Tafadhali tazama mwisho wa ujumbe huu, usome tuhuma na malalamiko ya Wanafunzi wa Tanzania walioko nchini Russia kuhusu Ubalozi wa Tanzania nchini humo, Bodi ya Mikopo na serikali kwa ujumla. Tuhuma na malalamiko hayo yamewasilishwa kwetu Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) na Rais wa .Umoja wa Wanafunzi wa Kitanzania(Patrice Lumumba University, Moscow), Bwana Boniphace Kanyathare.
Naomba muyachambue na kuchapa kama habari au makala ili umma wa watanzania uweze kufahamu malalamiko yao. BAVICHA tutafanya ufuatiliaji wa malalamiko hayo na kutoa tamko la kina siku chache zijazo.
Lakini, katika habari za kesho; pamoja na uchambuzi wa malalamiko hayo, mnaweza kuninukuu ifuatavyo:
TAARIFA KWA UMMA
· Naitaka bodi ya Mikopo hapa nchini ieleze wazi kwa umma fedha ambazo imeshapeleka mpaka sasa na fedha ambazo iliwajibika kuzipeleka ikiwemo kutaja majina ya wanafunzi waliostahili kupokea fedha hizo. Na ifanye utaratibu wa kupeleka fedha zilizobaki haraka iwezekanavyo ili kuokoa hatma ya vijana hawa.
· Nalaani vitendo vya unyanyasaji na uvunjaji wa haki za binadamu waliofanyiwa vijana hawa nchini Urusi vikihamasishwa, kushuhudiwa na kushabikiwa na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Urusi. Tunamtaka Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Jaka Mwambi atoe kauli ya haraka kueleza kadhia hiyo. Bwana Mwambi yuko nchini Urusi kwa gharama za kodi ya watanzania wote bila kujali itikadi kwa lengo la kutumikia umma na kuwakilisha maslahi ya watanzania nchini humo. Tulitarajia awe balozi mzuri wa kuhakikisha vijana hawa wanasikilizwa na kusaidiwa baadala ya kunyanyaswa. Tunamtaka Balozi afungue mara moja ukumbi wa majadiliano na vijana hao ili kulipatia ufumbuzi wa haraka suala lao. Serikali ichukue hatua za kinadhamu kwa maofisa watakaobainika kusababisha hali hii.
· Kwa kuwa vitendo kama hivi vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara(rejea tatizo la wanafunzi wa kitanzania waliokwama nchini Ukraine); ni wazi kwamba kuna tatizo la kimfumo ambao serikali ya CCM imeshindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu. Pia pamekuwepo na tuhuma za ufisadi katika mchakato wa malipo ya wanafunzi wa kitanzania wanaosoma nje ya nchi. Kuna haja ya wadau kuunganisha nguvu katika kulitafakari na kulipatia ufumbuzi tatizo la kuchelewa ama kupunjwa kwa malipo ya watanzania wanaosoma nje ya nchi. Aidha tunaitaka serikali ieleze kwa umma marekebisho yaliyofanyika toka ahadi za Rais Kikwete na viongozi wenzake wa serikali walizozitoa kuhusu kuboresha mfumo wa kupeleka vijana watanzania nje ya nchi kwa ajili ya masomo.
· Aidha serikali iliwahi kutoa tamko la kutaka kupunguza idadi ya watanzania wanaopelekwa kusoma nje ya nchi; wakati serikali imetoa tamko hilo, bado na ndani ya nchi mfumo wa elimu ya juu nao umekuwa ukiathiriwa na migomo na migogoro ya mara kwa mara inayosababishwa na sera mbovu ya ubebaji wa gharama za elimu ya juu(cost bearing). Serikali imekuwa ikiwaghilibu raia wake kuwa sera hii ni ya uchangiaji(cost sharing) wakati ambapo wanafunzi wamekuwa wakipewa mikopo ambayo wanajibika kuilipa baada ya masomo yao; lakini kibaya zaidi wanashindwa kupatika mikopo hiyo kwa asilimia mia moja na hivyo wengine kushindwa kumudu gharama za elimu ya juu. Wakati fedha za taifa letu zikiwa zinafujwa kupitia matumizi ya anasa ya serikali na ufisadi wa mabilioni unaofanywa kwenye kodi za wananchi; ni aibu kwa serikali hiyo hiyo kushindwa kugharamia elimu, ni aibu zaidi kwa serikali kushindwa hata kukopesha wanafunzi wa asilimia mia moja.
Tunataka watanzania waelewe kwamba taifa linahitaji mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu yetu. Kama kungekuwa na sera bora na mfumo mzuri wa kugharamia elimu ya watanzania, vijana watanzania wangeweza kusoma popote pale iwe ndani ya nchi au nje ya nchi bila kulazimika kufanya maandamano na migomo ya mara kwa mara yenye kuathiti hatma ya elimu yao. CHADEMA kikiwa ni chama mbadala kiko tayari kuwaongoza watanzania kufikia hatma hiyo.
Imetolewa 16 Novemba, 2008:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa
Na Kaimu Mkurugenzi Masuala ya Kimataifa
0754694553
MATATIZO YALIYOPEREKEA VIJANA WAKITANZANIA WANAOSOMA CHUOKIKUU CHA URAFIKI (PATRICE LUMUMBA-MOSCOW-RUSSIA) KUANDAMANA KWA SIKU YA TATUMFULULIZO NJE YA UBALOZI WA TANZANIA MOSCOW
Ndugu zangu watanzania, leo kwa mara nyingine nimeamua kuwaelezea kiundani matatizo yanayotukabili watoto wenu tulioletwa na serikali yetu ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kusoma mjini Moscow Russia,matatizo haya yameperekea baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo yao,na wengine kushindwa kukamilisha taratibu za awali ili waweze kuanza masomo.
Matatizo yetu yamegawanyika katika makundi yafuatayo
a).Wanafunzi wafuatao mpakasasa hawajaletewa fedha zao za kujikimu pamoja na ada .
1. BROWN ELIAS LEKULE – mwaka wa tatu
2. BONIPHACE ELPHACE KANYATHARE – mwaka wa tatu
3. ALLY MOHAMED LUSESA – mwaka wa pili
4. JACKSON JACKOB TEMU – mwaka wa kwanza
5. MUHAYA SAMWELI CHITIMBO – mwaka wa kwanza
6. KINANASY R. SEIF – mwaka wa kwanza
7. MARIA F. MAJIJI – mwaka wa pili
8. IS-HACK S. IS-HAK – mwaka wa kwanza
9. NICHOLAUS MBILINYI – mwaka wa kwanza
10. ANDULILE FRANCIS MWAIGWISA – mwaka wa kwanza
11. ANDREW MASHAMBA – mwaka wa tatu
12. MICHAEL MBASHA – mwaka wa pili
13. ABDALLAH MOHAMED OTHMAN ELNOFELY – mwaka wa kwanza
Wanafunzi hawa baadhi wapo kozi ya tatu na baadhi wapo kozi ya kwanza, wenzao wote wamepata fedha, wamezipata mwezi wa tisa mwishoni na wengine mwezi wa kumi mwishoni kwa maandamano,fedha walizozipata wanafunzi wa mwaka wa kwanza zilikuwa na mapungufu mengi sana kwani kwa hesabu za kawaida naomba uangalie mfano huu.
Kwa wanafunzi wanaosoma kozi ya “international relationship” wanapaswa kupatiwa fedha zifuatazo kwa mwaka
Tuition fees-4800 us.dollors
Health insurance-250 us.dollors
Meals and accommodation-5400 us dollors
Total amount -10450 us dollors
Kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma kozi hiyo ya “international relation” wametumiwa fedha zifuatazo
1.FATUMA RASHID MOHAMMED-9843 US dollars
2.ISAACK ALOIS ISANZU-7713 US dolars
Ikumbukwe kuwa hawa wanafunzi wote wanasoma kozi moja na wapo darasa moja , lakini wameletewa fedha pungufu na pia ni kiwango tofauti kwa kila mmoja. Mimi kama rais wa watanzania wanaosoma chuoni hapa, niliomba mchanganuo wa fedha hizo kutoka ubalozini lakini maafisa wa ubalozi wakasema hawajaletewa kutoka bodi, tulipo wasiliana moja kwa moja na bodi wakasema wametuma ubalozini , na jitihada hizo za kuupata mchanganuo huo mpaka sasa zimegonga mwamba. Kutokana na hali hii, kuna baadhi ya wanafunzi waliopata fedha ambao mpaka sasa wameshindwa kulipa ada kufuatia ukweli kwamba fedha walizotumiwa ni pungufu. Wanafunzi wapatao 80 wakiwemo mwaka wa kwanza, wa pili na watatu wanakumbwa na tatizo hilo.
B . Mnamo tarehe 29.10.2008 wanafunzi wapya kutoka Tanzania wapatao 28 waliwasili chuoni kutoka Tanzania na ilipofika tarehe 05.11.2008 kundi lapili la wanafunzi wapya kutoka Tanzania wapatao 34 nao waliwasili kutoka Tanzania, wanafunzi wa kundi la kwanza (28) na lapili (34), waliambiwa fedha zao tayari watazikuta urusi (ubalozini), lakini baada ya kufika uongozi wa wanafunzi uliwasiliana na uongozi wa ubalozi ili kujua mustakabali wa fedha zao lakini tulijibiwa kuwa hakukuwa na fedha zao mpaka wenzao waliobaki nyumbani ambao hawajapata barua za mwaliko watakapofika hapa Urusi ndipo fedha zao kwa pamoja zitatumwa ubalozini . Kulingana na taratibu za uhamiaji hapa Urusi, suala hili linaweza kuchukua mwezi mmoja ujao.
Baada ya uongozi kupata majibu hayo tuliamua kuwafahamisha vijana na baada ya vijana kutoridhika na majibu hayo walichagua wawakilishi walioandamana na baadhi ya viongozi kwenda ubalozini ili wapate maelekezo zaidi,
Siku ya tarehe 13.11.2008 ujumbe huo ulienda ubalozini ili kujua mustakabali wa fedha zao walipofika ubalozini, afisa mmoja wa ubalozi, akaamua kupigasimu kwa Mkurugegenzi wa Wizara ya Elimu , Prof Shao, vijana wakiwa wanasikiliza kupitia loud speaker ya simu ya Afisa huyo (Dismas Kajogoo), ndipo waliposhangazwa na maneno ya mkurugenzi wa wizara ya elimu kwa kusema kuwa hautambui ujio wa wanafunzi hao wala hajui kama wapo huku Urusi. Vijana walisikitishwa sana na kauli za afisa huyo wa serikali. Baada ya hapo akawaambia kuwa wafungue accounts ndipo fedha zao ziweze kutumwa , huo ulikuwa uamuzi wa kushangaza ,kwani ikumbukwe kuwa ili mwanafunzi mpya hapa Urusi aweze kufungua account katika benki yoyote ile urusi, ni lazima awe amesajiliwa nchini urusi (amekamilisha taratibu za kiuhamiaji) . Kutokana na ukweli kuwa vijana hawa toka wafike urusi wanamuda usiozidi wiki tatu,na hawajafanyiwa usajili huo kwani ili waweze kusajiliwa ni lazima wafanyiwe uchunguzi wa afya ambao unachukua wikimbili na nusu, baada ya hapo kuna gharama ambazo wanapaswa kulipia ili waweze kukamilisha usajili , na baada ya kukamilisha mambo hayo, usajili hupatikana baada ya mwezi mmoja na nusu au zaidi. Kutokana na mlolongo huo wa usajili nilioufafanua, ni dhahili kwamba zoezi la kufungua accounts linahitaji muda usiopungua miezi mitatu. Hii inamaanisha kwamba vijana hao wakae bila fedha kwa kipindi chote hicho(miezi mitatu na kuendelea). Ikumbukwe kuwa, vijana hao hawana fedha za kujikimu, fedha za mabweni, fedha za medical insurance, na fedha za ada. Pia, ni ukweli kwamba vijana wengi wametoka familia za kimaskini kama yangu na hawakuja na fedha zozote.
Baada ya uongozi wa ubalozi kuona vijana hao hawaridhishwi na majibu hayo ukaahidi kuwakopesha kila mmoja kiasi cha dola za kimarekani 150. Lakini kwa hali halisi fedha hizo ni ndogo sana hapa urusi na haziwezi kukidhi matatizo yao, kwani mwanafunzi mmoja ili aweze kukidhi mahitaji niliyoyataja, anatakiwa apewe dola za kimarekani 5400 kwa mwaka kwa ajili ya kujikimu tu. Wawakilishi hao waliamua kuwarudishia wenzao taarifa, ili waamue cha kufanya kwa pamoja.
Siku hiyo baada ya vijana kumaliza kikao chao ,mimi kama rais wa wanafunzi ambaye pia sijapata fedha za mkopo wangu toka Bodi, nilikwenda ubalozini pamoja na ujumbe wa vijana 13 (wa mwaka wa kwanza wa pili na watatu)ambao pia hawajapata fedha ili kujua mustakabali wa fedha zetu. Kama ilivyokawaida ya ubalozi, tulizuiliwa kuingia ili kuongea na viongozi wa ubalozi , tulikaa nje kwenye baridi kuanzia saa sita mchana mpaka saa kumi na moja jioni ndipo mimi rais nikaruhusiwa kuingia ubalozini, peke yangu na wanafunzi wenzangu wakaendelea kupigwa na baridi kali nje ya ubalozi wanchi yetu tuipendayo, mpaka saa tatu usiku hali zao zilipokuwa mbaya ndipo wakaamua kuondoka, nilipo fika ndani bahati nzuri kiongozi mmoja aliyeingia na vijana wale alibaki ndani na alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi ambao hawajapata fedha, hivyo tukawa waathirika wawili ,tukajaribu kuzungumza na uongozi wa ubalozi kutaka kujua watatusaidia vipi ili tuweze kuendelea na masomo yetu kwa manufaa ya taifa letu,lakini majibu tuliyopewa na viongozi hao wa ubalozi yalikuwa ya kukatisha tamaa na kusisitiza kuwa wao hawahusiki na matatizo yetu na wakasema tunawabebesha mzigo wasiostahili kwani eti wao siyo serikali. Maneno haya yalitolewa na Afisa wa ubalozi bwana Dismas Kajogoo ambaye alizidi kusisitiza bila uoga kwamba, “Serikali ni kikwete na aliounda nao baraza la mawaziri”. Ndugu zangu nguvu ziliniishia na nikashindwa kujua , taifa letu linaelekea wapi? Naje tutaishi vipi ughaibuni bila kuwa na fedha za kujikimu achilia mbali za kulipia ada ya shule pamoja na mabweni? Ikumbukwe kuwa miezi miwili na nusu imeshapita tangu tulipopaswa kupata fedha na mpaka sasa maishayetu yamekuwa ya kusuasua. Baada ya kutathmini pamoja na kiongozi mwenzangu ndipo tulipo amua kukaa ubalozini na kuomba kukutana na balozi ili kujaribu kumsihi afikirie namna ya kuweza kuwasaidia wanafunzi wote wenye matatizo ya fedha lakini ombi letu lilipuuzwa na wakatuacha kwenye chumba cha mkutano ubalozini bila kutusikiliza. kutokana na ukweli kuwa hatukuwa na namna nyingine ya kuweza kuishi tuliamua kulala kwenye viti ubalozini kwa nidhamu ya hali yajuu kwa taifa letu bila kumsumbua mtu yeyote, mpaka asubuhi ya tarehe 14.11.2008 bila kula chochote, ilipofika asubuhi wanafunzi wenzetu walipopata taarifa kuwa mimi rais wao na kiongozi mwingine tulilala ubalozini wanafunzi wapatao 90 ambao hawajapata fedha zao wakiwemo wale wapya wakaandamana wote kuja ubalozini ili waweze waweze kujua hatima ya fedha zao.Mimi pamoja na kiongozi mwenzangu, tuliendelea kukaa ndani ya ubalozi kwenye ukumbi wa mikutano mpaka saa saba mchana, huku wenzetu 90 wakiwa wanapigwa na baridi nje bila kufunguliwa mlango. Mimi na mwenzangu kule ndani tulishangaa kuona maaskari wapatao 11 wakiingia ndani tulikokuwa na kuanza ghafla kutukaba kama majambazi au wahalifu na kutuburuza huku wakituchania nguo zetu na kutukanyagia simu zetu za mikononi mbele ya watumishi wa ubalozi akiwemo Balozi Jaka Mwambi, mpaka nje ya ubalozi ambapo wengine walibaki wakitulinda na wengine wakarudi ndani ya ubalozi , baada ya muda mfupi walitoka na kutukamata tena na kutuingiza ndani ya gari kwa nguvu huku wakituelekezea bunduki kama majambazi mpaka kituoni ,tukaingizwa kwenye selo na kufungiwa kwa muda wa masaa matano bila kuhojiwa., Wakati tupo ndani ya selo wenzetu waliobaki pale nje ubalozini walianza kufanya jitihada za kuwashawishi maaskari watuachie lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda. Baadae mkuu wa kituo alikuja na kupokea maelezo kutoka kwetu ndani ya selo na akasema suala hilo la sisi kukamatwa ndani ya ubalozi wetu lilifanyika kimakosa. Mkuu huyo wa kituo cha polisi alitutaka radhi na akaendelea kufafanua kwamba, maaskari wake waliokuwa lindoni ubalozini siku hiyo walipokea agizo la maandishi lililotiwa sahihi na Afisa wa ubalozi bwana Dismas Kajogoo, akiagiza askari hao watukamate na kututoa ndani ya ubalozi wetu. Baada ya hapo, tuliachiwa huru na majeraha yetu tuliyoyapata wakati askari hao walipotukaba ubalozi.
Mpaka naandika maelezo haya bado wanafunzi wapatao 100 tunaendelea na maandamano mpaka tutakapo pata fedha zetu na balozi Jaka mwambi ametutumia taarifa kuwa kuanzia sasa hawashughuliki na maswala ya wanafunzi mpaka uongozi wa wanafunzi ubadilishwe, na wawekwe watu ambao hawawezi kudai haki zao wala kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya serikali yetu na serikali ya urusi mfano.
1) 1. MKATABA HUO UNASEMA KWA KILA WANAFUNZI WAWILI WANAOSOMESHWA NA SERIKALI YA TANZANIA, SERIKALI YA URUSI(CHUO) HUTOA NAFASI KWA MTU WA TATU KUSOMA BURE. LAKINI KWA WANAFUNZI WALIOFIKA HAPA CHUONI MWAKA 2007/2008 AMBAO WALIKUWA 78 NA BAADAYE KUBAKI 76 NI WANAFUNZI 17 TU NDIO WALIOPEWA NAFASI HIZO. HII NI KINYUME NA MKATABA HUO KWANI WALIOSTAHILI KUPATA UDHAMINI WA CHUO NI 24. KATIKA KUFUATILIA SWALA HILO UONGOZI WA WANAFUNZI ULIGUNDUA KUWA KATIBU WA UBALOZI BWANA MBAROUK N. MBAROUK KWA KUSHIRIKIANA NA AFISA MMOJA WA CHUO WANATUMIA NAFASI HIZO ZA WALALA HOI KWA MANUFAA YAO. HII INAMAANISHA KUWA, MWAKA ULIOPITA NAFASI 7 HAZIJULIKANI ZIMEKWENDA WAPI. UONGOZI WA WANAFUNZI UMEJARIBU KUFUATILIA SUALA HILI LAKINI MIMI BINAFSI KAMA RAIS WA UMOJA WETU PAMOJA NA MAKAMU KATIBU TULIKUMBANA NA VITISHO VYA KUFUKUZWA CHUO KUTOKA KWA AFISA WA CHUO (MRUSI) ANAYESHUGHULIKIA SUALA HILO, SUALA HILI NI VYEMA SERIKALI YETU IKALICHUNGUZA UPYA NA KWA MAKINI KWANI KUNA KILA DALILI ZA UFISADI. MAAFISA HAO WA UBALOZI HAWANA UCHUNGU NA NCHI YETU KWANI KUPATIKANA KWA NAFASI HIZO KUNGEPUNGUZA MALIPO YA FEDHA ZA ADA KWA WATU HAO, NA FEDHA HIZO ZINGEWEZA KUTUMIKA KUWASOMESHA WATOTO WA MASKINI AMBAO KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE WAMEKOSA NAFASI ZA KUSOMA.
2) PILI UMEZUKA MTINDO CHUONI WA KUWALAZIMISHA WANAFUNZI KUSOMA LUGHA KWA MUDA WA MIAKA MIWILI KINYUME NA MKATABA UNAOSEMA WAZI KWAMBA MWANAFUNZI ANAPASWA KUSOMA LUGHA KWA MWAKA MMOJA TU. BILA SABABU ZA MSINGI. NA KATIKA HILI KUNA MKONO WA MOJA KWA MOJA WA KATIBU WA UBALOZI BWANA MBAROUK N. MBAROUK . AFISA HUYO HUFAIDIKA NA UVUNJWAJI WA MKATABA HUO KWANI, MWANAFUNZI ANAPOSOMA LUGHA KWA MIAKA MIWILI, HULIPIWA ADA NUSU KWA ULE MWAKA WA KWANZA WA LUGHA. IKUMBUKWE KUWA KILA MWAKA SERIKALI HUTUMA ADA YA MWAKA MZIMA KWA KILA MWANAFUZI, HIVYO NI DHAHIRI KWAMBA NUSU YA ADA INAYOBAKI HUMNUFAISHA AFISA HUYO WA UBALOZI. TUNAOMBA SERIKALI IFANYE UCHUNGUZI WA KINA KWANI DOCUMENTS ZA USHAHIDI WA MALIPO HAYO TUNAZO, NA MOJA YA NYARAKA HIZO TUMEAMBATANISHA NA TAARIFA HII. MAJINA YALIYOWEKEWA TIKI NI YA WANAFUNZI WALIOLAZIMISHWA KUSOMA LUGHA KWA MIAKA MIWILI NA KULIPIWA ADA NUSU MWAKA. HUU NI UBADHILIFU WA HALI YA JUU KWA FEDHA ZA WANAFUNZI NA NI UDANGANYIFU KWA TAIFA. MIMI KAMA RAIS WA UMOJA WETU WA WANAFUNZI SITA RUHUSU LITOKEE KWANI NINAIPENDA NCHI YANGU NA NINAWAPENDA WANAFUNZI WENZANGU NA HILI SUALA LA KUSOMA LUGHA MIAKA MIWILI INABIDI LIISHE ,ILI MAFISADI WASIPATE MWANYA ,KWANI SISI TULIOKUJA 2005 KUNA BAADHI YA WANAFUNZI WALICHELEWA KUJA KWANI WALIFIKA URUSI JANUARI BADALA YA SEPTEMBER NA WALISOMA LUGHA KWA MUDA WA MIEZI MITANO BADALA YA MIEZI KUMI BILA KURUDIA MWAKA NA KWA SASA WAPO KOZI YA TATU. KUWALAZIMISHA WANAFUNZI KUSOMA LUGHA KWA MIAKA MIWILI ILI UBALOZI UNUFAIKE NA FEDHA ZA ADA,NI MPANGO MCHAFU UNAORUDISHA NYUMA MAENDELEO YA TAIFA ILI KUWAFAIDISHA WACHACHE.
NDUGU ZANGU WATANZANIA PAMOJA NA YOTE AMBAYO VIONGOZI WA UBALOZI WAMEFANYA ILI KUWEZA KUFICHA MAOVU HAYO MPAKA SASA WAMESHINDWA, NA KWASASA LENGOLAO WANAWATUMIA BAADHI YA WANAFUNZI WENZETU KWA KUWAPA RUSHWA ILI KUWEZA KUTUONDOA KWENYE UONGOZI , PAMOJA NA VITISHO MBALIMBALI KUTOKA CHUONI ILI TUSISIMAMIE HAKI ZETU, LAKINI HATURUDI NYUMA TUNAAMINI KWA DHATI KUWA TANZANIA INAHITAJI MABADILIKO NA MABADILIKO TUTAYALETA WENYEWE VIJANA HIVYO NAOMBA NITUMIE NAFASI HII KUWAOMBA VIJANA WENZANGU ,TUSIMAME IMARA ILI TUWEZE KUIOKOA NCHI YETU HUUNDIO WAKATI WETU.
BAADHI YETU WANASHINDWA KUSIMAMIA UKWELI KWA KUOGOPA KUWA FAMILIA WANAZOTOKA NI MASKINI , NAOMBA NIWAHAKIKISHIE KUWA FAMILIA ZETU MASKINI TUTAWEZA KUZIKOMBOA KWA KUSIMAMA IMARA NA KUTETEA KILE KILICHO CHEMA MBELE ZA MUNGU, NA SIYO VINGINEVYO , SINTORUDINYUMA NA UKWELI LAZIMA UFAHAMIKE ILI HAKI IWEZE KUTENDEKA MIMI KAMA RAIS WA UMOJA WA WANAFUNZI WA KITANZANIA KATIKA CHUOKIKUU CHA PATRICE LUMUMBA MOSCOW, NAOMBA KWAPAMOJA TUUKEMEE UBADHILIFU ILI TAIFA LETU LIWEZE KUSIMAMA IMARA.
TUNAENDELEA NA MGOMO WA AMANI MPAKA MATATIZO YETU YATAKAPO PATA SULUHISHO,KWANI KWA NJIA YA MAZUNGUMZO TUMEJARIBU LAKINI KILA MARA TUMEKUWA TUKIFUNGIWA NJE YA UBALOZI KWENYE BARIDI KALI BILA KURUHUSIWA KUZUNGUMZA NAO.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
BONIPHACE ELPHACE KANYATHARE
RAIS WA UMOJA WA WANAFUNZI WA KITANZANIA
(PATRICE-LUMUMBA UNIVERSITY). MOSCOW.RUSSIA