Sunday, December 6, 2009

Kauli zangu ziarani Ubungo

Jana Jumamosi tarehe 5 Disemba nimeanza ziara ya siku mbili katika Jimbo la Ubungo; kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Mkoa wa Kinondoni Kanda ya Dar es salaam. Nimefanya mikutano miwili ya hadhara. Mkutano wa kwanza nimeufanya katika Kata ya Ubungo kuanzia saa 10:30; jirani kabisa na kituo cha mabasi ya mikoani(Ubungo Bus Terminal).

Nikihutubia mkutano huu, niliwashukuru wananchi wa Dar es salaam waliotuunga mkono kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwapongeza kwa ushindi uliopatikana. Niliwaeleza kuwa mwaka 2004, CHADEMA ilishinda viti 2 tu katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Lakini mwaka huu wa 2009, pamoja na hujuma zote na uchaguzi kuwa ovyo ovyo; tumeweza kushinda viti 11 ambalo ni ongezeko la asilimia nyingi wakati vyama vingine idadi yao ya viti imeshuka.

Nikawaeleza hali hii inatia matumaini tunapoelekea uchaguzi wa mwaka 2010; na nikawaambia kwamba lazima Dar es salaam iwe kitovu cha mabadiliko nchini. Nikitumia nafasi yangu nyingine ya Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa nikawaeleza kwamba katika nchi nyingi za Afrika zilizofanya mageuzi chachu ya mabadiliko hayo huwa ni miji mikubwa kama Dar es salaam lakini inashangaza kwamba kwa upande nchi yetu hali ni tofauti.

Wakazi wa Dar es salaam wanafurahia hoja za wabunge wa upinzani kama wakina Dr Slaa ambao wamepatikana kwa kuchaguliwa majimbo ya vijijini, wakati ambapo majimbo yote saba ya Dar es salaam ni CCM. Hata kwenye udiwani; hakuna diwani hata mmoja mkoa mzima wa Dar es salaam kutoka upinzani. Hii ni aibu kwa taifa na ni matusi kwa wananchi ambao wanapata fursa ya kuwa karibu na vyombo vya habari na kwa sehemu kubwa ni watu waliopata fursa ya kwenda shule.

Hivyo ni muhimu wawezeshe harakati hizi za mabadiliko, na nikawatangazia kwamba siku hiyo tuanaanza kusambaza rasmi vipeperushi vya kuunga mkono CHADEMA kwa njia mbadala katika jimbo la Ubungo.

Nitawatangazia rasmi kwamba sasa wanaweza kujiunga ama kuchangia CHADEMA kwa kutuma neno CHADEMA kwenda namba 15710 kwa wateja wa Zain na Vodacom. Hii inafanya kwamba hata kama wametingwa na majukumu mengine bado wanaweza kabisa kufanya harakati za kisiasa kwa kutumia simu zao. Nikawatangazia pia kuwa kama wanataka kuwasiliana na CHADEMA jimbo la Ubungo watume ujumbe au wapige simu kwenda namba 0784222222.

Nikawaambia kwamba wakumbuke maneno tuliyowaambia mwaka 2005 kwamba mabadiliko ya kweli katika taifa letu; hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile; chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale kwa ari, nguvu na kasi mpya; na kwamba kwa falsafa ya chukua chako mapema(ccm) ya chama cha mafisadi(ccm) Tanzania yenye neema haiwezekani.

Nikawakumbusha kwamba mwaka 2005, wakati nagombea ubunge katika jimbo hilo, nilisimama katika eneo hilo hilo na kutangaza kwamba kuna ufisadi na upotevu wa mapato Mradi wa Kituo cha Mabasi Ubungo(UBT) ambao unafanywa na kampuni ya familia ya Kingunge na vigogo katika Halmashauri ya Kinondoni. Wakati huo, CCM wakiwemo baadhi ya vigogo hao walikanusha. Lakini sasa miaka michache baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amekwenda na kutaka ukaguzi maalum(Special Audit) ambayo imebaini mambo ambayo niliyashayasema mwaka 2005. Hata hivyo, kama kawaida ya CCM ya kulindana; Pinda mpaka sasa amekalia ripoti hiyo ya CAG. Amesubiri mkataba wa Kampuni ya familia ya Kingunge (Smart Holdings) umalizike badala ya kuvunja mkataba na kuwachukulia hatua za kisheria. Na kutokana na hayo, kampuni hiyo imehamishwa katika ulaji mwingine kwa kupewa katika mazingira tata tenda ya kukusanya mapato katika jesho la wamachinga(Machinga Complex). Hivyo, nikatoa mwito kwa Waziri Mkuu Pinda kuiweka hadharani mapema iwezekanavyo ripoti ya CAG kuhusu mradi wa UBT ili iweze kujadiliwa na umma tukiwemo wananchi wa ubungo ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa kampuni hiyo na wanafamilia hao ambao walikuwa wakidanganya kwamba mapato kwa siku ni milioni moja na ushee; wakati serikali imeanza tu kukusanya mapato imeweza kupata takribani milioni nne kwa siku. Pia, nikatoa mwito kwa wamachinga kupaza sauti kudai jingo lao kwani hata wao wanavikundi na vyama vyao ambavyo vinapaswa kuhusishwa kwenye ukasanyaji wa mapato.

Mkutano wa pili nimeufanya kata ya Kimara eneo la Kimara matangini ambapo pia nilianza kwa kuwashukuru wananchi wa kutuunga mkono katika uchaguzi wa mitaa ya kata hiyo. Niliwaeleza kwamba pamoja na hujuma walizofanyiwa ikiwemo makaratasi ya kupigia kura katika kata hiyo kuisha asubuhi, na mengine kuletwa jioni tena yakiwa yametolewa nakala(photocopy) kwenye maduka ya jirani hapo hapo Kimara kwa idadi isiyojulikana; bado upinzani uliokuwepo umeipa somo CCM na wenyeviti wake waliotangazwa kuwa wameshinda.

Niliwaleza kwamba mwaka 2004; wenyeviti hao walipita bila kupingwa lakini sasa wameshinda kwa ushindani mkali uliohusisha CCM kutoa wapiga kura maeneo mengine na kuwahamishia kupiga kura hapo Kimara kwa kutumia karatasi hizo zilizoongezwa. Nikawaeleza kwamba kutokana na hali hiyo, yapo maeneo ambayo tumefungua kesi kama Msewe, Baruti nk.

Nikawatangazia rasmi wenyeviti wa serikali za mitaa kwa tiketi ya CCM na viongozi wa chama chao kwamba wanapaswa kutekeleza wajibu wao ipasavyo wa kuwatumikia wananchi kwa kuwa tofauti na udiwani na ubunge ambapo kiongozi akichaguliwa amechaguliwa hakuna namna ya kumuondoa mpaka uchaguzi mwingine kwenye serikali za mitaa hali ni tofauti. Nikaweleza wananchi kwamba sheria inawaruhusu kupiga kura ya kutokuwa na imani na kuwaondoa kama watashinda kutekeleza wajibu ipasavyo ikiwemo kuitisha mikutano ya wananchi na kuwasomea taarifa za mapato na matumizi. Pia kama watashindwa kufuatilia kero za msingi za wananchi, mathalani katika Mtaa wa Golani kuna tatizo na daraja na kero kubwa ya maji. Kama viongozi hao watashindwa kushirikiana na wananchi kuondokana na kero hizo; CHADEMA tutashirikiana na wananchi kuchukua hatua zinazostahili kabla hata ya uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.

Nikawaeleza kwamba taifa letu kwa sasa linapita katika wakati mgumu kutokana na kukua kwa matabaka katika jamii. Nikawaeleza kwamba pamoja na kukua kwa tabaka kati ya masikini na matajiri tabaka baya zaidi ni lile la kukosekana kwa usawa katika utawala wa sheria na mifumo ya utolewaji wa haki. Mathalani watuhumiwa wa ufisadi tuliowataja kwenye orodha ya mafisadi, bado wengi wao wanatamba barabarani mpaka hivi sasa na kwa sehemu kubwa wakilindwa na vyombo vya usalama vinavyoendeshwa na kodi za watanzania; lakini kwa mwananchi mlipa kodi anayeishi Kimara hali yake ya usalama ni tete kutokana na majambazi kuruhusiwa kutamba mara kwa mara. Hivyo suluhisho ni kufanya mabadiliko ya kiuongozi na kisera ili kuunganisha nguvu ya umma kushughulikia masuala hayo. Nikawaeleza kwamba sera kuu ya CHADEMA ambayo tunaiita falsafa yetu ni Nguvu ya Umma ama people’s power. Chini ya Sera hii tunaamini kwamba rasilimali za watanzania iwe ni maliasili; kodi zetu ama vipaji vyetu vinapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi hivyo tunataka kujenga taifa lenye kutoa fursa.

Nikawaeleza changamoto iliyopo ni upotoshaji unaondelea wa kila kitu; hata ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka kuitwa kuwa unafanyika kwa maslahi ya Taifa. Nikatolea mfano kuwa baada ya ripoti ya UN kutolewa Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe alijitokeza na kuikana yote kwa ujumla wake kwa maelezo kwamba analinda maslahi ya Taifa. Waziri Membe katika hali hiyo, kama kweli angetaka kulinda kikamilifu maslahi ya taifa angetangaza kufanya uchunguzi juu ya watu waliotajwa ili kutetea taswira ya Tanzania kama nchi. Badala yake, kuikana ripoti nzima ni kufisha watu waliofanya vitendo haramu kwa kutumia kivuli cha maslahi ya taifa. Badala yake ni muhimu kwa serikali kuchukua hatua ikiwemo kuchunguza na kuchukua hatua; badala ya kubeza na kufunika hali ambayo inaweza kuiathiri zaidi nchi katika medani ya kimataifa. Ni kama ukiwa na mtaro wa uchafu, wakati mwingine unawajibika kuingia ukachafuka, ukausafisha na baadaye ukajisafisha. Tanzania itasafishwa kwa serikali kuingia katika mtaro kusafisha uchafu iliofanywa na watanzania wachache kwa maslahi yao binafsi; sio ya taifa ili nchi na watanzania wote kwa ujumla tuweze kusafishwa mbele ya jamii ya kiamataifa.

Leo nitakuwa na mikutano mingine Goba, Mbezi na Sinza ikiwa ni mwisho wa ziara ya awamu ya sasa.

No comments: