Katika kipindi cha Hot Mix cha EATV muda mfupi uliopita Waziri wa Fedha amesema kwamba mawazo ya kutoza elfu moja kwa mwezi kwenye kila laini ya simu ni ya wabunge.
Kauli inayokaribiana na hiyo imewahi kuandikwa pia na Naibu Waziri wa Wizara yenye dhamana na sekta mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni. Baadaye alifuata Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na sasa waziri mwenyewe. Mwaka 2012 nilitahadharisha kuhusu udhaifu wa Rais (na Serikali) na uzembe wa Bunge katika masuala yanayohusu maandalizi ya bajeti, hususan kutozingatiwa kwa mpango wa taifa wa maendeleo na ongezeko la mara kwa mara la gharama za maisha kwa wananchi. Kwa kauli hizi za Serikali udhaifu na uzembe huo unaendelea kujihidhirisha.
Kauli hizi za Serikali ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge.
Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Serikali ijitokeze itaje kwa majina na wabunge gani hasa walitoa mawazo hayo. Mimi sijawahi kutoa wazo hilo wala kuliridhia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwenye Hotuba yake juu ya Muswada wa Sheria ya Fedha ilipinga pendekezo hilo lililokuwepo katika jedwali la marekebisho lililowasilishwa na Wizara ya Fedha. Katika kuhakikisha kwamba kifungu hicho hakipitishwi, niliwasilisha jedwali la marekebisho ya sheria kutaka kifungu hicho kiondolewe katika muswada wa sheria ya fedha na marekebisho yake yaliyowasilishwa na Serikali.
Hata kama ikiwa ni ukweli kwamba wazo hilo ni la baadhi ya Wabunge (ambao ni muhimu wakatajwa kwa majina), Serikali inayokwepa kutetea maamuzi ambayo Serikali yenyewe imeyaunga mkono inadhihirisha kwamba imechoka na imepoteza uhalali kwa kimaadili kwa kushindwa kukubalika mbele ya wananchi wake yenyewe (illegitimate government) .
Mamlaka na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Katika kutekeleza mamlaka hayo, Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na chenye mamlaka pia ya kutunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi. Hata hivyo, ibara ya 99 ya Katiba imeweka mipaka kwa mamlaka hayo ya Bunge inapokuja suala la kutunga sheria ya fedha kama hii iliyoongeza mzigo wa kodi kwa wananchi. Mamlaka hayo yamewekwa kwa kiwango kikubwa mikononi mwa Rais kupitia Waziri wake mwenye dhamana.
Ninachofahamu mimi ni kwamba kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha aliposoma bajeti ya Serikali. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza kwamba imefutwa.
Waziri wa Fedha aeleze katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani mpaka likaingia katika kitabu cha hotuba yake na nini maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).
Kifungu hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kupitia jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Waziri wa Fedha mwenyewe. Hivyo, ajitokeze na kueleza katika hatua hiyo, ni wabunge gani waliotaka kodi hiyo iingizwe katika muswada huo na sababu za Wizara ya Fedha kukubaliana nao.
Uzembe wa Bunge usitumike kama kisingizio cha kuficha udhaifu wa Serikali katika suala hili na mengine. Ni wazi, kuna uzembe pia kwa upande wa Bunge kwa kuacha mapendekezo ya wabunge wachache yageuzwe kinyemela kuwa ni msimamo wa wabunge wote bila ya kuwa na azimio la Bunge kuhusu mapendekezo hayo.
Katika mchango wangu bungeni kuhusu muswada huo, nilifanya rejea ya inayoitwa Kamati Ndogo ya Spika ya kupanua wigo wa mapato iliyoundwa kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Bajeti; zote mbili zikiongozwa na Mh. Andrew Chenge (Mb).
Kamati hii ambayo haijawahi kuwasilisha ripoti yake Bungeni bali kwa Spika mwenyewe na hatimaye sasa ripoti kuwekwa kwenye maktaba ya Bunge, bila ya ripoti hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni kama taarifa ya kamati au walau kuwekwa mezani kama hati rasmi ya Bunge; sasa inatumika kusukuma mzigo wa lawama kwa Bunge na wabunge.
Baada ya kamati hii, majadiliano kati ya Serikali na Kamati ya Bajeti yaliyofanyika kwa nyakati mbalimbali yanatumika kuhalalisha maamuzi ya Serikali yenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi katika hali yenye kudhihirisha uzembe wa Bunge wa kuachia mamlaka na madaraka yake kutumiwa visivyo.
Katika muktadha huu, kulaumiana kati ya Serikali na Wabunge au kulalamika kwa wananchi pekee hakutoshelezi kuwezesha uwajibikaji au mabadiliko yanayokusudiwa. Lawama ziendelee kwa kuwa zinasaidia kuendeleza mjadala na kufanya ukweli uoendelee kutolewa na pande zote. Malalamiko ya wananchi yaendelee kwa kuwa inawezesha Serikali na wabunge kutambua athari za maamuzi hayo kwa wananchi.
Tunapaswa kwenda mbele zaidi kwa wewe, mimi na mwingine kuchukua hatua? Wewe unapendekeza hatua gani zichukuliwe? Nitatoa msimamo wangu kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa baada ya kupata maoni yenu kwa kuniandikia kupitia mbungeubungo@gmail.com. Maslahi ya umma kwanza.
John Mnyika (Mb)
11/07/2013
14 comments:
Serikali ya ccm halina jipya limefilisika kila idara na sekta zote, garama za maisha zipo juu, serikali imeshindwa kutafuta njia mbadala ya kumpunguzia mwananchi wa kawaida mzigo wa kodi nyingi badala yake wanazidi kutubana. Misamaha ya kodi kibao...! Tumewachoka wenye magamba.
hapana,hapana hapana kutukata kodi..makampuni ya simu ndio walipe na sio sisi..kwanza wanatuibia tu kila siku makato ktk cm..sitaki,nasema sitakiiii uuuuuwi,ukungaaaaaaaa
Tumechoka kukandamizwa na serikali inayoongozwa na watu wasiokuwa na huruma kwa wanyonge wake. Athari ya kodi ya sh 1000 ya laini ya simu ni kubwa sana ikiwa ni pamoja na kuongeza gharama ya maisha ya mwanainchi wa kawaida mara dufu, hivyo kuongeza kiwango cha umaskini tanzania. Hata hivyo walio wengi vijiji hutumia credit chini ya sh 1000 kwa mwezi kwa maana wengine wanasimu kwa kwa ajili ya kupokea tu kutoka kwa ndugu zao walio mbali. Kwanini serikali isitoze kodi kwa makampuni makubwa zilizowekeza nchini wanaotumia rasilimali zetu kwa manufaa yao tu? Serikali imeshindwa kucontrol mapato yake maana kuna makampuni na watu binafsi wanaofanya biashara lakini hawajatambuliwa na pengine wanafanya biashara kwa njia ya rushwa ili wasitozwe kodi. kuna mianya mingi ambazo hupoteza mapato ya serikali matokeo yake hii serikali isyomakini inakandamiza wanyonge kila mwaka huku gharama za maisha zikiendelea kuongezeka siku hadi siku. Hivi Mh. Mkapa aliwezaje kuthibiti mfumuko wa be kwa miaka yote kumi lakini serikali ya sasa mfumuko umeongezeka mara tatu na zaidi? Ni wakati wa kujitafakali sisi wanyonge ili tuweze kuchukua hatua dhidi ya serikali tulioiweka madarakani kwani imeshindwa kufikiri mbinu dhabiti ya kuongeza mapato yake.
Hata fedha zinazokusanywa haziwafikii wananchi ipasavyo maana wamegaji wa bajeti wamekuwa wengi ili wajinufaishe wenyewe. Wabunge mmepewa madaraka ya kuihoji udhaifu wa rais, kama ameshindwa basi aiachie ngazi, maana amekuwa rais wa kutuumiza sisi tuliyemuweka. HAKUNA KUTOZWA KODI YA LAINI, NA KATIKA HILI NI BORA TUSIWE NA WAWAKILISHI (WABUNGE) WANAOSEMA NDIYO KWA KILA KITU KWENYE VIKAO VYAO VYA BUNGE. CCM MMEZIDI KUTUBURUZA. MH. Mnyika tunakuomba upeleke hoja binafsi bungeni ya kupinga kodi hii na sisi tutakuunga mkono.
Lets accept change, we can't be ruled by the government with narrow thinking mind in collecting tax for its people's development and we are tired of you (Government)
ndugu yangu mnyika elimu uliyotoa ni nzuri sana ni kweli tunaumia sana lakini kuna wananchi wasio jua hili hivyo ningeomba kama uwezekano upo muwazungukie wananchi nchi nzima mi nadhani watawaelewa japo hata mimi mahali nilipo nitawaelimisha wananchi wanaonizunguka ili mwisho wa siku tuuzike ufisadi huu
Kwa kweli hii ni kuongeza ugumu wa maisha kwa mwananchi pasipo sababu za msingi . serikali imetoa misamaha kwa wawekezaji wa madini na matokeo yake ni kuachiwa mahandaki ambayo hayana manufaa kwetu .
Aisee, huku ni kutufirisi wananchi. mimi naamini kila tunaponunua vocha kuna sehema ya kodi tunayolipia. Elfu 1 kwa mwenzi ni pesa kubwa sana kwa mtanzania. Wafikilie tena kwakwel la sivyo 2tarud kwenye barua na ndipo tutazidi kuachwa nyuma kimaendeleo
Hapa mweshimiwa ccm badala ya kukaa na kujadili mambo ya msingi wanajadiri ujinga...mf Mabomu yalivolipuliwa Arusha chdm wakasema rais aunde kamati ya kimahakama kuchunguza ili jambo Kikwete kakas kimya,lakini alipockia Chadema sasa wanataka wawafundishe vjna wao kujilinda,hl ndo kalisikia eti anakemea vikundi vya mgambo...mm hapa najiuliza hv washauri wake ndo wanampotosha au inakuwaje? Yaani Tz hatuna viongozi labda Obama aje atuongoze.
Mi nauliza wale ndugu zangu wa kule nyasa ambao kwa mwezi anaweka vocha ya sh 500 au jititatu atalipaje au atalimbikiziwa deni. Ifike wakati sasa tukodi rais,na mawazili wazungu wakituchosha kama hivi tunawafusha
Kwenye kikao kijacho cha bunge, 27 August 2013 napendekeza kumlipisha mwananchi wa kawaida 1000/= kwa mwezi SI SAHIHI. Jamani ,ni kweli tozo za magari bandarini zimepanda na husikii mwananchi yeyote akilalamika kwa sababu hawaguswi sana LAKINI hili la laini za simu, CHONDE! CHONDE! Lifutwe la sivyo mwataka sema siku hizi kuwa na simu ni anasa kama pombe,sigara,magari? SIMU ni sawa na MAJI yaani uhai ,USIPOYANYWA basi UTAYAOGA! Inasikitisha sanaaaa...!
Kwenye kikao kijacho cha bunge, 27 August 2013 napendekeza kumlipisha mwananchi wa kawaida 1000/= kwa mwezi SI SAHIHI. Jamani ,ni kweli tozo za magari bandarini zimepanda na husikii mwananchi yeyote akilalamika kwa sababu hawaguswi sana LAKINI hili la laini za simu, CHONDE! CHONDE! Lifutwe la sivyo mwataka sema siku hizi kuwa na simu ni anasa kama pombe,sigara,magari? SIMU ni sawa na MAJI yaani uhai ,USIPOYANYWA basi UTAYAOGA! Inasikitisha sanaaaa...!
Swali kwenu waheshimiwa wote (Wabunge,Mawaziri,n.k). Ni kweli mlipitisha maazimio ya kuwatwisha mzigo wapiga kura wenu kwa tozo hizo la simcards, 1000/=? Je mkirudi kwenye kampeni 2015 mtawashawishi vipi wapiga kura wenu ili wawachague tena mkawakandamize na hiyo mizigo mizito mnayowatwisha? Nawaonea huruma, kwani wengine watapiga magoti na kutoa machozi bure! Au ndo ule usemi,"ALIYENACHO AONGEZEWE na ASIYENACHO ANYANG'ANYWE KIDOGO ALICHONACHO? Jamani muwe na huruma kwa Watanzania wenzenu na mkumbuke mlikotoka!
Mimi nafikiri tuisiishie kuwapa wawekezaji migodi tu,bali hata nafasi ya Rais na Waziri mkuu tutafute wawekezaji maana hawa hawatufai kabisa.
Heri utawaliwe na mende lakini sio hawa jamaa magamba. Mafuta ya taa walipandisha ili magari yao yasiharibike ila sisi tusio na magari tuumia tu maana sisi tuna vibatari. Yaani walalahoi tuko wengi kuliko magari yao lakini sisi hata tufe ni bora kuliko magari yao.Leo hii tena laini za simu du. Ee Mungu ikiwezekana kikombe hiki(CCM) kituepuke si kwa mapenzi yetu bali kwa mapenzi yako. Tumeichoka hii serikali na iende tu kuzimu maana haistahili kwenda peponi.
Nimeisoma bajeti yote na sijaona kodi hii. Nilichoona ni ongezeko la asilimia 2.5 kwenye kodi ya simu za mkononi badala ya airtime kama ilivyokuwa.
Sasa hii 2.5% inahusianaje na shs 1000?- kwa mwezi?
Inaumiza, imasikitisha na inakera.Kungekuwa na jinsi ningekimbia nchi..Wafanyabishara wanaingiza mabilion, hawakatwi kodi ama kodi inayopatikana wanagawana na maafisa wa TRA na kudanganya mapato yao halafu wanakuja kuwaumiza wananchi wa kawaida. HAPANA HAPANA. I SAY NO TO KODI YA SIM CARD NA NO TO O.25% DUTY ON MONEY TRANSFER..NO NO NO
Post a Comment