Natoa
mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuhudhuria mkutano wa wadau, wananchi na
watoa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi katika Jiji la Dar es salaam
ulioitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) tarehe
27 Septemba 2012 katika Ukumbi wa Land Mark Hotel River Side Ubungo kuanzia saa
3 asubuhi.
Aidha,
katika kujadili ajenda za mkutano huo zilizotolewa naitaka EWURA kuweka mkazo
katika kupokea maoni ya wananchi ili kuwezesha kuandaliwa kwa haraka kwa kanuni
za usimamizi na bei elekezi ya maji katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika
visima na malori binafsi kwa kuzingatia kuwa katika ziara yangu katika kata
nane za Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba 2012
nimepokea malalamiko mengi juu ya ongezeko la bei ya maji ambayo imefikia mpaka
shilingi mia tano kwa dumu moja la lita 20 bila udhibiti wowote.
Kwa
mujibu wa Tangazo la EWURA lililotolewa mwezi Septemba 2012 Mkutano huo ambao
wadau wote wa maji ikiwemo wananchi wanaalikwa kushiriki utajadili haki na
wajibu wa watoa huduma ya maji Jijini Dar es salaam; mwongozo wa watoa huduma
ya maji kwa visima na magari binafsi na utaratibu utakaotumiwa na DAWASCO
kusajili watoa huduma wa maji ya visima na wasambazaji wa maji kwa magari
binafsi.
Izingatiwe
kuwa katika mikutano yangu na wananchi ya awamu ya pili katika kata nane za
Jimbo la Ubungo kati ya Agosti na Septemba 2012 nilisisitiza kuwa EWURA ina
wajibu kama ilivyo kwenye mafuta na umeme kusimamia sekta ya maji siyo ya umma
tu hata binafsi, hata hivyo kwa sasa inasimamia zaidi bei na ubora kwa upande
wa mamlaka za umma.
Hivyo,
nilitoa mwito kwa wananchi kuungana kuitaka EWURA kueleza hatua iliyofikiwa
katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei
elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano
la Maji Ubungo mwaka 2011 suala ambalo lipaswa kuzingatiwa na wadau
watakaoshiriki kwenye mkutano unaofanyika tarehe 27 Septemba 2012.
Itakumbukwa
tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo pamoja na
mambo masuala mengine niliitaka EWURA kutoa kauli ndani ya kipindi cha wiki
moja kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya kanuni husika pamoja na
udhibiti wa bei ya maji ikiwemo kwenye sekta binafsi katika jiji la Dar es
salaam.
Katika
mkutano wangu na wanahabari tarehe 2 Machi 2012 nilieleza kuwa kupitia ziara ya
kikazi katika kata saba za Jimbo la Ubungo nilibaini kwamba kubwa ya ubora na bei ya maji jijini Dar es
salaam katika sekta binafsi; bei ya maji iko juu sana hali ambayo inashawishi
biashara haramu yenye kuhusisha hujuma katika miundombinu ya maji na ufisadi
wenye kuharibu ratiba ya mgawo wa maji ili kupanua soko kinyemela.
Tarehe
8 Machi 2012 Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa EWURA Titus Kaguo alinukuliwa
vyombo vya habari akinijibu kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi kwenye
maji kwa kuwa tayari ilishafanya hivyo mwaka 2010 bila kuzingatia kuwa bei
elekezi pekee iliyotolewa na EWURA ni katika visima, maghati na mabombo ya umma
yanayoendeshwa na DAWASA na DAWASCO.
Kufuatia
majibu hayo tarehe 8 Machi 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa kauli ya Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iliyonukuliwa na vyombo vya habari
tarehe 8 Machi 2012 kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi ya maji kwa
kuwa imekwishatoa tayari mwaka 2010 haipaswi kukubaliwa na wananchi na wadau wa
sekta ya maji katika Jiji la Dar es salaam.
Katika
taarifa hiyo niliitaka EWURA kutimiza kwa ukamilifu wake wajibu wake kwa mujibu
wa Sheria mbili muhimu za usimamizi wa sekta ya maji nchini (Water Supply and
Sanitation Act of 2009 and The Energy and Water Utilities Regulatory Authority
Act)
Katika
taarifa hiyo nilitoa mwito kwa EWURA kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua
iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya
mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi
kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011.
Pamoja
na kutoa taarifa hiyo kwa umma niliiandikia
barua EWURA itimize wajibu wake wa kusimamia ubora na bei hata hivyo
nilipokea majibu kuwa muongozo bado haujaandaliwa, hivyo mkutano huu wa tarehe
27 Septemba 2012 ni fursa muhimu ya kuharakisha maandalizi ya kanuni na
utaratibu husika.
Ufumbuzi
wa kudumu wa kushusha bei ya maji ni DAWASA na DAWASCO kuongeza uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji hata hivyo udhibiti wa EWURA kuhusu ubora na bei
katika kipindi hiki cha upungufu ni muhimu kuepusha madhara kwa umma ya kuuziwa
maji yasiyo na ubora na kwa bei ya kuruka hali ambayo inawathiri zaidi wananchi
wa kipato cha chini.
Imetolewa
tarehe 26 Septemba 2012 na:
John
Mnyika (Mb)
Jimbo
la Ubungo
No comments:
Post a Comment