Sunday, November 9, 2008

Taifa lenye utamaduni wa ufisadi

Leo niwapatie mchango wangu nilioutoa hapa kwenye mjadala unaoendelea kuhusu ufisadi: http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/20024-ccm-yafanya-maamuzi-mazito-kamati-kuu-22.html#post319258

"Muda mrefu sijachangia JF, ile hii post imenigusa sana.Maudhui yake yamehitimisha kile ambacho nimewahi kukisema na kukiandikia mara kadhaa kwamba nchi yetu imeingia katika 'utamaduni wa ufisadi'. Ambapo ile dhana ya kila 'mbuzi anakula kwa urefu wa kamba yake'(ongezea mahali pake)- soma 'kazini kwake', imekuwa ni jambo la kawaida katika maisha ya watanzania.Hili ndio tatizo na msingi ambalo kama taifa tunapaswa kulishughulikia kurejesha MAADILI na UWAJIBIKAJI.Wazee wetu wanatuambia enzi za miaka ya awali ya Mwalimu ufisadi hakuwa umeshika kazi na kupenya katika mishipa ya wananchi na viongozi kama ilivyo sasa.Swali la kujiuliza- ni kwa vipi tumefika hapa? Na tunarudi vipi katika misingi iliyokuwepo awali?Wengine wanasema ni kwa sababu ya mabadiliko ya kiuchumi kuelekea uchumi wa soko ambao wengine wanajenga hoja kuwa unaambatana na ubinafsi na kutaka kujilimbikizia. Wao wanaamini kwamba ujamaa ungekuwa suluhu ya kuendelea kuwa na maadili.Wengine waamini kuporomoka kwa uchumi kulikoleta hali ngumu ya maisha na hatimaye mishahara kushuka ukilinganisha na gharama za maisha kumepunguzia wananchi uwezo wa kununua na hatimaye sasa wafanyakazi wengine kugeuka wala rushwa mahali pao na watoa rushwa kwa wengine. Hawa wanajaribu kuelezea rushwa ndogo ndogo(petty corruption). Ukiwauliza ni kwa vipi matajiri wakubwa na viongozi wakuu wa serikali wenye mishahara mizuri na maslahi mazuri nao wanapokea na kutoa rushwa kubwa kubwa(grand corruption), wanakosa majibu mazuri.Katika kukubiliana na rushwa, wapo waomini kwamba tukiweka sheria kali na kujenga taasisi zenye nguvu, rushwa itaondoka. Lakini wanasahau kwamba sheria zinapaswa kusimamiwa na watu, taasisi nazo zinasimamiwa na watu. Kama ukiwa na taifa lenye utamaduni wa ufisadi, sheria hata ziwe nzuri haziwezi kusimamiwa(rejea kauli ya rais kwamba watakaorudisha fedha za EPA watasamehewa- nimeijadili kidogo hapa: JJ: Rais Kikwete: mene mene na tekel; taifa linagawanyika ); mnakumbuka pia mfano(rejea hapa:TAKURU inalinda na kutetea Rushwa? ) wa Taasisi ya TAKUKURU(wakati huo TAKURU) ilivyoisafisha RICHMOND na mchakato wake.Wengine wanasema basi tuanzie kwa kuweka viongozi waadilifu, halafu wao kwa maneno na matendo yao watasimamia utawala wa sheria na uwajibikaji wa taasisi hizo. Lakini uchaguzi kwenye taifa lenye utamaduni wa ufisadi mara nyingi huzaa viongozi mafisadi. Wananchi mafisadi huchagua viongozi mafisadi.Kwa hiyo hili suala la ufisadi, ni kama hadithi ya kuku na yai- ni mjadala unaozunguka kusema kwamba kipi kilianza.Kwa maoni yangu, sababu zote kila moja kwa nafasi yake inachangia katika utamaduni wa ufisadi. Ujamaa wa dola(naita ujamaa wa dola kwa kuwa nina mtazamo tofauti sana kuhusu uzuri na udhaifu wa ujamaa mfululizo wa uchambuzi wangu kuhusu hoja hii upo hapa: Tanzania, CHADEMA, CCM na mjadala wa falsafa na itikadi; Lipi ni jibu? ) ,ulizaa urasimu wa bidhaa na huduma ambao ulichangia katika baadhi ya wananchi kuanza kuweka pemebeni misingi ya maadili na uwajibikaji na kujiingiza katika utamaduni wa ufisadi. Viongozi waliochaguliwa baadaye walikuja tu kuchochea utamaduni wa ufisadi ambao tayari ilishaanza. Utadamuni ambao ulijengwa pia kwa raia kuweka mawazo yao yote kwa dola na serikali. Kushuka kwa hali ya maisha na kupungua kwa uwezo wa kununua kulikoambana na mishahara duni kuliongeza tu huu utamadauni wa ufisadi. Halafu ndipo tukaingia katika mduara ya ufisadi(the cycle of corruption); kwamba chama tawala na vingozi wake wanalinda ufisadi, wananchi nao wanazidi kuwa mafisadi katika mahali pao pa kazi na uchaguzi ukija mafisadi wengi zaidi wanachaguliwa; mzunguko unaoendelea. Sasa changamoto ni kuvunja huu mduara.Kwa bahati njema, si raia wote ni mafisadi. Si viongozi wote ni mafisadi. Bado kuna tabaka la watu wachache ambao si mafisadi. Hatua za haraka zinahitajika kuchukuliwa na tabaka hilo kuliokoa taifa. Uzoefu unaonyesha kwamba utamaduni wa ufisadi huwa ukikomaa una kawaida ya ama kuangusha dola au kuazaa taifa lenye matabaka kati ya walionacho na wasionacho na lenye vurugu za kijamii. Tunapaswa tusifike huko kama taifa.Kama ambavyo takaba la watu wachache liliamini kwamba mkoloni anaweza kutoka katikati ya tabaka la waliowengi waliomini kama mkoloni hawezi kushindika na kwamba kutawaliwa ni jambo la kawada na kwamba waafrika wameumbwa kutawaliwa; ndivyo inavyopasa kuwa kwenye suala hili la ufisadi.Suluhisho ni kurudi kwa umma. Hao waadilifu wachache kwenda kwa wananchi kutoa elimu ya uraia, wananchi wakaunga mkono kwamba ufisadi wao ndio kaburi lao; kwamba ufisadi wa watawala ni jeneza tu la kuwabeba na kuwazika. Kwamba ufisadi unawaathiri zaidi wao wenyewe. Wananchi wakaelewa uhusiano kati ya maisha yao kuwa mabaya, huduma za kijamii kuwa mbovu na ufisadi. Wananchi wakajua kwamba ufisadi ni dhambi si ya kuliathiri taifa tu bali kujiathiri mtu mwenyewe. Hapo ndio wananchi watachukua hatua kwa nguvu ya umma. Tararibu tutajenga taifa lenye utamaduni wa maadili ambao mimi huwa napenda kuuita utamaduni wa uwajibikaji. (Niliwahi kugusia kidogo hii dhana hapa: 45th Anniversary: My greetings to you and reflections with Mwalimu Nyerere). Katika taifa la namna hiyo, viongozi wanamachaguo matatu; ama kukubaliana na sauti ya umma na wao kuanza kusimamia uwajibikaji(Rais Kikwete kuunda kamati ya bomani na Bunge kuunda Kamati ya Richmond ni matokeo ya umma kuanza kuchukua hatua baada ya Hoja ya Zitto kuhusu Buzwagi na hoja ya Dr Slaa kuhusu BOT. Kupelekwa kwa kesi za EPA ni matokeo ya yaliyojiri baada ya Kutajwa kwa Orodha ya Mafisadi); ama watawala kunyamaza(na wakati mwingine kugeuka madikteta) na kuruhusu kuzuka kwa utamaduni wa hukumu ya ujmma(mob justice) ambao unaweza kuwa na faida katika usalama wa taifa ama unaweza kutishia utangamano wa umma(unaweza kuwa na mifano ya hivi karibuni) ama wananchi kuvuta subira na kusubiri kuchukua hatua wakati wa chaguzi(kuondoa madarakani utawala na watawala waolinda ufisadi).Lakini hatua hii inapaswa kwenda sambamba na umma kutaka hatua zichukuliwe ili kuboresha pia maeneo mengine mathalani suala la mishahara na usimamizi wa taasisi za uwajibikaji.Hii ni njia ya amani kuelekea maadili na uwajibikaji. Njia nyingine ni kikundi cha watu wachache kujitwalia madaraka ama kwa sanduku la kura lakini mara nyingi kwa mapinduzi na kujivika dhima ya kulitoa taifa kutoka katika utamaduni wa ufisadi na kuelekea katika maadili na uwajibikaji. Hawa huitwa madikteta wakarimu!(mifano imewahi kutokea katiika mataifa mengine). Hawa huweka adhabu kali dhidi ya aina zote za ufisadi na huzisimamia adhabu hizo na hatimaye kujenga hofu katika taifa kwa mafisadi na hiyo watu kuacha ufisadi si kwa kuelewa au kwa kupenda; bali kwa hofu! Tatizo la msingi la njia hiyo ni kuwa linaanzia kwenye njia yenyewe na hivyo baada ya muda fulani watawala hao hao wenyewe hugeuka kuwa mafisadi kwa kujilimbikizia kutokana na mamlaka makubwa wanayokuwa nayo ama huishia kukataa kutoka madarakani na hatimaye kuzua tena utadamuni wa ufisadi.Hivyo, nawapongeza Dr Slaa na Zitto kwa njia mliyoamua kuipitia. Mabadiliko huanzia kwa mtu mwenyewe, naamini kwa kukataa kwako umemuambukiza huyo mzee utamaduni wa uadilifu na uwajibikaji. Majaribu ni mengi lakini hakuna sababu ya kukata tamaa. Uovu hushamiri wema unapokata tamaa.Lakini tukumbuke pia rushwa kubwa kubwa katika mataifa ya Afrika inachangiwa pia na mataifa ya nje hususani kupitia makampuni makubwa(MNC). Nilikuwa napitia sheria za nchi mbalimbali, mataifa mengi yanakataza ndani ya nchi zao mashirika yao kutoa chochote kupata zabuni lakini mataifa hayo hayo yametunga sheria ambazo zinaruhusu mataifa yao kuwahonga viongozi wa kifrika katika kupata zabuni. Hivyo uhusiano wa kimataifa umejengwa katika misingi ya utadamuni wa ufisadi uliojificha katika vivuli vya commission nk.Jambo moja lazima tuamue, kama tunataka maendeleo ya taifa letu-hatuna jinsi zaidi ya kuendeleza utamaduni wa uwajibikaji. Ambapo kila mtu atawajibika kwa nafasi yake na atakayeshindwa kuwajibika atawajibishwa. Umaskini wetu umechangia katika ufisadi, lakini umaskini wetu sio chanzo kikuu cha ufisadi huu. Hivyo, lazima tufikiri zaidi na kuendelea kuchukua hatua.BTW 1: Thread inahusu Kamati Kuu ya CCM, mod aidha badilisheni heading au hii michango kuhusu ufisadi ianzishwe thread yake.BTW 2: Zitto, mpe hongera Chachage Jr.BTW 3: Unaweza kuwa ulishawahi kuwa fisadi, ama ulishawahi kuwa fisadi lakini kama kuna chochote kinaweza kukugusa katika mjadala huu, unaweza kuwa wakala wa mabadiliko unayotaka kuyaona. Kwenye kitabu kitakatifu kimojawapo kuna hadhithi ya Saul ambaye alikuwa anachinja watu wa dini, baadaye akaongoka na kuwa Paulo mweneza dini.BTW 4: Kwa fisadi yoyote anayesoma hapa-aelewe kwamba ufisadi ni uuaji wa taifa na wananchi walio wengi. Ni ubatili, sawa na kufukuza upepo! Ni raha ya muda fulani na karaha ya muda mrefu.Nawakatika mjadala mwema mpaka panapo majaliwa"

No comments: