Tarehe 8 Machi ni Siku ya Wanawake Duniani (IWD). Ujumbe wa siku hii kwa mwaka huu wa 2014 kwa mujibu wa internationalwomenday.com ni “inspiring change” (kuhamasisha mabadaliko). Wakati kwa mujibu wa unwomen.org ni “equality for women is progress for all” (usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote”.
Mchango wa wanawake katika taifa letu unapaswa kuheshimiwa na kila mtu; wanawake ni wazazi, walezi na ni wengi katika jamii yetu. Hata hivyo, ni kundi linalokabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni muhimu kuunganisha nguvu za pamoja katika kuzikabili.
Katika kuadhimisha siku hii ofisi ya mbunge jimbo la Ubungo inafanya kazi nne mahususi zenye kuhamasisha mabadiliko na maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla.
Mosi; kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano Ofisi ya Mbunge inapokea mapendekezo toka kwa wanawake na wadau wa masuala ya jinsia ya kuboresha rasimu ya katiba kwenye ibara zenye kasoro. Mkazo haupaswi kuwa kwenye uwiano wa kijinsia na haki za wanawake za ushiriki kwenye chaguzi na uongozi wa kisiasa pekee au kupata ujira sawa kama ilivyo sasa katika rasimu ibara ya 47, bali kuwezesha ushiriki wa wanawake katika uchumi, kumiliki mali na maendeleo kwa upana wake.
Pili; Ofisi ya Mbunge inahamasisha umma kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano kuzingatia kwamba wanawake na vijana wa kike wanaathirika zaidi na matatizo ya maji katika jamii. Tunafanya hivyo ikiwa ni mwaka mmoja toka niwasilishe hoja ya maji bungeni tarehe 4 Februari 2013 (nimeambatanisha nakala) ambapo Waziri wa Maji Prof Jumanne Maghembe kinyume za kanuni za Bunge aliwasilisha hoja ya kutaka hoja hiyo iondolewe. Waziri Maghembe alidai kwamba Serikali tayari imeshajipanga vizuri kumaliza matatizo ya maji, hata hivyo mwaka mmoja umepita Serikali haijakamilisha kutekeleza maazimio niliyotaka Bunge iyajadili ni kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa za kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka. Hivyo, kupitia siku hii ya wanawake natoa mwito kwa Waziri wa Maji Prof. Maghembe kujitokeza kwa umma kutoa maelezo ya hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo ya hoja hiyo na hatua nyingine za haraka zinazotarajiwa kuchukuliwa kupunguza tatizo la maji kwa wanawake na wakazi wengine kwa kuzingatia mapendekezo niliyotoa.
Tatu, ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo itakabidhi mchango wa ada kwa wanafunzi waliofaulu kujiunga na shule za Serikali katika Jimbo la Ubungo ambao ni yatima au wanalelewa na wajane na hawana uwezo wa kujilipia au kulipiwa ada. Wanafunzi hao ni wale waliowasilisha maombi katika ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo mwaka huu wa 2014. Tangu mwaka 2010 nimekuwa na kawaida kutenga asilimia 20 ya mshahara kwa ajili kuchangia mahitaji ya elimu hususan ada kwa wasio na uwezo, ununuzi wa vifaa vya kujifunza na kufundishia, uendeshaji wa asasi inayoshughulikia kuhamasisha maendeleo ya elimu na kuchangia katika ujenzi kwa nyakati mbalimbali. Kazi hii ni ya nyongeza juu ya kazi ya kawaida ya kibunge ya kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali kuwezesha fedha za umma kuwekezwa katika maendeleo ya elimu kupitia miradi inayotekelezwa na halmashauri/manispaa. Milango ipo wazi kwa wadau wengine kushirikiana nasi kwa hali na mali kwa kuwa orodha ya maombi na mahitaji ni kubwa ukilinganisha na michango ambayo tunaendelea kujitolea.
Nne, ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo inachambua maombi ya vikundi vya wanawake na vijana wa kike walioomba vifaa kwa ajili ya kazi za uzalishaji mali ama ujasiriamali za kuweza kujiajiri. Vikundi vitavyokidhi vigezo vya awali vitatembelewa na ajili ya uhakiki na hatimaye kununuliwa vifaa husika baada ya maombi kupitishwa na Kamati ya Jimbo. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) la Ubungo katika awamu ya sasa umetenga shilingi milioni kumi kwa ajili ya miradi ya kuchochea maendeleo kupitia kwa vikundi vya wanawake na vijana. Aidha, nitumie fursa hii kutoa mwito kwa Serikali, mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha kushirikiana kupunguza riba katika mikopo ya wananchi wa kipato cha chini na kurahisisha mifumo ya dhamana ili kupanua wigo wa ukopaji na upatikanaji wa mitaji hususan kwa wanawake na vijana.
Ujumbe wangu kwa wanawake na wadau wote wa masuala ya jinsia ni kwamba maadhimisho ya mwaka huu yasiwe ya maneno matupu bali matendo yenye dhima ya kuhamasisha mabadiliko kuwezesha kufikia dira ya usawa kwa wanawake na maendeleo kwa wote.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
08/03/2014
Dodoma
2 comments:
Kaka wewe ndiye mtumishi Wa uma unaetenda Kazi wananchi waliyokutuma unastahiki pongezi za dhati.
Brother, this calls for a wow! Endelea kutuwakilisha vema
Post a Comment