Nimepokea
mwaliko wa kikao maalumu cha kikao cha fedha na uongozi wa tarehe 3/01/2014
kikao kufanyika tarehe 06/01/2013 saa nane mchana kujadili mapendekezo ya
kuongeza maeneo mapya ya utawala katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na ajenda
zingine.
Nimeonelea
tija kuwasilisha mapendekezo yangu kwa maandishi kwa umma na baadae katika
kikao tajwa. Kwa hatua hii, ni fursa kwa kila mwananchi kutoa maoni yake juu ya
haya;
Kwa ukuaji wa kasi wa Dar es Salaam ambao
ndiyo mji mkubwa nchini Tanzania, jiji kitovu cha biashara na viwanda ambalo
kadiri ya takwimu linakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni nne na nusu. Jiji
hili limeshika nafasi ya tatu katika miji inayokuwa kwa kasi barani Afrika na miongoni
mwa miji kumi inayokuwa kwa kasi duniani.
Ifahamike pia, Jiji la Dar es Salaam ndilo
linashikilia asilimia themanini na tatu (83%) ya mapato ya serikali kitaifa na
takribani asilimia sabini (70%) ya kodi zote zinazokusanywa nchini Tanzania.
Yafuatayo ndiyo mapendekezo yangu ya
wasilisho la nyaraka ya mapendekezo yaliyoletwa katika ofisi yangu toka
Manispaa ya Kinondoni;
Mosi, Pendekezo
la kutumia “Manispaa” badala ya “Wilaya”:
Kadiri ya wasilisho, imetumika pendekezo la
“wilaya”. Ningeshauri na kupendekeza kutokana na uhalisia na ukuaji wa kasi
kutumika kwa “Manispaa” badala ya wilaya.
Pili, Pendekezo
bora la mgawanyo wa Manispaa:
Katika wasilisho lenye uwepo wa mapendekezo
saba. Ninaungana na kuafiki utumiaji wa pendekezo la pili lililowasilishwa la
kuwa na Manispaa tano (5) ambazo ni;
i.
Manispaa
ya Ilala
ii.
Manispaa
ya Temeke
iii.
Manispaa
ya Kinondoni
iv.
Manispaa
ya Kigamboni
v.
Manispaa
ya Ubungo
Sababu
muhimu:
1.
Ukubwa
kijiografia: Kwa kuongeza wilaya mbili mpya yaani Manispaa ya Kigamboni na
Manispaa ya Ubungo hii itasaidia wilaya hizi kuweza kuhimili ukubwa wa eneo wa
kijiografia ambalo kwa sasa inaelemea wilaya hizi za sasa yaani Manispaa ya
Kinondoni na Manispaa ya Temeke.
2. Ukuaji wa kasi wa
jiji: Katika ukuaji wa kasi unaoendelea jiji la Dar es Salaam maeneo yaliyopo
katika wilaya hasa ya Kinondoni na Temeke ndiyo ambayo yanaongoza pia katika
ukuaji huo wa kasi wa kimakazi na shughuli za kiuchumi kama viwanda na
uwekezaji. Hivyo kwa kuwa na Manispaa mpya mbili(Manispaa ya Ubungo na Manispaa
ya Kigamboni) zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kusimamia vyema mipango miji,
kuujenga vyema mji na kusimamia kihuduma.
3. Uwepo wa mipango ya
kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia miji ya pembezoni “satellite cities”: tayari serikali imeweka dhamira ya kuimarisha
ukuaji wa jiji kupitia satellite cities. Hivyo uwepo wa wilaya mbili yaani
Kigamboni (Satellite city Kigamboni)
na Ubungo (“Luguruni Satellite City” ndani
ya Kata ya Kwembe na Kata ya Kibamba) zitamudu kusimamia vyema ujenzi imara wa satellite cities na pia kuwezesha wilaya
zitakazoachwa kama wilaya ya Kinondoni kuwa na ahueni ya kuelemewa na kazi
hivyo nazo kusimamia vyema mipango ya ujenzi wa satellite cities zilizomo ktk maeneo hayo
Tatu, Ugawaji
wa kata ndani ya Manispaa mpya na kusimamia kata zilizopo:
Katika mapendekezo yaliyowasilishwa, kumekuwa
na mgawanyo mpya unaonyang’anya kata ambazo tayari zilikwisha kuwapo katika
baadhi ya maeneo mathalani ndani ya Manispaa ya Kinondoni. Mfano wa maeneo kama Kisopwa, Mloganzila. Maeneo tajwa yamekuwa
yakihamishwa toka Manispaa ya Kinondoni na kupelekwa Mkoa wa Pwani. Hivyo
kukizana hata na dhamira ya kujaribu kuchukua baadhi ya kata na maeneo ambayo
yapo katika miji inayokaribia jiji la Dar es Salaam katika dhamira ya kupanua
jiji.
Pia, kwa nyakati tofauti tumeshuhudia viongozi
wa kitaifa wakitaja mara kwa mara katika hotuba zao na matamko yako maeneo
yaliyopo ndani ya Manispaa ya Kinondoni kama eneo la Mloganzila kuyataja kuwa
katika Mkoa wa Pwani. Jambo hili si sahihi. Jambo hili limekuwa likiacha
maswali mengi kwa wananchi. Ifahamike tu, wananchi hawa wanatambulika chini ya
mifumo rasmi tuliyojiwekea inayowatambua kama wakazi wa Manispaa ya Kinondoni.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha
ufafanuzi mpana unawekwa na kusimamia uwepo wa maeneo haya yaendelee kuwapo
katika wilaya za Dar es Salaam.
Sambamba, kuna hitaji la haraka na muhimu
katika mchakato huu kuhakikisha migogoro ya ardhi ndani maeneo ya Kisopwa na
Mloganzila yapatiwe ufumbuzi wa kudumu. Pia kuhakikisha maeneo hayo yanabaki
katika kata ya Kwembe kwenye Manispaa inayopendekezwa ya Ubungo.
Nne, Kujifunza
toka miji na nchi zingine:
Kuna umuhimu mkubwa wa kupanua wigo wa miji
na nchi ambazo tunaweza kuchota uzoefu katika zoezi la kugawa wilaya mpya na
kupanua jiji la Dar es Salaam. Mifano minne kadiri ya wasilisho pekee haitoshi.
Napendekeza na kushauri kuongeza miji iliyopo katika nchi ifuatayo, miji ambayo
inashabihiana na sifa za jiji la Dar es Salaam la ukuaji wa kasi, mifumo wa
kiutawala, hali za kiuchumi na kimaendeleo ;
i.
Lagos-Nigeria
ii.
Johannesburg-South
Africa
iii.
London-Uingereza
iv.
New
Delhi-India
v.
Shangai,
China
Katika kusoma na kuchukua uzoefu toka katika
miji iliyowasilishwa katika pendekezo na hii mingine, tusiishie kuangalia
mifumo ya ugawaji, ukuzwaji na usimamizi bali pia twende hatua ya kuangalia
muundo wa utendaji wa miji hii ambayo yatasaidia sana katika kuboresha muundo
wa kiutendaji wa jiji la Dar es Salaam.
Tano, Mapendekezo
katika Muundo wa Kiutendaji wa Jiji la Dar es Salaam:
Nakubaliana na hitaji la kuwepo kwa Jiji la
Dar es Salaam kama chombo kikuu juu ya Manispaa zote tano zinazopendekezwa
zitakazokuwapo Dar es Salaam.
Pia, nakubaliana na kuunga mkono hitaji la
Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuchaguliwa na wananchi. Hii itatoa fursa katika
utendaji na uwajibikaji imara ambayo unaweza kupimwa na wananchi.
Hivi ndivyo majiji ambayo yamepiga kasi ya
kimaendeleo kama London (Uingereza) yanajiendesha. Pia hata majirani zetu kama
Kenya; nao wametambua mfumo huu na kuuchukua katika Katiba yao mpya.
Pendekezo muhimu; kuna haja ya Jiji la Dar es
Salaam likawa juu ya manispaa zote tano zinazopendekezwa na hivyo Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa isiwe na mamlaka na nguvu kulinganisha na Jiji la Dar es Salaam.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha pia
Jiji la Dar es Salaam linapatiwa mamlaka na madaraka ambayo hayaingiliwi na kuzuiwa
na wilaya nyingine zozote zilizopo chini yake.
Sita, kuunganisha
mapendekezo ya Muundo wa Mkoa wa Dar es Salaam na mchakato wa Katiba Mpya ya
Tanganyika:
Kwa kutambua nchi ipo katika mchakato wa
kuandika katiba mpya ya Tanzania. Mchakato ambao utatoa fursa ya uandishi wa
katiba mpya ya Tanganyika kuna umuhimu mkubwa wa kuanza kuandaa kisheria hoja
za kuwapo ndani ya katiba ya Tanganyika zenye kusimamia Muundo wa Jiji la Dar
es Salaam. Huu ukawa ni mfumo wa mfano “modal” katika ngazi za jiji zenye
kuhitaji kuwapo katika mfumo wa kikatiba. Hii ikiwamo na suala la Meya wa Jiji
kubwa kuchaguliwa na wananchi na mengineyo muhimu.
Kuna umuhimu pia wa kuwepo wa hoja ya
kikatiba katika upanuzi na ukuaji wa Manispaa na ngazi nyingine za miji ndani
ya Katiba. Hivyo, Katiba ya Tanganyika inahitaji kuwa nguzo muhimu.
Hitimisho:
Naomba wananchi wa Jimbo la Ubungo na
wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla kutoa maoni yenu ili hatimaye
tupate mfumo bora wa kiutawala kwa maslahi na ukuaji wa Jiji letu.
Wenu katika utumishi,
John J. Mnyika
Mbunge wa Jimbo la
Ubungo
06 Januari, 2013
2 comments:
Mimi si mkazi wa DSM lakini nimeishi DSM nikiwa chuo, mawazo yako ni mazuri lakini yamejikita haswa kwenye jimbo lako kuliko maeneo mengine. nasauri hivi:-
1. Kigamboni iwe Wilaya- Manispaa
Nimependekeza Kigamboni kwa sababu ya kijiographia
2. Tegeta iwe Wilaya - Manispaa
Kwa sababu ya upatikanaji wa huduma za kiutawala, Wnanchi wa Bunju kuja kupata huduma Magomeni kwangu naona sio huduma bali ni kero hivyo wasogezewe at list Tegeta isitoshe hivi saasa watu wengi wapo huko na mahitaji ya huduma yanahitajika.
3. Kibamba iwe Wilaya - Manspaa
hii itasaidia badala watu wote kuelekea Uande mmoja wakati wa asubuhi na jioni sasa wataelekea Kibamba kufuata huduma hivyo kupunguza foleni, pia Kibamba kuna maeneo yanayofaa ujenzi wa Maofisi
Nihayo tu kwa leo
Ninaunga mkono mapendekezo uliyoyatua, ndugu mbunge, japo yanaonekana kulipa uzito jimbo lako la ubungo.
Niungane na mchangiaji wa juu, kwamba kwa kinondoni, imekuwa ni kero kwa wakazi wa bunju, mabwepande, mapinga, kerege nakadhalika kuja magomeni. hivyo kuna haja ya kuwa na manispaa ambayo itakuwa na makao makuu Tegeta.
Post a Comment