Gazeti la Tanzania Daima Toleo na. 3280 la tarehe 26 Novemba 23 limenukuu kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene wakati akizungumza na kipindi cha Kumepampazuka kilichorushwa na Redio One juu ya Serikali kupandisha bei ya umeme kama Shirika la Umeme (TANESCO) lilivyoomba.
Katika habari hiyo Simbachawene amenukuliwa akisema kwamba endapo kuna mwananchi yeyote atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari au akae giza.
Rais Jakaya Kikwete anapaswa kumwagiza Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospter Muhongo kuwaomba radhi wananchi kwa kauli hiyo iliyotolewa na Naibu Waziri Simbachawene kwa niaba ya wizara anayoiongoza.
Aidha, ni vyema Rais Kikwete kwenye hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa mwezi huu akawaeleza wananchi iwapo uamuzi huo wa kupandisha kwa mara nyingine bei ya umeme ndio utekelezaji wa ahadi ya maisha bora aliyoitoa kwa watanzania kuanzia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.
Hii ni kwa sababu kupandisha bei ya umeme kuna athari ya kuchangia katika ongezeko la gharama na ugumu wa maisha kwa kuwa shughuli za uzalishaji na maisha ya kila siku zinategemea kwa kiwango kikubwa nishati.