UTANGULIZI
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Sura
ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati
Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya
ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la
Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa
Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri
kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano
wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo
wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”
Suala
hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu
iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph
Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu
ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya
muundo wa Muungano.”[1]