Katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe
21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza
la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.
Narudia tena kuwashukuru vijana
na wadau tulioshirikiana kuandaa muswada huo na naomba kuendelea kupata
ushirikiano wenu wa karibu katika hatua zinazoendelea.
Kuanzia tarehe 21 Oktoba 2014
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeanza vikao vya kupokea maoni
ya wadau kuhusu muswada huo. Nakala tete ya muswada huo inapatikana hapa,
tafadhali pakua pitia na wasilisha maoni yako sasa.
Unaweza kuandika maoni yako
kwenye mtandao wa http://mnyika.blogspot.com
au kutuma kwa barua pepe kwenda mbungeubungo@gmail.com
na nakala kwa Kamati husika ya Bunge kupitia tanzparl@parliament.go.tz.
Ikiwa unataka kutumia njia
nyingine kuwasilisha maoni yako tafadhali wasiliana na Gaston Garubimbi 0715/0767-825025
kwa maelezo zaidi. Mdau wa masuala ya vijana zingatia kwamba zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha
mchakato wa kuanzishwa kwa baraza la
Vijana la Taifa zimekuwa zikitolewa bila utekelezaji kamili na wa haraka.
Baraza la Vijana la Taifa
pamoja na malengo mengine litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa mpaka
taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa kike na wa kiume kwa
ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Aidha, Baraza hilo litafuatilia
pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana kwenye
Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa
maendeleo.
Pia, Baraza la Vijana
litafuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha
kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana
kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Kwa upande wangu nitashukuru
ikiwa nitapokea maoni hayo kabla ya tarehe 28 Oktoba 2014, niweze kuyachambua
na kutoa mrejesho mapema kuwezesha muswada kusomwa kwa mara ya pili Bungeni
katika Mkutano wa 16 uliopangwa kuanza tarehe 3 Novemba 2014.
Kwa mujibu wa Hansard tarehe 21
Disemba 2013 baada ya Muswada kusomwa kwa mara ya kwanza, Spika wa Bunge Anna
Makinda alisema yafuatayo Bungeni “…muswada binafsi…. sasa utaanza kuwepo
kwenye website ya Bunge na utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya
kujadiliwa na utapelekwa kwenye kamati zitakazohusika wakati muafaka”.
Majibu yanapaswa kutolewa na
mamlaka husika ni kwanini toka wakati huo haukuwahi kuwekwa kwenye Tovuti ya
Bunge pamoja na kukumbushwa. Hata hivyo nashukuru kuwa hatimaye sasa muswada
huo umepelekwa kwenye Kamati, hivyo ni wakati muafaka kwa vijana na wadau wote
kupata nakala ya muswada huo hapa na kutoa maoni ya kuboresha ili Baraza la
Vijana la Taifa liweze kuundwa.
Kujadiliwa kwa muswada huo ni
hatua ya pekee katika historia ya harakati za vijana nchini kwa kuzingatia kuwa
Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba
kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala
hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.
Hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa
kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa kwa wakati pamoja
na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini. Hivyo
pakua nakala pekua toa maoni; boresha muswada tupate baraza bora.
John Mnyika (Mb)
23 Oktoba 2014
No comments:
Post a Comment