Monday, February 22, 2010

Kauli ya Waziri Mkuu Pinda juu ya Rostam Aziz ‘imepinda’ na ‘inapindisha’ mambo

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewashauri wananchi wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora wasimkatae Mbunge wao Rostam Aziz wakati wa uchaguzi mkuu ujao kwa kusikia maneno yanayosemwa bungeni, badala yake wazingatie kile alichowafanyia. “Iwapo mnataka kumchagua tena Rostam zingatieni amewafanyia nini katika ubunge wake. Msisikilize kile kinachosemwa bungeni juu yake. Bunge lina mambo yake, mimi kama Waziri Mkuu nafahamu mambo ya pale bungeni,” alisema Waziri Mkuu. (Chanzo, Habari Leo-Gazeti la umma).

Kauli hii ya Pinda ‘imepinda’ na inajaribu ‘kupindisha’ mambo:
Kwanza amefanya kampeni za kumnadi mbunge wa chama chake CCM kwa kutumia cheo chake cha Uwaziri Mkuu katika ziara ya Kiserikali inayogharamiwa na kodi za wananchi wote bila kujali itikadi; huu ni ubaguzi na matumizi mabaya ya madaraka kwa mujibu wa katiba na sheria.
Pili, amebeza bunge kuwa lipuuzwe kwa kuwa linayoyajadili hayana maana kwa wananchi hivyo wazingatie yanasemwa bungeni. Ni muhimu angeyataza hayo ‘mambo yake’ ya bunge ambayo yeye kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni anayafahamu. Huku ni kudharau hadhi ya bunge kwa mujibu wa katiba na sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge.
Tatu; kwa hiyo kwa mantiki ya waziri mkuu ni kwamba mtu akifanya ufisadi na/ama matumizi mabaya ya madaraka lakini akatumia sehemu ya fedha zake kwenda kuwafanyia kuwafanyia wananchi wa jimbo lake ‘mambo kadhaa’ basi huyo aendelee tu kuwa na haki zote za kuwa kiongozi wa umma.

Waziri Mkuu akasome tena Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka namba 13 ya mwaka 1984( iliyofuta sheria namba 9 ya mwaka 1983) pia akasome Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 5 ya mwaka 2001 na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini namba 11 ya mwaka 2007; halafu ajibu kwanza tuhuma kuhusu Richmond, Dowans, Kagoda nk kabla ya kuanza kutoa kauli za kusafisha watuhumiwa waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi (List of Shame). Lakini siwezi kushangaa sana, ni Waziri Mkuu Pinda huyu huyu alilidanganya bungeni kuwa Meremeta ni Siri ya Jeshi hivyo hawezi kujibu chochote; kampuni yenye tuhuma ya ufisadi wa mabilioni mengi kuliko kashfa ya akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu (BOT). Huwa najiuliza, kama huyu ni Pinda maarufu kama mtoto wa Mkulima anayetajwa pia kuwa ni mtumishi wa usalama wa taifa; ni nani atakayesimama ndani ya Serikali na CCM kusimamia maadili na uwajibikaji?

Haya ndio matokeo ya uongozi kuingia madarakani kwa kufadhiliwa na watuhumiwa wa ufisadi. Narudia tulichosema mwaka 2005: Mabadiliko ya Kweli, hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale kwa Ari, Nguvu na Kasi(ANGUKA) mpya. Kwa falsafa ya chukua chako mapema (ccm) Tanzania yenye neema haiwezekani. Tunahitaji mabadiliko ya uongozi na mfumo wa utawala kuondoa hodhi(monopoly/dominance) ya chama kimoja katika bunge, halmashauri na siasa za nchi kwa ujumla. Waziri Mkuu Mizengo aache 'mizengwe' ya kisiasa, awaachie wananchi wawe huru kuwahukumu viongozi kwa maneno na matendo yao sio tu majimboni mwao; bali ndani na nje ya nchi yetu.

4 comments:

Anonymous said...

Mnyika JJ,

Umejitahidi kujenga hoja nyingi kwa kutumia sheria zaidi ya mbili kuonesha Waziri Mkuu alikosea kumuunga Mkono Rostam.

Hivi List of shame ni uthibitisho tosha kuwa Rostam ni mwizi na alihusika na Kagoda?

nimechoka kusikia maneno na tetesi zisifanyiwa kazi na hii inaonesha ni maneno tu kama alivyosema mheshimiwa Pinda.

kama una ushahidi tosha wa Rostam kuhusika basi ufikishe mbele ya sheria!

nimechoka kusoma mawazo ya wanasasa wanaopenda mambo mepesi mepesi na kujiunga kwenye mkumbo.

hili ndilo tatizo kubwa sana na vyama vya upinzani vya nchi yetu;hamjipangi

ray05 said...

naomba nimjibu huyo bwana fulani hapo juu(anonymous) ambaye amechoka kusikia maneno ya wanasiasa.
Hivi usiposikiliza maneno ya wanasiasa ni vp utaijua siasa?usipoijua siasa ni vip utaijua system ya uongozi nchini kwako while leadership is all about politics?
kinachotakiwa ni wewe kuwa makini na hao unaowasikiliza,kuchambua kipi kinafaa na kipi hakifai.na waziri mkuu hata mimi hayaniingii akilini kwasababu sidhani kama alikwenda kuwaambia wananchi wamchague Rostam au la,ilihali wao wenyewe wanajua amewafanyia nini na kama anafaa au hafai.

Anonymous said...

John Mnyika,
Awali ya yote hongera sana kwa hoja zako unazozitoa kwa kweli nadiriki kusema zinagusa pale ambapo mamilioni ya watu wenye kupenda ukweli....mimi ndio nimejitokeza baada ya kukusikia katika BBC kwenye mjadala kuhusiana na TEKNOHAMA kwa wale waliosikiliza watakubaliana nami muda ungeongezwa kwani mafundisho yalikuwa mengi...
Nije katika harakati za kisiasa napenda nikupongeze kwa ujasiri wako wa kuamua kugombea tena Ubungo...kama utakuwa na kumbukumbu uliwahi hojiwa na Jenerali Ulimwengu katika kinyang'anyiro cha 2005 msema kweli ni mpemzi wa Mungu watu wengi walifarijika sana kutokana na hoja ambazo ulizijenga kuhusiana na Ubungo,katika yote na ambalo bado nalishangaa ni kitendo cha Ubungo kutokuea na maji ili hali mabomba ya kutoka Ruvu yanapita hapo.NAPENDA NIKUTAKIE KILA LA HERI KATIKA VITA HII....HAKUNA KULALA MPAKA KIELEWEKE
By Allan
Email allan.katondo@yahoo.com

Anonymous said...

Huyo bwana anayesema kachoka hoja za sheria ni mamluki wa ccm hakika.Kama anamtetea rostam amshauri akafungue kesi mahakamani kwa kudhalilishwa kwamba ni mwizi.Kila mara tunawasikia Rostam na lowasa wanasema wamechoka kudhalilishwa wataishitaki chadema mara Mwanahalisi lakini hawafanyi hivyo sasa kama wanasingiziwa mbona hawafungui mashitaka wanayosema kila siku watafungua?Tafakari kabla hujatoa hoja zako ndugu.Na inaonyesha hauna uchungu na taifa lako lililobarikiwa kila kitu lakini bado tunaomba omba mataifa ya watu.Hii ni aibu kuu.Tulimtegemea sana Pinda lakini katuangusha sana.Yeye ni mwana wa mkulima jina na sio uhalisia wa matendo.EE MUNGU TUNAOMBA UIREHEMU TANZANIA NCHI YA MAZIWA NA ASALI LAKINI HATUIFAIDI HATA KIDOGO.AMEEN