MWISHO wa mwaka ni wakati wa kutafakari tulikotoka, tulipo na tunakotaka kwenda katika mwaka mpya. Ni kipindi muhimu kwa taasisi na hata watu binafsi kufanya tathmini na kujiwekea malengo. Kwa binadamu mmoja mmoja yanaweza kuwa ni malengo ya kiuchumi, kijamii na hata ya kisiasa.
Maamuzi ya masuala ya kiuchumi na kijamii mara nyingi ni masuala binafsi. Hata hivyo, malengo ya kisiasa hususan yale yanayohusu utumishi wa umma ni muhimu kwa maamuzi yake kufanyika kwa kuzingatia mwelekeo wa kiongozi husika lakini pia kwa kurejea utashi wa wananchi iwe ni faraghani au hadharani.
Hii ni kwa sababu uongozi wa umma wa kuchaguliwa hufanyika katika medani ya demokrasia ambayo inahusisha utawala wa watu kwa ajili ya watu.
Katika uchaguzi yapo mambo manne ya muhimu katika kuhakikisha ushindi. Mosi, ni mgombea: haiba, wasifu na uwezo wake kwa ujumla. Pili ni ajenda: ujumbe wenye dira unawagusa wapiga kura na kuamsha kuungwa mkono.
Tatu ni oganaizesheni: huu ni mtandao mzima wa kuratibu vuguvugu la ushindi, unaweza kuwa wa kijamii, kisiasa ama kitaasisi. Nne, rasilimali: hii ni kwa ajili ya kuwezesha kwa hali na mali kampeni husika, iwe ni fedha, zana, mawazo au nguvu kazi.
Baadhi ya watu hudhani kwamba rasilimali ni jambo la kwanza kuwezesha ushindi, uzoefu wa kimataifa unadhihirisha kuwa katika kufanikisha kampeni za uchaguzi kipaumbele cha kwanza ni mgombea, cha pili ujumbe, cha tatu ni oganaizesheni.
Rasilimali huongezeka kwa kadiri ya tija na ufanisi wa vipaumbele vitatu vinavyotangulia kwa nadra mtiririko huu unaweza kubadilika kutokana na upekee wa kimazingira ya kisiasa.
Tumebakiza siku chache kuingia mwaka 2010, kipindi kingine cha kuelekea uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais nchini. Tayari heka heka zimeshaanza na kauli mbalimbali zimeshaanza kutolewa za kheri na za shari.
Kwa kweli fikra kuhusu uchaguzi ujao zilishaanza toka 14 Desemba mwaka 2005 kwa wale wanaoamini kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine.
Binafsi nakumbuka mwaka huo wa 2005 wakati mjadala ukiendelea kuhusu utata wa matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Ubungo ambapo mimi nilikuwa mmoja wa wagombea tayari wadadisi wengine wameanza kuulizia masuala ya uchaguzi wa 2010.
Hali hii ilijitokeza hata katika mkutano wangu na wanahabari Desemba 22, 2005 kwa ajili ya kuwashukuru wapiga kura na kuelezea mafanikio yaliyopatikana, mapungufu yaliyojitokeza na hatua ambazo nilipanga kuzichukua.
Hata baada ya kutoa msimamo huo, bado mjadala uliendelea katika kipindi cha Januari mpaka Mei 2006; takribani nusu mwaka baada ya uchaguzi mkuu kumalizika. '
Hivyo, baadhi ya masuala hayo niliwajibika kuyajibu kupitia hotuba yangu ya kuwashukuru wananchi na kuelekeza mwelekeo niliyohutubua jimboni Ubungo Mei 28, 2006.
Ilinibidi niandike pia waraka kwa wananchi wa ubungo na watanzania Juni 4, 2006 wakati huo nikiwa ziarani nchini Marekani waraka ambao ulisambaa kwa umma kupitia vyombo vya habari na njia zingine za mawasiliano ya umma ikiwemo mikutano ya hadhara niliporejea. Waraka huo uliobeba ujumbe ‘kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi’ uliweza kutuliza kwa muda mjadala.
Katika waraka huo nilielezea masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa azma ya kufungua kesi namba moja ya mwaka 2006 katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Ubungo.
Kesi hiyo ambayo nilisimamiwa na Wakili Tundu Lissu ilipigwa danadana za kiufundi kipindi chote na kuishia hewani mwaka 2007 kwa kile kilichoelezwa na wakili wangu kuwa ni kukosekana kwa dhamira ya dhati ya kuisikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, miaka takriban mitatu iliyopita ya 2006, 2007, 2008 na hata mwaka huu wa nne unaomalizika wa 2009, swali ambalo nimekuwa nikiulizwa ni kugombea ubunge wa jimbo la Ubungo 2010.
Nimekuwa nikiulizwa swali hili katika mikutano ya hadhara ya kisiasa katika ziara ambazo tumekuwa tukizifanya katika kata zote za jimbo la Ubungo. Katika kipindi chote hicho swali hilo hilo limekuwa likiulizwa hata kwenye shughuli na matukio ya kijamii yawe ni ya kirafiki, kidini, misiba, harusi, michezo, miradi ya jumuiya, ufuatiliaji wa kero za wananchi nk.
Wakati wote majibu yangu yamekuwa kati ya haya matatu nitajibu wakati muafaka ama umma utajibu ama Mungu akipenda! Najua katika kipindi chote majibu haya yamekuwa yakiwaweka katika mkanyiko waulizaji kwa sababu mbalimbali.
Wapo wenye mtazamo kwamba majibu kama hayo ni ishara ya kutokuwa na uhakika ama kupima upepo. Wapo wenye imani kwamba kwenye uongozi wa kuchaguliwa sifa mojawapo ya uongozi ni kuutaka uongozi.
Wapo ambao katika kipindi hicho hicho wamekwenda mbele zaidi kuweka msimamo wao bayana kwamba ni lazima nigombee tamko la wazi la hivi karibuni likiwa ni la mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Makoka na wananchi wa eneo hilo la Novemba 29, 2009. Msimamo huo waliutoa kwenye mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi ambao walinialika kama mgeni rasmi.
Kilichonisukuma kuandika makala hii ni majadiliano yanayoendelea hivi sasa kwenye mtandao kupitia www.facebook.com/john.mnyika kuhusu ‘Ubunge Ubungo 2010: Nigombee Nisigombee?’
Wachangiaji wote waliotoa maoni yao mpaka sasa wamenitaka nigombee huku wakitoa sababu mbalimbali. Wapo waliotoa hoja ya kutambua uwezo, haja ya kubeba harakati za kizazi kipya kushiriki kwenye uongozi wa taifa letu, kufanya vizuri mwaka 2005 na kuhoji kuhusu mikakati ya kuhakikisha ushindi mwaka 2010.
Mchangiaji mmoja alirejea mfano wa Barack Obama ambaye alikuwa na mashaka kuhusu kugombea kwake lakini mmoja wa washauri wake wa karibu akamweleza kwamba ‘usipogombea umechagua kushindwa; lakini ukigombea una chaguo la kushinda ama kushindwa’. Walatini wana msemo ‘Sauti ya watu ni sauti ya Mungu’. Si lengo la makala haya kujadili hoja mbalimbali ambazo zimetolewa katika mjadala huo.
Naandika makala kuwezesha tafakari ya wengine ambao ni sehemu ya wapiga kura ama wananchi kwa ujumla hawana fursa ya kushiriki majadiliano kwenye tovuti.
Tafakari pana zaidi tunapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010; nini kinawasukuma wagombea kujitokeza kugombea: dhamira binafsi ama msukumo wa umma au vyote?
Mwaka 2005 wakati huo nikiwa na miaka 24 nilipojitokeza kugombea kwa mara ya kwanza nilieleza kwamba ilikuwa ni dhamira yangu binafsi baada ya kuona nina kipawa/kipaji cha uongozi.
Kusukumwa na dhamira ya ndani inaweza kuwa jambo la kawaida kwa mgombea ambaye utumishi wake bado haujaonekana kikamilifu mbele ya umma.
Lakini vipi kwa mgombea ambaye anafahamika tayari: nguvu alizonazo, udhaifu alionao, fursa alizonazo na vikwazo vinavyomkabili, naye asukumwe na dhamira binafsi pekee?
Kwa mgombea ambaye tayari anafahamika ni muhimu pamoja na dhamira yake binafsi pawe pia na msukumo wa umma hii ni kwa sababu nafasi za kuchaguliwa kama ubunge ni za kuwakilisha wananchi.
Ni muhimu sehemu ya wananchi iwe ni wanachama wa chama, wapiga kura ama baadhi ya watu katika jumuia waone haja hiyo.
Kuungwa mkono kwa namna hiyo katika dhamira ya kugombea na kuhusisha umma katika kufikia maamuzi nyeti kama hayo yanaweka msingi muhimu wa kuwa mwakilishi wa wananchi husika na hata kuwashirikisha wananchi katika kukabiliana na changamoto za kimaendeleo.
Kwa upande mwingine, kupanua wigo katika kufikia azma ya kugombea ni njia ya kuunganisha nguvu ya umma hata katika kampeni za uchaguzi. Katika siasa za ushindani ni muhimu harakati za uchaguzi zikaendeshwa katika mfumo wa vuguvugu hususan kwa wagombea wanaopitia vyama mbadala ambavyo havitegemei nguvu ya dola.
Hivyo, ni muhimu kwa yoyote anayetaka fulani agombee katika eneo fulani, mosi, amtake kugombea kama sehemu ya msukumo wa umma. Pili, ajiunge na harakati za kufanikisha ushindi wake kwa hali na mali.
Ushindani wa namna hiyo ulijidhihirisha nchini Marekani mwaka 2008 mpaka 2009 kwa wagombea kuungwa mkono na umma; kuanzia wakati wa kura za maoni za ndani ya vyama mpaka kwenye kampeni za uchaguzi mkuu.
Tunaweza kushiriki kuleta mabadiliko kwa kugombea na kuchaguliwa ama kwa kuchagua viongozi kwa kupiga kura. Ndio maana nachukua fursa hii kuwahimiza Watanzania ambao watakuwa na umri wa miaka 18 na kuendelea mwaka 2010 kutimiza wajibu huu wa kiraia.
Hivyo, kwa wapiga kura wapya na wote ambao kwa sababu moja au nyingine hawana kadi za mpiga kura wajitokeze kujiandikisha kupitia uboreshaji wa daftari la kudumu unaoendelea ambao kwa upande wa Dar es salaam utafanyika mapema mwaka 2010.
Izingatiwe kuwa hii ni awamu ya mwisho kabisa ya mchakato huo; kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba hivyo kukosa kujiandikisha ni kujikosesha haki ya kikatiba ya kuchagua kiongozi unayemtaka.
Hata hivyo, izingatiwe kuwa kushiriki kuleta mabadiliko ni zaidi ya matukio ya kugombea ama kupiga kura ni pamoja na kushiriki katika mchakato mzima wa kuleta mabadiliko kwa njia mbalimbali. Mwito wa Mahatma Gandhi kuwa wakala wa mabadiliko unayotoka kuyaona’ unabeba dhana hii.
Swali la kujiuliza, je wewe uko tayari kuwa wakala wa mabadiliko unayotaka kuyaona? Kama Ndio; je umeshawasiliana na chama ambacho unaamini ni chombo cha kuwezesha mabadiliko hayo na kuwaunga mkono viongozi hata ikiwa ni kwa kuwapa ushauri? Ama umeshashirikiana kwa hali na mali au walau kuwasiliana na mgombea mtarajiwa ambaye unaamini anaweza kupeperusha bendera ya kuongoza mabadiliko?
Kugombea nafasi za kuchaguliwa zinazohusisha kuwakilisha umma hakupaswi kuwa suala la mtu binafsi. Matokeo ya kuwaachia wagombea binafsi ama vyama vyao pekee ni kuwa na viongozi ambao baada ya kuchaguliwa kwao kwa sababu waliingia kwa dhamira zao na wakafanya kampeni ‘kivyaovyao’; hawawajibiki kwa umma.
Hivyo tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ni muhimu kwa wapiga kura na wananchi kwa ujumla kutambua kwamba suala la uongozi wa kuchaguliwa kuwakilisha umma ni wajibu wa pamoja.
Ni wajibu wa yoyote anayetambua kwamba Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yetu na watu wake rasilimali; iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu ama maliasili: Hivyo tunawajibika kujenga taifa lenye kutoa fursa ya ustawi wa wananchi. Pamoja Tunaweza!
Ni wajibu wa pamoja wa watumishi wa umma iwe ni walimu, polisi, wahudumu wa sekta ya afya n.k, ama wafanyakazi binafsi ambao wanataka mabadiliko kutoka katika mishahara midogo na mazingira magumu ya kazi, maslahi duni na kujenga taifa lenye kuthamini utaalamu. Pamoja Tunaweza!
Ni wajibu wa wazazi, wanafunzi, wazee, wanawake na masikini kwa ujumla wenye kuathirika na kuongezeka kwa gharama za maisha na kuporomoka kwa huduma za kijamii nchini iwe ni elimu, afya, maji, mafao ya wastaafu na waotaka pawepo mifumo thabiti ya usalama na haki katika jamii ili kuepusha migogoro. Pamoja Tunaweza.
Ni wajibu wa Watanzania wote wenye kukerwa na ufisadi unaolitafuna taifa huku hatua zinazostahili kushindwa kuchukuliwa kutokana na ufisadi kutapakaa katika mfumo mzima wa utawala na kuteteresha hata utawala wa sheria. Tufanye mabadiliko turejeshe uwajibikaji na maadili ya taifa. Pamoja Tunaweza!
Ni wajibu wa matajiri na wenye fursa wanaoona hatari inayolinyemelea taifa kutokana na kuongezeka kwa pengo kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho, ukosefu wa ajira hususani kwa vijana nk ambayo ni mabomu ya wakati yenye athari vizazi hata vizazi yanayoweza kuepukwa kwa kuweka pembeni ubinafsi na kujali maendeleo ya sekta zinazogusa mustakabali wa waliopembezoni. Pamoja Tunaweza!
Ni wajibu wa wapenda demokrasia wote wanaotambua kwamba hujuma za kwenye uchaguzi zinaweza kudhibitiwa kwa kuunganisha nguvu ya umma ikiwemo kwa kujenga vuguvugu thabiti la ulinzi wa kura. Pamoja Tunaweza!
Tukumbuke; mabadiliko ya kweli katika taifa letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale. Kwa falsafa ya Chukua Chako Mapema; Tanzania yenye neema haiwezekani. Tuunganishe nguvu kubadili mfumo wa utawala; mabadiliko yanawezekana.
Tunahitaji uongozi wenye dira na uadilifu wa kulikomboa taifa; hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha viongozi tunaowahitaji wanashinda. Kwa maneno ya Mwalimu Nyerere jukumu la namna hii linaweza kutekelezwa kama kila mmoja akitimiza wajibu wake; umoja ni nguvu. Kidole kimoja hakivunji chawa; kuelekea uchaguzi mkuu 2010: pamoja tunaweza!
John Mnyika anapatikana kupitia 0754694553 na mnyika@chadema.or.tz; makala hii imetoka: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=11672
1 comment:
Mnyika, nimekupata barabara. naamini ulichokiandika ndicho kinachotakiwa kufanyika ili kufikia mabadiliko tunayoyatarajia. lakini nyenzo ni zipi?
Kuna mmomonyoko wa maadili ambao ni chanzo kikuu cha ufisadi, uongozi wa kupeana, rushwa, kutojali wanyonge, kutowajibika kwa viongozi na hata wananchi wa kawaida na mambo mengine kama hayo.
Tuanzie wapi sasa? Tuna kazi kubwa lakini ni lazima ifanyike tena kwa ustadi maalumu kama tunataka kuona mabadiliko katika nchi na jamii zetu.
Asante kwa mchango wako.
Post a Comment