Sunday, April 5, 2009

Tubadili mfumo wa uchaguzi tupate uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia-2

Tubadili mfumo wa uchaguzi tupate uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia-2

Na John Mnyika
Katika makala yangu iliyotangulia nilianza kutoa mwito kuhusu haja ya kubadili mfumo wa uchaguzi kwa lengo la kupata uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia. Katika makala hiyo nieleza uhusiano baina ya demokrasia na mfumo wa uchaguzi wenye uwiano wa kijinsia. Niliuchambua mfumo wa uchaguzi ambao tunautumia hivi sasa hapa nchini wa wengi wape na pia mfumo wa uwiano ambao kwa sasa unatumika Tanzania kwa wanawake pekee ukifahamika zaidi kama viti maalumu. Nilitoa mifano ya ujumla kuhusu uteuzi wa viti maalum ulivyofanyika mwaka 2005 ndani ya CCM na ndani ya CHADEMA. Pia, nilidokeza mabadiliko ambayo CHADEMA imefanya katika katika katiba yake mwaka 2006 ambayo sasa yametoa mamlaka kwa Baraza la Wanawake wa CHADEMA(BAWACHA) kufanya utuezi wa nafasi za viti maalum za wanawake katika chama. Katika makala hii nachambua mfumo mpya wa uteuzi wa wabunge wa viti maalum ambao CCM imeupitisha na kutoa mapendekezo ya mfumo mbadala ambao kama taifa ni vyema tukauzingatia wakati wa kubadili mfumo wa uchaguzi katika nchi yetu.

Tarehe 7 mwezi Machi mwaka 2009, halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) ya CCM chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ilijadili ajenda ya kuwapata Wabunge/Wawakilishi Wanawake ili kufikia lengo la asilimia 50. Lengo hilo liliwekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ili kutimiza malengo yaliyowekwa katika matamko na makubaliano mbalimbali ya kimataifa kuhusu uwiano wa kijinsia.Katika kikao hicho Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliazimia kupendekeza kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kuwa idadi ya Wabunge katika Bunge la Muungano iwe na ukomo wa viti 360. Uamuzi huu wa CCM unalenga kuongeza zaidi idadi ya wabunge nchini, katikati ya mjadala ambao unaendelea hivi sasa kuhusu gharama kubwa ya fedha za walipa kodi inayotumika kuwalipa wabunge ukilinganisha na watumishi wengine wa umma mathalani polisi, walimu, wauguzi nk na pia ukiwianisha na hali ya uchumi wa taifa. CCM inaamua kuongeza tena idadi ya wabunge takribani 40 wapya bila kulieleza kwanza taifa tija ambayo imepatikana kwa ongezeko ambalo lilifanyika hapo awali.

Katika kikao hicho, CCM imeamua pia kwamba nchi iendelee na utaratibu uliopo sasa wa kuwapata Wabunge/Wawakilishi wa Viti Maalum Wanawake. Mfumo ambao katika makala yangu iliyopita nimechambua udhaifu wake. Isipokuwa CCM sasa inataka kwamba idadi yao katika kila chombo ipatikane kutokana na asilimia 50 ya Wabunge/Wawakilishi wote wa majimbo yaliyopo (232). Hapa maana yake ni kwamba CCM imeamua kuacha kutekeleza ahadi ambayo iliitoa kwenye ilani ya kutaka kutekeleza makubaliano ya kimataifa ambayo serikali ya CCM ilisaini yanayotaka uwiano wa asilimia 50 kati ya wanawake na wanaume. Kizio cha kupima uwiano kilipaswa kiwe idadi ya wabunge wa bunge zima na si idadi ya wabunge wa majimbo pekee. CCM pia wamekubaliana kuwa kwa kuzingatia kwamba Bunge litakuwa na ukomo wa viti 360 na kwamba idadi ya majimbo ya uchaguzi yaliyopo sasa ni 232, idadi ya Wabunge Wanawake itakayopatikana ni 116 sawa na asilimia 50 ya Wabunge wote wa Majimbo. CCM imeamua kuwa pawe na Wabunge Wanawake 7 watakaopatikana kwa mujibu wa Katiba ya nchi; hivyo kwa utaratibu huu, Wanawake 109 ndio watakaopatikana kupitia Viti Maalum. Kwa upande mwingine CCM inataka Rais apewe mamlaka makubwa zaidi ya kuteua wabunge kutoka 10 mpaka 14. Suala la Rais kuteua wabunge limekuwa likipingwa kutokana na kuongeza mwingiliano kati ya mihimili ya dola lakini pia uteuzi wenyewe kutokuwa na vigezo na mfumo wa uthibitisho (vetting). Idadi ya Wabunge 116 ukilinganisha na bunge zima linalopendekezwa la wabunge 360 maana yake ni kwamba idadi ya wabunge wanawake ambao itahakikishwa kwa mujibu wa katiba na sheria ni asilimia 33 tu. Hii si asilimia 50 inayotakiwa chini ya mfumo wa uwiano wa kijinsia unaoelezwa kuwa wa 50 kwa 50. Hivyo, wadau wa masuala ya jinsia wanapaswa kuelewa kwamba kauli zinazosemwa na wanasiasa wa CCM kwenye majukwaa kuwa tayari chama hicho kimekubaliana na mfumo wa 50 kwa 50 ni tofauti na maamuzi yao ambayo wameshayafanya katika vikao vyao kuhusu uwiano wa kijinsia utakaokuwepo katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ukweli ni kuwa CCM imeshakwepa kutekeleza ahadi ambayo iliitoa katika ilani yake ya uchaguzi mwaka 2005 badala ya 50 kwa 50 badala yake imekuja na mfumo wa uwakilishi wa 33 kwa 67. Maelekezo ya kwamba asilimia 17 iliyobaki itapatikana kwenye majimbo ni ya kisiasa ambayo hayajawahi kutekelezwa katika chaguzi zote tangu Uhuru wa Tanzania.CCM pia katika kikao hicho imepitisha azimio la kuielekeza Serikali ya Muungano irekebishe Katiba ya nchi na sheria ya Uchaguzi ili kuweka ukomo wa idadi ya Wabunge katika Bunge la Muungano kuwa 360, na pia kuhalalisha kisheria utaratibu huu mpya wa kuwapata Wabunge Wanawake kupitia Viti Maalum. Hapa CCM imeguza suala la Katiba ya nchi kuwa hodhi ya chama hicho badala ya mabadiliko yake msingi wake kuwa ni ridhaa ya watanzania wote. Ni dhahiri kwamba bila wananchi kupaza sauti maamuzi haya ya chama kimoja yatageuzwa kuwa ya taifa kwa kutumia vibaya uwingi wao bungeni, tumeona hivyo katika mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa. Lakini pia huu ni ushahidi wa wazi kuwa CCM imeshafanya maamuzi ya kutotimiza ahadi ya kuweka mfumo wa 50 kwa 50 katika uchaguzi wa mwaka 2010. Hata hivyo, katika kikao hicho, CCM haikupitisha azimio lolote kuhusu uwiano wa kijinsia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2009 ambao kimsingi ulipaswa uwe ndio msingi wa mwanzo kabisa wa kuhakikisha uwiano wa makundi mbalimbali ya kijamii kiuwakilishi.
Ni wazi suala hili sasa linahitaji mjadala mkubwa wa umma kwa sababu mabadiliko ya katiba na sheria za nchi si hodhi ya chama chochote cha siasa au kikundi cha watu wachache; ni suala la maslahi na matakwa ya umma.

Kwa ujumla, sikubaliani na marekebisho ya mfumo wa uchaguzi yaliyopitishwa na CCM na dhamira ya makala haya ni kutoa mwito kwa wadau wote kulijadili suala hili na kutoa mwelekeo unaostahili. Kwa maoni yangu mfumo wa Uchaguzi urekebishwe na kuruhusu mfumo mchanyato wa uwiano wa kura na mfumo wa “first-past-the-post” badala ya mifumo hiyo iliyotangulia. Mfumo wetu wa uchaguzi unataka Wabunge na Madiwani kupatikana kutoka katika majimbo na kata tu. Marekebisho yaliyopitishwa na CCM yanaturudisha nyuma zaidi. Kwa mfumo wa sasa wabunge wanawake hupatikana kwa uwiano wa kura za Wabunge nchi nzima na Madiwani wa wanawake kutokana na uwiano wa viti vya udiwani ambao kila chama kimepata. Lakini Wabunge Wanawake hawana mamlaka ya kisheria kwa eneo maalumu. Kwa sasa ni rahisi kusema kuwa wanatoka mikoani, lakini hii ni kwa sababu tuna chama kimoja kikubwa na hivyo kupata kura za kuenea mikoa yote. Huko mbele, tena na hawa wagombea binafsi, itatokea mikoa ambayo haitapata wabunge wanawake kwa sababu kura hazitotosha kwa chama kimoja kugawa wabunge kila mkoa. Umefikia wakati sasa kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchaguzi ili kuingiza uwakilishi wa uwiano. Kama nchi tutafakari mambo yafuatayo yanayohusu mabadiliko ya mfumo wa kisiasa wa nchi yetu: Mosi; Wabunge wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi watokane na Halmashauri za Wilaya za sasa. Mfano, badala ya Wilaya ya Manispaa ya Kinondoni kuwa na Wabunge watatu wa Ubungo, Kinondoni na Kawe, iwe na Mbunge mmoja tu atayewakilisha wilaya nzima. Halmashauri ya Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji ndio iwe Jimbo la Uchaguzi. Katika ngazi hii wagombea wasio na vyama waruhusiwe pamoja na wale wenye vyama. Kwa hali ya sasa tutapata Wabunge takribani 130 kutoka kundi hili. Idadi yao itaongezeka kutokana na kuongezeka kwa Halmashauri zitakazoundwa pindi mahitaji yanapotokea. Ikumbukwe kwamba katika ngazi ya chini kitovu cha mamlaka ni halmashauri, ambao ni msingi pia hata katika upangaji wa bajeti taifa.
Haitakuwa tena kazi ya Tume za Uchaguzi kuunda Majimbo ya uchaguzi bali vile vigezo vya kuunda Halmashauri (Baraza la Madiwani) vilivyopo kisheria (Local Government Authorities Acts) ndio vitatumika. Pili; Wabunge kati ya 150 na 200 watokane na kura za uwiano (idadi tofauti inaweza kupendekezwa). Vyama vya siasa vitapata viti kutokana na uwiano wa kura ambao kila chama kimepata katika Mkoa/majimbo.
Chama cha siasa ni lazima kiwe kimepata kwanza asilimia tano ya kura zote zilizopigwa katika Mkoa husika ili kigawiwe viti. Kwa hiyo kila chama kitatengeneza orodha ya wagombea wake kwa kila Mkoa na kuipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Orodha hii iwe katika hali ambayo kama jina la kwanza ni Mwanaume la pili awe Mwanamke, hali kadhalika kama jina la kwanza ni Mwanamke katika orodha la pili liwe la mwanaume. Mikoa itapata idadi ya Wabunge kutokana na vigezo maalumu, mfano idadi ya watu n.k. Kwa mapendekezo haya tuna uhakika wa kuwa na Wabunge wanawake zaidi ya theluthi moja katika Bunge. Lakini pia tutakuwa na uhakika kwamba kila Mkoa utakuwa na Mbunge au Wabunge wanawake. Ama kama tutakubaliana kwa pamoja kama taifa katika lengo la kuongeza idadi kubwa ya wanawake kuelekea uwiano wa hamsini kwa hamsini(50-50), robo tatu ya wabunge wa uwiano inaweza kuwa ni orodha ya wanawake na robo ikabaki kwa ajili ya wanaume. Lengo la kuwa na orodha ni kuwezesha pia vyama kutumia orodha hiyo kuhakikisha uwakilishi wa makundi ya kijamii mathalani walemavu, vijana na viongozi muhimu wa kijamii ambao ni muhimu kuwepo bungeni.
Mabadiliko haya ya mfumo wetu wa Uchaguzi yana faida nyingi sana. Moja ya faida ni kuvigeuza vyama vyetu vya siasa kutoka katika kushindanisha watu tu, bali pia kushindanisha sera. Kwa sababu wananchi watakuwa wanapiga kura mbili. Kura moja ya chama na kura nyingine ya ama diwani au Mbunge na Rais. Kura ya chama ndio itatufanya kupata wabunge wa uwiano. Wala hatutatumia mfumo mmoja kuzalisha mfumo mwingine. Bali kila mfumo utazalisha Wabunge kuunda Bunge letu. Sisi hatutokuwa wa kwanza kufuata mfumo huu wa uwiano-Msumbiji, Afrika ya Kusini, Ujerumani, Uswidi na hata India.
Vyama vikianza kushindanisha sera tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana kama nchi katika kuimarisha mfumo wa demokrasia na kwa kweli hatutokuwa na wasiwasi wa vyama kudhoofika kutokana na wagombea Binafsi kuruhusiwa. Demokrasia ndani ya vyama itaimarika kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi itahakikisha vyama vinapata wawakilishi wake katika Orodha ya Mikoa kidemokrasia. Sehemu ya kuanza kutumia mfumo huu wa uchaguzi wa ni kupitia uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2009 ambapo tunaweza kupima mafanikio na kuboresha mfumo mzima wa kitaifa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2010. Ili kutimiza azma hiyo, ni muhimu kufanya marekebisho katika sheria zinazohusu uchaguzi huo lakini pia inabidi kupanua makubaliano ya wadau yaliyofikiwa baina ya vyama na serikali mwezi Februari mkoani Morogoro ili kanuni zitakazotungwa zihusishe uwiano wa kijinsia katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, suala kipaumbele halipaswi kuwa kuhakikisha uwiano wa kijinsia tu; suala halipaswi kuwa idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi, bali ubora wa wawakilishi katika vyombo vya maamuzi na tija yao kwa taifa. Wapo watu wanaopinga wanawake kupewa nafasi katika vyombo vya maamuzi kwa kigezo tu kuwa nafasi za uwakilishi zisitolewe kwa jinsia bali uwezo. Lakini ukiangalia kwa upande mwingine, katika vyombo vyetu vya maamuzi hivi sasa kuna wanaume wengi wenye uwezo mdogo. Kwa mantiki hilo, suala la kuhakikisha kwamba kama taifa tunakuwa na viongozi bora kwenye vyombo vya maamuzi linapaswa kutizamwa kwa upana wake bila kujali jinsia. Pia ieleweke kwamba kipaumbele sio uwepo tu wanawake katika vyombo vya maamuzi, bali uwepo wao unapaswa kuambana na ubora wa kushughulikia masuala yanayohusu umma ikiwemo kuweka mkazo katika masuala yanayowagusa wanawake. Mathalani, wabunge wengi wa viti maalum wameshindwa kushughulikia masuala yanayogusa umma wa watanzania lakini pia wameshindwa hata kuweka mkazo katika masuala yanayogusa wanawake wenzao mathalani vifo vya watoto wadogo na wakina mama wajawazito kutokana na mazingira mabovu katika sekta ya afya nchini.

Ni vyema pia wadau wa masuala ya jinsia wakatazama masuala haya kwa upana wake, kwamba kuwekwa pembezoni kwa kundi moja kijamii mathalani wanawake ni matokeo ya mifumo ya kisiasa kuweka pembezoni makundi ya kijamii kwa ujumla wake. Kwamba kama wadau wakiungana kuhakikisha kuna uwanja sawa wa kisiasa wenye uchaguzi huru na haki ni wazi kuwa makundi yote ya kijamii iwe ni wanawake au walemavu wanaweza kushiriki. Hivyo, haja ya kufanya mabadiliko ya katiba na kisheria yenye kujenga misingi ya haki katika taifa ieleweke kwamba ni ajenda ya pamoja katika taifa. Kurekebisha mfumo wa uchaguzi ili kupata uongozi wenye uwiano wa kijinsia ni sehemu mojawapo ya msingi katika harakati pana zaidi za kupambana na ufisadi, kutetea rasilimali na kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa wote.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com

No comments: