Tuesday, May 24, 2011

Kauli kuhusu mauaji na kukamatwa na wabunge Tarime

KAULI YA KATIBU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU VITENDO VYA JESHI LA POLISI KWA RAIA NA KUKAMATWA KWA WABUNGE WA CHADEMA

Katibu wa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA nalaani vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Polisi kwa kusababisha mauji ya raia na kukwepa kufanya uchunguzi kamili na huru kuhusu wahusika wa vifo hivyo na kuingilia haki za msingi za jamaa za marehemu na wananchi wa eneo husika kushiriki katika maziko ya wakazi wenzao na hatimaye kupatiwa haki nyingine zinazostahili kutokana na madhila yaliyotokea.

Aidha nakemea hatua ya jeshi la polisi ya kuwakamata wabunge wa CHADEMA, Tundu Lissu na Esther Matiko wakiwa katika kazi ya kuwatumikia wananchi na natoa mwito waachiwe mara moja; wao pamoja na wote waliokamatwa nao.

Tundu Lissu (Mb) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba aliitwa na wahanga wa tukio husika pamoja na chama kwenda kusimamia haki za msingi za familia za marehemu baada ya polisi kukataa kufanya uchunguzi na pia kuminya mazingira ya haki kupatikana.

Akiwa katika kutekeleza wajibu huo, jana (23 Mei 2011) alitaarifiwa na familia za marehemu na wananchi wengine kwamba polisi ina mpango wa kuchukua miili ya marehemu usiku na kuipeleka kusikojulikana na kuombwa kuungana nao katika kuwapa huduma za kisheria katika hatua zote. Aliambatana na familia za marehemu, wananchi na viongozi wa chama kufuatilia suala hilo ndipo alipokamatwa yeye na wengine na kuwekwa rumande kuanzia jana mpaka hivi sasa.

Esther Matiku ambaye ni mbunge wa viti maalum kupitia mkoa wa Mara anayetokea Tarime akiwa katika eneo lake la kazi leo (24/05/2011) alijulishwa na wananchi wa Nyamongo kwamba maiti ambazo walizichukua polisi kwa nguvu zingine wamezitelekeza njiani na kuitwa kwa ajili ya kushuhudia na kuchukua hatua zinazostahili kwa niaba ya wananchi. Akiwa katika kushughulikia suala hilo naye alikamatwa na jeshi la polisi na kuwekwa rumande mpaka hivi sasa.

Ifahamike kwamba matukio ya Nyamongo na Tarime kwa ujumla ni matokeo ya uongozi wa serikali kushindwa kusimamia vizuri sekta ya madini ikiwemo kuacha kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati wa miaka kadhaa sasa kutokana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria na mikataba vinavyofanywa na kampuni Barick Africa Gold na vile vinavyofanywa na polisi na vya kifisadi vinavyofanywa na viongozi wengine wa kiserikali wanaonufaika na hali hiyo yenye athari kwa wananchi katika maisha yao kutokana na mauji, uchafuzi wa mazingira, upotevu wa mapato ya umma na watanzania wa eneo husika kutokunufaika kwa rasilimali.

Naungana mkono na wananchi na wadau wote waliotoa mwito kufanyika kwa uchunguzi huru wa vifo (inquest) ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa na kwa nafasi yangu nyingine kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitatoa tamko karibuni lenye kueleza kwa kina udhaifu wa serikali ulivyosababisha mauji hayo na kutaka wahusika akiwemo waziri kuwajibika.

Aidha, kwa mara nyingine narudia tena kutoa pole kwa familia za marehemu ambao wanapitia kipindi kigumu wakati huu kutokana na matukio yanayoendelea; Mwenyezi Mungu awape uvumilivu wa kusimamia haki na ukweli kwa mustakabali wa taifa.

Imetolewa tarehe 24 Mei 2011 na:

John Mnyika (Mb)
Katibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Na Wabunge wa CHADEMA

No comments: