Monday, February 23, 2015

Rai Maalumu kwa Zoezi la Uandikishaji ktk Daftari la Kudumu kwa mfumo wa BVR

Nimeingia katika Mkoa wa Njombe kwa ajili ya uzinduzi wa R2R BVR (Region by Region Biometricn Voter Registration) kwa Mkoa huu (Njombe) leo Jumatatu 23 Februari, 2015 utakaofanyika Njombe Mjini.

Baada ya uamuzi wa NEC kwamba uandikishaji unaanza Halmashauri ya Mji Mdogo wa Makambako pekee, nimeanzia katika mji huo na kubaini kwamba bado kuna udhaifu katika maandalizi ya BVR hata katika eneo hilo dogo tofauti na kauli ya uongo ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchini kwamba maandalizi yote yako kamili ikiwemo ushiriki wa wadau. 

Itakumbukwa wakati Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva alipotangaza kusogeza mbele uandikishaji toka 16 Februari, 2015 mpaka 23 Februari, 2015 alisema lengo ni kuvipa vyama nafasi ya kujiandaa na kuweka mawakala. Lakini mpaka sasa vyama havijapewa orodha ya vituo kwa ajili ya kuweka mawakala na kuna utata kuhusu idadi halisi ya vituo hata kwa upande wa eneo dogo la Makambako. 

Halmashauri imeitisha kikao kwa niaba ya NEC ikasema vituo ni 44 bila kutoa orodha wala kuelekeza viko wapi, baadae ghafla wamebadili na kusema ni 87 lakini hata hivyo hawajatoa orodha mpaka sasa

Hivyo basi, nimeagiza viongozi wetu wa Makambako wawasiliane na NEC yenyewe moja kwa moja kutaka orodha na kuonyeshwa vilipo vituo. Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva na Mkurugenzi wake, Mallaba wasikubali Mkuu wa mkoa na Mkurugenzi wakawaharibia zoezi hata katika eneo dogo tu la Makambako. 

Mkuu wa Mkoa ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo NEC iondoe udhaifu huu haraka ama sivyo itakuwa imekubali itumike kuhujumu vyama kuweka mawakala wake katika vituo na kuachia mianya ya uchakachuaji wa uchaguzi kuanzia katika hatua ya uandikishaji.

Aidha, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye ni msimamizi wa wakuu wa mikoa na wakurugenzi aeleze amechukua hatua gani hivi sasa juu ya watajwa kushindwa kufanya maandalizi yanayokusudiwa hali ambayo inaweza kusababisha madhara kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hali hiyo inadhihirisha haja ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi sio tu katika ngazi ya Taifa bali kuwa na watumishi huru wa tume mpaka kwenye ngazi za chini wa kuratibu kazi kwa uhuru na ufanisi kwa niaba ya NEC.

Kufuatia hali hiyo, Rais kikwete anapaswa kukumbushwa kuetekeleza ahadi yake kwa wakuu wa vyama kupitia TCD ya kuwezesha marekebisho ya mpito ya kikatiba na kisheria yatakayofanya tume iwe huru, matokeo ya urais kuweza kupingwa mahakamani, mshindi wa urais kupata kura zaidi ya 50%+1 na kuwa na wagombea binafsi. 

Ili kutekeleza haya, muswada wa sheria wa marekebisho ya katiba na sanjari na muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali inapaswa kuwasilishwa kwa nyakati tofauti katika mkutano wa 19 wa Bunge unaotarajiwa kufanyika Machi ambao ni wa mwisho wa kawaida kabla ya Bunge kuvunjwa kwa kuwa baada ya hapo ni mkutano wa 20 wa Bunge la Bajeti. 

Aidha, baada ya kubaini kwamba NEC na hata Serikali kupitia Halmashauri na Sekretariati ya Mkoa hawajatoa elimu ya Mpiga Kura ya kutosha wala kufanya uhamasishaji inavyostahili nimeagiza viongozi wetu wa ngazi zote Makambako kushirikiana na wadau muhimu kufanya uhamasishaji wa ziada ili wananchi wajitokze kwa wingi kujiandikisha. 

Kwa wanaotaka kupiga kura Makambako Oktoba hii ni fursa pekee popote walipo waje wajiandikishe!

Mpenda mabadiliko yeyote toka popote aliyetayari kuwezesha Operesheni R2R BVR naomba awasiliane na Zainab Ashraff kupitia 0764-892 468 au 0686-863 979 au 0717-174 776 kwa kuzingatia kuwa uandikishaji katika daftari la kudumu la upigaji kura ndio msingi wa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa udiwani, ubunge na urais nchini.


Wenu katika demokrasia na maendeleo,
John Mnyika
Naibu Katibu Mkuu (Tanganyika)

2 comments:

Unknown said...

wewe ni fala mkubwa katika nchi hiii unashindwa kutafakari mambo ya msingi unaleta ushoga kweli we kiongozi wa wananchi

Unknown said...

nafikiri ni wakati wa wanachama wa chadema kujitafakari upya juu ya mwenendo wa nchi hii kuhusu uimarawamaswalya kisiasa na kuletausawa na haki katika jamiiyetu