Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amesema kuwa mgogoro kuhusu eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Mburahati umeelekea kupatiwa ufumbuzi ambapo sasa mapendekezo ni kujenga shule hiyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 katika eneo la wazi jirani na kituo cha polisi katika kata hiyo hivyo wakazi wanapaswa kutoa maoni yao iwapo pendekezo hilo ni muafaka.
Wednesday, October 3, 2012
Wednesday, September 26, 2012
Shiriki mkutano wa EWURA na wananchi kuhusu udhibiti wa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi kesho 27 Septemba, 2012; toa maoni kuandaliwe kanuni za kudhibiti ubora na kuwezesha kutolewa kwa bei elekezi
Natoa
mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuhudhuria mkutano wa wadau, wananchi na
watoa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi katika Jiji la Dar es salaam
ulioitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) tarehe
27 Septemba 2012 katika Ukumbi wa Land Mark Hotel River Side Ubungo kuanzia saa
3 asubuhi.
Aidha,
katika kujadili ajenda za mkutano huo zilizotolewa naitaka EWURA kuweka mkazo
katika kupokea maoni ya wananchi ili kuwezesha kuandaliwa kwa haraka kwa kanuni
za usimamizi na bei elekezi ya maji katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika
visima na malori binafsi kwa kuzingatia kuwa katika ziara yangu katika kata
nane za Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba 2012
nimepokea malalamiko mengi juu ya ongezeko la bei ya maji ambayo imefikia mpaka
shilingi mia tano kwa dumu moja la lita 20 bila udhibiti wowote.
Kwa
mujibu wa Tangazo la EWURA lililotolewa mwezi Septemba 2012 Mkutano huo ambao
wadau wote wa maji ikiwemo wananchi wanaalikwa kushiriki utajadili haki na
wajibu wa watoa huduma ya maji Jijini Dar es salaam; mwongozo wa watoa huduma
ya maji kwa visima na magari binafsi na utaratibu utakaotumiwa na DAWASCO
kusajili watoa huduma wa maji ya visima na wasambazaji wa maji kwa magari
binafsi.
Izingatiwe
kuwa katika mikutano yangu na wananchi ya awamu ya pili katika kata nane za
Jimbo la Ubungo kati ya Agosti na Septemba 2012 nilisisitiza kuwa EWURA ina
wajibu kama ilivyo kwenye mafuta na umeme kusimamia sekta ya maji siyo ya umma
tu hata binafsi, hata hivyo kwa sasa inasimamia zaidi bei na ubora kwa upande
wa mamlaka za umma.
Hivyo,
nilitoa mwito kwa wananchi kuungana kuitaka EWURA kueleza hatua iliyofikiwa
katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei
elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano
la Maji Ubungo mwaka 2011 suala ambalo lipaswa kuzingatiwa na wadau
watakaoshiriki kwenye mkutano unaofanyika tarehe 27 Septemba 2012.
Itakumbukwa
tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo pamoja na
mambo masuala mengine niliitaka EWURA kutoa kauli ndani ya kipindi cha wiki
moja kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya kanuni husika pamoja na
udhibiti wa bei ya maji ikiwemo kwenye sekta binafsi katika jiji la Dar es
salaam.
Katika
mkutano wangu na wanahabari tarehe 2 Machi 2012 nilieleza kuwa kupitia ziara ya
kikazi katika kata saba za Jimbo la Ubungo nilibaini kwamba kubwa ya ubora na bei ya maji jijini Dar es
salaam katika sekta binafsi; bei ya maji iko juu sana hali ambayo inashawishi
biashara haramu yenye kuhusisha hujuma katika miundombinu ya maji na ufisadi
wenye kuharibu ratiba ya mgawo wa maji ili kupanua soko kinyemela.
Tarehe
8 Machi 2012 Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa EWURA Titus Kaguo alinukuliwa
vyombo vya habari akinijibu kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi kwenye
maji kwa kuwa tayari ilishafanya hivyo mwaka 2010 bila kuzingatia kuwa bei
elekezi pekee iliyotolewa na EWURA ni katika visima, maghati na mabombo ya umma
yanayoendeshwa na DAWASA na DAWASCO.
Kufuatia
majibu hayo tarehe 8 Machi 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa kauli ya Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iliyonukuliwa na vyombo vya habari
tarehe 8 Machi 2012 kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi ya maji kwa
kuwa imekwishatoa tayari mwaka 2010 haipaswi kukubaliwa na wananchi na wadau wa
sekta ya maji katika Jiji la Dar es salaam.
Katika
taarifa hiyo niliitaka EWURA kutimiza kwa ukamilifu wake wajibu wake kwa mujibu
wa Sheria mbili muhimu za usimamizi wa sekta ya maji nchini (Water Supply and
Sanitation Act of 2009 and The Energy and Water Utilities Regulatory Authority
Act)
Katika
taarifa hiyo nilitoa mwito kwa EWURA kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua
iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya
mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi
kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011.
Pamoja
na kutoa taarifa hiyo kwa umma niliiandikia
barua EWURA itimize wajibu wake wa kusimamia ubora na bei hata hivyo
nilipokea majibu kuwa muongozo bado haujaandaliwa, hivyo mkutano huu wa tarehe
27 Septemba 2012 ni fursa muhimu ya kuharakisha maandalizi ya kanuni na
utaratibu husika.
Ufumbuzi
wa kudumu wa kushusha bei ya maji ni DAWASA na DAWASCO kuongeza uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji hata hivyo udhibiti wa EWURA kuhusu ubora na bei
katika kipindi hiki cha upungufu ni muhimu kuepusha madhara kwa umma ya kuuziwa
maji yasiyo na ubora na kwa bei ya kuruka hali ambayo inawathiri zaidi wananchi
wa kipato cha chini.
Imetolewa
tarehe 26 Septemba 2012 na:
John
Mnyika (Mb)
Jimbo
la Ubungo
Thursday, September 20, 2012
MREJESHO: Matatizo ya Maji Kata ya GOBA
Pamoja
na manispaa ya Kinondoni kutoa shilingi milioni moja na nusu tarehe 14 Septemba
2012 kwa ajili ya kufunga mita na kuanza kusukuma maji ya mradi wa Goba, tarehe
19 Septemba 2012 wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani nimemtaka Mkurugenzi
wa Manispaa ya Kinondoni kuwawajibisha watendaji waliozembea na kusababisha
matatizo hayo kudumu kwa muda mrefu.
Izingatiwe
kuwa kiasi hicho ni nyongeza baada ya awali kutolewa milioni tatu na Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo la Ubungo (CDCF) kwa ajili ya kuwezesha huduma ya maji
kupitia mradi huo kurejea.
Ikumbukwe
kuwa mwezi Agosti 2011 maji yalikatwa kwenye kata ya Goba kutokana na DAWASCO
kuidai kamati ya mradi wa maji shilingi milioni 18 na katika kufuatilia deni hilo
nilipata taarifa za Kamati ya Maji kuwasilisha malalamiko DAWASCO ya
kutokukubaliana na kiwango hicho cha deni na pia kwa Manispaa ya Kinondoni
kuhusu matatizo ya kiutendaji na kifedha katika mradi huo wa maji ikiwemo ya
upotevu wa fedha.
Tarehe
5 Septemba 2011 niliwaunganisha wananchi kwa pamoja tukaandamana kwenda ofisi
ya DAWASCO makao makuu ambapo tulikutana na mtendaji mkuu wa kampuni husika na
kufanya mazungumzo ambayo yalisaidia baadhi ya hatua za msingi kuchukuliwa
ikiwemo DAWASCO kurejesha huduma ya maji katika bomba kuu baada ya sehemu ya
deni kulipwa na makubaliano kufikiwa kuhusu malipo ya kiwango kilichobaki.
Pia
tarehe 24 Oktoba 2011 niliandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni
kutoa mwito wa hatua za dharura kuchukuliwa ili kuhakikisha uhakiki unafanyika
wakati huo huo wananchi wengine wanaendelea kupata huduma ya maji; lakini
udhaifu wa kiutendaji umefanya hatua ziwe za kusuasua.
Hata
hivyo, pamoja na huduma ya maji kurejeshwa katika bomba kuu haikuweza
kusambazwa kwenye mabomba ya wananchi pamoja na vioski vya kutolea huduma kwa
sababu ya udhaifu wa utendaji katika ngazi ya kata na katika kamati ya maji
hivyo tarehe 26 Januari 2012 niliwaunganisha wananchi kufika Manispaa ya
Kinondoni kwa ajili ya hatua za haraka za Mkurugenzi wa Manispaa.
Kufuatia
hatua hiyo Mkurugenzi wa Manispaa Fortunatus Fwema alifanya ziara katika kata
ya Goba tarehe 31 Januari 2012 na kuagiza kwamba ndani ya tano maji yatoke
katika kata hiyo na kuagiza Mhandisi wa maji na timu yake waweke kambi katika
kata ya Goba mpaka maji yatoke kwa gharama za halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni.
Hata
hivyo, muda huo ulimalizika bila maji kupatikana na kikosi kazi kilikabidhiwa
jukumu tarehe 28 Februari 2012 kushughulikia kile kilichoelezwa kuwa ni kuanza
uchunguzi wa Bomba la Maji kuanzia Tanki Bovu hadi kwenye tanki la Matosa ili
kubaini wizi, upotevu wa maji na uharibifu wa miundombinu.
Katika
kipindi cha kati ya Februari mpaka Agosti 2012 nimefuatilia Manispaa kwa njia
mbalimbali na wakati wote maelezo yamekuwa kazi hiyo inachukua muda mrefu kwa
sababu ya urekebishaji wa miundombinu ambapo Manispaa ya Kinondoni ilikubali
kutoa mita 15 pamoja na stendi za bomba mpya kwa ajili ya kufunga katika bomba
kubwa kwenye njia zinazoelekea kwa wananchi ili kudhibiti wizi na upotevu wa
maji pamoja na kufanya marekebisho katika mabomba na gate-valves
zilizohujumiwa.
Ikumbukwe
kuwa matatizo ya maji kata ya Goba yanafahamika kwa mamlaka zote husika kuanzia
Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na vyombo vya dola
kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2012 lakini hatua kamili hazijachukuliwa kwa
wakati.
Wananchi
wa Goba wamepoteza uvumilivu kwa kuwa hatua hazichukuliwi kwa haraka na
kutokana na hali hiyo mbunge kama mwakilishi wa wananchi nimeumua kuungana nao
katika kutaka uwajibikaji wa watendaji wote waliozembea na kusababisha matatizo
hayo kudumu kwa muda mrefu.
Nimefikia
hatua hiyo kwa sababu njia zote za kawaida kupitia vikao na mawasiliano ya
kiofisi zinaelekea kukwamishwa na uzembe, hujuma na urasimu na udhaifu wa
kiutendaji katika ngazi mbalimbali.
Katika
kushughulikia masuala la maji kwenye kata ya Goba, narudia kusisitiza hatua
zifuatazo kuendelea kuchukuliwa kwa haraka na mamlaka zifuatazo:
Mosi;
Mamlaka za Manispaa ya Kinondoni zikiongozwa na Meya na Mkurugenzi zinapaswa
kufuatilia kwa haraka kuhakikisha maji yanarejeshwa Goba. Hatua hii iende
sambamba na kupanua wigo wa maji Goba kwa kutekeleza kwa haraka upatikanaji wa
maji kutoka pia mradi wa maji toka Madale Kisauke.
Manispaa izingatie matatizo
yaliyopo kwenye miradi ya maji inayoendeshwa na manispaa pamoja na kamati za
wananchi au vyama vya watumia maji katika maeneo mbalimbali. Hivyo, pamoja na
kuchukua hatua kuhusu mradi wa maji wa Goba, Manispaa ichukue hatua juu ya
miradi iliyokwamba ukiwemo wa Mbezi Msumi na Makabe. Pia, Manispaa ya Kinondoni
inapaswa kufanya mabadiliko kwenye idara ya maji kwa kuwa ina udhaifu mkubwa wa
kiutendaji.
Pili;
Wizara ya Maji, Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) na Kampuni ya maji
safi na maji taka (DAWASCO) zizingatie kwamba maeneo ya pembezoni ya Dar es
salaam ambayo awali yalikuwa vijiji sasa ni mitaa yenye wakazi wengi. Hivyo,
maeneo kama kata ya Goba na mengine ya pembezoni yanapaswa kuunganishwa moja
kwa moja na mtandao wa maji chini ya mamlaka husika kwa mujibu wa sheria
iliyounda DAWASA badala ya mfumo uliopo ambalo haulingani na mahitaji.
Tatu;
vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kushughulikia vyanzo vya migogoro badala
ya kusubiri mpaka matatizo yanapoibuka kwa kushughulikia kwa wakati malalamiko
yanayotolewa. Mathalani, Jeshi la Polisi (Ofisi ya DCI) na TAKUKURU wanapaswa
kutoa kauli kuhusu hatua zilizochukuliwa juu ya tuhuma za ufisadi na ukiukwaji
wa sheria katika mradi wa maji Goba ambazo zimetolewa na wananchi kwa mamlaka
husika kuanzia mwa 2007.
Mamlaka
husika zizingatie kuwa tarehe 27 Februari 2011 na 6 Machi 2011 nilifanya
mikutano na wananchi katika kata ya Goba ambapo risala ya wananchi pamoja na
ripoti ya ukaguzi wa mradi wa mradi wa maji Goba ya mwaka 2007 zilizosomwa
ambazo zilieleza bayana matatizo yaliyokuwepo kwenye kamati ya maji pamoja na
mradi kwa ujumla ikiwemo yaliyohusu upotevu wa fedha ambayo vyombo vya dola
vilipatiwa taarifa lakini hatua hazikuchukuliwa kwa wakati.
Kwa
nyakati mbalimbali nimeziandikia barua rasmi mamlaka husika kuhusu masuala haya
na mengine na kutokana na kutochukua
hatua kwa wakati mwezi Agosti 2012 kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge
nilikutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kumweleza haja ya kuingilia kati ili
ufumbuzi upatikane mapema.
John Mnyika (Mb)
19/09/2012
Wednesday, September 19, 2012
Hatimaye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External pamoja na daraja unaanza!!
Tayari taratibu za zabuni zimeshakamilika na
mkandarasi anapaswa kuanza ujenzi. Manispaa ya Kinondoni imeshaweka alama ya "X" katika
majengo ambayo yatapaswa kubomolewa kuwezesha upanuzi wa barabara husika
unaofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam (TANROADS).
Tarehe
15 Septemba 2012 nilifanya mkutano wa hadhara Jimboni Ubungo kwenye kata ya
Makuburi ambapo pamoja na maswali mengine niliulizwa ni lini ujenzi wa Barabara
kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External ukiambatana na ujenzi wa
daraja katika barabara husika utaanza.
Pamoja
na kueleza hatua iliyofikiwa mpaka sasa nilitoa mwito wananchi wote ambayo
makazi yao yamewekewa alama ya "X" ikiwa si wavamizi wa barabara wawasilishe kwa Manispaa
ya Kinondoni maelezo na vielelezo vyao kwa kuzingatia Wakala wa Barabara Mkoa
wa Dar es es salaam (TANROADS) wao wana bajeti ya ujenzi pekee na madai ya
fidia kwa wenye uhalali yako chini ya Manispaa ya Kinondoni; tayari 17 Septemba
2012 baadhi ya wananchi wamewasilisha nyaraka zao.
Ikumbukwe
pia kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za
kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa
hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha
2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.
Niliziandikia
mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa
katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi
awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko
chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa
njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza
barabara hiyo katika vipaumbele vyake na kutenga fedha za ujenzi wa kiwango cha
lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.
Aidha,
pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi
2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia
Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo
kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External suala ambalo pia kwa nyakati mbalimbali
nilihoji utekelezaji wake.
Izingatiwe
kwamba tarehe 21 Machi 2012 niliunganisha wananchi kuchangia hatua za dharura
za kufanya matengenezo ili kupunguza kero lakini nikasisitza kuwa suluhisho
muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili
kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami
hatua ambayo sasa inaelekea kuchukuliwa kwa haraka.
John
Mnyika (Mb)
18 Septemba, 2012
Tuesday, September 18, 2012
“Waziri Tibaijuka aeleze uendelezaji wa Mji wa Luguruni Kibamba na eneo la Kwembe Kati”.
|
| |
