Itakumbukwa kwamba tarehe 29 Aprili 2014 kupitia Hotuba ya Msemaji wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini (nimeambatisha
nakala) juu ya mapitio ya utekelezaji wa
Bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara
tajwa kwa mwaka 2014/2015 nilieleza ufisadi na udhaifu uliopo katika Wizara
hiyo na mashirika yaliyo chini yake.
Kutokana na kukithiri kwa ufisadi na udhaifu huo nilipendekeza hatua
zifuatazo ziweze kuchukuliwa katika Mkutano wa 15 wa Bunge uliokuwa ukiendelea
wakati huo, nanukuu:
“Mosi, Spika aruhusu kabla ya mjadala
huu kuendelea ziwekwe mezani nakala ya ripoti zote za kamati za uchunguzi
kwenye Sekta ya Nishati na Madini zilizoundwa na matokeo yake kutowasilishwa
bungeni mpaka sasa.
Pili, Wizara ya
Nishati na Madini itakiwe kabla ya mjadala huu kuwasilisha kabrasha la majibu
ya michango ya wabunge juu ya makadirio ya mwaka 2013/2014.
Tatu, mara baada
ya hoja hii kuamuliwa naeleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka
kuundwe kamati teule ya kuchunguza masuala tete na tata tuliyoyaeleza katika
maoni haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Nne, Waziri Mkuu
kwa mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba ya Nchi
atakiwe katika mkutano huu wa Bunge kuelekeza Serikali iwasilishe Taarifa
Bungeni juu ya maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi uliofanyika kwa nyakati
mbalimbali juu ya masuala yanayogusa sekta za nishati na madini kama
tulivyoyaeleza.”, Mwisho wa kunukuu.
Hata hivyo, katika majumuisho ya mjadala huo hatua hizo hazikuchuliwa na
badala yake Waziri wa Nishati Prof. Sospeter Muhongo akaendelea kusema uongo
Bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda akapindisha maelezo niliyoyawasilisha
Bungeni na Spika Anna Makinda akaikinga Serikali dhidi ya usimamizi wa kibunge.
Matokeo yake ni kuwa ufisadi na udhaifu huo katika Wizara ya Nishati na Madini
na mashirika yaliyo chini yake umeendelea kulindwa mpaka hivi sasa.
Hivyo, kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito
kwa Waziri Muhongo, Waziri Mkuu Pinda na Spika Makinda kujitokeza mbele ya umma
na kueleza hatua ambazo wamechukua juu ya ufisadi na udhaifu toka kumalizika
kwa Mkutano wa 15 wa Bunge mpaka wakati huu.
Aidha, iwapo hawatafanya hivyo ndani ya siku tatu kuanzia tarehe ya
kutolewa kwa mwito huu nitaurejesha mjadala juu ya ufisadi na udhaifu huo
katika Wizara ya Nishati na Madini katika Mkutano wa 16 wa Bunge unaotarajiwa
kuanza tarehe 3 Novemba 2014 ili kuisimamia Serikali na kuchangia katika
uwajibikaji kwa maslahi ya nchi.
Wenu katika
uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
27 Oktoba 2014.
No comments:
Post a Comment