Rais Kikwete: mene mene na tekel; taifa linagawanyika
Ni saa sita na ushee usiku. Siku mpya imeanza, ni Novemba Mosi; ni siku ya vijana Afrika. Najaribu kutafakari maudhui ya siku hii ya pekee kwa vijana Afrika kama ilivyopitishwa na umoja wa Afrika. Natafakari ujumbe wa mwaka huu “Maadili chanya ya kiafrika, amani na mshikamano”. Tafakari yangu inanirudisha nyuma katika hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa umoja wa Afrika aliyoitoa usiku wa Oktoba 31 mwaka 2008. Mwangi wa maneno ya Rais wa nchi yangu unarindima katika kichwa changu na kunikosesha usingizi. Si kwa uzito wa maneno bali kwa hofu yangu juu ya madhara ya wepesi wa maneno yenyewe kwa mwelekeo wa taifa.
Nagutuka; nagundua natafakari ubatili, najihisi kama afukuzaye upepo. Haraka nachukua moja ya vitabu vitakatifu, najaribu kutafuta maneno ya kupoza hisia zinazoniandama. Napekua pekua bila kujua nini hasa natafuta kusoma, nakutana na kisa cha Mfalme Nebukadneza. Napata shauku ya kurudia kisa chake nilichokikariri nilipokuwa mtoto, nakutana na maneno ‘mene mene na tekel’. Najikumbusha maana yake; ‘ufalme wake umepimwa na umeonekana haufai’!
Natabasamu kwa uchungu. Ni kama nimeona kidole kikiandika maandishi hayo katika ukuta wa taifa letu. Naukumbuka mjadala ulioibuliwa na Katibu wa Itikadi wa CCM, John Chiligati, ambaye pia ni Waziri katika serikali ya Rais Kikwete wa kubeza na kutweza wenye kuhoji uwezo wa Rais Kikwete. Nakumbuka kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwamba nchi imekwama Rais Kikwete ameelemewa. Nakumbuka maneno ya Mbowe akitangaza kwamba Rais Kikwete ameshindwa kuliongoza taifa na hivyo kuna haja ya watanzania kutompa kura yeye na chama chake katika uchaguzi wa mwaka 2010. Nakumbuka maneno ya Waziri Mkuu na Jaji mstaafu Joseph Warioba kwamba nchi si shwari. Mene mene na tekel!
Napata nguvu ya kuamka na kuandika; Rais Kikwete amenidhihirishia mimi niliye mdogo, ambaye sistahili hata kufungua kidamu za viatu vyake kwamba anaipeleka nchi harijojo. Katiba ya nchi yetu inatamka kwamba kila mtu anastahili heshima lakini katika medani ya uongozi; heshima ya mtawala inalindwa kwa maneno na matendo yake. Namheshimu Rais Kikwete lakini maneno na matendo yake, yanastahili kukosolewa. Hakika hotuba ya Rais wetu imenidhihirishia pia kuwa hata wale washauri na wasaidizi wake waliopo pale Ikulu na serikalini wanapaswa kutuambia watanzania kwanini kodi zetu zitumike kuendelea kuwalipa mishahara kama wanashindwa kutimiza wajibu wa kulinda heshima ya taasisi ya Urais. Nakabiliwa na mtanziko bado, kati ya kuandika vile ninavyoamini na kuonekana kwamba sinaheshima kwa Amiri Jeshi mkuu. Ama kusema ukweli, nikiamini kwamba Rais aliye kioo cha taifa letu atachukua hatua za haraka kujirekebisha na kurekebisha hali ya mambo inavyokwenda katika taifa letu. Rais Kikwete aliwahi kusema kwamba alikuwa mwanafunzi mzuri wa Mwalimu Nyerere; hivyo naamini amesoma waraka wake wa ‘tujisahihishe’. Kutenda kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
Kadiri hotuba ya Rais ilivyokuwa ikicheleweshwa ndipo matumaini yalipozidi kwamba pengine kulikuwa na mambo mazito ambayo mkuu wa nchi alikuwa akiyaandaa. Shauku ya kukosa hotuba za Rais kwa mwezi wa Septemba tofauti ya utaratibu ambao Rais amejiwekea ikazimwa kwa hotuba ambayo kimaudhui inafafana na hotuba ambayo tayari Rais alishaitoa Bungeni mwezi Agosti na kauli zake zilizofuatia katika ziara zake. Nikajiuliza; yamfaa nini mwanadamu kusema kama hana cha kusema?.
Rais wangu alionekana kuelemewa na mambo moyoni, haiba yake imegubikwa na uchovu pengine kutokana na ziara nyingi ama ni msongo wa mawazo au ni tatizo la macho yangu la kuona yasiyopaswa kuonekana. Rais alikuwa akihutubia kwa kutazama huko na kule kama vile palikuwa na nguvu za giza pembeni zikimzinga asitoe mwanga kwa taifa letu analoliongoza. Wanasaikolojia wanajua, jinsi ujumbe unavyotolewa unaweza kusema mengi kuliko hata ujumbe wenyewe.
Rais akaanza kwa kugusa suala tete la Tanzania kujiunga na OIC. Moja kwa moja akawaasa watanzania wasiuendeleze mjadala huo. Mjadala ambao umeendelezwa na serikali yake yenyewe, mjadala ambao yeye mwenyewe katika hotuba yake ameweka bayana kwamba serikali inauendeleza. Nikashangaa! Lakini nikashangaa zaidi kwa Rais Kikwete kutofautina wazi wazi na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Benard Membe ambaye Rais Kikwete amemuita kuwa ndio ana dhamana ya suala hilo. Wakati Rais anasema kwamba utafiti wa suala hilo bado haujakamilishwa na Waziri Membe, waziri mwenyewe wakati anahutubia bunge Agosti 22 mwaka huu huu alitangaza kwamba wizara yake imeshakamilisha utafiti. Nani mkweli kati yao Mungu ndio ajuaye. Lakini Mwalimu Nyerere, katika kitabu cha Uongozi wetu na hatma ya Tanzania, alizungumza vizuri kuhusu serikali. Mwalimu aliweka wazi, mkusanyiko wa mawaziri wasiokuwa na dira ya pamoja na uwajibikaji wa pamoja, wanabaki kuwa serikali kwa mujibu wa sheria tu. Lakini kimaadili na kimantiki; hakuna serikali! Rais anataka kila mtu akae kimya aiachie Wizara imalize kazi yake, kama vile wizara ni chombo kisikokuwepo Tanzania kisichowajibika kufanya kazi kwa kuzingatia hisia na matakwa ya watanzania. Kwa mtindo huu wa funika kombe, Rais Kikwete anazidi kuligawa taifa chini kwa chini; ni kama kujaribu kufunika moshi na kujifariji kuwa hakuna moto.
Liliamshwa la mpasuko Zanzibar; likajadiliwa, likakwamishwa. Liliibuliwa na mahakama ya kadhi; likakolezwa, likafunikwa. Likaibuliwa la mafisadi; likavumishwa, likatulizwa. Limeibuka la OIC; likachochewa, limefutikwa. Uongozi wa kuahirisha matatizo badala ya kuyatatua! Haya na mengine ni mabomu ya wakati.
Zoezi la kutumia visingizio kuahirisha matatizo likaendelea katika suala la walimu pia. Nilitaraji walau kwa mara hii Rais awaombe radhi walimu kwa ahadi yake aliyoitoa awali ambayo haikutimizwa katika tarehe ambayo aliitaja mwenyewe. Kwa kuwa sakata hili liko mahakamani; niishie hapa, nivute subira. Walimu waendelee tu kusota kwa sababu ya udhaifu wa serikali wa kutoweka kumbukumbu vizuri za waliofariki na zile za kutambua stahiki za kila Mwalimu. Serikali isiyoweza kuwatambua wafanyakazi wake inaweza kweli kuwakumbuka wananchi wa kawaida?
Ndipo Rais alipohamia kwenye changamoto ya hali ya uchumi ya dunia na hasa wa mfumo wa fedha unaozikabili nchi zilizoendelea. Kilichonishangaza ni Rais kutumia muda mrefu kuhutubia yale yale ambayo aliyasema kwa taifa Katika hotuba yake ya Tanga wakati wa sherehe za kuzima Mwenge na maadhimisho ya miaka tisa ya kifo cha, hayati Mwalimu Julius Nyerere. Halafu Rais katika kutafuta suluhisho la suala hilo, hoja kuu aliyoitoa ni kukaribisha wazo la Rais George Bush wa Marekani la kuitisha mkutano maalum wa kimataifa wa kuzungumzia tatizo la kifedha la kimataifa!. Utegemezi wa mawazo toka Washington ndio unaotufanya tusahau kulinda mihimili ya kiuchumi ambayo awamu zilizopita za utawala wa nchi yetu zilijaribu kuiweka. Kubwa zaidi, nilitarajia Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuwaeleza watanzania ni jinsi gani anakusudia kuziunganisha nchi zingine za Afrika kuhakisha nafasi ya Afrika inahakikishwa. Badala yake Rais Kikwete ameishia kulalamika tu kwamba “kwa bahati mbaya afrika imesahaulika katika mkutano huo”. Rais Kikwete walau angetumia nafasi hiyo kueleza mikakati ya bara la Afrika hususani ile ya kuunganisha jumuia mbalimbali za kiuchumi iliyojadiliwa nchini Uganda ambapo yeye alishiriki kama sehemu ya ujenzi wa nguvu ya kiuchumi ya bara letu. Uthabiti na ueledi kama huo ungekuwa ni zawadi nzuri kwa vijana wa Tanzania wakati wanaungana na wenzao kuadhimisha siku ya vijana Afrika.
Kama ilivyotarajiwa na wengi Rais Kikwete akagusia suala la mauji ya Maalbino, ikiwa ni siku chache toka alizungumze suala hilo kwa kina Oktoba 19, 2008. Mara hii Rais akiwataka wananchi watoe kwa siri taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo hivyo. Binafsi nilitarajia badala ya kutaka orodha mpya, Rais Kikwete kama alitaka kuzungumzia tena suala hili, angeueleza umma wa watanzania orodha za mwanzo za watuhumiwa wa mauaji ya maalbino ambazo ziliwasilishwa kwa vyombo vya dola ikiwemo kwa kufuatilia mtandao ulioanikwa na mwandishi wa habari wa BBC, Vicky Ntetema. Lakini haya mambo ya Rais Kikwete kutaka orodha za siri hayakuanza leo, aliwahi kutaka orodha ya watuhumiwa wa biashara ya madawa ya kulevya, akapatiwa; kimyaaa. Zikafuata orodha nyingine mbalimbali; hakuna hatua zinazoeleweka. Ndipo ikafuata ile orodha ambayo kwa ushujaa wa Dr Wilbroad Slaa(Mb) na viongozi wenzake wa upinzani waliamua kuitoa orodha hiyo hadharani kabisa pale Uwanja wa Temeke Mwembe Yanga. Orodha ya Mafisadi(list of shame) ikawekwa hadharani; hasara ya ufisadi uliotajwa inasababisha vifo vya watanzania wengi zaidi kila siku mpaka leo.
Kama kila siku wakina mama wajawazito wanakufa kwa kukosa huduma bora za kujifungua. Kama kila siku watanzania masikini wanakufa kwa kushindwa kuweza kununua dawa za kutibu malaria. Kama helikopta mbovu zinanunuliwa na kuua. Kama watoto wanakufa kwenye kumbi za disco kwa kukoseshwa hewa. Basi mafisadi ni sawa wauaji! Taifa linazidi kugawanyika, kati ya tabaka lenye kufa taratibu kwa kunyonywa kwa ufisadi na tabaka lililojifungia kwenye pepo ya akaunti za vijisenti mpaka nje ya nchi.
Rais Kikwete akaendelea kuikwepa Orodha ya Mafisadi kwa ukamilifu wake, akaendelea kuzungumzia suala la EPA tu. Akaendelea kukwepa kusema chochote kuhusu Meremeta, Tangold, Deep Green na ufisadi mwingine ambao kwa ujumla wake ni mara kumi ya bilioni 133 za EPA.
Lakini hata kwenye EPA kwenyewe, Rais Kikwete katika hotuba yake ameendelea kukwepa kuchukua uamuzi; amepalilia mche wa mbegu ya ubaguzi katika utawala wa sheria ambayo aliipanda Agosti 21 mwaka 2008 kupitia hotuba yake bungeni.
Rais Kikwete ameendelea kuliganya taifa kwa kuwalinda mafisadi na kugeuza suala lao kuwa la madai badala ya jinai.
Katika hotuba yake Rais Kikwete anatoa pongezi kwa Kamati ya Mwanasheria Mkuu “kwa kazi nzuri iliyofanya ambayo mbali na kubaini namna ya tuhuma za uhalifu zilivyofanywa, pia ilibaini wahusika na kuwabana kiasi cha kufanikiwa kurejeshwa kwa fedha ambazo vinginevyo zingepotea kabisa. “
Kama Rais Kikwete mwenyewe anakiri kwa maneno yake mwenyewe kwamba kamati yake imebaini uhalifu na wahalifu sasa ni vipi Rais huyu huyu anawapa msamaha wahalifu kabla ya kufikishwa mahakamani? Anawapa msamaha huu kwa sheria ya nchi gani? Maana Katiba ya nchi na sheria ambazo Rais ameapa kuvilinda vinampa mamlaka chini ya utaratibu maalum wa kusamehe watu kwa sababu Fulani Fulani baada ya kushtakiwa na kuhukumiwa(clemance/parole). Hakika Rais Kikwete amekiuka katiba kwa kuendesha nchi kwa ubaguzi na kuvunja sheria za nchi kwa kulinda wahalifu. Kwa mantiki hii, na vijana wezi nao wakirudisha mali za wizi nao waachiwe huru tu ili tujenge taifa la misamaha ili wajumuike na hao mafisadi walioghushi nyaraka na kuhujumu uchumi wa taifa. Milango ya magereza na ifunguliwe ili majambazi waachiwe huru, na milango ya mahakama ifungwe ili wezi wasishitakiwe tena; ili tujenge taifa lisilo na utawala wa sheria, linaoendeshwa kwa kanuni za mwituni. Mene mene na tekel!
Namsikiliza Rais wangu kwa mara nyingine akitaja kiwango cha fedha kilichorudishwa bila kuwa na hakika. Kwa mara nyingine akitoa maagizo ya kufungua mashtaka kwa watu ambao hawajarudisha fedha; maagizo ambayo aliyayatoa siku nyingi. Kwa yale makampuni mengine tisa yaliyofisadi bilioni 40 Rais ndio kwanza ‘anakusudia’ kuwataka polisi waendelee na uchunguzi. Na kati ya hayo ipo ile kampuni ya Kagoda Agricultural Limited iliyochota takribani bilioni 30 ambazo nyingine zimeelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa zilitumika kwenye kampeni za uchaguzi zilizomweka yeye na chama chake cha CCM madarakani. Rais Kikwete amekosa uthubutu na uthabiti wa kuwataja hadharani maswahiba wake na kuwachukulia hatua. Mene mene na tekel.
Rais Kikwete amemalizia hotuba yake kwa kutusihi watanzania tujiepushe na mambo yanayoweza kutugawa na kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu na badala yake tuimarishe maelewano, mshikamano na umoja wa kitaifa. Misingi ambayo yeye mwenyewe ameibomoa kwa maneno na matendo yake. Ukiona wananchi wanazomea viongozi, wanarusha mawe, wanalala barabarani ujue migawanyiko imeshapandikiza mbegu ya chuki na kukata tamaa. Vitabu vitakatifu vinaeleza kwamba amani ni tunda la haki. Maelewano tunayopaswa kuyaimarisha ni yale ya kutambua asili na matitizo yanayolikabili taifa letu na kuelewana suluhu tunayohitaji. Mshikamano tunapaswa kuuimarisha ni wa kuunganisha nguvu ya umma katika kuleta mabadiliko tunayoyahitaji. Umoja wa kuimarisha ni unaojengwa kwa misingi ya uadilifu na fikra mbadala zenye kupinga aina zote za ufisadi na kutetea rasilimali za taifa.
Daima tukumbuke; mabadiliko ya kweli katika taifa letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale kwa ari, nguvu na kasi mpya. Kwa falsafa ya chukua chako mapema(ccm), Tanzania yenye neema haiwezekani. Ni wakati wa kusimama na kujitambulisha; ama upande wa kuliunganisha taifa ama kuligawa, historia itakuhumu kwa kadiri ya maamuzi yako ya leo. Mene mene na tekel. Tuombe ulinzi wa Mungu tuvuke salama!
John Mnyika
Novemba Mosi, 2008-Mwanza, Tanzania
No comments:
Post a Comment