Tuesday, July 21, 2009

“Ruksa” kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-4


“Ruksa” kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-4

Na John Mnyika


Makala zilizotangulia zimedokeza wakina nani ni watumishi wa umma na ushiriki wao katika siasa katika vipindi vilivyotangulia; wakati wa mfumo wa chama kimoja 1965 mpaka 1992 na kipindi cha awali cha mfumo wa vyama vingi 1992 mpaka 2000. Pia nilianza kufanya mapitio ya kuhusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanzia mwaka 2000 na tunapoelekea katika chaguzi za mwaka 2009 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Katika makala hii tutafanya mapitio ya mambo ambayo watumishi wa umma wanaruhusiwa kuyafanya kama sehemu ya ushiriki wao katika siasa. Makala ijayo tutafanya mapitio ya mambo yasiyoruhusiwa kufanywa na watumishi wa umma katika ushiriki wao kwenye siasa.

Kwa ujumla washiriki wa umma wanaruhusiwa kushiriki katika siasa. Ikumbukwe kuwa utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na Sheria ya Utumishi Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kinampa mamlaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi kutoa waraka kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa umma.

Chini ya Mamlaka hayo, Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo akiwa Martem Y.C. Lumbanga tarehe 26 Juni, 2000 alitoa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma na. 1 wa mwaka 2000 wenye kumb. Na. SHC/C.180/2/113. Waraka huu ulihusu maadili ya Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Waraka huo ulianza kutumika kuanzia Julai Mosi, mwaka 2000.Waraka huo umetoa ruhusa kwa watumishi umma kushiriki katika mambo ya siasa na umeelekeza wazi kwamba wanaweza kushiriki katika shughuli ambazo tutazipitia katika makala hii.

Mtumishi wa umma anaruhusiwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa anachokipenda isipokuwa watumishi wachache ambao wametajwa kwenye waraka huo. Tafsiri ya waraka huo ni kwamba wafanyakazi mbalimbali wa serikali na taasisi zake wanaweza kujiunga na vyama vya siasa mathalani Rais, Mawaziri, wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na Mashirika ya umma, watendaji wa kata nk. Orodha hii inahusisha pia waajiriwa wa kawaida wa serikali mathalani walimu wa shule za umma, watumishi wa sekta ya afya wa serikali, maofisa wote waajiriwa wa halmashauri/serikali za mitaa nk. Kumekuwa na baadhi ya watumishi waandamizi wa serikali wanawakataza watumishi wa kawaida mathalani walimu kujiunga na vyama vya siasa wanavyovipenda; ni vyema ikaeleweka kwamba vitendo hivyo ni vya uvunjaji wa haki za kikatiba, kisheria na kitaratibu hivyo watumishi hao wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwa vyombo na wadau wanaohusika kwa ajili ya hatua kuweza kuchukuliwa.

Watumishi pekee wa umma wasioruhusiwa kushiriki katika mambo ya siasa ni wale walio katika makundi ya utumishi maalum.

Hawa ni watumishi ambao katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza wazi kwamba hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa. Ni kundi la watumishi wa umma ambao hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli zozote zingine za kisiasa isipokuwa kupiga kura tu. Ibara ya 147(3) na (4) ya Katiba imewataja Askari wa Jeshi la Wananchi(JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), Polisi na Magereza. Pia Ibara ya 113A imewakataza majaji na mahakimu wa ngazi zote. Kadhalika Ibara 74(14) na (15) imewazuia wajumbe na watumishi wa Tume ya Uchaguzi na Wasimamizi wa Uchaguzi.

Pia waraka huo na. 1 wa mwaka 2000 umeyataja makundi mengine ambayo pamoja ni kuwa hayajakatazwa na katiba kushiriki kwenye shughuli za kawaida za kisiasa ikiwemo kujiunga na vyama vya siasa. Mathalani, watumishi wa idara ya usalama wa taifa, taasisi ya kuzuia rushwa(sasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU), watumishi wa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, watumishi wa ofisi ya bunge na mawakili wa serikali. Hata hivyo, nao wanaweza kushiriki kwenye siasa kwa kupiga kura. Hivyo, kwa ujumla, raia wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliofikia umri wa kupiga kura wanaruhusa ya kushiriki kwenye siasa ikiwemo watumishi wote wa umma kwa kupiga kura.

Haki na wajibu huu wa watumishi wa kupiga kura unazaa ruhusa ya watumishi wa umma kuhudhuria mikutano halali ya kisiasa nje ya saa za kazi kama msikilizaji. Inafahamika kwamba wapo watumishi wa umma ambao huwatishia watumishi wao wa kawaida wasihudhurie mikutano ya kisiasa hata baada ya kazi. Utata wa ziada unaibuka hapa ni kuhusu watumishi wa umma ambo kwa asili ya kazi yao hawaruhusiwi ‘kujihusisha na shughuli za kisiasa isipokuwa kupiga kura’. Swali la kujiuliza: Je, zuio hili linahusu vile vile kuwazuia kushiriki mikutano ya hadhara ya vyama wakati wa kampeni na wakati wa kawaida kwa ajili ya kusikiliza sera ama ilani za vyama na viongozi ama wagombea? Kwa tafsiri ya kawaida; jibu ni ndio. Kama hivyo ndivyo, sasa kundi hili ina maana limepewa haki ya kupiga kura lakini halina haki ya kusikiliza ili kuweza kufanya maamuzi sahihi ya nani mtumishi husika wa umma ampigie kura? Hivyo, ni vyema waraka husika ukafanyiwa marekebisho katika eneo hili ili kuondoa utata wa tafsiri. Katiba, Sheria na Taratibu zinapaswa tu kuwakataza watumishi hawa maalumu wa umma kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa, na si kuwakataza hata kuhudhuria mikutano halali ya kisiasa.

Pia, waraka huo umeelekeza kwamba watumishi wa umma wanapaswa kuhudhuria mikutano ya kisiasa kama wasikilizaji tu. Huku ni kuminya uhuru wa kikatiba wa kutoa maoni na wa kuzungumza. Haiwezekani ukawa na raia ambaye amepewa haki ya kujiunga na chama cha siasa lakini hana haki ya kuzungumza katika mikutano, tafsiri yake ni kwamba hana hata haki ya kuzungumza katika vikao vya wanachama. Lakini tumeona wakati wote watumishi wa umma, ikiwemo waandamizi wa serikali wakivunja kipengele hiki kwa kuzungumza katika mikitano ya kisiasa; ya ndani na hata ya hadhara. Hivyo, kifungu hiki nacho kinapaswa kufanyiwa marekebisho kwa kuwa hakitekelezwi wala hakitekelezeki.
Waraka Na. 1 wa Mkuu wa Utumishi wa Umma pia umeruhusu mtumishi wa umma kutoa michango yake binafsi kwa ajili ya chama chake akiwa nje ya mahali pa kazi na nje ya saa za kazi. Haki hii inamaanisha kwamba mtumishi wa umma anaweza kutumiza wajibu wa kuchangia chama chake kwa maana ya kulipa kiingilio na ada ya uanachama. Hii inamaanisha pia kwamba watumishi wa serikali wa uhuru wa kuchangia rasilimali zao kwa ajili ya kufanikisha harakati za kisiasa, hii ni pamona na kuwa na ruhusa ya kuchangia wagombea katika kampeni za uchaguzi. Hata hivyo, ruhusu hii nayo ina utata wa kitafsiri kwa kuwa hakuna mali kumefafanuliwa maana ya neno ‘michango’. Kwa tafsiri ya juu juu na kwa kuzingatia mipaka ilidokezwa hapo juu ya kumtaka mtumishi husika kuwa msikilizaji pekee; tafsiri ya michango inayokusudiwa hapa inaweza kuonekana kuwa ni michango ya fedha na mali.

Hata hivyo, ieleweke kwamba katika medani ya siasa, uzoefu wa kimataifa unaonyesha kwamba katika michakato ya kidemokrasia michango ni zaidi ya fedha na mali. Rasilimali kwa sasa zinatafsiriwa kwa upana wake kujumuisha nguvu kazi ikiwemo vipaji, utaalamu na hata mawazo. Kwa maneno mengine, michango ambayo mtumishi wa umma anaweza kutoa kwa chama chake inaweza pia kuhusisha kuchangia mawazo, kutumia muda wake, vipaji vyake na utaalamu wake. Jambo hili ni muhimu sana likatafakariwa kwa umakini wake kwa kuwa kati ya changamoto zinazokabili ujenzi wa oganizesheni ya vyama vya siasa hususani vya upinzani ni upungufu wa rasilimali watu ya kutosha yenye utaalamu mbalimbali. Kitendo cha kuwazuia watumishi wa umma, ambao kwa kiasi kikubwa wanahusisha kada ya wasomi hususani katika maeneo ya vijijini kunaacha vyama vya siasa kuungwa mkono na umma wa wananchi wa kawaida bila mchango wa kutosha wa kada hii muhimu kwa mwelekeo wa taifa.

Katika muktadha huo, kama sehemu ya ushiriki wao katika siasa watumishi wa umma wanapaswa wakiwa nje ya maeneo ya kazi na nje ya saa za kazi kuchangia katika mwelekeo wa vyama vya siasa. Mathalani, mwalimu anaweza kabisa kuchangia mwelekeo wa kisera wa chama cha siasa kuhusu masuala ya elimu na haki za walimu. Kadhalika mtumishi wa sekta ya afya anaweza kufanya hivyo hivyo kwenye eneo lake la uzoefu. Maofisa Kilimo ama Madini nao wanaweza kutoa mchango mkubwa kutokana na utaalamu wao. Kwa ujumla kama ambavyo watumishi wa umma wanapaswa kusaidia watumishi wengine wa kiserikali wakiwa kazini ndivyo ambavyo wanapaswa kusaidia kimawazo na kirasilimali viongozi wa vyama vyao vya siasa. Yapo mambo ambayo kutokana na tofauti za kiitikadi na kisera, mtumishi wa umma anaweza akayependekeza lakini yasiweze kutekelezwa na chama kilichoko madarakani. Masuala kama hayo anaweza kuyatoa katika chama chake chenye mwelekeo anaoubaliana nayo na pindi yakiweza kutekelezwa matokeo yake yanaweza kuleta tija kwa taifa kwa ujumla. Hizi ndizo siasa ambazo zinafanywa na nchi ambazo zina demokrasia ya vyama vingi kwa muda mrefu zinazotambua kwamba siasa sio uadui bali ni mfumo wa uwagawanyaji rasilimali unaopaswa kuongozwa kwa ushindani wa hoja mbadala.


Pamoja na kutumia fursa zilizomo kwenye waraka Na. 1 wa Mkuu wa Utumishi wa Umma kama nilivyozidokeza na haja ya kufanya marekebisho katika waraka huo ili kutoa tafsiri zinazoeleweka ni muhimu pia kuendeleza harakati za kufanya mabadiliko ya kweli katika sekta ya utumishi wa umma. Harakati hizi zinapaswa kuendeshwa na vyama vya wafanyakazi hususani wa sekta ya umma. Mabadiliko hayo ya kikatiba, kisheria na kimitazamo yatawezesha kuwa na tunu za kitaifa, misingi kamili ya haki za raia, mifumo ya uwajibakaji wa viongozi na uwanja sawa wa kisiasa. Mabadiliko hayo yatawezesha pia kujenga taasisi za kitaifa, uongozi bora na dira ya pamoja yenye kuunganisha nguvu za umma katika kupambana na ufisadi, kutetea rasilimali na kusimamia fikra mbadala zenye kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa wote. Taifa wananchi wanaweza kuneemeka na uwezo ambao wamejaliwa wao na nchi kwa ujumla. Watumishi wa umma wanapopigania ongezeko la mishahara na uboreshwaji wa maslahi waelewe kwamba uongozi wa kisiasa umeshikilia hatma yao. Hivyo, ushiriki wa watumishi wa umma kwenye siasa ni suala lenye maslahi kwao binafsi na kwa taifa kwa ujumla. Watumishi wa umma Tanzania wakumbuke wosia wa Hayati Kwame Nkurumah ya kwamba ‘utafuteni ufalme wa siasa’ na yote mtaongezewa.

Mwandishi wa Makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje(CHADEMA) anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com


No comments: