Tuesday, December 8, 2009

Miaka 48 ya Uhuru: Huu ni wakati wetu; tusidanganyike!

Wakati wetu ni huu, tunapoadhimisha miaka 48 ya uhuru. Ni wakati wa kutafakari taifa letu lilipotoka, lilipo na tunapotaka liende. Makala hii inakulenga zaidi wewe uliyezaliwa baada ya uhuru; tunaounda sehemu kubwa ya taifa hili. Ni kwa ajili pia ya watanzania wote wenye kuamini kwamba uhuru wa kweli, si uhuru wa bendera bali ni uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi. Uhuru wa kweli, ni uhuru wenye kuleta maendeleo kisiasa, kijamii na kiuchumi. Uhuru huu utapatikana kupitia mabadiliko ya kweli, yenye kuhimili misukosuko ya ukoloni mamboleo; na kujenga taifa lenye kutumia vizuri rasilimali katika kutoa fursa kwa raia wake.

Wakati wa uhuru taifa hili lilikuwa na watu chini ya milioni 10; sasa Dar es salaam pekee ina wananchi takribani milioni nne, karibu nusu ya Tanzania ya wakati huo ikiwa Tanganyika. Sasa taifa lina watu takribani milioni 40; hivyo taifa letu watu wake takribani robo tatu ni kizazi cha baada ya uhuru. Maanake katika kila watu kumi tunaopishana nao barabarani, saba ni kizazi cha baada ya uhuru. Hiki ni kizazi chetu, hili ni taifa letu. Huu ni wakati wetu, tusidanganyike kwamba wakati wetu bado.

Si nia yangu kuanzisha mgogoro kati ya kizazi kipya na kizazi cha zamani cha taifa hili; na wala si kusudio langu kusema kwamba hatuwahitaji wazee katika harakati za demokrasia na maendeleo. Kwani ni afadhali kuwa na kiongozi mzee mwenye maono na maadili kuliko kuwa na kiongozi kijana fisadi asiyekuwa na dira wala mwelekeo. Taifa hili ni la watanzania wote, wa rika zote, wa hali zote, kila mmoja ana umuhimu na nafasi yake kama kilivyo kila kiungo katika mwili wa binadamu. Dhamira yangu, ni kusema kwamba wakati huu ni wetu; tusidanganyike. Yoyote yule, ambaye anaukubali ukweli huu, awe ni kijana wa sasa ama kijana wa zamani, huyo tukubaliane nae.

CHADEMA inaukubali ukweli huo; tangu wakati wa kuanzishwa kwake. Vijana wa zamani katika CCM, walipoudumaza uzao wao kwa kuwaita vijana kuwa ni taifa la kesho, na Umoja wa Vijana wa chama hicho chini ya nidhamu ya uoga kukubaliana ukandamizaji huo. Utawala huo uliposhindwa kuhimili kuingia kwa mfumo wa vyama vingi kutokana na shinikizo la ndani na nje, vijana wa zamani wenye fikra mbadala na moyo wa ujana walioanzisha CHADEMA kama Wazee Edwin Mtei na Bob Makani wakaja na kauli mbiu mbadala kuwa: Vijana; Taifa la leo mnamo mwaka 1992. Baadaye kauli mbiu hii ilibadilika kuwa: Vijana; Nguvu ya Mabadiliko.

Kwa sasa serikali ya CCM na hata Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) wote wanamtafiri kijana kuwa ni binadamu mwenye umri usiozidi miaka 35(wakianzia miaka 12, 15, 16 au 18 kutegemea muktadha); ni takribani asilimia 40 ya watanzania. Watoto na vijana kwa ujumla wetu tunakaribia asilimia 70 kwa watu wote nchini. Sisi vijana peke yetu ni zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania. Ndio roho na injini za taifa letu. Huu ni wakati wetu, tusidanganyike.


Pamoja na kuwa harakakati za uhuru zilifanyika kona zote za nchi wakazi wa Dar es salaam, wanabeba historia ya harakati za uhuru wa taifa letu; ni wakati muafaka kutafakari masuala haya, mwaka huu ambapo kumbukumbu ya uhuru inafanyikia kitaifa katika mkoa huu. Harakakati za uhuru wakati huo ziliratibiwa kwa busara za wazee wenye imani kwa vijana kuwa vijana ni nguvu ya mabadiliko.

Ni wazee wa Dar es salaam ndio waliomuita Mwalimu Nyerere toka Pugu, kwa mchango wao wa hali na mali, kijana wao, akawa mwenyekiti wa taifa wa chama cha wakati huo cha TANU akiwa na miaka 32, akaongoza harakati za uhuru, mpaka nchi ikapata uhuru. Akiongoza nchi hii vizuri katika miaka ya kwanza ya uhuru, akiweka misingi ya muda mrefu ya taifa yenye kutazama mbele kwa miaka mingi kiuchumi, kisiasa na kijamii; misingi ambayo wazee wa leo wa CCM na vijana wao wameitupilia mbali baada ya kufa kwake.

Kosa moja la Nyerere lilikuwa ni kuweka mkazo sana kwa dola kwa maana ya serikali kumiliki njia za uzalishaji; badala ya uchumi kimilikiwa na umma. Kosa hili lilifanya serikali ishindwe kubeba mzigo mkubwa wa kusimamia sera kisiasa wakati huo huo kufanya utekelezaji kwa kuendesha njia za uzalishaji mali za kiuchumi wakati huo huo ikiwa inatoa huduma za kijamii. Kwa ujumla pamoja na kuimba haja ya kujitegemea, dola ikazalisha raia wategemezi kifikra, ambao chini ya mfumo wa chama kimoja na mwelekeo finyu wa kiuchumi; walipoteza ujasiri wote wa ushindani. Ni kosa hili, ndio lilifanya wakina Mtei kuanzisha CHADEMA yenye inayoamini katika mfumo wa soko la kijamii; lenye kuhakikisha kwamba uchumi unamilikiwa na wananchi. Huu ni mfumo wa kiuongozi wa kisera na kirasilimali ambao unahakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya maisha ya wananchi wake; kwa kujenga taifa lenye kutoa fursa. Mjadala huu wa dhima ya itikadi katika nadharia ya maendeleo nimewahi kuuandikia makala za kadhaa cha kiuchambuzi zinazopatikana kwenye tovuti: www.chadema.or.tz.

Lakini afadhali kosa la Nyerere linaweza kusameheka, lakini makosa ya warithi wake, baada ya kung’atuka kwake na baadaye kufa kwake yameacha majeraha makubwa yanayohitaji taifa hili likombolewe upya. Wakati wetu ndio huu; tusidanganyike.

CCM hiyo yenye kuongozwa kwa fikra za kifisadi na utupu wa kiitikadi, ikaondoa nchi katika ujamaa, ikaipeleka katika soko holela; sio soko huria. Chini ya sera zake na uongozi wake, njia za uzalishaji mali zikauzwa kwa bei chee; toka kwa dola kwenda kwa wageni, na kwa tabaka la wachache linalojifunika kwa kivuli cha mabepari uchwara wa ndani; wengi wao wakiwa kwenye korido za utawala wa CCM na serikali yake. Marehemu Profesa Chachage, aliwaita watu hawa, makuwadi wa soko huria- hawa kwa kweli, ni makuwadi wa kiuchumi (Economic Hitmens).

Wakahitimisha kwa maamuzi ya Zanzibar, ya kufuta misingi muhimu ya maadili ya uongozi mnamo mwaka 1991; kwa hiyo wakati CHADEMA inaanzishwa, waasisi wake walizitafakari hali hizi.

Halafu bado miaka 48 baada ya Uhuru; CCM wanaendelea kuwadanganya watanzania, na hata kushinikiza katiba ya nchi hii kuwa nchi hii inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea. Chama kinachotawala kinapoongoza huku kina ombwe na kiitikadi, kimefilisika kimaadili; lazima taifa litakuwa na uongozi dhaifu.

Na kwa kweli si maneno yangu kwamba CCM inawadanganya watanzania, ni maneno ya Mwasisi wa chama hicho, na mwandishi wa Azimio la Arusha ambaye kabla ya kufa kwake aliandika moja ya kitabu chenye sehemu ya wosia wake wa mwisho kwa taifa; Kitabu cha uongozi wetu na hatma ya Tanzania; Nyerere ameandika wazi, CCM inawadanganya wa Tanzania, namnukuu: “Halmashauri Kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi. Na walikuwa na haki ya kufanya hivyo, maana sera ni yao, ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya kwa hila na janja janja, na hadi sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM bado ni Ujamaa na Kujitegemea”

Kwa hiyo nchi hii iko rehani; kiuchumi, kijamii na hata kisiasa kama ambavyo nitaelezea katika mfululizo wa makala hizi za kumbukumbu ya miaka 48 ya Uhuru wa nchi yetu. Kiuchumi, tukashuhudia viwanda vikiuzwa kwa bei ya kutupa na vingine kugeuzwa magofu baada ya kuuzwa kwake. Hapa Dar es salaam, ambapo maadhimisho yanafanyika mwaka huu, ukienda Jimbo la Kawe, utaona yale mahame ya Tanganyika Packers, kile kilikuwa ni kiwanda cha kusindika nyama, kilichokuwa kikitoa ajira kwa vijana kwa watanzania. Kile kilikuwa kinawezesha bidhaa za wafugaji kusindikwa. Sasa, mpaka vijana wa kimasai nao wanakimbilia kwa wingi Dar es salaam kuwa wasusi na walinzi. Kiwanda hiki ni mfano wa viwanda vingi vilivyoingia hali hii inayochangia katika ukoloni wa kiuchumi; wa kutegemea kuwa bidhaa za nje na kutegemea kusafirisha bidhaa ghafi kwenda nje ya nchi. Pale Jimbo la Ubungo, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kinazidi kudidimia; nyumba za wafanyakazi ziliuzwa kinyemela kwa kivuli cha ubinafsishaji, mpaka mitambo mingine imeuzwa kama chuma chakavu; pamoja na wafanyakazi kulipwa mishahara duni hata maghorofa ya wafanyakazi yanaendeshwa kibiashara badala ya kuwa huduma ya msingi kwa wafanyakazi. Hii ni mifano tu, hali hii ni maeneo mengi ya taifa letu.

Miundombinu nayo imeachwa hohehahe, hali ya usafiri wa reli inazidi kuwa mbaya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia hii unazidi kupungua mwaka hadi mwaka; mathalani kutoka tani 1,169,000 mwaka 2005 mpaka tani 429,000 mwaka 2008. Serikali inazidi kuingiza fedha za walipa kodi katika uwekezaji wa kibadhirifu na kudhoofisha miundombinu iliyojengwa kwa jasho la umma. Hali ya viwanja vyetu vya ndege na shirika la umma la ndege (ATCL) ni ya kuliaibisha. Utawala wa CCM unaolinda, kila wakati unatuingiza katika kugharamia shirika hili kwa maamuzi mabovu katika vipindi tofauti tofauti. Serikali inayoongozwa na CCM imeshindwa kufanya upanuzi wa Bandari kubwa; badala yake wameingia mikataba mibovu ya upakuzi wa mizigo inayopelekea kupunguza hata kiasi cha shehena kinachohudumiwa katika bandari zetu. Wakati washindani wetu nchi za jirani, ambao wametoa fursa kwa vijana wenye kufiria na kuona mbali na kuunga mkono vyama vyenye sera mbadala; wanapanua bandari zao na kuwekeza katika miundombinu, sisi ambao tuko katika nafasi bora zaidi ya bandari zetu kupata soko kubwa la nchi za maziwa makuu tunabaki tumetahayari kutokana na sera legelege na uongozi mbovu chini ya CCM. Wakati wetu ni huu, tusidanganyike. Wakati wa kudai uhuru, ni vijana makuli wa pale bandarini ndio waliokuwa mstari wa mbele kwenye kudai uhuru; hawakuigopa serikali dhalimu ya kikoloni kwa kuwa hawakuwa na cha kupoteza kama wenye kazi za kola nyeupe(white collar) waliokuwa kwenye serikali ya mkoloni. Ndio maana huwa nafarijika kila ninapoona vijana wasio na ajira na watanzania wa kawaida kwa ujumla wakitaka mabadiliko ya kweli ili kupata uhuru wa kweli. Tabaka hili, halina cha kupoteza isipokuwa umasikini wao na malipo watakayopata ni kuishi kwenye taifa lenye kutoa fursa.

Serikali ya CCM inapita ikijivuna kuboresha miundombinu kwa kutumia takwimu za kuongezeka kwa idadi ya wanaotumia simu za mkononi; lakini hebu tuiangalie kwa undani hii sekta. Ukuaji wake umekuwa kwa nguvu ya sekta yenyewe kwa sababu za nje ya sera za serikali, hii imefanya mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa na hata kubadili kipato cha watanzania mmoja mmoja mwenye simu kuwa ni finyu. Tathmini ya serikali ya CCM yenyewe ya hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya nchi inaonyesha kwamba katika kila watanzania kumi (10) wenye simu, ni watanzania wawili(2) ndio wanatumia simu zao kwa matumizi binafsi na biashara; hivyo asilimia kubwa ya watanzania watumia simu kwa matumizi binafsi pekee na si biashara ama shughuli za uzalishaji. Kwa hiyo, tuitumie teknolojia hii hii kuleta ukombozi, ndio maana namuomba kila mwenye simu hapa ya mtandao wa Zain au Vodacom atume neno CHADEMA kwenda namba 15710 kama mchango wake katika kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa. Kwa wenye mitandao mingine huduma hii itafuata katika siku za usoni; huu ndio ubunifu wa kisiasa ndani ya chama kinachoongozwa na kizazi kipya.

Tumehadithiwa na wazee wetu, kwamba wakoloni walitutawala ili kupata nguvu kazi ya bei chee; kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyao na kupata masoko kwa ajili ya bidhaa zao. Tulipotafuta uhuru, ilikuwa ni dhamira yetu kuondoa udhalili huu. Miaka 48 baada ya uhuru, tujiulize; je hali hii imebadilika? Ukweli uko tofauti na kuondoa tabasamu lote la kusherehekea uhuru wetu. Mfumo mpya wa kikoloni ndani ya taifa lenye uhuru wa bendera; ndio unaofanya wafanyakazi kutoa nguvu kazi yao kwa bei chee kwa kulipwa mishahara midogo na kupata maslahi duni. Sasa utumwa huo unabisha hodi kwa wakulima, kupitia mikakati ya kilimo mipya inayoendelezwa hivi sasa yenye kupokonya ardhi kwa watanzania wa kawaida kwa kisingizio cha kupanua mashamba kumbe mwishowe watanzania watakuja kuwa manamba. Mgogoro wa ardhi huko Zimbabwe unapaswa kutufundisha somu kuwa kumiliki ardhi ndio ishara kuu zaidi ya uhuru wa mwananchi. Miaka 48 baada ya uhuru viwanda vyetu vinaendelea kufa huku tukilazimishwa kisera kujibidiisha kuwa watafutaji wa malighafi na kuzisafirisha kwenda viwanda vya nje zikiwa ghafi na hivyo kushindwa kuwa na uwiano wa kimalipo(Balance of Payment). Wakati tukiua viwanda vya ndani na kupunguza uzalishaji; tunafungua mipaka yetu kwa kiwango cha ajabu na kuingiza bidhaa za nje zikiwemo zisizokuwa na kiwango. Taratibu tunajenga uchumi wa kuwa wachuuzi wa bidhaa kutoka nje. Uhuru wetu uko wapi?

Lakini athari kubwa zaidi ya kiuchumi ni utegemezi ambao taifa letu limeingizwa kwa kutegemea misaada kutoka nje huku rasilimali za taifa zikifyozwa kibeberu. Ni ukoloni huu mpya ndio ambao unanifanya nitamke kwamba tunahitaji kudai uhuru wa Tanzania. Tunahitaji uhuru wa kweli. Wakati wetu ni huu, tusidanganyike. Mwanafalsafa Frantz Fanon, aliwahi kusema kwamba kila kizazi lazima, nje ya uvungu uvungu kiutambue utume wake; ama kiutumize au kiusaliti. Kizazi cha wakati huo, kilidai uhuru, na kujenga misingi ya taifa(national building) ingawa misingi hiyo imekuja kuvurugwa na kuturudisha kwenye ukoloni mambo leo(neo colonialism). Ni wajibu wa kizazi chetu; kudai uhuru wa kweli, uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi; hatuwezi kudai uhuru huo bila kumpiga vita adui ufisadi. Wajibu wa kizazi chetu ni kuweza kupambana katika mazingira ya ushindani wa ndani na nje ya nchi yetu; kujenga taifa tukitazama kizazi chetu na kijacho.

Kwa hiyo, mkazi wa kule Loliondo na majirani zake wanaoswagwa wao na mifugo yao, huku Waziri wa Serikali yake ya CCM akiwalinda raia wa nje, na hata kutochukua hatua pale ambapo hata mawasiliano ya simu katika eneo hilo yanasomeka kama vile eneo hilo na ni miliki ya nchi nyingine; anahitaji uhuru wa kweli. Huyo ni mfano tu, watanzania waliowengi; wanatoka maeneo mbalimbali ya nchi yenye rasilimali ambayo yameporwa; iwe ni maeneo ya migodi, maeneo ya uwindaji, maeneo ya uwekezaji katika kilimo cha mashamba makubwa. Sasa hii laana ya rasilimali (resource curse) kwangu mimi ni moja ya visababishi vya kuvunjika kwa amani nchini. Tunaelekea kwenda kuchimba mafuta na uranium; nchi hii iko mashakani kama hatutabidili sera. Wakati huu ni wetu, tusidanganyike. Mwenyezi Mungu ametujalia rasilimali, lakini tukiendelea kuacha uongozi mbovu madarakani; rasilimali hizi ni tishio kwa usalama wetu wenyewe. Hivyo, tusake mabadiliko ya kweli; tupate uhuru wa kweli.

Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje(CHADEMA) anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.or.tz na http://mnyika.blogspot.com

No comments: