewa kwa mikataba kinachopatikana kwenye mikataba mingi ya madini ili kurejea makubaliano yaliyoafikiwa na kuhakikisha kuwa Serikali inajiepusha na kutoa matamko ya potofu ambayo yanaenda kinyume na matakwa ya mikataba husika. 

    1. ii. Aidha ili kuhakikisha maslahi ya Taifa na maslahi hayaathiriki ni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa Serikali iyaite makampuni ya wawekezaji kwenye madini na kujadiliana nayo jinsi ya kufanya marekebisho yanayohitajika.

    1. iii. Serikali iboreshe usimamizi kwa makampuni binafsi yanayofanya kazi za kutafuta na kuvumbua miamba yenye madini ili kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa sahihi na za ziada zitakazoisaidia kwenye majadiliano na kufanya maamuzi. 
    1. 2. Madhaifu ya sheria za kukusanya mapato kwenye sekta ya Madini
Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi kirefu Taifa hili linakosa mapato yanayotokana na rasilimali za Taifa kutokana na sababu mbali mbali, ambazo miongoni mwake ni sababu zinazotokana na madhaifu ya sheria zetu. Aidha miongoni mwa sheria ambazo zinachangia Taifa kukosa mapato kwenye sekta ya Madini ni pamoja na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Kwa mujibu wa sheria hii, kifungu cha 55(1) cha sheria hii, kinatoa mwanya kwa migodi ya uchimbaji wa madini kupewa marejesho ya Kodi ya VAT. Sheria hii, sawa na sheria za zamani kwa pamoja zinaruhusu tozo ya kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha sifuri kwa bidhaa zinazosafirishwa kuuzwa nje ya nchi.
Mheshmiwa Spika, Ni wazi kwamba soko kubwa la Madini liko nje ya nchi na kwa sababu hiyo madini yote yanayopatikana yanauzwa nje ya nchi. Hii inapelekea kodi inayotokana na manunuzi ya bidhaa za mtaji, mafuta na gharama nyingine yanayofanywa na makampuni ya migodi ndani ya nchi kuzidi ile inayotokana na mauzo (Output Tax). Hivyo, migodi hiyo kustahili marejesho ya kiasi kilichozidi kutokana na kifungu cha 83(2) cha sheria ya Kodi ya ongezeko la Thamani.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali kutoza kodi ya ongezekeo la thamani kwa kiwango cha sifuri kwenye bidhaa zote zinazosafirishwa kuuzwa nje ya nchi ilikuwa ni kukuza viwanda vya ndani. Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inazo zinaonesha kwamba migodi mikubwa minne (4) ya dhahabu Geita, Bulyanhulu, Mara Kaskazini, Pangea na mmoja wa Almasi wa Williamson kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia Mwaka 2012 ilirejeshewa marejesho makubwa ya kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiasi cha shilingi bilioni 1,144.
Mapungufu yanayoonekana ni kwa Sheria hiyo kutokuweka makundi ili kuonyesha ni bidhaa zipi zinazostahili motisha hiyo na hivyo kusababisha madini ambayo kwa namna yoyote lazima yauzwe nje ya nchi nayo pia kunufaika na motisha hiyo kama vile ambavyo bidhaa za kilimo na viwandani zinavyonufaika. Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu;
    1. i. Ni lini hasa Serikali italeta ndani ya Bunge lako tukufu Mabadiliko ya sheria ya Ongezeko la thamani VAT ili kuondoa tozo ya kiwango cha sifuri kwenye mauzo ya madini na vito nje ya nchi kwa kuweka makundi yanaoonesha ni bidhaa zipi zinazostahili motisha ya tozo ya kiwango cha sifuri na kuziacha bidhaa za kilimo na Viwanda zikiendelea kunufaika?
    2. ii. Kwa kuwa mabadiliko ya sheria hii, yataathiri mikataba iliyopo kati ya Serikali na makampuni ya Uchimbaji Je, Ni lini Serikali itaanzisha majadiliano na makampuni ya uchimbaji madini kuhusu matokeo ya mabadiliko hayo kwenye Mikataba yao (MDAs)? 
    1. 3. Utofauti wa Kodi kwenye sekta ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Sote tunafahamu kwamba mikataba ya uchimbaji madini kati ya Serikali na makampuni ya uchimbaji katika migodi ya dhahabu ya Mara Kaskazini, Geita, Buzwagi na Bulyanhulu ilisainiwa kabla Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 haijatungwa, isipokuwa mkataba wa uchimbaji wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliosainiwa 2007. Kwa muktadha huo viwango vya tozo za kodi katika mikataba hiyo vilitokana na sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 na havijabadilishwa kuendana na sheria mpya kutokana na kuwapo kwa kifungu kinachozuia mabadiliko ya viwango vya tozo za kodi kwenye mikataba hiyo. 
Mheshimiwa Spika, Ifuatayo hapa chini ni baadhi ya mifano inayotokana na baadhi ya maudhui ya mikataba hiyo;
    1. i. Mikataba hiyo inaainisha viwango vya zuio la kodi katika ada ya usimamizi pamoja na huduma za kiufundi kati ya asilimia 3 mpaka 5. Hali hii ni tofauti na matakwa ya Sheria ya Kodi ya Mapato ambayo inataka viwango vya zuio la kodi katika ada ya usimamizi pamoja na huduma za kiufundi kuwa asilimia 15.
    2. ii. Mikataba hiyo pia inataka ushuru wa halmashauri ulipwe kwa kiwango kisichozidi Dola za Kimarekani 200,000 kwa mwaka. Takwa hili pia ni kinyume na kifungu cha 6 (1) (u) cha sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 inayotaka ushuru wa ndani ulipwe kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mauzo ya mwaka. 
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mifano tajwa hapo juu ni ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa Serikali inapaswa kujadiliana na makampuni ya uchimbaji madini kupitia kifungu cha utakaso wa mkataba kinachopatikana kwenye mikataba takribani yote ili kurekebisha viwango vya tozo za kodi kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi vinavyobadilika kufuatana na muda tangu kusainiwa kwa mikataba hiyo na hivyo kuliwezesha Taifa kupata mapato yanayostahili kulingana na rasilimali hii.

    1. 4. Misamaha ya tozo na Ushuru, sekta ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Misamaha kwenye tozo na ushuru wa mafuta ilitolewa kwa makampuni ya madini ili kuyapunguzia gharama za uzalishaji umeme kwa ajili ya kuendeshea mitambo. Kifungu cha 8 cha Sheria ya Tozo za Ushuru wa Mafuta na Barabara ya mwaka 1985 kinampa Waziri wa Fedha mamlaka ya kutoa msamaha wa tozo ya ushuru wa mafuta kwa kutangaza kwenye gazeti la Serikali. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba Serikali, kupitia gazeti la Serikali Namba 190 lililochapishwa tarehe 15 Julai 2011, ilitoa msamaha wa tozo ya ushuru wa mafuta kwenye mafuta yanayoagizwa au kununuliwa na makampuni makubwa ya madini yanoyojihusisha na uchimbaji wa dhahabu nchini. 
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa toleo hilo, Serikali pia ilibatilisha matoleo yote yaliyowahi kutolewa awali kuhusu misamaha ya kodi; na tangazo hilo likaweka utaratibu wa kutumiwa na makampuni husika ili kuweza kupata msamaha huo. Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba migodi mikubwa minne ya Geita Gold Mine, Bulyanhulu, Buzwagi na Mara Kaskazini inayojihusisha na uchimbaji wa dhahabu nchini imesamehewa tozo za ushuru wa ndani na mafuta kiasi cha shilingi bilioni 126.7 kwa mwaka 2015 na 2016. 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia ushauri iliotoa kwenye mgodi uliochini ya STAMICO kwamba, Serikali, kupitia Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, kuhakisha inapeleka umeme kwenye migodi mikubwa nchini ili kuiondolea Serikali sababu za kusamehe kodi kwenye mafuta. Kitendo cha kuipelekea migodi umeme, kitasaidia kuongeza mapato kwenye Serikali yatayotokana na kuuza umeme kwenye makampuni hayo. 
5. Misamaha ya kodi za Mafuta yanayonunuliwa nje kwa matumizi ya uchimbaji wa madini: 1URAYA Ta yaN

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 190 na 191 la mwaka 2011 na jedwali la tatu la sheria ya kodi ya ongezeko la thamani ya mwaka 1997 limetoa msamaha wa malipo ya ushuru wa bidhaa, ushuru wa mafuta, na kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta yanayoingia kwa lengo la kutumika katika migodi kwa ajili ya uchimbaji wa madini. 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa zinazoeleza kwamba mafuta yamekuwa yakisafirishwa kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea kunakodaiwa kuwa ni kwenye migodi ya uchimbaji wa madini lakini hakuna uthibitisho unaoonesha kwamba mafuta hayo yalifika katika migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu. Aidha Sehemu ya 2(g) ya jedwali la Tangazo la Serikali namba 190 na 191 la mwaka 2011 inasema kwamba tofauti yoyote inayosababishwa na kutokupokea mafuta yaliyotoka katika makampuni ya masoko ya mafuta, ukaguzi, matumizi ya mafuta kwa mtu mwingine zaidi ya makampuni ya migodi au matumizi yoyote yasiyokusudiwa yanatakiwa kutozwa kodi itakayokatwa kutoka kwenye akaunti ya escrow.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kufahamu hatua ambazo Serikali inachukua ili kuthibiti tabia hii ambayo inasababisha ukosefu wa mapato yanayotokana na kutolipiwa ushuru wa forodha.
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa pia zinazohusu mapungufu yaliyojitokeza katika uondoshaji wa mafuta ya migodini kwa kutumia maghala yanayohifadhi bidhaa zinazosubiri kulipiwa kodi.  Ikumbukwe kwamba, Kifungu 74-75 cha Kanuni ya Ushuru wa Forodha Afrika Mashariki ya mwaka 2010 inahitaji mlipa kodi kupata leseni na kutimiza masharti yote yaliyoainishwa katika kifungu 74(1-4) na 75(1-2) ili kuweza kuendesha ghala linalohifadhi bidhaa zinazosubiri kulipiwa kodi. Zaidi ya hayo, kifungu 76 kinahitaji mmiliki leseni wa ghala linalohifadhi bidhaa zinazosubiri kulipiwa kodi kutekeleza dhamana kwa bidhaa zinazohifadhiwa katika ghala linalohifadhi bidhaa zinazosubiri kulipiwa kodi
Mheshimiwa Spika, taarifa zaidi zinasema kwamba lita 3,500,000 za mafuta ya petroli yaliyonunuliwa na kampuni ya mafuta ya Oryx na yaliondoshwa kupitia TANSAD yenye kumbukumbu namba TZSR-14-1171746 ya tarehe 10/12/2014. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka ufafanuzi kuhusu maswala yafutayo:
    1. i. Kama Serikali inaouhakika na ushahidi kwamba M/S Oryx Oil Company Limited ilikuwa na leseni ya kuendesha ghala linalohifadhi bidhaa zinazosubiri kulipiwa kodi; 
    2. ii. Serikali inasema nini kuhusu mizigo iliyookolewa chini ya usimamizi wa ghala linalohifadhi bidhaa zinazosubiri kulipiwa kodi bila dhamana kinyume na kifungu 76 cha Kanuni ya ushuru wa forodha Afrika Mashariki ya mwaka 2010; 
    3. iii. Serikali inao uhakika na ushahidi kama lita 49,046 za mafuta ya petrol zilihamishwa kwenda kampuni ya migodi (North Mara) na kampuni ya mafuta ya Oryx; na kama sivyo, inachukua hatua gani kwenye jambo hili.
    4. iv. Kwa kuwa taarifa zinasema kwamba Oryx ndiye muingizaji wa mafuta; na siyo North Mara ambaye alifuzu kupata msamaha wa kodi, Serikali imechukua hatua gani dhidi ya Oryx?
    1. 6. Kampuni ya STAMICO na mgodi kutopatiwa umeme na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia STAMICO, ilichukua mgodi wa dhahabu wa Tulawaka kutoka kampuni ya Afrikan Barrick  Gold (ABG). Mkataba wa kuhamisha umiliki ulifikiwa tarehe 15 Novemba, 2013 na jina la mgodi likabadilika toka mgodi wa Tulawaka kwenda mgodi wa Biharamulo. Hata hivyo ili kuendesha mgodi, STAMICO iliunda kampuni mpya kwa jina la STAMIGOLD. 
Mheshimiwa Spika, Kwa taarifa zilizopo kuhusu ufanisi wa mgodi chini ya usimamizi wa kampuni ya STAMIGOLD ni kwamba, Wizara ya Nishati na Madini imechelewesha ruhusa ya Leseni Kubwa ya Uchimbaji Madini kwenda STAMIGOLD. Kwa mujibu wa Kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Madini ya 2010 kunahitaji kuwepo kwa kibali cha maandishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini kabla umilikishwaji wa leseni kubwa ya kuchimba madini haijaamishwa kutoka kwa kampuni moja kwenda nyingine. Taarifa zinaonesha kuwa baada ya STAMIGOLD kuchukua mgodi walihitaji pia kurithi mkataba uliokuwepo awali kati ya Afrikan Barrick  Gold (ABG) na Serikali ili nao waweze kupata faida na motisha alizokuwa anapata muendeshaji wa awali. 
Mheshimiwa Spika, kuchelewesha kutoa kibali cha kuhamisha leseni ni kuwanyima haki STAMIGOLD kutumia fursa kama vile misamaha ya kodi zinazopatikana kwenye mkataba waliorithi kutoka African Barrick Ltd kuna athari za kiutendaji kwa Kampuni hii ya Umma ukilinganisha na manufaa wanayopata makampuni binafsi kwa mfano msamaha wa kodi ya mafuta (Fuel levy & excise duty) 
    1. 7. Mgodi kutopatiwa umeme na TANESCO
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na hitaji la muda mrefu la mgodi kuunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa na au kupatiwa umeme kutoka shirika la umeme nchini TANESCO bila mafanikio. Aidha kwa sasa mgodi unatumia umeme unaozalishwa kwa kutumia majenereta. Taarifa ya kila mwezi ya uendeshaji mgodi inaonyesha kuwa mahitaji ya umeme kwa mwezi mgodini ni takriban kilowati milioni 1.1 ambazo zinazalishwa na lita 300,000 za mafuta ya dizeli ambayo inagharimu takriban shilingi milioni 670. Kwa Uchambuzi uliofanywa na STAMIGOLD unaonyesha kuwa hizo kilowati zinazohitajika kama zikipatikana kutoka TANESCO, gharama zake ni takribani shilingi milioni 273.79 (gharama ikihusisha tozo zote zilizopo kwenye umeme kama VAT (18%) REA (3%) na EWURA (1%) 
Mheshimiwa Spika, Kwa kutumia umeme wa TANESCO, STAMIGOLD itaokoa karibia nusu ya gharama inazoingia sasa kuzalisha umeme wa mafuta. 
Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inapenda kupata ufafanuzi kutoka Serikalini kuhusu mgodi huu kama ifuatavyo:
    1. i. Ni lini Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini itakamilisha mchakato wa kuipatia STAMIGOLD kibali cha kutumia mkataba wa kuchimba madini aliokuwa anautumia Afrikan Barrick Gold (ABG).

    1. ii. Kwa kuwa mgodi huu ukiunganishwa kwenye gridi ya Taifa, kutasaidia kupungua kwa gharama hizi na kupelekea mchango chanya kwenye faida ya kampuni na mapato kwa taifa. Je, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, itaunganisha lini mgodi wa STAMIGOLD kwenye gridi ya taifa ili kuupunguzia gharama za kujiendesha; na hivyo, kuuongezea fursa ya kupata faida kwa mgodi huu?

    1. iii. Kwa kuwa migodi mingine mikubwa na ya kati inapata msamaha wa kodi ya mafuta (fuel levy & excise duty) Je, Serikali itatoa lini msamaha huo ili mgodi huu upate msamaha sawa na migodi mingine?

    1. 8. Mgodi wa MMG Gold Ltd
Mheshimiwa Spika,  kuna Mgodi unaoitwa MMG Gold Ltd, upo kwenye kijiji cha Seka, Jimbo la Musoma Vijijini kilometa zipatazo 42 kutoka Bunda mjini, ukiwa unaelekea upande wa Ziwa Victoria. Kimsingi, mgodi upo karibu sana na Ziwa, hata maji ya kufanyia shughuli zake wanavuta kutoka ziwani. MMG Gold Ltd ni Kampuni Tanzu ya Kampuni ya MUTUS LIBER INTERNATIONAL LTD (MLI) yenye makao yake makuu Dubai –Falme za Kiarabu na inafanya kazi zake nchini Ghana, Djibouti, Kenya, Madascar na Oman.

Mheshimiwa Spika, uendeshaji wa mgodi huo bado unaendeshwa kama vile ni mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo, kwa maana kwamba watumishi/wafanyakazi wao hawapo kwenye mfumo wa hifadhi za jamii, hawakatwi kodi ya mshahara na hivyo Serikali kupoteza mapato yake. Na mbaya zaidi ni kwamba “Gold Pregnant Carbon” zinaenda kuchomwa Mwanza kinyemela na hivyo kutokuwemo kwenye mfumo rasmi wa ukaguzi wa Wakala wa Madini (TMAA). 

Mheshimiwa Spika, Mgodi huu bado ni mpya na kama taasisi zetu za ukaguzi na uthibiti utashindwa kufanyakazi kama inavyotakiwa ni dhahiri kabisa, tutakuwa tunaambiwa kwamba mgodi unazalisha hasara na hivyo wanashindwa kulipa kodi ya makampuni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kwamba yale yote yanayoendelea katika Mgodi yanafahamika na Wizara hivyo tunaitaka Serikali ilieleze Bunge hadi sasa utendaji wa mgodi huo ukoje na kodi ya wafanyakazi (PAYE) inalipwa kwa kiwango gani?

    1. 9. Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira: 
Mheshimiwa Spika, Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira kwa sasa unamilikiwa na Serikali kupitia STAMICO. Kabla ya mwaka 2005, mgodi huu ulikuwa chini ya usimamizi wa STAMICO. Lakini kufuatia sera ya ubinafsishaji ya Chama Cha Mapinduzi, mwaka 2005, 70% za umiliki wa mgodi huu zilihamishiwa kampuni iitwayo 'Tan Power Resources Ltd'. Mwaka 2008 hisa zikachukuliwa na Serikali kupitia Msajili wa Hazina na umiliki wa mgodi huu ukarudishwa chini ya STAMICO mwaka 2014. Kwa taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira haujaanza tena kuchimba makaa ya mawe tokea ulipochukuliwa na Serikali. 
Mheshimiwa Spika, taarifa mbalimbali zinaonesha kuwa mgodi wa Kiwira unakumbana na vikwazo vya Kisheria, kwa mfano ipo changamoto inayohusu cheti cha hisa cha Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira (KCML) ambacho bado hakijahamishiwa STAMICO; na hivyo cheti hicho bado kinasomeka kwa jina la Tan power Resources Ltd. Kwa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba, hali hii imesababishwa na kitendo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania kutotoa hati ya kuthibitisha ulipaji wa kodi (tax clearance certificate) kwa kampuni ya Tan power Resources. 
Mheshimiwa Spika, madhara ya kutobadilishwa kwa jina hilo, kulipelekea Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa mujibu wa kifungu 18(2)(b) cha Kanuni za Ukaguzi na Tathmini ya Athari za Mazingira (the Environmental Impact Assessment and Audit Regulations) 2005, kuikataa taarifa ya Tathmini ya Athari za Mazinigra ya STAMICO (Environmental Impact Assessment (EIA) report) kwa sababu hati ya hisa za kampuni hii ilikuwa bado inasomeka kwa jina Tan Power Resources Ltd. 
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kukosekana kwa hati ya umiliki yenye jina la STAMICO inakwamisha juhudi za shirika kuendeleza mgodi na pia inawia vigumu shirika kuingia ubia na wawekezaji wengine, Je Serikali, kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inafanya juhudi gani kuhakikisha hati ya kutodaiwa inapatikana na hati hiyo ya hisa inatolewa kwa jina la STAMICO. 
Mheshimiwa Spika, changamoto za kiutendaji zinazoukabili mgodi wa makaa ya mawe ya Kiwira ni pamoja na ukweli kwamba toka mgodi huu uhamishwe STAMICO mwaka 2014, hakuna fedha za maendeleo zimewahi kupelekwa. Suala hili limesababisha kushindwa kuanza kuzalisha. 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inataka kufahamu ni lini Serikali itapeleka fedha katika mgodi huu kama ambavyo zimekuwa zikipangwa lakini hazipelekwi huko? Pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka majibu kujua ni lini Kiwira italipa shirila la umeme TANESCO deni la muda mrefu la kiasi cha shilingi bilioni 1.8.?
    1. 10. Mgodi wa Cata Mining Company

Mheshimiwa Spika, kuna kampuni ya uchimbaji madini inayoitwa CATA MINING COMPANY LTD yenye Mining License Na. 483/2013, inayofanya shughuli zake katika eneo la Kiabakari, Wilaya ya Musoma Vijijini. Kampuni hiyo iliyokuwa na leseni 16 za uchimbaji mdogo (Primary Mining License-PML) zilizokuwa zinamilikiwa na Ndugu MAHUZA MUMANGI  NYAKIRANG’ANI.

Mheshimiwa Spika,  wananchi wa vijiji vya Kiabakari na Nyamisisye wanalalamika kuhusiana na uharibifu wa nyumba zao takriban mia saba (700)  uliotokana na milipuko ya baruti za kupasua miamba na hivyo kupata hasara kubwa sana. Aidha,wananchi hao wanatuhumu pia kwamba sehemu ya uchimbaji huo unafanyika ndani ya Kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania. Kwa mujibu wa ramani ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani inayo nakala eneo la uchimbaji linaonekana kuwa ni kijiji cha Kyawazaru/Katario na Kitongoji cha Kyarano na si eneo la jeshi lililoko kijiji cha Nyamisisye.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inazo taarifa kwamba  Wizara ya Nishati na Madini ilishapewa malalamiko hayo lakini hajayapatia ufumbuzi unaostahili.  Hivyo, Waziri atoe maelezo Bungeni ni kwanini ameshindwa kumaliza mgogoro huo mpaka sasa?

    1. 11. Wachimbaji wadogo wadogo
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa changamoto zilizoko katika sekta hii ni pamoja na changamoto zinazowahusu wachimbaji wadogo wadogo. Pamoja na maelezo ya Serikali kuhusu hatua ambazo Serikali imekuwa ikichukua dhidi ya kundi hili lakini bado uchimbaji mdogo wa madini umekuwa ukiendelea kwa kutumia nyenzo na teknolojia duni ya uchimbaji na kukosa taarifa sahihi za mashapo katika maeneo wanayochimba. Pamoja na kutengwa kwa maeneo machache ya wachimbaji, kupewa leseni za uchimbaji lakini bado wachimbaji wadogo wadogo wanapewa maeneo ya kuchimba bila kuwa na uhakika wa uwepo wa madini kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa wakipata mikopo kidogo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za uchimbaji na kwa kuwa Serikali imekuwa ikiwatengea maeneo machache ya kufanya uchimbaji huo lakini baada ya muda wachimbaji wanalazimika kuhama maeneo hayo kwa kile wanachodai maeneo hayo hayana madini. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata maelezo ya Serikali ni lini sasa Serikali itasaidia kufanya utafiti wa awali kwenye maeneo ili wanapokuja kuwagawia wachimbaji wadogo wadogo hawa, uwepo uhakika kwa wachimbaji wadogo wadogo hao kupata madini kipindi wakipewa maeneo husika?

    1. 12. Ukaguzi wa Mazingira Migodini
Mheshimiwa Spika, uchafuzi wa mazingira migodini ni tatizo ambalo linaikumba migodi mingi iliyopo hapa nchini. Wakati swala la mazingira lipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais,  Wizara ya Nishati na Madini pia inahusika na madhara ya mazingira yanayotokana na shughuli za uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo wadogo, wachimbaji wa kati pamoja na wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini (Tanzania Mineral Audit Agency) zilisaini hati za makubaliano na baraza la taifa la mazingira NEMC ili kuwawezesha TMAA kufanya ukaguzi wa uchafuzi wa mazingira migodini. Hata hivyo taarifa inaonesha kwamba mara nyingi migodi inapokuwa inafanya uchafuzi wa mazingira hutozwa faini kulingana na uchafuzi ulifanywa na kutakiwa kumaliza tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, mgodi wa Tulawaka Gold Mines Project uliwahi kukutwa na tatizo la kutiririsha kemikali na mgodi huo ulipaswa kulipa faini ya shilingi milioni 25 na mgodi ulilipa faini hiyo, aidha tatizo siyo ulipaji wa faini hiyo ila tatizo linaonekana kuwepo kwenye kutokusitisha uchafuzi huo wa mazingira. Mgodi wa Kilimanjaro Mine ltd ulitozwa faini ya shilingi milioni 6 lakini zililipwa mil 2 pamoja na kwamba kiwanda kiliomba NEMC kuwapunguzia adhabu. Migodi ambayo imewahi kutembelewa na kubainika matatizo ya uchafuzi wa mazingira ni pamoja na Golden Pride Ltd uliotozwa faini ya milioni 60 kutokana na kosa la kutiririsha uchafu wenye madhara, mgodi wa Bulyanhulu –kutiririsha uchafu hatarishi, mgodi wa North mara, Geita Gold Mines na mgodi wa Williamson Mines Ltd.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini- TMAA kwa kushirikiana na NEMC kuhakikisha inafanya ukaguzi kwa lengo la kuangalia ni kwa kiasi gani, matatizo yaliyopelekea migodi hiyo kutozwa faini yaliweza kuhitimishwa.

    1. H. UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA BUNGE
Mheshimiwa Spika, Bunge hili limekuwa likitoa maazimio mbalimbali yanayohitaji utekelezaji wa Serikali, lakini kwa bahati mbaya sana, Bunge limekuwa halipatiwi mrejesho wa utekelezwaji wa maazimio hayo. Tafsiri ya jambo hili ni dharau au ni kutokana na ukweli kwamba Bunge hili halina meno.
Mheshimiwa Spika, Bunge la 10 lilipitisha maazimio baada ya Kamati ya PAC kupitia taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kuhusiana na fedha za Capacity Charge ambazo TANESCO ilikuwa inatakiwa kuilipa IPTL lakini kukawepo na kesi ya kupinga kiwango hicho cha malipo na kulazimu fedha hizo ziwekwa Benki Kuu kwa kufungua akaunti iliyoitwa “Tegeta Escrow Account”.

Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Novemba, 2014 Bunge lilipitisha maazimio nane (8) kuhusiana na uporwaji wa mabilioni ya fedha za Serikali zilizokuwa zimewekwa Benki Kuu. Lakini azimio moja lilikuwa na uhusiano  wa moja kwa moja na utendaji wa TANESCO kwa kupunguza nguvu ya shirika nalo ni Azimio Namba 7- lililosema kwamba nanukuu “Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo”.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa Bunge halipewa taarifa ya utekelezaji wa azimio hilo na hadi sasa TANESCO bado inalipa kiasi cha shilingi bilioni 4.3 kila mwezi. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ni kwanini Serikali imeshindwa kutekeleza azimio hilo na kuendelea kumlipa mtu aliyeinunua IPTL katika mazingira yenye ufisadi?

Mheshimiwa Spika, Spika Anne Makinda aliunda Kamati Maalumu ya Bunge kwenda kuzungumza na wananchi wa Mtwara kuhusu sakata la ujengwaji wa bomba la gesi asilia kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam, kufuatia kuzuka kwa vurugu tarehe 22 Mei 2013. Kamati hiyo ya Mheshimiwa Spika Makinda ilikuwa chini ya Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM). 

Mheshimiwa Spika, Kamati hii ya Bunge ilitumia fedha za walipa kodi na ilifanya kazi na kuiwakilisha kwa Mheshimiwa Spik tarehe 20 Desemba, 2013. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Spika kuwezesha taarifa hiyo kuwasilishwa Bungeni ili mapendekezo ya kamati hiyo yajadiliwe na Bunge na kuwa maazimo rasmi ya Bunge na kuweza kutekelezwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, aidha yamekuwepo pia maazimio mengine ya Bunge juu ya uchunguzi kuhusiana na mapato kwenye gesi asilia hususani juu ya Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) ambayo nayo Serikali haijawasilisha Bungeni taarifa ya kuhitimisha utekelezaji. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuwasilisha taarifa maalum Bungeni juu ya utekelezaji wa maazimio yote ya Bunge yanayohusu Wizara ya Nishati na Madini ambayo hayajatekelezwa mpaka sasa.

    1. I. MWENENDO USIORIDHISHA  WA MPANGO WA UWAZI NA UWAJIBIKAJI KATIKA TASNIA YA UZIDUAJI TANZANIA-TEITI

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji(EITI) ni  wa kimataifa ulioanzishwa mwaka 2003 kwa utiwaji saini  kanuni 12 za uwazi katika malipo na mapato ya sekta ya uziduaji ili kuongeza uwazi katika uendeshaji wa tasnia  ya uziduaji. Mpango huu ni umoja wenye uwakilishi sawa baina ya Serikali, Makampuni na Asasi za kiraia.

Mheshimiwa Spika, Kimataifa, mpango huu unasimamiwa na Bodi ya Kimataifa yenye uwakilishi wa Serikali zinazotekeleza mpango huu, makampuni na asasi za kiraia zinazounga mkono uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uziduaji. Baada ya kusainiwa kwa kanuni hizo, mpango huu umeungwa mkono na asasi za kiraia, wawekezaji wakubwa karibia wote na mataifa 52 Tanzania ikiwemo. Tanzania ilijiunga na mpango huu tarehe 16 mwezi wa pili mwaka 2009 kwa tamko la Rais. 

Mheshimiwa Spika, toka Tanzania ianze kutekeleza mpango huu, wananchi wamepata fursa ya kupata baadhi ya taarifa za mapato yanayotokana na madini na gesi asilia, tofauti kati ya malipo yaliyofanywa na makapuni na mapato yaliyopokelewa na Serikali.  Pia taarifa juu ya makampuni gani yanalipa kodi kwa kiasi gani na yapi hayalipi tozo na kodi mbalimbali stahiki zimetolewa.

Mheshimiwa Spika, hii imesaidia ukuaji wa mapato kutoka kwenye sekta ya uziduaji kwani uwazi na uwajibikaji umeongezeka kiasi. Tanzania imekwisha toa ripoti 6 za mlinganisho wa malipo na mapato ya tozo na kodi mbalimbali ambazo zilifichua upungufu wa  takriban TZS  63,748,566,888.00 ambazo ni fedha za tozo na kodi zilizolipwa Serikalini kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi 2014 kama ifuatavyo:

2008/9 
                23,738,542,000.00 
2009/10
                   5,002,169,000.00 
2010/11*
11,000,000,000
2011/12
                   2,148,537,891.00 
2012/13
                12,920,549,420.00 
2013/14
                   8,938,768,577.00 
Total
                 63,748,566,888.00 

* Ripoti ya tatu imeondolewa kwenye mitandao yote kwa shinikizo la makampuni 

Mheshimiwa Spika, toka mpango huu uanze, fedha zilizoripotiwa kupotea zimekuwa zikipungua kila mwaka kama ilivyooneshwa hapo juu na mapato yaliyoripotiwa kupatikana yamekuwa yakipanda kama ifuatavyo; ripoti ya kwanza Bil. 128, ripoti ya pili Bil. 435,  ripoti ya tatu takribani Bil.500, ripoti ya nne takribani Bil.700, ripoti ya tano Bil. Takribani 900 na ripoti ya sita takribani Tril.1.2 fedha za kitanzania.  

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2015 mpango huu ulipewa nguvu ya kisheria kwani baadhi ya Taasisi na makampuni yalikuwa hayatoi ushirikiano ipasavyo. Pamoja na mapungufu yaliyopo kwenye Sheria, sheria imeunda Kamati ya kutekeleza mpango huo iitwayo Kamati ya TEITI chini ya kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania Na. 23 ya 2015. Chini ya Sheria hii, Kamati hiyo inapaswa kuwa  na Mwenyekiti anayeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wengine wasiopungua kumi na tano wakiwemo  watano wanaoteuliwa na Waziri wa Nishati na Madini (Serikali), watano kutoka kampuni za uziduaji na watano kutoka asasi za kiraia zinazojihusisha na masuala ya utawala bora katika tasnia ya uziduaji.  

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni za kimataifa za mpango huu na kifungu cha 8 cha Sheria hii, Kamati ya TEITA inapaswa kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu na wajumbe wanaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kingine kimoja tu. Kutokana na ukweli kuwa kamati hii ilianza kabla ya sheria kuanza, Kamati iliundwa mara ya kwanza mwaka 2009 na kumaliza muda wake mwaka 2012, uchaguzi na uteuzi wa wajumbe na mwenyekiti ulifanyika, japo baadhi ya wajumbe walirudi kwani kanuni ziliruhusu. Wajumbe hao wa mwaka 2012 walimaliza muda wao mnamo mwaka 2015 na uchaguzi na uteuzi wa wajumbe wengine ulifanyika mwaka 2016 kwa mujibu wa sharia ya TEITI. Mchakato huu uliingia doa kubwa la kisheria. 

Mheshimiwa Spika, kinyume na matakwa ya Sheria, hususan kifungu cha 5(1) kinachompa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Mwenyekiti, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo akiwa anafahamu hana mamlaka alimteua Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo nafasi ambayo haipo kisheria. Kaimu huyu ameendelea kuwepo na anaendesha shughuli za Kamati huku akiwa hana mamlaka kisheria na hivyo yote yanayofanyika chini yake ni batili licha ya fedha zinazoendelea kutumika kuyafanya hayo wakati wakitambua kuwa si halali mbele ya sheria.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kuwa Kamati ya Uteuzi ya Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI inayoundwa chini ya kifungu cha 6(1) iliitoa tangazo la wananchi kupeleka maombi ya kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti. Kinachoibua maswali  ni kuwa Kamati hii ya Uteuzi baada ya kufanya usaili na wananchi walioomba kujaza nafasi hiyo ilitoka na majibu kuwa wote walioomba hawana uwezo wa kuijaza nafasi hiyo. 

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Kamati ya TEITI tulitarajia, Kamati ya uteuzi ingelirudia zoezi hilo mara moja au kutumia njia nyingine bora ili ipendekeze majina kwa Rais kwaajili ya uteuzi.  Hadi leo, ni mwaka umekwisha pita  na hakuna lililofanyika. Inashangaza zaidi hata Kamati ya TEITI iliyoko madarakani inayoongozwa na Kaimu Mwenyekiti  ilipoomba kupata majina ya walioomba kujaza nafasi hiyo, mpaka leo haijawahi kupewa majina hayo ili ijiridhishe kuwa ni kweli hawana sifa, japo uchunguzi wa suala hili unaonesha kuwa CAG Mstaafu Utuoh ni mmojawapo wa watanzania walioomba kujaza nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, Katika mazingira hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa ni dhahiri kuwa Serikali haina utashi wa dhati wa kushiriki mpango huu wa uwazi na uwajibikaji? Na hata kama hakuna utashi wa kisiasa, je ni halali kuvunja sheria halali iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makusudi?

Mheshimiwa Spika, ni muhimu pia ikafahamika kuwa katika kifungu cha 10(2) cha Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji ya Mwaka 2015, Kamati ya TEITI imepewa majukumu makubwa na muhimu, baadhi yakiwemo ni kufanya uchunguzi wa jambo lolote linalohusu uziduaji ikiwemo viwango vya uzalishaji wa makampuni ya uziduaji. 

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, Waziri bila kuwa na mamlaka na kinyume cha sheria hususan kifungu cha 5(4) cha sheria hiyo Na. 23 ya 2015 hakutangaza mjumbe mmoja aliyechaguliwa kihalali na asasi za kiraia kama inavyotakiwa kisheria. Ifahamike kuwa, wajumbe watano toka asasi za kiraia wanapaswa kuchaguliwa na asasi za kiraia kwa utaratibu wao na kupelekwa kwa Waziri ili watangazwe kama walivyo na sio vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, bila kuwa na mamlaka na huku akivunja sheria, Waziri aliacha kutangaza jina moja la mwakilishi wa asasi za kiraia kutoka kwenye majina matano yaliyowasilishwa kwake bila kutoa sababu zozote. Tunafahamu kuwa yapo malalamiko ambayo yalipelekwa kwa Waziri juu ya mchakato wa kuwapata wawakilishi hao watano ila hata baada ya juhudi za  Waziri kueleweshwa juu ya kutokuwepo kwa uhalali wa malalamiko hayo kuliko fanywa na muungano wa asasi za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya uziduaji uitwao HAKIRASILIMALI, bado Waziri hakulifanyia kazi jambo hilo ambalo tarehe 30/05/2017 lilikamilisha mwaka. Pia ni vyema ikafahamika chini ya Sheria hiyo Namba 23 ya 2015, Waziri hana mamlaka kupokea rufaa za uteuzi wa wawakilishi wa asasi za kiraia wala wale wa kampuni za uziduaji.  

Mheshimiwa Spika, ukiacha uvunjaji huo wa sheria ya uwazi, Sekretariat ya TEITI imekumbwa na kashfa ya kimataifa ya wizi wa kimtandao ambayo inalichafua jina la Taifa letu kitaifa na kimataifa. Sekretariat ya TEITI iliingia mkataba na asasi ya Ujerumani-Open Oil, ikiwapa kazi ya kutoa mafunzo juu ya uwazi wa mikataba ya sekta ya uziduaji. Katika makubaliano yao, TEITI ilipaswa kuilipa Open Oil baada ya kutoa mafunzo.

Mheshimiwa Spika, Open Oil walimaliza kazi yao na kudai malipo ambayo inasemekana yalilipwa kwa njia ya mtandao kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwenda kwenye akaunti namba 26110562 iliyopo benki ya Llyods ya mjini London, Uingereza inayosemekana ni ya Open Oil UG baada ya mazungumzo na mwakilishi wa Open Oil. Hata hivyo, baada ya muda sio mrefu, OpenOil walidai malipo yao na kuambiwa kuwa yalishalipwa. Baada ya uchunguzi wa awali wa Serikali, iligundulika kuwa domain name ya Open Oil ilikuwa imedukuliwa na hivyo malipo hayakwenda kwa mlengwa Open Oil. Serikali ilianzisha uchunguzi wa udukuzi huo kupitia Interpol lakini uchunguzi huo haujakamilika mpaka sasa toka mwaka 2016 ulipoanza huku kukiwepo na taswira ya udanganyifu kwa upande wa taasisi za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Uvunjwaji huu wa sheria katika uteuzi wa Kaimu Mwenyekiti na kutokutangaza Mjumbe wa tano aliyechaguliwa kihalali na asasi za kiraia na kutokufuatilia ipasavyo upotevu wa malipo ya Open Oil umelitia doa taifa letu na Serikali ya Awamu ya Tano kitaifa na kimataifa kiasi kwamba, Tanzania iko mbioni kuondolewa kwenye utekelezaji wa Mpango huu wa Uwazi na Uwajibikaji wa Kimataifa.

Maswali ya msingi kwa  Wizara ya Nishati na Madini ni kama ifuatavyo; 

    1. i. Je, Serikali inaelewa umuhimu wa kutatua matatizo haya mapema kwani ikichelewa Tanzania itaondolewa kwenye ushiriki wa mpango huu?
    2. ii. Je, Serikali inaweza kulihakikishia Bunge hili kuwa bado inathamini uwazi na uwajibikaji na hivyo bado inaunga mkono mpango huu.
    3. iii. Je, Serikali inaweza kulihakikishia Bunge hili ni lini itayatatua matatizo haya ikiwemo ni pamoja na kumtangaza mwakilishi wa tano wa asasi za kiraia, Rais kumteua mwenyekiti mahsusi wa Kamati hii nyeti na kukamilisha uchunguzi wa malipo ya Open Oil na kuchukua hatua?
    4. iv. Je, wizara inamelezo gani kuhusu kuondolewa mtandaoni kwa taarifa ya tatu ya TEITI (2011/12)? 

    1. J. MKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2017/ 2018
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara ya Nishati na Madini inakadiria kutumia jumla ya shilingi 998,337,759,500 ikilinganishwa na shilingi 1,122,583,517,000 zilizoidhinishwa na Bunge mwaka 2016/2017, sawa na upungufu wa 11%. Sababu zinazotolewa na Serikali za kupungua kwa Bajeti ni kupungua kwa makadirio ya fedha za nje kutoka shilingi 331,513,169,000 mwaka 2016/ 2017 hadi shilingi 175,327,327,000. 

Mheshimiwa Spika, madhara ya kukosekana kwa fedha za nje, yanaonekana kuendelea kuiathiri Bajeti ya Serikali hii kwa kuwa, kwa mujibu wa makadirio ya Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini, Wizara imetenga kiasi cha shilingi 938,632,006,000 ikilinganishwa na shilingi 1,056,354,669,000 zilizotengwa mwaka 2016/17, sawa na upungufu wa 11.1%. Aidha wakati mwaka huu 2017/2018 bajeti ya wizara hii ikipunguzwa asilimia 11.1%, bajeti ya 2016/2017 Wizara ya Nishati na madini ilipewa na hazina 404,120,668,889.00 sawa na 36% ya fedha zote za bajeti ya wizara hii iliyopitishwa 2016/2017.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inaona haya ni madhara ya Serikali kutopenda ushauri na kuona haipangiwi cha kufanya. Kwa muktadha huo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka majibu kutoka Serikalini kuhusu mambo yafuatayo:
    1. i. Ni sababu zipi za msingi zinazopelekea kupungua kwa fedha za nje kwenye Bajeti ya Wizara.
    2. ii. Miongoni mwa vyanzo vya fedha kutoka chanzo cha nje kilikuwa ni fedha kutoka Millenium Challenge Corporation, na MCC ilisitisha msaada wake kwa Tanzania kutokana na kukosekana kwa utawala bora, kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar na kuvunjwa kwa Haki za Binadamu, Je Serikali inachukua hatua gani za kuondoa sababu zilizopelekea wadau wa maendeleo kusitisha misaada yake kwa Tanzania likiwemo shirika la misaada la Marekani MCC

    1. K. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kusisitiza kama ambavyo imekuwa ikifanya katika hotuba zilizowahi kutangulia kwamba, sehemu kubwa ya matatizo ya Wizara ya Nishati na Madini yamechangiwa na yanaendelea kuchangiwa na sababu za kibinadamu ikiwemo ukosefu wa utashi wa kisiasa huku maswala muhimu yakiachwa. 
Mheshimiwa Spika, Taifa lilihitaji na bado linahitaji mabadiliko ya kimfumo ili kuwezesha hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti katika sekta nyeti za Nishati na Madini, pamoja na kuchukua hatua stahiki ili kuziwezesha sekta hizi za Nishati na Madini kuongeza pato la Taifa na kupelekea wananchi kuzifaidi rasilimali zao, kuliko matamko hewa ambayo yanalenga kupata umaarufu wa kisiasa, huku hatua zinazopaswa kuchukuliwa zikiachwa miaka nenda miaka rudi.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kuwashukuru wananchi wa jimbo la Kibamba na Wilaya mpya ya Ubungo kwa kukikataa Chama Cha Mapinduzi, nawashukuru kwa kunipatia ushirikiano wao katika kazi za kuwawakilisha kwenye vyombo vya maamuzi na kuhamasisha maendeleo jimboni kwetu. Kwa namna ya pekee Nitambue mchango wa Meya wetu wa Ubungo, Mheshimiwa Boniface Jacob pamoja na madiwani wote ambao hufanya kazi kwa niaba yangu jimboni ninapokuwa kwenye majukumu mengine ya kitaifa. Nawashukuru Viongozi mbalimbali kwa ushirikiano wao, viongozi wa kidini na kiroho na wanafamilia ya Marehemu Mzee wetu John Michael  Dalali kwa ushauri wao na kunipatia ujasiri wa kuendeleza uadilifu katika kusimamia ukweli, haki na ustawi wa jamii ya watanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hao, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naomba kuwasilisha!

……………………
John John Mnyika (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara ya Nishati na Madini

01/06/2017
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHESHIMIWA JOHN JOHN MNYIKA (MB), KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2016/2017 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/ 2018

(Inatolewa chini ya 99(9) ya kanuni za Bunge, Toleo la Mwaka, 2016)

  1. A. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Awali ya yote niungane na wenye mapenzi mema katika kuomba ulinzi wa mwenyezi Mungu wakati wa kutimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuishauri na kuisimamia Serikali kwa Wizara ya Nishati na Madini juu ya bajeti ya mwaka 2016/2017 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, nitumie fursa hii kuwatakia waislamu wote mfungo mwema katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, Nitambue mchango Mheshimiwa John Heche, Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini alioutoa katika maandalizi ya hotuba hii. Aidha tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona na kurejea katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa familia ya marehemu Mzee Philemon Ndesamburo, wanachama wa CHADEMA kote nchini, wananchi wa Moshi Mjini, wabunge na watanzania wote walioguswa na msiba huu. Marehemu atakumbukwa kwa mchango wake kama mmoja wa waasisi wa chama chetu, Mbunge Mstaafu na Mfanyabiashara Mashughuri. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema.

No comments: