Thursday, April 16, 2009

Sakata la DECI:Serikali iwajibike kuheshimu utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu

Sakata la DECI:

Serikali iwajibike kuheshimu utawala sheria na kulinda haki za binadamu

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu suala la DECI, nikiwa mmoja wa watu waliokuwa na matarajio kwamba pande zote zinazohusika zitachukua hatua stahili kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia pia haki za binadamu. Hata hivyo, mtiririko wa suala lenyewe unatia mashaka kadiri siku zinavyokwenda. Sakata la DECI linazidi kuchukua sura mpya, hali inayotoa ishara mbaya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa washiriki na washirika wa sakata hilo na watanzania kwa ujumla.

Izingatiwe kuwa baada ya wananchi kulipa kodi, wajibu mmojawapo mkubwa wa kikatiba na kisheria wa serikali ni kuhakikisha kodi hizo pamoja na mambo mengine zinatumika kwa ajili ya ulinzi na usalama wa maisha na mali za raia. Katika kutimiza wajibu huo, wananchi wanatarajia kuwa serikali itaweza kuongoza kwa kuona mbali, na kwa kutimia vyombo vyake kuwalinda raia ikiwemo kuwaelimisha mapema juu ya masuala ambayo yanaweza kuwaathiri wao na mali zao na kukabiliana uvunjifu wa sheria.

Nimefadhaishwa na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye pamoja na kueleza wazi wazi kuwa DECI imekuwa ikifanya biashara haramu ya upatu wa mfumo wa piramidi(pyramid scheme) bila hata ya kuwa na leseni kwa kazi hiyo ambayo ni kinyume cha sheria. Bado Waziri Mkuu, ameendelea kuruhusu biashara hiyo kuendelea wakati serikali inafanya uchunguzi, huku wakati huo huo akiwataka wananchi kuacha kuendelea ‘kupanda’ fedha zao katika kampuni hiyo. Huu ni undumilakuwili na ugeugeu katika uongozi na usimamizi wa utawala wa sheria na haki za binadamu.

Kigugumizi hiki cha serikali katika kuchukua hatua, kinatokana na uzembe ambao serikali ya CCM imeufanya tangu awali ambao umesababisha kampuni hiyo kufanya kazi kwa miaka zaidi ya miwili huku ikilindwa na vyombo vya dola na ikitoa kodi kwa serikali. Idara ya Usalama wa Taifa, inapaswa kulieleza taifa ilikuwa wapi wakati wote biashara hii ilipoanza na kumea. Kitengo cha Ushushushu(Intelejensia) wa Kifedha na Kiuchumi, kinapaswa pia kuwajibika kutokana na kadhia hii.

Nachukua fursa hii kuitahadharisha serikali kwamba uzoefu wa kimataifa katika nchi mbalimbali ambazo biashara hii ya upatu imefanyika, umeonyesha kwamba mara zote miradi ya namna hiyo imeshindwa kuwa endelevu baada ya muda na kufikia kiwango cha juu cha mtaji na wateja huvunjika na kuacha washiriki wengi wakiwa na hasara. Hasara hizo huchukua sura ya kiuchumi, kisiasa na hata kijamii. Nchini Albania , biashara ya upatu wa piramidi ilipovunjika ilisababisha machafuko katika nchi ambayo yalichangia kwa namna moja au nyingine katika kuondolewa kwa serikali iliyokuwa madarakani katika nchi hiyo. Nchini Kenya, vurugu zilizotokea baada ya kuvunjika kwa biashara kama hiyo zilisababisha vurugu ikiwemo baadhi ya washirika kutupwa kutoka ghorafani. Nchini Ireland (2006) biashara kama hiyo imeelezwa kuleta madhara. Nchini Colombia (2008) machafuko yalitokea katika manispaa za Pasto, Tumaco, Popayan na Santander de Quilichao. Serikali ya nchi hiyo ilibidi kutangaza hali ya hatari ya kiuchumi na kukukamata mali za washirika kwa ajili ya kuwakoa washiriki.

Pamoja na uchunguzi unaoendelea, kwa kuwa serikali imeshakiri kwamba kuna ukiukwaji wa sheria mpaka sasa; serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kulinda mali za wananchi. Kwa kuwa tayari serikali imeshatoa matangazo ya kuwaonya wananchi kuendelea ‘kupanda fedha’ chini ya mfumo huo wa piramidi, kupungua kwa wananchi ‘wanaopanda fedha’ kwa sasa, kutafanya DECI ishindwe kuwalipa ambao walipanda awali, katika mazingira hayo DECI inaweza kufunga yenyewe ofisi zake kabla ya kufungiwa. Uamuzi wa kufunga ofisi kabla ya serikali kuingilia kati utaibua tafrani miongoni mwa washiriki waliojisajili na kupanda fedha zao mpaka sasa; hali ambayo inaweza kuibua matatizo ya kiuchumi yenye athari pia za kisiasa na kijamii. Katika mazingira hayo, serikali inawajibu wa kusimamia sheria wakati huo huo kusimamia haki za binadamu, raia wa Tanzania ambao ni washiriki katika piramidi hilo. Kwa kuwa serikali imezembea na kuachia wananchi(iwe kwa uzembe ama kwa kutokujua) kujiingiza katika hatari hiyo, serikali ina wajibu wa haraka wa kuwaokoa wananchi hao kutoka athari hizo za kiuchumi na kulinda maisha yao.

Aidha wakati suala hili likiendelea kushughulikiwa tunatoa mwito kwa viongozi wa dini kukaa na baadhi ya viongozi wenzao wa dini ambao wanatetea biashara hii ya upatu wa piramidi kuweza kuwaasa kurejea katika misingi ya utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu za waumini wao na watanzania wengine wa dini na imani mbalimbali. Viongozi wote wa dini waweze kuweka mkazo kuhakikisha fedha 'zilizopandwa' zinarejeshwa kwa wahusika na serikali inatimiza wajibu wake wa kulinda raia na kusimamia utawala wa sheria. Pia, washiriki wa DECI na washirika wao wanapaswa kuwa na utulivu katika kipindi kuepusha madhara yoyote ambayo yanaweza kutokea kama suala hili lisiposhughulikiwa kwa umakini mkubwa.

Serikali isipochukua hatua za haraka kunusuru mwelekeo wa mambo kuhusu kadhia hii wafuatao watawajibika kwa yote yatayotokea: Waziri Mkuu Mizengo Pinda(kwa kushindwa kusimamia utawala wa sheria); Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu(kwa kushindwa kusimamia sekta ya fedha ikiwemo kutoa ushauri kwa vyombo vya dola kuchukua hatua za haraka); Waziri wa Mambo ya Ndani(Kwa kushindwa kulinda mali za raia, na kwa polisi kulinda biashara haramu kwa muda mrefu bila kuchukua hatua za mapema); Usalama wa Taifa(kwa kushindwa kutoa tahadhari ya mapema ya kishushushu ya kuzuia biashara ya upatu wa piramidi kupanuka na kuwa na wateja wengi); Mamlaka ya Mapato(kwa kukusanya kodi bila kuchunguza uhalali kamili wa biashara inayohusika na hivyo kujenga hisia kwamba upatu huo wa mfumo wa piramidi ulikuwa biashara inayotambuliwa na serikali).

Baada ya kuibuliwa kwa ufisadi katika Benki Kuu(BOT) uliohusu akaunti za madeni ya nje(EPA) na masuala mengine kama Meremeta, Tangold na Deep Green ilitarajiwa kwamba vyombo vya serikali vingekuwa vimeamka na kubaini aina zote za hujuma kabla ya kuleta athari kwa wananchi na taifa kwa ujumla, lakini suala hili la DECI limedhihirishwa kwamba bado kuna matatizo makubwa katika mfumo wetu wa utawala. Namna ya kudumu ya kukabiliana na hali hii na kujenga taifa lenye kuheshimu utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu ni kuunganisha nguvu ya umma katika kufanya mabadiliko ya kweli katika taifa letu. Mabadiliko hayo yatawezesha kuwa na uongozi wenye kusimamia ipasavyo taasisi za umma na vyombo vya dola katika kupamba na aina zote za ufisadi, kutetea rasilimali za nchi na kuhimiza utamaduni wa uwajibikaji kupitia dira/sera mbadala zenye kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa kila raia kuendelea kwa kadiri ya fursa na vipaji ambavyo Mwenyezi Mungu amejalia taifa letu na wananchi wake.

Na John Mnyika
Mkurugenzi ya Mambo ya Nje
0754694553
http://mnyika.blogspot.com/
mnyika@chadema.net

No comments: