Sunday, July 31, 2011

Ufisadi Kituo cha Ubungo(UBT) na Usafiri DSM (UDA)-Majibu Bungeni

Ripoti ya Uchunguzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi ya Ubungo (Swali la Nyongeza kuhusu Ufisadi kwenye Shirika la Usafiri Dar es salaam –UDA)

MKUTANO WA NNE: Kikao cha Ishirini na Sita – Tarehe 15 Julai, 2011

MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-

Tarehe 15 Machi, 2009 Serikali kupitia Waziri Mkuu iliagiza ufanywe uchunguzi
maalum kuhusu makusanyo ya kituo cha Mabasi cha Ubungo ili kuboresha mapato ya Jiji
la Dar es Salaam. Tarehe 28 Julai, 2009, Serikali ilikabidhi ripoti ya uchunguzi huo kwa

CAG ambayo pamoja na mambo mengine ilieleza kasoro za ukusanyaji na tuhuma za
ubadhirifu wa mapato ya kituo.

Mosi; Je, ni lini Serikali itaweka wazi taarifa hiyo?

Pili; Je, Serikali imechukua hatua gani juu ya kasoro zilizobainishwa kuhusu
mikataba ya kampuni ya Smart Holdings, Rick Hill Hotel, Abood Bus Services, Clear
Channel, Globe Accounting Services na Scandinavian Express Services, ambayo
imesababisha hasara na upotevu wa mapato?

Tatu; Je, Serikali iko tayari kufuatilia na kuchukua hatua za haraka juu ya
malalamiko yanayotolewa na ukusanyaji wa mapato unaofanywa sasa ili kunufaisha
umma kikamilifu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NAQ
SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la
Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Ubungo, lenye (a) (b) na (c) kama
ifuatavyo:-

Mosi; Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
(CAG) alifanya uchunguzi maalum katika kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo na
kubaini kasoro mbalimbali. Aidha, hoja zilizojitokeza katika taarifa ya Uchunguzi ya
CAG katika kituo hicho zimejitokeza pia katika taarifa ya mwaka ya ukaguzi ya CAG ya
mwaka 2009/2010 ambayo iliwasilishwa hapa Bungeni na hoja hizo zimeaza kufanyiwa
kazi na Halmashauri ya Jiji.

Pili; Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa kasoro zilizojitokeza katika Kituo
hicho, Serikali inapitia upya mikataba ya makampuni na kuhuisha viwango
vinavyotakiwa kukusanywa kulingana na sheria ndogo ya Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam inayosimamia ushuru huo.

Marekebisho ya viwango hivyo yatasaidia kuongeza mapato yanayokusanywa
katika kituo hicho na kuondoa kasoro zilizokuwepo za ukusanyaji wa mapato.

Ukusanyaji wa ushuru katika kituo hicho kwa sasa unafanywa na Halmashauri ya Jiji la
Dar es Salaam kupitia kwa Wakala aitwae KONSAD INVESTMENT LIMITED ambaye
anakusanya ushuru huo kwa wastani wa shilingi milioni 4 hadi milioni 5.7 kwa mwezi.

Tatu; Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingaia malalamiko yaliyopo, Serikali
tayari imebadilisha Menejimenti ya kituo na itaendelea kuboresha miundombinu yake.
Aidha, katika Bajeti ya mwaka 2011/2012, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
imetenga kiasi cha shilingi milioni 85 kwa ajili ya kufanya matengenezo katika eneo a
maegesho ya magari. Mpango wa muda mrefu wa Serikali ni kukijenga upya kituo cha
Mabasi kama ilivyoainishwa katika mpango wa biashara wa mwaka 2007.


MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu
yaliyotolewa, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu Naibu Waziri ameeleza kwamba
mkandarasi KONSAD Investment anakusanya milioni Nne hadi milioni Tano kwa
mwezi, lakini kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kwamba toka Mkandarasi aingie
mkataba mwezi Oktoba mwaka 2010, kwa mujibu wa Mkataba alipaswa kukusanya
shilingi milioni 5.6 lakini alifanya hivyo kwa siku mbili tu (mara mbili tu) baada ya hapo
toka wakati huo Oktoba 2010 mpaka leo amekuwa hatekelezi mkataba na ameandika
barua Ofisi ya Waziri Mkuu na inaelekea anakingiwa kifua kuutekeleza huu mkataba.

Mosi; Ningependa kupata kauli kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na ninajua inafahamu
hili jambo kwa undani, Je, iko tayari sasa kuiruhusu Jiji la Dar es Salaam liweze kuvunja
huu mkataba ambao haunufaishi wananchi wa Dar Es Salaam?

Pili; Suala la udhaifu wa kimikataba wa kituo cha mabasi ya Ubungo ambayo
yanahusisha vile vile sehemu ya eneo litakalohusiana na mradi wa mabasi yaendayo kasi
ambayo linahusiana na Kampuni ya UDA yamefikia kiwango cha juu sana, ninaelewa
kwamba ofisi ya Waziri Mkuu iliandika barua ya kusitisha taratibu za uuzwaji wa hisa za
kampuni ya UDA ambazo zimeuzwa na upotevu wa mali nyingi; ninaomba kauli ya Ofisi
ya Waziri Mkuu kuhusiana na ufisadi uliopo kwenye kampuni ya UDA unaoendelea hivi
sasa, na iko tayari kutoa maelekezo kwa Jiji la Dar es Salaam kuweza kusitisha taratibu
zinazoendelea?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA
NAQ SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, nataka
niseme hapa kwamba, Waziri Mkuu alikwenda akamwelekeza CAG aende katika kituo
hiki cha mabasi, akamtaka afanye uchunguzi pale. Walipokwenda pale kwa mara ya
kwanza walikuwa wanakusanya milioni 1.5 kwa siku.

CAG alipofanya marekebisho yale wakafanya na mahesabu na wakamaliza
wakaweka na Menejimenti nyingine pale, ikapanda mpaka milioni 5.7
ninazozizungumza, siyo kwa mwezi ni kwa siku, na kama alivyosema Mbunge kwamba
kampuni ilikusanya kwa siku ya kwanza na siku ya pili na baadaye kukawa na matatizo
hawakukusanya kiasi hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mnyika analifahamu jambo hilo kuliko
sisi sote hapa, tunachojua ni kwamba kuna kampuni nyingine mpya ambayo imekwenda
pale inafanya kazi na hivi tunavyozungumza hapa wanao huu mgogoro anaozungumza na
wameanza kupelekana mpaka mahakamani, kuna mambo ambayo wakati anakwenda kuoperate
ameona kwamba yanakwenda kinyume na jinsi walivyokuwa wamekubaliana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza hapa sasa hivi, tumemwita
Mkurugenzi Mtendaji Kingopi hapa Dodoma tukamuuliza hili analolizungumza hapa,
wameniambia kwamba hili wameliona na wanalifanyia kazi.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mnyika ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri hii
tunayoizungumza yaani (DCC) avute subira katika jambo hili. Hili jambo jingine jipya
sasa linaanza kwa sababu huyu ni mpya ambaye tumesema kwa taratibu hizi mpya akaye
pale, kama ikiwezekana tukubaliane leo tukitoka hapa nimwuite Kingobi na wenzake
tukae na tuseme ni nini kilichotokea kwamba kiasi hiki sasa hakiendelei kukusanywa
kama ilivyokuwa siku ya kwanza na siku ya pili kama anavyosema Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la DART analolizungumza hapa, huu ni
mpango mwingine unaokuja, DART tunasimamia sisi Ofisi ya Waziri Mkuu na ujenzi ule
utafanywa chini ya Wizara ya Ujenzi, na hili suala la UDA analolizungumza hapa kwa
pamoja mimi ningemuomba tukutane kwa sababu linahitaji details zaidi ili tuliangalie
pamoja na lile ambalo tumelizungumzia.

Saturday, July 30, 2011

Salam za Mshikamano kwa Mdahalo wa Katiba

Nikiwa bungeni Dodoma nimefuatilia kupitia vyombo vya habari mdahalo wa katiba ambao umefanyika Ubungo Plaza. Natoa salamu za mshikamano na pongezi kwa waandaaji, watoa mada na washiriki wa mdahalo huu wenye kuchangia katika mjadala wa katiba mpya.

Kupitia kongamano hilo maoni mbalimbali ya maudhui hususani masuala ya muafaka wa kitaifa, ardhi na rasilimali za nchi, jinsia, muungano, haki za binadamu ikiwemo za makundi mbalimbali katika jamii, mgombea binafsi, bunge, mahakama, wananchi kuwa na mamlaka juu ya dola, maadili ya taifa nk

Kongamano pia limejadili masuala mbalimbali kuhusu mchakato wa katiba ikiwemo kasoro katika muswada wa kuandikwa kwa katiba mpya, muundo wa vyombo vitavyoratibu mchakato wa katiba mpya, haja ya kuwa na mkutano mkuu wa katiba, nafasi ya bunge katika mchakato wa katiba na umuhimu wa kupunguza mamlaka ya Rais katika mchakato wa katiba nk.

Hata hivyo, imezungumzwa katika mdahalo kuwa muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba utawasilishwa katika mkutano wa nne wa bunge unaoendelea hivi sasa. Natoa tahadhari kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuzingatia kuwa muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba umeondolewa kinyemela katika ratiba ya mkutano wa nne wa bunge, kilichobakishwa kwenye ratiba ni semina tu ya wabunge kuhusu muswada husika.

Hivyo, pamoja na kujadili kuhusu maudhui ni vizuri katika hatua ya sasa mkazo ukawekwa katika kujadili mchakato wa katiba mpya hususani kuhusu hatma ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba. Hii ni kwa sababu maoni kuhusu maudhui hayatazingatiwa kikamilifu ikiwa sheria ya kusimamia mchakato wa katiba mpya itacheleweshwa na itatungwa sheria mbovu.

Ikumbukwe kwamba hati ya dharura kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ilipoondolewa katika mkutano tatu wa Bunge mwezi Aprili serikali iliahidi muswada huo utajadiliwa katika mkutano wa nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa baada ya kupata maoni ya wananchi. Serikali haikutimiza ahadi ya kuwashirikisha wananchi kwa upana na uwazi kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba wala ahadi ya muswada huo kujadiliwa katika mkutano wa nne wa Bunge kama ilivyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Aidha wakati wa mkutano wa nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani akijibu maswali alieleza kwamba serikali imeshawasilisha kwa bunge marekebisho ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na Spika wa Bunge Anne Makinda akaongezea majibu kuwa sasa muswada huo uko kwa bunge ambalo ndilo litakaloamua hatma ya muswada husika.

Marekebisho ambayo serikali imeyawasilisha mpaka hivi sasa pamoja na kuyatafsiri kwa lugha ya Kiswahili (sio kuutunga upya) hayajazingatia hoja za msingi zilizotolewa na wananchi na wadau mbalimbali wakati walipoukataa muswada wa awali wa sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011 (The Constitutional Review Act 2011) uliochapwa katika gazeti la serikali toleo No. 1 Vol. 92 la tarehe 11 Machi 2011 na kuwasilishwa bungeni mwezi Aprili 2011.

Natoa mwito wa Kituo Cha Sheria za Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuelekeza nguvu katika hatua ya sasa kutaka muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba ulioandikwa upya kuwekwa hadharani hivi sasa. Pia kuitaka Serikali na Bunge kuzingatia kwa ukamilifu hatua zinazohusika kwa mujibu vifungu vya 80, 83 na 84 vya Kanuni za Kudumu za Bunge baada ya kuondolewa kwa hati ya dharura ikiwemo kutoa ufafanuzi kuhusu utata uliopo hivi sasa kuhusu muswada husika. Muswada mbovu wa sheria ya mabadiliko ya katiba utatuletea katiba bomu isiyo na uhalali wa kukubaliwa na umma na kuongeza mpasuko katika nchi badala ya kuwa na muafaka wa kitaifa na misingi muhimu ya uwajibikaji kwa ustawi wa wote.

John Mnyika (Mb)
29/07/2011

Friday, July 15, 2011

Hotuba Mbadala Wizara ya Nishati na Madini

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHE. JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2010/2011 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika; awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha maoni haya ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa mujibu wa kanuni za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7) ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa bunge wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo kwa kuniamini bila kujali tofauti zingine na kunituma kuwawakilisha kwa kunitunuku heshima ya kuwa mtumishi wa umma. Nawashukuru pia kwa kunipa madiwani wa kufanya nao kazi. Asanteni wazee kwa busara zenu, wanawake kwa sala zenu na vijana wenzangu tuliokuwa pamoja kipindi cha kampeni na kukesha wote Loyola katika kulinda ushindi.

Tumeandika historia kwamba hakuna hujuma inayoweza kudhibiti nguvu ya umma (people’s power) mabadiliko yameanza kuonekana na kwa pamoja tuendelee kutimiza wajibu kwa kurejea dira yetu: A.M.U.A; Maslahi ya Umma Kwanza.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wanafamilia yetu ya Dalali; wazazi wangu na ndugu zangu kwa upendo wenu ambao umechangia katika furaha yangu na motisha ya kuendeleza ujasiri na uadilifu katika kusimamia ukweli, haki na ustawi.

Mheshimiwa Spika; Natambua kwa shukrani mchango wa viongozi wenzangu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) makao makuu, Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum Dar e salaam, Jimbo la Ubungo na wa kambi rasmi ya upinzani bungeni katika hatua ambayo tumefikia; mahitaji na matumaini ya watanzania yanatutaka tuendelee kuongoza kwa umoja, umakini na uwajibikaji mpaka kieleweke dhidi ya ubinafsi, uzembe na ufisadi ambao unazidi kushamiri katika taifa letu.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wote katika mamlaka ambao mmenipa ushirikiano kwenye serikali kuu, manispaa ya Kinondoni, katika kamati ya nishati na madini na wabunge wengine kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya kibunge kwa manufaa ya taifa letu na watu wote.

Mheshimiwa Spika; Wizara ya Nishati na Madini ambayo tunatolea maoni bajeti yake leo ni wizara nyeti sana katika taifa letu nyakati za sasa na kwa vizazi vijavyo. Sekta ya nishati ni moyo wa taifa wakati madini ni mtaji wa nchi yetu.

Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi watu, ardhi yenye rutuba , maji (bahari, mito na maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara, mali asili ikiwemo za utalii na madini. Hata hivyo, tunaelekea kuwa na laana ya rasilimali hali ambayo inafanya wananchi walio wengi kuendelea kuwa katika lindi la umasikini na wakiendelea kusukumwa pembezoni nje ya urithi ambao taifa linao.

Mheshimiwa Spika; Tishio la usalama na amani katika taifa letu kwa sasa sio migomo wala maandamano bali ni migogoro inayoendelea ya kirasilimali maeneo mbalimbali ya nchi ambayo ni bomu la wakati litakalolipuka iwapo kasi ya ukuaji wa uchumi wenye kutoa fursa kwa wengi haitaongezwa. Sekta ya nishati ni moyo wa kurekebisha hali hii na sekta ya madini ni mtaji wa kufanikisha dhamira hiyo.

Mheshimiwa Spika; tunakutana leo ikiwa ni miezi michache kuelekea kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru taifa likiwa gizani kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea, idadi ndogo ya watanzania waliounganishwa kwenye gridi ya taifa na matatizo ya sekta ya nishati kwa ujumla. Tunakutana wakati ambao urithi wetu mkuu ambao mababu zetu waliupigania wakati wa kudai uhuru; ardhi na rasilimali zake ikiwemo madini ukiwa mashakani kutwaliwa na kutawaliwa kwa ubeberu mamboleo.

Mheshimiwa Spika; Mnamo tarehe 21 Juni 2011 Bunge lilipitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ambapo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani tulipiga kura ya HAPANA; lakini ikapita kutokana na uwingi wa wabunge wa upande wa pili bila kuzingatia maslahi ya umma.

Tulipiga Kura ya HAPANA kwa kuwa ilikuwa ni bajeti yenye maneno matupu bila matendo katika mipango na utekelezaji; athari za bajeti hiyo zimeshaanza kudhihirika kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi wa kawaida. Bajeti ya mwaka 2011/12 ilielezwa kwa maneno matupu kuwa imeweka nishati kuwa ni kipaumbele cha kwanza. Hata hivyo vitabu vya Bajeti ya Serikali iliyopitishwa vinadhibitisha ukweli mchungu kwamba jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya nishati na madini ni bilioni 539.3 tu.

Kwa mujibu wa Vitabu vya Bajeti ya Serikali 2011/2012 iliyopitishwa, Wizara ya Nishati na Madini imetengewa jumla ya shilingi 402.4 bilioni kwenye Fungu 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi shilingi 76,953,934,000 na bajeti ya Maendeleo zimetengwa shilingi 325,448,137,000 tu. Fedha nyingine kidogo za maendeleo bilioni 126.6 zipo kwenye Fungu la 50 miradi ya MCC kwa kutegemea wahisani.

Hivyo; bajeti hii haijaichukulia kwa uzito unaostahili sekta za nishati na madini hususani umeme hali ambayo inaibua maswali iwapo serikali ina dhamira ya dhati ya kukabiliana na changamoto za msingi zinazolikabili taifa hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani imepitia kitabu cha pili cha matumizi ya kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini ( Volume II Supply Votes) Fungu la 58 vifungu 1001-1009, 2001-2012 na 3001 na kubaini kwamba hii ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho na ufujaji. Mathalani Idara ya Kitengo cha Mawasiliano katika kulipana posho zitatumika Sh. Milioni 405.62 sawa na asilimia 63% ya fedha yote iliyotengwa Sh. Milioni 641.99 kwa idara hii.

Idara ya fedha na uhasibu itatumia Sh milioni 598.49 sawa na asilimia 42% ya fedha yote iliyotengwa. Kanda ya Ziwa – Mwanza kulipana posho inatumia Sh. milioni 389.68 sawa na asilimia 40% ya fedha yote iliyotengwa. Kuna posho kuwanunulia mavazi wafanyakzi wanao safiri nje ya nchi, sherehe na maonesho, chakula na vinywaji, huduma kwa wageni, posho za kukaimu nafasi na posho nyingine.

Kwa ujumla Wizara ya Nishati na Madini inakadiriwa kutumia Sh. Bilioni 7.9 kulipana posho na matumizi mengine ya kawaida ya anasa. Kwani jumla hii ni nje ya posho za msingi kama vile; posho za uhamisho, posho za mafunzo, nyumba, maji na umeme.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali ifanye marekebisho kwenye bajeti ili fedha hizi zipunguzwe ziweze kuongezwa kwenye kuongeza ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na na kuongeza kiwango cha fedha katika mfuko wa wachimbaji wadogo wa madini. Aidha yako matumizi mengine ya ujenzi wa maofisi na gharama kubwa za kisheria ambayo yanapaswa kuhamishiwa katika miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo ya umeme vijijini.

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Juni 2011 Kambi ya upinzani iliwasilisha bajeti mbadala ambayo ilitenga fedha za kutosha katika kukabiliana na changamoto za sekta za nishati na madini. Bajeti mbadala ilitenga fedha za maendeleo Sh. Bilioni 977 kwa ajili ya Wizara ya Nishati na Madini ukilinganisha na ile serikali iliyotenga Sh. Bilioni 452 kwa maendeleo (Fungu 58 na 50); ambayo ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100 (100 %).

Kambi rasmi ya upinzani inataka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo viweze kuzingatiwa kwa uzito unaostahili: · Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane kuwekeza katika Bomba la Gesi kutoka Mtwara, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari, viwandani na majumbani. ·

Kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme kila mwaka ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme. Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini.

Mheshimiwa Spika; Tunatambua kwamba wakati wote serikali imekuwa ikitoa visingizio kuwa kiasi cha fedha kilichopo ni kidogo na hivyo kutegemea zaidi fedha za wahisani. Hivyo, kambi rasmi ya upinzani imewasilisha vyanzo vya mapato ambavyo vinaweza kutumika kuongeza kiwango cha bajeti kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Baadhi ya misingi muhimu ya mapato ambayo tumeiwasilisha ni pamoja na: · Kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta Kampuni za Madini peke yake kutaongeza mapato ya shilingi bilioni 59. ·

Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini kwa Kurekebisha Kodi Sekta ya Madini peke yake tunaweza kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. · Kupunguza fedha kwenye Wizara zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima na kuelekeza fedha katika miradi ya maendeleo hususani ya umeme na gesi.

Mheshimiwa Spika; katika muktadha huo pamoja na kifungu cha 106 cha Kanuni za Bunge kutenguliwa kuruhusu sheria ya fedha 2011 kupitishwa tarehe 22 Juni 2011; ni muhimu mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini uhusishe pia kupitia kitabu cha kwanza cha mapato (Volume 1- Revenue Estimates) ili kuongeza wigo wa mapato.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuzingatia maoni na mapendekezo yanayoendelea kutolewa na kuwasilisha marekebisho (amendments) ya sheria ya fedha ili kuongeza wigo wa mapato. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka kuwasilisha bajeti ya Nyongeza (Supplimentary budget) kwa ajili ya Wizara ya Nishati na Madini ili kuwa na makadirio ya nyongeza ya matumizi kwa mujibu wa kanuni 107 kwa ajili ya miradi ya umeme na gesi asilia.

Umeme Mheshimiwa Spika; Tatizo sugu la mgawo wa umeme ambalo sasa limekomaa na kuwa janga la taifa limetokana na ufisadi na udhaifu wa kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini kuanzia awamu ya pili, likaongezeka katika awamu ya tatu na kukomaa katika awamu ya nne ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufisadi na udhaifu huo wa kiutendaji unajidhihirisha zaidi katika maamuzi mbalimbali yaliyofanyika awamu ya pili hususani 1990 mpaka 1995; awamu ya tatu hususani 1996 mpaka 2004 na awamu ya hususani 2006 mpaka 2011 kwenye maamuzi na mikataba mbalimbali mathalani kashfa ya IPTL, hasara ya mchakato wa ubinafsishaji wa TANESCO, uzembe wa Net Group Solution, ufisadi wa Kiwira, kashfa ya Alstorm Power Rentals, sakata la Songas/Pan African Energy, ufisadi wa Richmond, madhara ya Dowans (ambayo sasa mitambo yake iko chini ya Symbions bila serikali kutoa kauli, kashfa kuhusu mitambo hiyo zimekwisha baada ya umiliki kuhamia kwa kampuni ya Marekani na iwapo taratibu za zabuni zilifuatwa) ambapo mkazo haukuwekwa katika mipango ya muda mrefu ya kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme nchini ambayo imetajwa bayana katika nyaraka mbalimbali za mipango ya kiserikali.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na maamuzi ya Bunge la tisa ya kuhusu masuala hayo bado kambi ya upinzani inataka hatua kamili kuchukuliwa kwa wahusika wa kashfa hizo kama walivyotajwa kwenye orodha ya mafisadi ili kujenga msingi wa kuepusha hali kama hiyo kujirudia katika uwekezaji unaondelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika,athari za upungufu wa umeme kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi ni makubwa sana. Taarifa za Serikali zinaonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato inapoteza mapato ya Bilioni 840 kwa mwaka kutokana na mgawo wa umeme na ripoti za wadau wengine zimeeleza bayana upungufu wa ajira unaosababishwa na mgawo wa umeme.

Mheshimiwa Spika; Ikumbukwe kwamba katika mkutano wa pili wa Bunge kikao cha sita tarehe 15 Februari 2011 Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli bungeni kuhusu mipango ya dharura ya serikali kupunguza tatizo la mgawo wa umeme. Kati ya hatua ambazo zilielezwa ni ukodishaji wa mitambo ya dharura ya MW 260 na kuongeza matumizi katika mitambo ya IPTL.

Kambi rasmi ya upinzani imefadhaishwa na taarifa iliyotolewa kwa umma na TANESCO wakati wa kuanza kwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa kuwa umechangiwa na mitambo ya IPTL kuzalisha chini ya kiwango kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO) suala ambalo linatosha kwa serikali kuwajibika kutokana na uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa sababu suala hili lilikuwa likijulikana kwa miezi mingi bila hatua stahili kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika; Tarehe 1 Aprili 2011 Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi kupitia hotuba yake kwa taifa kwamba mitambo ya MW 260 ingekodishwa na kuanza kufanya kazi mwezi Julai kukabiliana na mgawo wa umeme.

Kambi ya Upinzani haijaridhika na visingizio ambavyo vimekuwa vikitolewa na serikali kwa kutumia sababu za matatizo ya nje ya nchi kuelezea uzembe wa kiutendaji wa kushindwa kusimamia maamuzi ya ndani na inaitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze kwa uwazi na ukweli sababu za kuchelewa kwa mpango huo na hivyo kuongeza kwa kiwango kikubwa muda na kiwango cha mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; kwa upande mwingine mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa ni matokeo ya serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa kuweka mitambo ya MW 100 Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato (Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango wa umeme wa mwaka 2009 ambao ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya mwaka fedha 2010/2011 Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi kukamilisha uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mpango huo na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa kutokana na udhaifu huo.

Mheshimiwa Spika; Ni aibu kwa taifa kuendelea kutegemea vyanzo ambavyo vilianzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati Mwalimu Nyerere na awamu zilizofuata sio tu kushindwa kuongeza kasi ya kuzalisha umeme bali pia kushindwa kukarabati mitambo hiyo na hivyo kuzalisha chini ya kiwango. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa vituo vyetu vya umeme vinazalisha 3694.74 jigawati kwa saa yaani MW 421.8 sawa na asilimia 53.5 ya uwezo wa vituo hivyo MW 788.68.

(Rejea Kielelezo cha Pili). Sababu zinazotolewa za uzalishaji kidogo ni uchakavu wa mitambo na ukame unaoliathiri taifa. Kambi ya Upinzani inaishauri serikali kuacha kuwalaghai wananchi kwa sababu zisizo za msingi kwani ikumbukwe kwamba zipo nchi zilizo katika hali ya jangwa lakini vituo vya kuzalisha umeme vina uwezo wa kuzalisha umeme wa wastani wa zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Spika; Mwaka 2010 Serikali ilieleza kupitia taarifa ya hali ya uchumi kwamba mahitaji ya umeme yalifikia MW 791 na Waziri wa Nishati na Madini akatoa matumaini hewa kwa wananchi kupitia bajeti ya mwaka 2010/2011 kuelekea uchaguzi kwa kutaja miradi ambayo jumla yake iliahidi uzalishaji wa MW 2,960; hata hivyo serikali haikutenga fedha za kutosha kufanikisha mipango husika au walau kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi zingine na sekta binafsi kwa ujumla kufanikisha utekelezaji hali ambayo imejirudia tena katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika; Kutokana na hali hiyo ya mgawo wa umeme unaoendelea na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme vijijini na majibu yaliyotolewa na Serikali kupitia kwa maswali ya papo kwa papo ya Waziri Mkuu tarehe 14 Julai 2011 yameonyesha kwamba serikali halichukulii tatizo la umeme kwa udharura na uzito unaostahili. Hivyo, kambi rasmi ya upinzani inatoa hoja kwa bunge kupitisha azimio la kutangaza kwamba ukosefu wa nishati ni janga la taifa na kupitisha maamuzi ya hatua za haraka ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji wa pamoja.

Bunge lichukue nafasi yake kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 (2) (3) ili kuisimamia serikali kuondoa janga hili la taifa; maazimio ya bunge yatawezesha taarifa za mara kwa mara kutolewa bungeni kuhusu hatua za utekelezaji na adhabu kutolewa kwa mawaziri wa serikali watakaozembea katika kuchukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa miaka mitano (2011/2012-2015/2016) umelenga kuongeza uzalishaji wa umeme mpaka kufikia MW 2780 kwa kuongeza MW 1788 kwa mujibu wa miradi iliyotajwa kwenye mpango. Lengo hili ni dogo ukilinganisha na rasilimali ambazo zipo katika taifa letu; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kufanya mapitio ya mpango huo na kuongeza miradi mingine mikubwa ukiwemo wa Stiggler Gorge ambao una uwezo wa kuzalisha MW 2100 na kuingiza pia makadirio ya ujumla ya MW zinazotokana na miradi midogo midogo itakayoanzishwa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini kwamba hata lengo hili dogo la MW 1788, ambalo ni sawa na ongezeko la wastani wa MW 360 kila mwaka; halijaanza kutekelezwa kwa ukamilifu. Hii ni kwa sababu katika mwaka wa fedha 2011/2012 serikali imepanga katika bajeti kuongeza MW 160 ambazo kimsingi zilipaswa ziwe zimekamilika mwaka wa fedha 2010/2011.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza mradi mwingine wa MW 200 ambao unapaswa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi husika. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba mradi wa Kiwira wa MW 200 awamu ya kwanza upewe kipaumbele maalum katika mwaka huu wa fedha ili kuweza kuziba pengo lililopo. Kambi rasmi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusu pendekezo letu la kutenga fedha za ndani kutekeleza mradi wa njia za kusafirisha umeme huo kutoka Kiwira mpaka Mbeya katika mwaka wa fedha 2011/2012 .

Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza miradi iliyosalia kwa wakati Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza mazingira wezeshi ambayo yanakusudiwa kuandaliwa ili miradi ifuatayo iweze kupata rasilimali kwa wakati na makubaliano kukamilishwa mapema: Dar es salaam-Kinyerezi (Gesi Asilia MW 240), Iringa-Mchuchuma na Ngaka (Makaa ya Mawe-300), Mtwara – Somanga Fungu (Gesi Asilia-MW 300) na Morogoro/Iringa- Ruhudji (Maji- MW 358).

Mheshimiwa Spika, Uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2010/2012 na makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 unaonyesha uwezo mdogo na kasi ndogo ya kufikisha umeme vijijini. Mathalani katika bajeti yake ya mwaka huu Wizara imetenga Sh Bilioni 1.1 kupeleka umeme katika vijijini 4 tu ( Kijiji cha Magindi, kijiji cha Mbwewe, Kijiji cha Mgwashi, kijiji cha Kiwanga) kati ya vijiji 12,176 vilivyosajiliwa kutokana na taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Kwa hali hiyo itachukua karibu miaka elfu mia mbili sawa na karne mbili kufikisha umeme katika vijiji vyote; kama ambavyo tumetumia miaka 50 ya uhuru kuunganisha umeme kwa 14% tu kwenye gridi ya taifa. Kasi ndogo ya kusambaza umeme inadhihirishwa na idadi kubwa ya maombi ya wananchi wanaotaka kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO) likiwajibu kuwa halina uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali iliahidi kutekeleza Mradi wa MCC (Millenium Challenge Cooperation) wa kuvipatia umeme vijiji 289 katika mikoa 6. Mwanza (42), Tanga (129), Dodoma (45), Mbeya (18), Iringa (17) na Morogoro (38). Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa taarifa ya kina ya utekelezaji kutokana na malalamiko ya kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi kwa kulinganisha na kiwango cha fedha kilichotumika. Aidha tathmini ifanyike kuhusu utekelezaji wa mradi husika ili kuwezesha umeme kuweza kufika vijijini kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulieleza kwenye bajeti mbadala 2011/2012 kwamba Kipaumbele chetu cha muhimu ni Kuwezesha Ukuaji wa Sekta za Uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini ili kuboresha kilimo, kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani za bidhaa, kuongeza ajira na kupunguza umasikini kwa wananchi walio wengi.

Mkakati huu ambao utapunguza vijana wengi kukimbilia mijini na kuliokoa Tanzania kuwa taifa la wachuuzi unahitaji uwekezaji wa kutosha kwenye miundombinu ya vijijini ikiwemo ya umeme. Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutenga bilioni 150 kwa ajili ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya uzalishaji wa umeme toka vyanzo vidogo vya maeneo mbalimbali pamoja na usambazaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

Chanzo cha nyongeza ikiwa ni fedha ambazo zinaendelea kutozwa hivi sasa kutokana na ongezeko katika kodi ya mafuta ya taa ambayo ikiendelea kwa mwaka mzima serikali kukusanya kiasi kisichopungua bilioni 70. Mheshimiwa Spika; tunatambua kwamba utekelezaji wa mradi kabambe wa kusambaza umeme katika mikoa 16 unasuasua kutokana na serikali kutokupeleka fedha kwa REA kwa mujibu wa bajeti zinazopitishwa na serikali.

Mpaka mwezi Mei mwaka 2011 serikali ilikuwa imepeleka bilioni 23.3 tu kwa ajili ya malipo ya wakandarasi wakati ambapo fedha zinazohitajika ni shilingi bilioni 78.3. Kwa mwaka wa fedha 2008/2009 fedha ambazo hazikutolewa na hazina ni bilioni 25.3 huku mwaka wa fedha 2010/2011 mpaka mwezi Mei zikiwa zimetolewa bilioni 13.6 tu ambazo ni sawa na chini ya robo (23%) ya bajeti iliyopangwa.

Aidha kambi ya upinzani inashauri mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) afanye ukaguzi wa ufanisi wa miradi inayoendelea kutekelezwa ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa mapema kuwezesha wananchi wa vijijini kupata umeme.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani hairidhiki na kasi ya kuboresha utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) na tunataka serikali ieleze hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya shirika (2006-2010). Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali iwaeleze watanzania ni lini mapitio ya mikataba ambayo inaipa mzigo mkubwa wa kifedha TANESCO na kusababisha bei ya umeme kupanda itafanyiwa mapitio.

Aidha, serikali imekuwa ikiidhamini TANESCO kupata mikopo ambayo kwa sehemu kubwa imekuwa ikitumika kwenye kukodi mitambo ya dharura; hivyo kambi rasmi ya upinzani inashauri kuwe na udhibiti wa kutosha ili mikopo hiyo isigeuke kuwa mzigo kwa taifa baadaye. Kwa upande mwingine, TANESCO imekuwa ikizidai wizara, idara na taasisi za serikali Ankara za umeme zinazofikia bilioni 76; hivyo serikali inapaswa ionyeshe mfano kwa kufanya malipo kwa wakati.

Mheshimiwa Spika; Pia pamekuwepo malalamiko mbalimbali kuhusu mazingira ya kupitishwa kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB, East African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na vingine vikididimia.

Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuandaa mkakati wa kupunguza gharama za manunuzi na pia kupunguza kiwango cha uagizaji wa nguzo na vifaa vingine kutoka nje ili kutumia rasilimali za ndani ili kuchangia katika kukuza uzalishaji na uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani hairidhiki na hatua ambazo serikali inachukua katika kupunguza gharama wanazotozwa wananchi za kuunganishiwa huduma ya umeme suala ambalo linapunguza kasi ya uunganishwaji wa umeme. Tumepokea malalamiko toka kwa wananchi wanaotakiwa na TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za kuunganishwa umeme kwa kiasi kinachozidi milioni moja ambacho ni vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu.

Hivyo, serikali itoe kauli ya hatua inazopanga kuchukua ikiwemo za kubadili mfumo wa Ankara ili kuruhusu kuingiza kwa mteja gharama hizo kidogo kidogo katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, TANESCO inahimizwa kutangaza kwa umma Kanuni za Sheria ya Umeme zilizotolewa kwenye gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63) ambazo kifungu cha nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya usambazaji pale ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Spika; kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme, pamoja na kuondoa kodi katika vifaa vya umeme wa jua; serikali ieleze hatua ilizochukua katika kuweka mazingira wezeshi kwa vifaa vya umeme wa dharura kuweza kupatikana kwa urahisi mathalani vifaa vya kuhifadhia umeme (invetors). Aidha, serikali iongeze kasi ya kutekeleza miradi ya kuhamasisha nishati mbadala hususani vijijini kwa kufanya marekebisho ya msingi katika sheria ya fedha na sheria ya umeme.

Gesi Asilia Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi. Gesi asili iligunduliwa nchini mwaka 1974, ikaanza kutumika kuzalisha umeme viwandani 2004 mpaka sasa inatumika kuzalisha MW 440 sawa na 60% ya matumizi yote ya umeme kila siku na inatumiwa na takribani viwanda 25 kwa uzalishaji.

Kwa mujibu wa tafiti tuna zaidi ya 12 tr cf za gesi na uko uwezekano wa kugundua zaidi kutokana na utafutaji unaoendelea. Taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali. Hata hivyo kwa mwelekeo wa ufisadi na udhaifu wa kiuongozi unaoendelea hivi sasa rasilimali hii inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kupitia Dar es salaam mpaka Tanga uwekwe kipaumbele katika Bajeti ya nyongeza ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Hivyo, serikali itenge bilioni 200 kwa ajili ya kuchangia kwenye mradi wa Bomba la Gesi na kuchangia katika ujenzi wa Kiwanda cha Gesi kama sehemu ya mkakati wa kushughulikia upungufu wa nishati kama janga la taifa.

Aidha usiri katika majadiliano ya mradi wa bomba la gesi ni muhimu ukaondolewa kwa wakati nyaraka rasmi za kiserikali zinaonyesha majadiliano yanayoendelea kati ya Tanzania na China kuhusu mradi husika; kambi rasmi ya upinzani inayo mawasiliano baina ya watendaji wakuu wa kampuni ya Orca Exploration Limited na baadhi ya maofisa wa ikulu kutaka kupatiwa mradi husika; wakati kampuni yao tanzu ya Pan African Energy Tanzania (PAT) imekuwa ikilalamikiwa kuhusu mradi mwingine wa gesi.

Mheshimiwa Spika; kambi ya rasmi ya upinzani inasisitiza mradi kwa kujenga kiwanda cha kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) na mradi wa usambazaji wa gesi Dar es salaam pamoja na mradi matumizi ya gesi kwenye magari inayotekelezwa na Shirika la Petroli Nchini (TPDC) inapaswa kuongezewa rasilimali katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Hatua hii itapunguza pia matumizi ya umeme katika maeneo yenye kuweza kutumia gesi na kubakiza umeme mwingine utakaoweza kutumika kwenye maeneo ikiwemo ya viwandani yenye upungufu wa nishati mbadala. Uamuzi huu utawezesha pia kupunguza gharama za uzalishaji na za maisha zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta ambayo pamoja na mizigo ya kodi na gharama zinazotokana na mfumo mbovu wa uingizaji inasababishwa pia na kupanda kwa bei katika soko la dunia.

Aidha ili kuongeza mapato kwa serikali na TPDC kambi rasmi ya upinzani inataka mrabaha wa asilimia 12 kwenye gesi uanze kutozwa kwa mujibu wa sheria na isitishe mara moja utaratibu wa baadhi kuachiwa kutokulipa malipo husika kwa mujibu wa wa sheria. Mapitio ya kitabu cha mapato yameonyesha kwamba wakati kwenye kifungu cha 2001 cha madini kuna mrabaha hakuna kasma hiyo kwenye kifungu 3001 kinachohusika na gesi na mafuta.

Mheshimiwa Spika; ili kujiandaa kitaaalumu kama taifa kwa mipango kabambe ya gesi, kambi rasmi ya upinzani itekeleze mkakati wa kuwaambatanisha wataalamu wazawa na makampuni makubwa yenye uzoefu wa sekta husika. Aidha, kambi rasmi ya upinzani inataka Wizara ya Nishati na Madini iharakishe kukamilisha mtaala wa uhandisi wa gesi na mafuta ili fani hizo ziweze kutolewa kwenye Chuo Cha Madini Dodoma. Aidha, kwa kuwa serikali wakati wa kuhitimisha mjadala wa mpango wa mpango wa taifa wa miaka mitano; serikali ilikubali pendekezo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara.

Kambi rasmi ya upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza maandalizi ambayo inakusudia kuyafanya kwa kushirikiana na mamlaka zingine husika ili kuwezesha uanzishwaji wa chuo kikuu hicho muhimu ambacho kitatoa mchango mkubwa kwa taifa katika masuala ya gesi na bidhaa zitokanazo na gesi.

Mheshimiwa Spika; kwa muda mrefu sasa taifa letu limekuwa likitegemea mradi mkubwa wa Songo Songo kwa shughuli za uendelezaji, uzalishaji, usafishaji na usafirishaji ambao uko chini ya Kampuni ya Songas. Hata hivyo, kampuni ya Songos imeiajiri Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAT), ambayo ni mshirika wa TPDC katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa gesi asili. PAT imepewa pia Mradi wa Kusambaza Gesi Asili (Ring Main and CNG Project) jijini Dar es Salaam. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa Kampuni ya PAT ililipwa kiasi kikubwa cha fedha zaidi gharama ilizoingia wakati wa kujenga mtandao wa usambazaji wa gesi asili.

Mheshimiwa spika, Aidha upo mwenendo usioridhisha wa kampuni hii ambao unapelekea upungufu wa gesi unaosababisha mgawo wa umeme, mfumo wa bei kubwa unaoongeza mzigo wa watumiaji na pia upotevu wa mapato ya serikali. Hivi karibuni kampuni hii ilipewa na TPDC mabilioni ya fedha kinyume cha taratibu mpaka sasa serikali inadai; ni muhimu serikali ikawaeleza watanzania ni viongozi gani walinufaika na malipo hayo na kiasi gani mpaka sasa hakijarejeswa.

Kutokana na uzito wa tuhuma na usiri katika mikataba; Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuundwe kamati teule ya bunge itayofanya mapitio ya mikataba, sheria, kanuni pamoja na tuhuma za upungufu wa mgawo wa mapato na ufisadi kutokana na mauzo ya gesi kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010.

Mafuta Mheshimiwa Spika; Taarifa za Hali ya Uchumi nchini zinaeleza kuwa mfumuko wa bei unaombatana na kupanda kwa gharama za maisha unazidi kuongezeka katika taifa letu kutoka asilimia 4.2% Oktoba mpaka 6.4% Aprili, na kama utaendelea kupanda hivi kwa ari, nguvu na kasi zaidi kwa miezi michache ijayo utakuwa zaidi ya tarakimu moja.

Kambi rasmi ya upinzani inatambua kwamba ukiondoa kupanda kwa bei ya chakula kunakutokana na kushuka kwa uzalishaji, chanzo kikuu cha hali hii ni ongezeko la bei ya nishati hususani mafuta, umeme na gesi hali ambayo isipodhibitiwa kwa mikakati makini ni tishio kwa utulivu wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Juni 2011 kambi rasmi ya upinzani iliishukuru serikali kwa kutoa kauli ya kukubali matakwa ya umma na pendekezo la kambi rasmi ya upinzani la kupunguza kodi na tozo kwenye bidhaa za mafuta ili kupunguza bei na mzigo mkubwa wa gharama za wananchi na kuonyesha mashaka kuhusu kiwango ambacho kitaondolewa na serikali.

Mheshimiwa Spika, Mashaka hayo yalidhihirisha kwenye kupitishwa kwa muswada wa sheria ya fedha tarehe 22 Juni 2011 ambapo serikali haikuonyesha kivitendo dhamira ya kupunguza kodi kwenye mafuta kwa kiwango cha kuwapunguzia ugumu wa maisha badala yake ikajikita kwenye kupunguza tatizo la uchakachuaji pekee ambalo limedumu kwa sababu ya serikali kushindwa kusimamia utawala wa sheria. Ushahidi ni kwamba katika marekebisho ya kodi; serikali haikupunguza hata senti moja katika mzigo wa kodi kwenye petrol. Aidha, serikali ilipunguza kodi ya dizeli kwa shilingi 99 tu huku ikiongeza kodi ya mafuta ya taa kwa shilingi 358.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani ilikuwa na dhamira ya kuwianisha bei ya mafuta ya taa na dizeli ili kupunguza tatizo la uchakachuaji; lakini si kwa kuongeza kwa kiwango kikubwa kodi ya mafuta kama ilivyofanya serikali. Matokeo ya uamuzi huu ni kwamba wakati bei ya petroli na dizeli zikibaki bila kupungua au zikipanda katika maeneo mengi ya nchi; bei ya mafuta ya taa imepanda kwa ari, nguvu na kasi zaidi.

Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta marekebisho ya sheria ya fedha ili kurekebisha hali hiyo na kueleza mkakati wa kweli wa kupunguza gharama za maisha kwa wananchi. Aidha, serikali ijieleze bungeni kutokana na udhaifu ulionyeswa na taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) katika kusimamia bei elekezi na kupunguza bei za mafuta ambazo serikali iliahidi bungeni kuwa zingepungua kuanzia Julai 2011.

Aidha kama sehemu ya mchakato wa kupunguza gharama za mafuta kufuatilia mabadiliko ya kodi, tozo na mfumo wa uingizaji wa mafuta serikali ifanye mapitio ya mkataba baina ya EWURA na kampuni ya Global Fluids International (T) Ltd kuhusu ufanisi na gharama za kuweka vinasaba na kuleta vifaa maalum vya kupima ubora (XRF).

Mheshimiwa Spika, ukiondoa kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na ukubwa wa kodi zinazotozwa na serikali bei ya mafuta inakuwa juu kutokana na mfumo mzima wa uagizaji, usafirishaji, uingizaji na usambazaji. Mfumo uliopo sasa unanufaisha makampuni makubwa mengi yakiwa ya kigeni na wafanyabiashara wachache wa ndani pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa waadilifu kwa kulinyonya taifa na kuongeza gharama za maisha kwa watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika; Hali hii ndiyo iliyokwamisha kwa muda mrefu kuanza kwa mfumo wa uagizaji na uingizaji wa mafuta ya pamoja (Bulk Procurement System) ili kupunguza gharama; suala ambalo Julai 2010 serikali ilisema liko katika hatua za mwisho na Julai 2011 mwaka mmoja baadaye bado serikali bado inatumia lugha ile ile. Aidha Serikali iwajibike kwa kutoanzisha hifadhi ya mafuta mpaka hivi sasa wakati mwaka 2010 ilitoa kauli ya kufufua kampuni ya taifa ya mafuta (COPEC); kwa ujumla kupanda kwa gharama ya mafuta kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa serikali wa kutochukua hatua zinazostahili kwa wakati.

Kama imeshindwa kufufua kampuni ya taifa ya mafuta itekeleze pendekezo lililotolewa na kambi rasmi ya upinzani la kuchukua hisa 100% katika kampuni ya BP ambayo serikali ina hisa na kuigeuza kuwa chombo cha kutimiza azma husika. Aidha Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua mahususi za kulinda maslahi ya nchi katika kampuni ya TIPER ambayo serikali ina hisa 50% katika hatua za uingizaji na uhifadhi wa mafuta.

Mheshimiwa Spika; Ili kuongeza tija na ufanisi wa TPDC, kambi rasmi ya upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu hatua iliyofikiwa katika kutekeleza ushauri wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma wa kulifanyia marekebisho shirika hilo ili kuwa na mamlaka itakayohusika na kutoa vibali kwenye leseni na kusimamia uchimbaji wa mafuta na gesi na kampuni itakayoshiriki katika biashara ya mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upizani Bungeni inaendelea kusikitishwa na uamuzi uliofanywa wa tarehe 22 Juni 2011 wa kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji ya mafuta na Gesi. Uzoefu kutokana na misamaha ambayo imekuwa ikitolewa kwa makampuni ya madini unadhihirisha kwamba makampuni mengi yanatumia mwanya huo kuleta mafuta yasiyo na kodi na kuyaingiza kwenye soko la ndani la reja reja. Mathalani takwimimu zimedhihirisha kuwa kupitia misamaha iliyotolewa kwa makampuni matano tu ya madini ni karibu robo ya mafuta yote ya Dizeli yaliyoingia nchini na kampuni hizi zililipa dola laki mbili tu.

Mheshimiwa Spika; Misamaha hii haina maslahi ya taifa na ni mianya mingine ya uhujumu uchumi; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kufikiria upya uamuzi huo na kuleta marekebisho ya sheria ya fedha ili kuufuta msamaha hiyo kwa kuwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi zinayofursa kwa mujibu wa mikataba (PSA) kurejeshewa gharama zao mara baada ya mafuta kupatikana. Aidha, uamuzi huu uhusishe pia kampuni za madini bila kujali mikataba (MDA) kwa kuwa imethibitika kampuni hizi zote hutengeneza faida nono bila kulipa kodi inavyostahili.

Madini

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa sekta ya madini mwaka 2010/2011 kumekuwa na ongezeko la uzalishaji huku mauzo ya nje ya madini yakiwa yameongezeka; dhahabu pekee ikifikia thamani ya dola 1,516.6. Hata hivyo mchango kwenye mauzo ya nje umeendelea kuwa ule ule wa asilimia 3.3 wa mwaka 2009/2010 na mchango kwenye pato la taifa ni asilimia 7.1 tu licha ya maelezo matamu ya serikali kuwa mapato yameongezeka kutokana na kutungwa kwa sheria mpya ya madini.

Mheshimiwa Spika, Nyaraka ambazo kambi rasmi ya upinzani inazo toka vyanzo vya kiserikali yanaonyesha kwamba sehemu kubwa ya makampuni yenye mikataba yamekataa kukubaliana na serikali. Hatua za haraka zinahitajika kulinusuru taifa na hali hii ambapo utajiri wetu unaendelea kuondoka huku watanzania wakiendelea kuwa masikini; hatua ambazo zitahusisha mwingiliano baina ya sekta ya madini na sekta nyingine.

Mheshimiwa Spika; Ukirejea kitabu cha kwanza cha mapato ya serikali kwa mwaka 2011/2012, nchi yetu itakusanya bilioni 99.5 tu; hii ni aibu ya taifa ukilinganisha na mauzo ambayo sekta hii inauza nje hasa kwa kuzingatia sehemu kubwa ya kampuni hizo hazilipi kodi inavyostahili.

Kambi ya Rasmi ya Upinzani inaishauri Wizara ya Nishati na Madini kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa kampuni za madini ili malipo ya kila kampuni na mchangunuo wake yafahamike kwa umma badala ya mfumo wa sasa ambapo hurundikwa pamoja katika takwimu za idara ya walipa kodi wakubwa. Aidha, Wakala wa Madini (TMAA) ufanye ufuatiliaji maalum wa madini ya Tanzanite; ambapo bei katika soko iko kati ya dola 250-400 na zaidi kwa kwa karati wakati viwango vinavyotumiwa na mamlaka husika kukadirani vidogo hali inayosababisha upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Spika; Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana na uchimbaji wa madini; kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza bayana hatua ambazo imechukua kufuatia ripoti ya tume/kamati mbalimbali ambazo ziliundwa na serikali kwa nyakati mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Mathalani ripoti za karibuni za Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008) zilieleza bayana namna ambavyo makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia sehemu kubwa ya uwekazaji wao kama mkopo (debt financing).

Kambi Rasmi ya Upinzani, inatambua kwamba makampuni hayo yamekuwa yakitumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali iwaeleze watanzania ni trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 katika kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida kubwa.

Mheshimiwa Spika; ukipitia kitabu cha mapato serikali imeweka malengo madogo ya mapato kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini hali ambayo inadhihirisha kwamba inakusudia kuendelea kutoza mrabaha wa asilimia 3; tofauti na mapendekezo ya Kamati ya Bomani ya asilimia 5 na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo inaitaka serikali kutoza asilimia 4. Kwa upande mwingine bado serikali inaachia mianya kwa makampuni ya madini kutotoa mrabaha baada ya kuondoa gharama za usafiri (net back value) badala ya kutoa kwenye mahesabu ya ujumla (gross); Hatua hizi zikichukuliwa zinaweza kuongeza mapato ya serikali kufikia zaidi ya bilioni 200.

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti hali hii ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 kambi Rasmi ya Upinzaniinaitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua mahususi ambazo itazichukua kutekeleza mapendekezo yafuatayo yaliyotolewa kwenye bajeti mbadala:

Kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi 70% ya mtaji; Kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi; Kufanya marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains) inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania; kambi rasmi ya upinzani inaishauri Wizara ya Nishati na Madini kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha katika kuweka mikakati na usimamizi wa kuhusisha sekta ya madini katika kuimarisha fedha yetu. Kwa kuwa mauzo ya madini yetu yanaongezeka huku shilingi ikishuka;

Kambi Rasmi ya Upinzani, inaitaka Wizara ieleze hatua ilizochukua za kushirikiana na Wizara ya Fedha katika kuwezesha Benki kuu kutunza sehemu ya hifadhi yetu ya fedha za kigeni katika mfumo wa madini ya dhahabu. Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na benki kuu kuweka mfumo wa kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo na pia kutoza sehemu ya mrabaha wa dhahabu kwa ajili ya uhifadhi kama ilivyoshauriwa na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Taratibu hizi ziende sambamba na kusimamia mfumo wa kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanatunza sehemu kubwa ya fedha za nje (walau 60%) kwenye benki za ndani ili kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika; Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imeipa majukumu muhimu STAMICO ya kuwa mwakilishi na msimamizi wa rasilimali za madini nchini kwa niaba ya serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani hairidhishwi na kasi ya kuliwezesha shirika hili muhimu kutekeleza wajibu wake. Mwaka mmoja umepita bila ya serikali kukamilisha mchakato wa marekebisho ya STAMICO kuweza kukidhi haja. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze ni kwa nini marekebisho ya sheria ndogo iliyoanzisha STAMICO (Establishment order) katika mwaka wa fedha 2010/2011 kama ilivyoahidiwa na kurejesha fedha za nyumba nne za STAMICO ambazo ziliuzwa na wakala wa majengo Tanzania (TBA)?

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Msingi katika sekta ya madini ni kuhakikisha watanzania wanaumiliki katika miradi mikubwa ya madini ama kupitia hisa za makampuni hayo kuwekwa katika soko la ndani (DSE) au kwa kampuni ya umma kushikilia sehemu kubwa ya uwekezaji hasa katika madini nyeti ikiwemo urani. Hivyo, ni lazima mtaji wa STAMICO uongezwe haraka kwa kurekebisha sheria na kanuni lakini pia kuongeza mtaji wa shirika. Ukiondoa albaki ya bilioni 5.25 bilioni Serikali ieleze hatua ambazo inakusudia kuongeza mtaji wa STAMICO katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika; tunatambua kwamba Wakala Jiolojia (GST) anaendelea na utekelaji wa mradi wa kutambua maeneo ya madini. Kambi ya upinzani inataka mradi huu uende sambamba na kufanya tathmini ya kina (mineral appraisal) ya madini yetu na kupendekeza mabadiliko ya kisheria na kimikataba ambayo yatawezesha utajiri wa madini yetu kutumika kama mtaji na dhamana katika hatua ya kuhakikisha taifa letu linanufaika na rasilimali zake.

Pia; ili kuongeza uwezo wa GST kutimiza wajibu wake malipo yote yanayopaswa kutolewa kwa mujibu wa sheria ndogo iliyounda wakala husika (Establishment Order) yafanyike kwa mujibu wa taratibu kuanzia mwaka wa fedha 2011/2012. Aidha; ramani na ripoti zinazotokana na utafiti na uchunguzi huo zitolewe kwa uangalifu ili kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote.

Mheshimiwa Spika; tunasikitishwa na maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi yanayohitajika suala ambalo litaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia itahatarisha usalama.

Kambi ya Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ya kina kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato. Mauzo hayo ambayo yanaelezwa kimataifa kuwa yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 bilioni ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 2. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River (Namtumbo) na Bahi Kaskazini (Dodoma).

Mheshimiwa Spika, Iwapo tungepata asilimia 30 tu ya mauzo hayo kama kodi taifa letu lingepata 600 bilioni ambayo ni fedha nyingi kuliko bajeti nzima ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka. Izingatiwe kwamba eneo husika lina madini ya urani takribani paundi 108 milioni sawa na asilimia 77 ya uchimbaji wote wa urani kwa mwaka jana. Hii ni aibu kwa taifa linalokwenda nje kuomba huku ikiachia bwerere fursa za rasilimali za ndani na kufikia hatua hata ya mbuga za wanyama kuvamiwa kwa uchimbaji usio kuwa na tija ya moja kwa moja kwa watanzania walio wengi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kusimamisha kwa muda taratibu zinazoendelea za uchimbaji wa urani mpaka maandalizi ya msingi yafanyike yatakayohakikisha umiliki, manufaa na usalama.

Mheshimiwa Spika; pamoja na ahadi ya serikali kumaliza migogoro katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo pamoja na kuepusha migogoro ya leseni mathalani mgogoro wa wachimbaji wadogo eneo la Winza wilaya ya Mpwapwa ambao serikali iliahidi bungeni tarehe 9 Julai 2010 kuumaliza.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusu mgogoro huo kwa kuwa tayari wachimbaji wadogo wameanza kuhamishwa kwa nguvu toka maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pia migogoro ya wafanyakazi katika makampuni ya madini. Wizara ya Nishati na Madini ilieleze taifa hatua ilizochukua kushirikiana na Wizara nyingine husika kutatua malalamiko ya wafanyakazi wa Tanzanite kuhusu ongezeko la wafanyakazi wageni; Wafanyakazi walioachishwa katika kampuni ya Bulyankulu; kampuni ya Caspiani katika mgodi wa Mwadui Shinyanga ambayo yapo Wizarani kwa muda mrefu bila hatua za msingi kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 25 Mei 1946 kampuni iitwayo Alamasi Limited ilipewa leseni ya kuchimba madini ya almasi kaskazini ya kijiji cha Luhumbo katika eneo la Mwadui, Wilaya ya Shinyanga. Leseni hiyo ijulikanayo kama Hati ya Uchimbaji (Mining Lease) Na. 224 ilitolewa chini ya Sheria ya Madini ya mwaka 1929 iliyokuwa inatumika wakati huo na ilihusu eneo la ukubwa wa ekari 3007. Ili kuchimba almasi katika eneo hilo, Alamasi Ltd. ilipewa Hati Milki ya ardhi Na. 5954. Muda wa leseni hiyo ulikuwa miaka ishirini na moja kuanzia tarehe 14 Juni 1944 na ulitakiwa kwisha tarehe 31 Mei 1965.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa leseni hiyo, Alamasi Limited ilitakiwa kulipa kodi ya ardhi ya senti hamsini kwa ekari moja kwa nusu ya mwaka 1944 iliyokuwa imebakia, na baadae kodi ilitakiwa kupanda hadi shilingi moja kwa ekari kwa mwaka 1945; shilingi moja na thumni kwa mwaka 1946; shilingi mbili kwa mwaka 1947 na baada ya hapo kodi ilitakiwa kuwa shilingi mbili na thumni kwa ekari kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, Ilipofika Januari Mosi 1963, Alamasi Ltd. ilihamisha umiliki wa leseni hiyo kwa muda uliobakia kwa kampuni mpya iitwayo New Alamasi (1963) Limited. Uhamisho wa milki hiyo ulithibitishwa na Msajili wa Hati Msaidizi mnamo tarehe 23 Mei 1963 baada ya taratibu zote za kisheria za uhamisho kukamilika. Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hati Mkuu Msaidizi Mary J. Mziray iliyotolewa tarehe 30 Januari 2006, milki ya leseni ya New Alamasi (1963) Ltd. ilikwisha muda wake tarehe 31 Mei 1965, na eneo la leseni hiyo lilirudishwa katika milki ya Rais.

Kwa sababu hiyo, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 27 Machi 2006, Leseni Na. 224 Hati Milki Na. 5954 ilifutwa katika rejesta ya leseni za madini.

Mheshimiwa Spika, Licha ya muda wa leseni Na. 224 kwisha na leseni yenyewe kufutwa katika rejesta ya leseni za madini, New Alamasi (1963) Ltd. iliendelea kuchimba madini ya almasi katika eneo hilo na kuyauza nchi za nje bila ya kuwa na leseni yoyote ile kwa miaka thelathini na tano! Aidha, kwa kipindi chote hicho, hakuna takwimu zozote zinazoonyesha kiasi cha almasi iliyochimbwa kinyume cha sheria na wala fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya almasi hiyo na zilikoenda fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi juu ya shughuli za New Alamasi Ltd., uhalali wa shughuli zake za uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo, kiasi cha almasi iliyochimbwa kwa kipindi chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 na zilizokoenda fedha zilizotokana na mauzo ya almasi hiyo! Aidha, Serikali ieleze ni kwa nini kampuni iliruhusiwa au iliachwa kuendesha shughuli za uchimbaji haramu wa almasi kwa miaka thelathini na tano na hatua ambazo zimechukuliwa au zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika na ukiukaji huu mkubwa wa sheria za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 9 Mei 2000, Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Mh. Dr. Abdallah Omari Kigoda aliipatia New Alamasi (1963) Ltd. leseni Na. ML. 71/2000 kwa ajili ya kuchimba almasi katika eneo hilo hilo kwa kipindi cha miaka ishirini na tano. Kwa mujibu wa Kamishna wa Madini kwa barua yake ya tarehe 21 Machi 2006, tarehe 25 Mei 2005, “eneo lililokuwa na leseni hiyo liliunganishwa pamoja na maeneo mengine na kuwa leseni ya uchimbaji Na. SML 216/2005 ya Williamson Diamond Ltd. kwa maombi ya wamiliki wa leseni hiyo ya awali.”

Hii ina maana kwamba wamiliki wa New Alamasi (1963) Ltd. waliomba leseni yao iunganishwe na maeneo mengine na leseni hiyo mpya kukabidhiwa kampuni ya Williamson Diamond Ltd. ambayo imekuwa ikichimba almasi katika eneo la Mwadui kwa zaidi ya miaka sitini.

Mheshimiwa Spika, Kuna shaka kubwa na ya kimsingi juu ya uhalali wa milki hii mpya ya leseni ya uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo. Kwanza, kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 iliyokuwa inatumika wakati huo, leseni pekee inayoweza kutolewa kisheria kwa ajili ya uchimbaji almasi ni Leseni ya Uchimbaji wa Mawe ya Vito (Gemstone Mining Licence). Leseni ya Uchimbaji (Mining Licence) hutolewa tu kwa madini yasiyokuwa mawe ya vito au dhahabu. Hii ndio kusema kwamba ML. 71/2000 isingeweza kuwa leseni halali kwa uchimbaji wa almasi katika eneo la Luhumbo au eneo lingine lolote nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 27 Machi, 2006, ML. 71/2000 iligeuzwa na kuwa Leseni Maalum ya Uchimbaji (Special Mining Licence) Na. 216/2005 mnamo tarehe 25 Mei 2005. Hii ndio inayosemekana kuwa leseni ya Williamson Diamond Ltd. na ina ukubwa wa kilometa za mraba 29.73. Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 1998, madini ya almasi hayawezi kuchimbwa kihalali kwa kutumia Leseni Maalum ya Uchimbaji kwani leseni ya aina hii hutumika tu kwa uchimbaji wa madini ya vyuma (metals) kama vile dhahabu na sio kwa mawe ya vito.

Mheshimiwa Spika, madai yaliyotolewa kwa maandishi na Kamishna wa Madini kwamba ML. 71/2000 iliunganishwa na leseni nyingine na kugeuzwa kuwa SML. 216/2005 yanaelekea kutokuwa na ukweli wowote. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 19Aprili 2008, leseni pekee ambayo Williamson Diamond Ltd. wanayo katika eneo la Mwadui ni Leseni ya Uchimbaji namba ML 02/92 iliyotolewa tarehe 20 Mei 1992 na aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete.

Eneo la leseni hiyo ni kilometa za mraba 12.33. Kwa mujibu wa barua nyingine ya Kamishna wa Madini ya tarehe 21 Aprili 2008, ML 02/92 bado ‘iko hai’ na “haijaunganishwa na eneo au maeneo ya mining licence nyingine”!

Mheshimiwa Spika, Miezi mitatu baadae, Kamishna wa Madini alipigilia msumari wa mwisho katika madai haya alipoandika ifuatavyo mnamo tarehe 24 Julai 2008: “Hapakuwa na leseni ya uchimbaji madini ya Williamson Diamond Limited iliyotumika kuunganishwa na leseni namba ML 71/2000 na kuwa moja Special Mining Licence SML 216/2005”! Ni wazi, kwa nyaraka hizi za Serikali, kwamba kuna jambo ambalo limefichwa kuhusiana na shughuli za uchimbaji almasi za New Alamasi (1963) Ltd. na uhalali wa shughuli hizo.

Kambi ya Upinzani ,Tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi ya kufafanua mustakabali wa sasa wa eneo la iliyokuwa Hati ya Madini Na. 224. Tunaitaka Serikali ifafanue utaratibu wa kisheria ambao umeiruhusu Williamson Diamond Ltd. kuendelea kuchimba almasi katika eneo la Luhumbo wakati haina leseni halali katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika; Ni nani hasa walikuwa wamiliki na wakurugenzi wa New Alamasi Ltd? Kwa mujibu wa waraka wa Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) juu ya kampuni hiyo, wamiliki wa New Alamasi Ltd. walikuwa ni mabwana Sylvanus Mipawa aliyekuwa na hisa tatu na Phares Kitanzi Songo aliyekuwa na hisa na Williamson Diamonds Ltd. iliyokuwa na hisa 96!

Aidha, kampuni hiyo ilikuwa na mtaji wa shilingi za Tanzania 2000 ikiwa na maana kwamba kila hisa ilikuwa na thamani ya shilingi ishirini tu! Waraka huu wa BRELA uliandikwa tarehe 22 Septemba, 2006. Kufuatana na waraka huu, kuanzia mwaka 2002 New Alamasi (1963) Ltd. ilipeleka fomu za annual returns ambazo hazikukamilika. Aidha, “... wenye hisa wawili Sylvanus Mipawa na Phares Kitanzi Songo hawaonekani katika returns na maelezo na utaratibu wa kutoka katika kampuni haukuzingatiwa.”

Mheshimiwa Spika, Vile vile, kwa mujibu wa waraka wa Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Makampuni wa BRELA wa tarehe 13 Julai 2007, kati ya mwaka 1965 na 1970, wakurugenzi wa kampuni hiyo walikuwa mabwana George Faulkner Hunt, Gabriel Jacobus Du Toit na Ian David Livingstone. Kati ya mwaka 1970 na 1972, wakurugenzi walikuwa George Faulkner Hunt, Gabriel Jacobus Do Toit na Alexander John Prescott.

Aidha, kati ya mwaka 1973 na mwaka 1983 watu waliopata kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo ni pamoja na Samuel Lweyemamu Lwakatare, Robert Macbain Bisset, Ignace Herack Marandu, Jeremias Norbert Rweyemamu, William Henry Manning, John Robert Dawson Kiwia na Phares Kintazi Songo. Kwa mujibu wa waraka wa BRELA wa Septemba 2006, wakurugenzi wa kampuni hii wanaonekana tofauti “... lakini utaratibu wa mabadiliko haukufuatwa.” Tunaitaka Serikali itoe maelezo sahihi ya kuhusu wamiliki na wakurugenzi wa kampuni hii na kwa nini taratibu za kisheria hazijafuatwa kwa miaka mingi. Aidha, tunaitaka Serikali itoe maelezo iliwezekanaje kwa kampuni yenye mtaji wa shilingi 2000 imeweza kuchimba almasi kwa zaidi ya miaka arobaini!

Mheshimiwa Spika, Uhusiano kati ya New Alamasi (1963) Ltd. na Williamson Diamonds Ltd. umegubikwa na utata mkubwa. Hii ni kwa sababu mnamo tarehe 21 Machi, 2006, wakati akijibu swali la mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru aliyetaka kujua uhusiano wa makampuni haya mawili, Kamishna wa Madini alidai kwamba yeye hatunzi kumbu kumbu za makampuni hivyo “... siwezi kujua uhusiano wa New Alamasi (1963) Ltd. na Williamson Diamonds Ltd. Na kama tulivyoona, taarifa zilizotolewa na BRELA Septemba 2006 zinaonyesha kwamba Williamson Diamonds Ltd. ina 96% ya hisa zote za New Alamasi (1963) Ltd.

Hata hivyo, katika tarehe isiyojulikana ya mwaka 1992, New Alamasi (1963) Ltd. iliingia mkataba na Williamson Diamonds Ltd. ambao kwayo New Alamasi (1963) Ltd. ilifutwa kwa hiari na kuhamisha hisa na mali zake zote “zilizoko kwenye Hati ya Madini Na. 224 Hati Milki Na. 5954” kwa Williamson Diamonds Ltd. Mkataba huu unaelekea ulisainiwa na Sylvanus Mipawa kwa upande wa New Alamasi na watu watatu wasiojulikana kwa niaba ya Williamson Diamonds Ltd.

Mheshimiwa Spika; Mkataba huu kati ya New Alamasi (1963) Ltd. na Williamson Diamonds Ltd. umezua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu kutoka kwa Serikali. Kwanza, mkataba huu unatamka kwamba kinachohamishwa ni Hati ya Madini Na. 224 na mali zilizoko kwenye eneo hilo ambavyo kama tulivyoonyesha ilikwisha muda wake tarehe 31 Mei 1965.

Pili, mkataba huu unataja Hati Milki ya Ardhi Na. 5954 ambayo nayo ilikwisha kurudi kwenye milki ya Rais tangu mwaka 1965 leseni ya uchimbaji ilipokwisha muda wake! Tatu, mkataba huu unaonyesha ulifanyika chini ya Mining Ordinance ya mwaka 1929 ambayo ilikwisha kufutwa tangu mwaka 1979 wakati Sheria ya Madini ya mwaka huo ilipotungwa! Nne, makubaliano haya yanataja makubaliano mengine ya kuhamisha haki za New Alamasi (1963) Ltd. yanayodaiwa kufanyika tarehe 31 Januari 1967, 17 Januari 1972 na 14 Februari 1978.

Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote wa makubaliano ya aina hiyo kati ya makampuni haya mawili kwa vipindi vilivyotajwa. Aidha, makubaliano yanadai kwamba New Alamasi (1963) Ltd. walipewa leseni ya eneo hilo tarehe 25 Mei 1965 kwa kipindi cha miaka kumi na sita kuanzia tarehe 13 Juni 1965 “ambayo ilisajiliwa na Idara ya Madini.” Hata hivyo, kama tulivyoona, Idara ya Madini yenyewe imekanusha madai hayo kwa kuonyesha kwamba Hati ya Madini Na. 224 ilikwisha muda wake tangu tarehe 31 Mei 1965!

Mheshimiwa Spika; Taarifa tulizonazo zinaonyesha kwamba mkataba kati ya New Alamasi (1963) Ltd. sio halali bali uligushiwa kwa lengo la kuwezesha uchimbaji wa almasi kuendelea katika eneo hilo kinyume cha sheria na ili kuendeleza wizi wa rasilimali ya nchi yetu ambao umeendelea kwa miaka zaidi ya arobaini! Tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi na sahihi juu ya uhusiano huu kati ya makampuni haya mawili.

Mheshimiwa Spika, Mamia ya wananchi waishio maeneo jirani na eneo la New Almas wamekuwa wakinyanyaswa kwa miaka mingi na vyombo vya dola kama vile polisi, mahakama na vyombo vya utawala kwa madai kwamba ni wavamizi wa eneo la leseni ya New Alamasi. Watu kadhaa wameuawa na askari polisi na mgambo baada ya kukutwa ndani ya eneo hilo.

Wengi wengine wamepigwa na kuteswa katika vituo vya polisi na wengine wengi wamefungwa kwa tuhuma za uongo za kuvamia eneo la Mgodi wa New Alamasi (1963) Ltd. na kwa kutumia hati za kugushi za kuonyesha umiliki wa eneo hilo. Wote hawa walioteswa namna hiyo na/au ndugu zao wanastahili sio tu kuombwa msamaha kwa mateso ya miaka mingi na ya bure, bali pia wanastahili kulipwa fidia kwa madhara yote waliyoyapata katika muda huo.

Kambi ya Upinzania , Tunaitaka Serikali itoe kauli kama iko tayari kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapata haki zao kutokana na uovu waliotendewa na vyombo vya serikali. Aidha, Serikali itoe taarifa rasmi juu ya hatua inazotarajia kuzichukua dhidi ya Williamson Diamonds Ltd. kwa kushiriki katika kugushi nyaraka za kuiwezesha kuchimba almasi kinyume cha sheria.

HITIMISHO Mheshimimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani inapenda kuhitimisha kwa kusisiza kwamba kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali kuanzia kwa viongozi wakuu wa nchi, Waziri mwenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi; wahusika wanapaswa kuwajibika.

Mheshimiwa Spika; uwajibikaji huo unapaswa kufuatiwa na hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni moyo wa taifa na sekta ya madini ni mtaji wetu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba, kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kwa ujumla kuwajibika.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba bunge lako lijadili makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa ya kuongeza bajeti ya wizara husika; kupokea mapendekezo yatayopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika sheria ya fedha na kupitisha maazimio mahususi ikiwemo ya kukabiliana na upungufu wa nishatia mbao sasa ni janga la taifa pamoja na kuhakikisha taifa letu linanufaika na madini; aidha iwapo Serikali haitakubali hoja hizi za msingi za kuinusuru nchi yetu kuzifanyia kazi, basi tutaunganisha nguvu ya umma kupitia maandamano na kitaeleweka. Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha,


John Mnyika (Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani

Wizara ya Nishati na Madini

15/07/2011

Thursday, July 7, 2011

Kuhusu uwajibikaji na bajeti ya ofisi ya Rais

Niliyozungumza bungeni tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala bora na Uhusiano na Uratibu)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Ninaomba Mwenyezi Mungu aniongoze na kunilinda, nitakapotoa mchango huu kwa siku ya leo. La kwanza, niseme kwamba, siungi mkono hoja iliyoko mbele yetu. Jana Hotuba iliposomwa wakati wa mapumziko nilipigiwa simu na baadhi ya Wananchi kutoka kwenye Jimbo langu; wazee, akina mama na vijana, wakanieleza kwamba, nisiunge mkono hoja hii iliyoko mbele yetu. Kwa sababu moja; Watumishi wa Umma wamepewa ahadi hewa, tafsiri inayojaribu kujengwa ni kama vile mishahara itaongezeka kwa asilimia 40, kitu ambacho sicho.

Mheshimiwa Spika, fungu lililozungumzwa la takriban shilingi trilioni 1.2 na kadhalika, limehusisha vitu vingi sana; wafanyakazi wapya, uhamisho wa wafanyakazi na mambo mengi sana, si kwa ajili ya mishahara peke yake. Kwa hiyo; ni vizuri kwanza wakati wa kuhitimisha hoja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), awaeleze Watanzania hali halisi ilivyo. Pamoja na majadiliano yanayoendelea, uzoefu wa nchi mbalimbali umeonesha kuwa, kima cha chini cha mshahara na kima cha juu cha mshahara siyo siri. Kwa hiyo, isemwe wazi kabisa ili pengo lijulikane na hali halisi ijulikane.

La pili, Bajeti hii inahusu ofisi nyeti kuliko zote katika nchi yetu, Ofisi ya Rais. Ofisi ya Rais kwa mujibu wa Katiba pamoja na kasoro zake, ibara ya 33 mpaka ibara ya 50, imeeleza ukuu wa Taasisi ya Rais, mamlaka makubwa aliyonayo Rais kama Amiri Jeshi Mkuu, kama Mkuu wa Shughuli zote na Kiongozi Mkuu wa Serikali, kama Mwajiri na Mwajiriwa Mkuu; ni mamlaka makubwa sana. Kwa hiyo, utumishi wote wa umma; iwe Watumishi wa Kawaida, Mawaziri au waziri mkuu, wote wanafanya kazi tu kwa niaba ya kumsaidia Rais; tafsiri yake ni nini?

Upungufu wowote ule tunaoweza kuuzungumza wa utekelezaji wa bajeti iliyopita, wa kuwajibika kwanza kabisa ni Ofisi ya Rais. Iwe ni upungufu wa TAKUKURU, mgao wa umeme na kadhalika, ndiyo Ofisi Kuu. Siungi mkono kwa sababu taarifa ya utekelezaji ya mwaka mzima, lakini ikiwa ni miezi sita toka Serikali iingie madarakani, haileti matumaini ya Ofisi hii kusimama ipasavyo kushughulikia kero za msingi za Wananchi.

Mheshimiwa Spika, sababu ya tatu, halafu nitajielekeza kwenye vifungu vya bajeti iliyoko mbele yetu; nimepitia Hotuba ya Waziri, ukurasa 61, linazungumzwa jambo linalogusa Wananchi wa Jimbo ambalo wamenituma kuwawakilisha. Kifungu cha (4) pale kinasema: “Mpango wa Urasimishaji katika miji imetajwa vilevile eneo la Kimara Baruti, Dar es Salaam, kwenye Mradi wa MKURABITA. Sasa kama Chombo cha Serikali kinaweza kuzungumza kwa mwaka mzima wa bajeti kufanya urasimishaji kwenye mtaa mmoja tu, Dar es Salaam, Kimara Baruti, mtaa tu siyo Kata wala siyo Jimbo; tupo kwenye hali mbaya kama Taifa na tupo kwenye hali hii kwa sababu ya kukosa vipaumbele.

Mheshimiwa Spika, ukiingia kwenye Kitabu cha Bajeti ya Maendeleo, Fungu 30, ukurasa wa 33, MKURABITA imetengewa shilingi bilioni tatu peke yake mwaka huu wa fedha wakati mwaka uliopita wa fedha ilitengewa shilingi bilioni sita. Tafsiri yake ni kwamba, tunarudi nyuma kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Sasa ningependa kupata ufafanuzi kuhusu hili suala la MKURABITA, urasimishaji eneo la Kimara Baruti. Kwa sababu nina ushahidi wa barua ambayo ipo Ofisi ya Rais (Ikulu), ya Kampuni inayoitwa Twiga Chemical Industry Limited, ikisema kwamba, Wananchi wa Kimara Baruti, eneo la ekari nane waondolewe. Sasa hili jambo kwa sababu tunajadili kuhusu TAKUKURU na Usalama wa Taifa, hapa ndiyo nafasi yao sasa. Hili jambo ni ufisadi mkubwa, Kampuni hii imelipwa shilingi bilioni tatu au milioni 3,000 fedha za umma kama fidia kwenye mazingira yasiyoeleweka kuhusiana na ardhi hii hii kinyume na agizo la Kamati ya Deni la Taifa katika kikao chake cha mwaka 2006 na inakusudiwa kulipa pesa nyingine shilingi bilioni 4.5. Sasa kama tuna pesa nyingi za namna hii za kulipa; kwa nini hatuzipeleki MKURABITA wakafanya urasimishaji wa Jiji zima la Dar es Salaam?

Ningeomba TAKUKURU na Usalama wa Taifa wachunguze mazingira ya malipo kwa Kampuni hii ya Twiga na tuelezwe ni kigogo gani ndani ya Serikali yuko nyuma ya Kampuni hii ya Twiga Chemical Industry. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaomba sasa nijielekeze kwenye vifungu vya bajeti hii, ambayo tunayo hapa na tunaipitia. Nimezungumza kuhusiana na Fungu la 30 - Ofisi ya Rais. Sasa ukilinganisha Kitabu cha Maendeleo na Kitabu cha Matumizi ya Kawaida, Ofisi ya Rais kwenye Matumizi ya Kawaida, imetengewa pesa nyingi kweli kweli, yatakuja kwenye takwimu kuliko matumizi ya maendeleo. Sasa kitu ambacho kinanifanya nisiunge mkono Bajeti hii mpaka nipewe maelezo ya kina sana ni kasma mojawapo, kasma ndogo inayoitwa Matumizi ya Kitaifa. Kwanza, ninaomba wakati Waziri atakapohitimisha hoja, alieleze Bunge kwa nini baada ya kuwasilisha Randama ya Wizara yake, hatujapewa nakala, kwa sababu tungepewa nakala, tungeingia ndani ya vifungu? Mimi ninafahamu kwenye kasma hii, shilingi bilioni 135 hazina mchanganuo, zinaitwa tu Matumizi ya Kitaifa. Halafu Bunge tunatakiwa tupitishe Matumizi ya Kitaifa Ikulu, shilingi bilioni 135.

Mheshimiwa Spika, ninataka atueleze fedha za bajeti iliyopita zilitumikaje kwa sababu tunaelewa fungu hili ndilo ambalo linatumika ukisikia safari nyingi sana za Rais nje ya nchi? Msafara mmoja wa Rais kwenda nje unagharimu kidogo sana ni shilingi milioni 50 na wakati mwingine msafara unakwenda mpaka shilingi milioni 200 na safari ni nyingi kweli kweli. Hatukatai Rais kusafiri; Mwalimu Nyerere, alikuwa anasafiri, wazee wangu walioko hapa wanajua kwamba, Mwalimu alikuwa anakwenda Marekani kipindi chote cha Urais wake, alikuwa akienda Marekani basi anakwenda kwenye Kikao cha Umoja wa Mataifa (UN). Kama amekwenda kwa shughuli za kawaida, State Visit Marekani, Mwalimu Nyerere alikwenda Marekani mara mbili au tatu kipindi chote. Safari nyingine ni za kwenda Umoja Mataifa.

Mheshimiwa Spika, tungekuwa na muda tungeingia ndani zaidi Zambia, nina kabrasha hapa la Bajeti ya Zambia.

(Hapa Mheshimiwa Mbunge alionesha kabrasha la Bajeti ya Zambia)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Zambia, Bajeti inaonesha kwa kina mpaka Rais anakwenda safari ngapi? Ninachosema, kupanga ni kuchagua, tupunguze kwenye fungu la shilingi bilioni 135 tuongeze pesa kwenye MKURABITA, tuwasaidie Watanzania waweze kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumza kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa na TAKUKURU. Ningeomba pamoja na kukimbizana na mambo mengine haya, Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya TAKUKURU, watusaidie maeneo ambayo yana kero zaidi kwa Wananchi. Kule ninapotoka, Jimbo la Ubungo, kero kubwa ni maji; sasa mtu atashangaa Usalama wa Taifa na TAKUKURU wanahusika vipi na maji? Kule kuna kero ya maji, kwa sababu kuna rushwa kwenye mtandao mzima wa maji na Mradi wa Maji uliopo pale wa mabomba ya Wachina, uliwekwa ovyo ovyo; rushwa; wizi.

Mimi ninatarajia kwamba, Vyombo vya Dola, pamoja na kazi za kawaida za Mawaziri, TAKUKURU ikachunguze mambo haya ya maji. Kule tunakerwa kweli na migogoro ya ardhi, wengine wanasema sasa TAKUKURU inahusika na Usalama wa Taifa wanahusika vipi na ardhi?

Mheshimiwa Spika, Usalama wa Taifa ulikuwa na mwakilishi ndani ya Kamati iliyoundwa ya Kuchunguza Migogoro ya Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam. Kulikuwa na Mjumbe wa Usalama wa Taifa. Ninataka kujua, baada ya hapo, pamoja na kwamba Ripoti imekuwa ni ya siri na inapaswa kuwa wazi; mapendekezo yaliyokuwa mle ndani ya Ripoti ni pamoja na hatua ambazo Usalama wa Taifa na TAKUKURU wanapaswa kuzichukua. Ninataka kujua kwenye mwaka wa fedha uliopita, Idara hizi zimefanya nini kushughulikia kero hizi za Wananchi wa kawaida sana.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba; ninaamini kwamba, ili tuendelee, pamoja na yale aliyoyazungumza Mwalimu, tunahitaji misingi mikubwa miwili, kwa maana ya kuwa na maono (Vision) na kuwa na maadili (Values). Sasa hii inatutaka tutoke kama Taifa kuwa na utamaduni wa haya mazoea ya ufisadi na tuanze kuwa na utamaduni wa uwajibikaji. Binafsi, nilisema na nirudie kusema hapo kwamba; kwa hali iliyofikia ya mgao wa umeme hivi sasa; ni wazi kwamba, Waziri wa Nishati na Naibu wake kimsingi nilisema mwezi Februari na ninarudia tena leo, wanapaswa kujiuzulu.

Kujiuzulu kwao hakutatoa tija zaidi ya tija ya uwajibikaji kwa Taifa kama Ofisi ya Rais, haitafanya maamuzi magumu. Tarehe 15 Februari, 2011, Baraza la Mawaziri lilikaa likapitisha maamuzi wakati ule, mimi nikatahadharisha kwamba, haya maamuzi yasiposimamiwa vizuri, tutakuwa na mgao; na Rais tarehe 1 Aprili 2011; na ndiyo maana nimesema Rais aanze kwanza kusafisha Ikulu. Kuna watu wanamshauri Rais vibaya, Rais akatoa Hotuba kwa Taifa kwamba, Julai, megawati 260 zitafanya kazi. Hii ni Julai; kuna mgao na kuna mgao mkubwa zaidi unakuja kwa sababu ya ufisadi kwenye Sekta ya Umeme na kwenye sekta ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasema hapa panahitaji uwajibikaji wa pamoja, siyo Wizara ya Nishati tu. Nimesoma kauli ya leo ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda na nilitarajia kauli ile ingetolewa Bungeni; Waziri Mkuu, hajatoa kauli Bungeni kuhusu mgao wa umeme. Kauli aliyoitoa Dar es Salaam kwenye matembezi ya Maonyesho Saba Saba siyo ya Wizara ya Nishati, siyo TANESCO, inalipotosha Taifa vilevile. Katika hatua tuliyofikia hivi sasa, ninahitaji kwenye majumuisho hayo ya Hotuba ya Rais, tupate kauli kutoka Ofisi ya Rais, kuhusu mgao wa umeme.

Tuesday, July 5, 2011

Maji Mavurunza, Kilungule, King'ongo kata za Kimara na Saranga

Nawahimiza DAWASCO/DAWASA kusimamia vizuri wakandarasi ili kukamilisha haraka taratibu za uwekaji wa miundombinu na ufungaji wa vifaa ikiwemo kushirikiana na TANESCO kufikisha umeme katika visima vya maji ili kuwapunguzia kero ya maji wananchi wa kata za Kimara na Saranga.

Hivi karibuni nimefanya ziara katika kata za Kimara na Saranga na kubaini kwamba ukamilishaji wa visima katika mitaa ya Mavurunza, King’ong’o na Kilungule unasuasua kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa nyakati mbalimbali nimekuwa nikifuatilia agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwa DAWASCO tarehe 24 Mei 2010 la kuchimbwa kwa visima vinane ili kupunguza kero ya maji kwa wananchi wa baadhi ya mitaa ya pembezoni mwa kata za Kimara na Saranga.

Visima hivyo vyenye mtandao wa maji ni suluhisho la mpito la tatizo la maji katika maeneo ya King’ong’o, Kilungule na Mavurunza wakati tukiendelea kufuatilia suluhisho la kudumu linalopaswa kuhusisha pamoja na mambo mengine kuongeza ufanisi wa DAWASCO katika kuwahudumia wateja, kudhibiti ufisadi unaofanywa katika mtandao ikiwemo kukabiliana na upotevu wa maji unaondelea, kuongeza kiwango cha maji toka Ruvu juu kupitia ujenzi wa bomba jipya na Bwawa la Maji Kidunda.

Kupitia kongamano la maji Jimbo la Ubungo la tarehe 31 Januari 2011 tulibaini kwamba ahadi hiyo ilikuwa imesahauliwa na watendaji wakuu wa mamlaka husika hivyo tukakubaliana na wananchi wa maeneo husika kwamba tuunganishe nguvu ya umma katika kuifuatilia itimizwe kwa wakati.

Kwa upande mwingine natoa mwito kwa wananchi wa maeneo husika kuendelea kufuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha kwamba inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Kisima cha King’ong’o namba moja iliahidiwa kwamba kitakamilika mwanzoni mwa mwezi huu na kuzalisha lita 13, 200 kwa saa na kuhududimia wakazi 3100; ujenzi wa matanki na uwekaji wa pampu unapaswa kuharakishwa.

Kisima cha King’ong’o namba mbili uchunguzi wa miamba wa eneo husika ulikamilika toka mwezi Mei 2011 hivyo utaratibu wa zabuni unapaswa kuharakishwa kwa majibu wa sheria hili huduma ya maji iweze kupatikana kwa wananchi.

Kisima cha Kilungule A uchimbaji wake ulianza toka mwezi Oktoba mwaka 2010 kikitarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 19,800 na kuhudumia wastani wa wakazi 4,000; hata hivyo ujenzi wa mtandao, tenki na vioski vitatu ulichelewa kuliko kawaida. Katika hatua ya sasa tayari TANESCO wamekamilisha uchambuzi kwa ajili ya makadirio ya gharama za umeme hata hivyo bado taratibu za kufikisha umeme kwa ajili ya wananchi kupata huduma ya maji zinasuasua.

Kisima cha Kilungule B taratibu zake zilichelewa kuanza mpaka msukumo wa ziada ulipotolewa na eneo na kuchimba kutafutwa mwezi Machi 2011. Hata hivyo, hatua za uchimbaji zimekwama kutokana na wataalamu kuchagua eneo ambalo maji yake hayana ubora wa kutumiwa na binadamu. Hivyo, taratibu za kupata eneo mbadala zinapaswa kuharakishwa ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji.

Kisima cha Mavurunza namba moja ujenzi wake ulianza mwezi Agosti 2010 kikikadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 19,800 na kuhudumia wakazi wapatao 4700. Hata hivyo ujenzi wa mtandao pamoja na ufungaji wa pampu ulisimama kwa muda mrefu. Mnamo mwezi Mei ulikamilika kwa majaribio lakini ulishindwa kuanza kazi kutokana na makosa ya TANESCO ya kufunga umeme wa njia moja (single phase) badala ya njia tatu (three phase); hivyo hatua zinahitajika kurekebisha hali hiyo.

Kutokana na ziara nilizofanya nimebaini kwamba visima ambazo taratibu za ujenzi zinaendelea mpaka sasa ni vitano; wakati ahadi ya Rais Kikwete ilikuwa ni ya visima nane. Hivyo, nahimiza DAWASCO kuanza ujenzi wa visima vingine vitatu katika maeneo ya pembezoni ya kata ya Kimara na Saranga kwa kushirikiana na manispaa ya Kinondoni.

Aidha ni muhimu kwa Wizara ya Maji kuwa na mfumo wa kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu miradi inayoendelea kwa kuwa wakati Rais Kikwete alipotembelea Wizara hiyo yenye makao yake makuu katika jimbo la Ubungo tarehe 24 Machi 2011 alipewa taarifa potofu kuhusu hatua ambayo imefikia katika ukamilisha wa ahadi zilizotolewa kuhusu uchimbaji wa visima. Suala hili ni muhimu kwa kuwa miradi mikubwa inayotaka kuanza kutekelezwa ya ujenzi wa bwawa la Kidunda na ujenzi wa bomba kubwa la maji kwa upande wa Ruvu juu litakaloongeza uwezo wa kusambaza maji kwa wananchi wa kata mbalimbali za jimbo la Ubungo na maeneo mengine unahitaji ufuatiliaji makini na ushirikishwaji mpana wa umma.

Nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha kwa kushirikiana nami kuwakumbusha mawaziri wenzake kuhusu ahadi za maji na barabara alizozitoa Rais Kikwete kata ya Kimara kama nilivyomuomba wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mavurunza mwezi Mei mwaka 2011.

John Mnyika (Mb)
Bungeni, Dodoma-4/7/2011

Sunday, July 3, 2011

Mgawo wa umeme umalizwe na mihimili ya dola

Tatizo sugu la mgawo wa umeme ambalo sasa limekomaa na kuwa janga la taifa limetokana na ufisadi na udhaifu wa kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini kuanzia awamu ya pili, likaongezeka katika awamu ya tatu na kukomaa katika awamu ya nne ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufisadi na udhaifu huo wa kiutendaji unajidhihirisha zaidi katika maamuzi mbalimbali yaliyofanyika wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi (hususani 1990 mpaka 1995) , Rais Benjamin Mkapa (hususani 1996 mpaka 2004) na Rais Jakaya Kikwete ( hususani 2006 mpaka 2011) kwenye matendo na mikataba mbalimbali mathalani kashfa ya IPTL, hasara ya mchakato wa ubinafsishaji wa TANESCO, uzembe wa Net Group Solution, ufisadi wa Kiwira, kashfa ya Alstorm Power Rentals, sakata la Songas/Pan African Energy, ufisadi wa Richmond, madhara ya Dowans (ambayo sasa mitambo yake iko chini ya Symbions) ambapo mkazo haukuwekwa katika mipango ya muda mrefu ya kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme nchini ambayo imetajwa bajana katika nyaraka mbalimbali za mipango ya kiserikali.

Hivyo ufumbuzi wa tatizo hili katika hatua ya sasa ambapo taifa limefikia unahitaji uongozi na uwajibikaji wa ngazi za juu zaidi katika mihimili ya dola ya serikali, bunge na mahakama katika kuchukua hatua zinazostahili kwa kushirikisha wadau wengine hususani sekta binafsi badala ya kutegemea Wizara ya Nishati na Madini.

Katika muktadha huo nawapongeza Umoja wa Wafanyabiashara wa Makampuni Makubwa 55 nchini (CEOrt) kwa tamko lao kuhusu mgawo wa umeme na naitaka serikali hususani Rais Kikwete kuzingatia na kuchukua hatua za haraka kuhusu madai yaliyotolewa na watendaji wakuu wa makampuni hayo kupitia kwa mwenyekiti wao.

Rais Kikwete kwa nafasi yake ya kuongoza mhimili mmoja wa dola anapaswa kuitisha kikao cha baraza la mawaziri na kufanya maamuzi mazito yenye kuhusisha kutangaza mgawo wa umeme kuwa ni janga la taifa na kuunganisha wadau wote katika kuchukua hatua za dharura; ili kuweka uzito wa kiutendaji katika kauli ya kisiasa iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.

Kwa upande mwingine Spika wa Bunge kwa wajibu wake wa kuongoza mhimili mwingine wa dola anapaswa kutumia kanuni ya 53 (2) au 55 (1) au 114 (17) kuwezesha kuwepo kwa mjadala bungeni kwa ajili ya kupitisha maazimio ya dharura ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme kutokana na kauli ya serikali ama Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini kama sehemu ya wajibu wa kikatiba wa Bunge wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Izingatiwe kwamba katika tamko lao watendaji hao wameeleza athari za kiuchumi za mgawo wa umeme unaondelea kwenye kushuka kwa mapato ya serikali na pia kupungua kwa ajira; madhara ambayo yamewahi kuelezwa pia na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) mwezi Februari mwaka 2011.

Aidha katika tamko lao kama lilivyonukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 2 Julai 2011 wameeleza kwamba serikali imekuwa ikitoa kauli za kisiasa na kutaja miradi bila hatua za haraka na mkakati bayana wa kiutekelezaji hususani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012. Pia, katika tamko lao wameeleza tatizo la umeme kuwa ni janga la taifa na kutaka serikali iitishe mjadala wa kitaifa utakaohusisha pia sekta ili kupata majibu ya kitaalamu na kushirikiana katika utekelezaji.

Tamko hilo limesadifu kauli ambazo nimezitoa kuhusu mgawo wa umeme hususani tarehe 15 Februari 2011, tarehe 2 Aprili 2011, tarehe 22 Mei 2011 na tarehe 25 Juni 2011 na kuweka bayana hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na serikali kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu mbalimbali.

Hata hivyo, mwelekeo wa matatizo ya mgawo wa umeme umevuka uwezo wa Wizara ya Nishati na Madini na kuwa tatizo la kitaifa ambalo linahitaji uwajibikaji wa pamoja katika serikali ndio maana tarehe 30 Juni 2011 nilitaka kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kutumika kupata majibu. Baada ya kanuni kupindishwa kumlinda Waziri Mkuu Pinda kutoa kauli ya pamoja kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni kwa niaba ya Rais nilitoa mwito kwa Waziri Mkuu Pinda kutumia majumuisho ya mjadala wa bajeti ya wizara yake kutoa majibu.

Lakini Waziri Mkuu Pinda hakutumia nafasi hiyo kueleza hatua za dharura ambazo zinachukuliwa na serikali kukabiliana na mgawo wa umeme pamoja na kufahamu kwamba yeye mwenyewe katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 aliahidi kwamba mitambo ya umeme ya MW 100 Ubungo na MW 60 Mwanza ingenunuliwa kwa wakati; suala ambalo kama angelisimamia ipasavyo lingeweza kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kupunguza kwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa.

Kutokana na Waziri Mkuu kutokutoa kauli kuhusu dharura ya mgawo wa umeme katika hotuba yake ya bajeti tarehe 23 Juni 2011 na wakati wa majumuisho ya hotuba hiyo tarehe 1 Julai 2011 ilinibidi nishikilie mshahara wake kwa mujibu wa kanuni 101(3) kupata maelezo wakati bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Tarehe 1 Julai 2011 nililieleza bunge kuwa mgawo wa sasa umesababishwa na udhaifu wa kiutendaji wa kutokufanya maandalizi kwa wakati ikiwemo kuchelewa kufanya manunuzi kwa ajili ya mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya IPTL, kuchelewa kutekeleza miradi wa MW 100 Ubungo, MW 60 Mwanza na MW 260 kupitia mitambo ya dharura na kutaka ufafanuzi kutoka kwa Waziri Mkuu. Hata hivyo, ufafanuzi haukutolewa na Waziri Mkuu badala yake maelezo yalitolewa na Waziri wa Nishati na Madini ambayo hayakujitokesheleza.

Kadhalika lipo tatizo na upungufu wa nishati ya kuendeshea mitambo ya umeme ikiwemo upungufu wa mafuta mazito na gesi asilia hali ambayo isipochukuliwa hatua za dharura itasababisha mgawo wa umeme kuendelea hata baada ya mitambo ya dharura kuletwa nchini. Hivyo, mapitio ya haraka ya mikataba ya uwekezaji wa gesi pamoja na ujenzi wa Bomba la Gesi ambao haukuzingatiwa kikamilifu katika bajeti ya serikali 2011/2012 inapaswa kufanyika. Maamuzi hayo magumu yanapaswa kuambatana na hatua za kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa nishati na pia katika uingizaji wa vifaa vyenye kusaidia kupunguza makali ya mgawo wa umeme.

Hivyo, ni muhimu Rais Kikwete akatimiza wajibu wake wa kikatiba kwa kuingilia kati tatizo la mgawo wa umeme kwa kurejea pia maelekezo yake ambayo aliyatoa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 15 Februari 2011 na ahadi alizozitoa kwa taifa katika hotuba yake ya tarehe 1 Aprili 2011. Hatua hizo zitaepusha matamko yanayoendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari badala yake uwajibikaji wa pamoja wa dharura utafanyika kupitia baraza la mawaziri, bunge na mikutano na wadau muhimu kukabiliana na janga la taifa la mgawo wa umeme.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
3 Julai 2011; Bungeni-Dodoma

Saturday, July 2, 2011

Kanuni zimepindishwa kumlinda Pinda

Sijaridhika na maamuzi ya Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene kupindisha kanuni tarehe 29 Juni 2011 na 30 Juni 2011 kwa ajili ya kumlinda Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutekeleza wajibu wa kujibu maswali ya papo kwa papo ya wabunge kama kanuni zinavyohitaji.

Kutokana na hali hiyo nakusudia kuwasilisha malalamiko tarehe 2 Julai 2011 kwa katibu wa bunge kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu 5(2) na 7(3) ili sababu hizo ziwasilishwe kwa Spika aitishe kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge kwa kurejea kanuni 5(5) na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi mbadala utakaotolewa.

Tarehe 30 Juni 2011 niliomba muongozo wa mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni 68 (7) kutokana na tarehe 29 Juni 2011 Mwenyekiti wa Bunge, Simbachawene kutoa taarifa ya bunge kuwa hakutakuwepo na maswali na majibu kwa Waziri Mkuu tarehe 30 Juni 2011 kwa kuwa kanuni zilitenguliwa 22 Juni 2011 kumruhusu Waziri Mkuu kujiandaa kuwasilisha hotuba yake tarehe 23 Juni 2011.

Niliomba mwenyekiti atoe muongozo kuwa kanuni za bunge zilikiukwa tarehe 29 Juni 2011 kwa kutoa taarifa ya kupindisha kanuni kumlinda Waziri Pinda asijibu maswali ya wabunge wa papo kwa papo bila kufuata utaratibu wa kutengua kanuni.

Nikalieleza bunge kwamba kanuni ya 150 imekiukwa ambayo kipengele cha 150(1) ambacho kinaelekeza bayana kwamba ili kanuni itenguliwe kwa madhumuni mahususi ni lazima waziri, mwanasheria mkuu wa serikali au mbunge yoyote lazima atoe hoja hiyo na kifungu cha 150 (3) kinataka maelezo ya hoja hiyo yakiwemo madhumuni yatolewe jambo ambalo halikufanyika tarehe 29 Juni 2011.

Hivyo, nikalijulisha bunge kwamba kwa kuwa kuna masuala tata na tete yanayoendelea katika taifa ambayo yanahitaji kauli za serikali ilikuwa ni muhimu kwa kipindi cha maswali na majibu kwa waziri mkuu kuendelea kama kanuni zinavyohitaji tarehe 30 Juni 2011 ili Waziri Mkuu Pinda atimize wajibu wa kutoa majibu.

Mathalani nililieza bunge kwamba vyombo vya habari vimenukuu Waziri Mkuu Pinda akitoa maelekezo potofu kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu mchakato wa katiba kabla ya sheria kupitishwa. Maelekezo ambayo yalifuatiwa na uamuzi wa kuondolewa kwa muswada wa sheria ya mapitio katiba kuondolewa katika ratiba ya mkutano wa nne wa bunge kinyume mipango iliyotangazwa awali.

Pia, nililieza bunge kuwa serikali inapaswa kutoa kauli bungeni ya kumaliza mgawo wa umeme unaondelea na kuathiri taifa ikiwemo wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam. Nililieleza bunge kuwa wananchi wanakusudia kuandamana hivyo majibu kwa Waziri Mkuu Pinda kupitia maswali ya papo kwa papo yangeweza kueleza ufumbuzi wa suala hilo.

Kadhalika, nililieleza bunge kuwa vyombo vya habari vimewanukuu wakuu wa wilaya wakitoa maelekezo kwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kuwabagua wanafunzi kwa misingi ya vyama vyao wakati wa kuwarejesha chuoni kwa kuanza kuwarejesha kwanza wanachuo ambao ni wanachama wa CCM. Aidha nilidokeza kuwa kauli hiyo ilifuatiwa na waraka wa Wizara ya Elimu na Ufundi ambao umetoa maelekezo maalum ya ubaguzi kwa bodi ya mikopo na UDOM. Matokeo ya maelekezo hayo ni UDOM kutoa taarifa yenye masharti magumu ya kuwataka wanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Cha Sanaa na Sayansi za Jamii waliosimamishwa masomo kuripoti chuoni huku ikiwabagua wanafunzi 15 ambao wametajwa kwa majina.

Kutokana na masuala hayo na mengine toka kwa wabunge wengine yanayohitaji majibu toka kwa Waziri Mkuu Pinda kama kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni niliomba muongozo kwa mwenyekiti ili kanuni ya 30 (6) itumike kuagiza utaratibu wa kuwezesha shughuli ya maswali kwa waziri mkuu kuweza kuendelea kama kawaida.

Nilitaka muongozo kanuni za bunge zisipindishwe kumlinda Pinda kwa kuwa kifungu cha 38 (5) kinaeleza bayana kwamba hakutakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu iwapo hayupo kwa sababu maalum na kwamba siku ya leo ya alhamisi tarehe 30 Juni 2011 Waziri Mkuu Pinda alikuwepo bungeni katika kipindi husika cha maswali. Hata hivyo, pamoja na maelezo hayo Mwenyekiti Simbachawene aliendelea kutoa miongozo yenye kukiuka kanuni za bunge hususani vifungu 5(1), 7(3), 30(6), 38(5), 150 (1) na 150 (4).

Kwa upande mwingine, naelewa kwamba kanuni za bunge zinaelekeza hoja ambazo mbunge anaweza kuziwasilisha hivyo, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Pinda kwa kuwa kanuni zilipindishwa kuondoa kipindi cha maswali kwake atumie kipindi cha majumuisho ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kesho tarehe 1 Julai 2011 kutoa majibu ya kina kuhusu kauli zake juu ya mchakato wa katiba mpya, kauli ya serikali kumaliza mgawo wa umeme na hatma ya wanafunzi 15 wa UDOM waliobaguliwa katika taratibu za kurejeshwa chuoni.

Aidha, Waziri Mkuu Pinda atambue kwamba wanachuo wengine nao wanamalalamiko ya kupewa muda mfupi wa kurejea chuoni na masharti magumu ya malipo ambapo wanapaswa kurejea tarehe 2 na 3 Julai pekee na kutangaziwa kuanda mtihani tarehe 4 Julai 2011 siku moja baada ya kurejea; na kwamba wanafunzi ambao hawatafika na hati za malipo hawatapokelewa.

Natoa rai kwa Waziri Mkuu Pinda kuzingatia ukweli kwamba mgogoro wa wanachuo wa UDOM ulianza mwaka 2009/2010 wakati wanafunzi walipotumia njia zote za kawaida za mawasiliano na serikali na utawala wa chuo hicho kutaka madai yao ya kutaka serikali kuingiza kozi ambazo hazikuwa katika mpango wa mafunzo kwa vitendo (PT-Practical Training).

Baada ya mgomo wa wanafunzi wa tarehe 21 Disemba 2010 alikwenda Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Shukuru Kawambwa akiongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Nahodha na watendaji wakuu wa mamlaka zinazohusika na elimu ya juu walifika katika Chuo hicho kuzungumza na wanachuo na kubainika kwamba wanachuo wenye kusomea shahada za Utawala wa Biashara (BBA) na Sanaa ya Lugha (BA LT) ambao kutokana na kozi zao kwa kadiri ya Prospectus walipaswa kwenda mafunzo kwa vitendo lakini serikali ilikiri kutotimiza wajibu wa kuwaingizia fedha kama ilivyohitajika. Pia, maelekezo yalitolewa kwa kozi ambazo hazijawekewa mafunzo kwa vitendo (field) kwenye bajeti zifikazo 14 ziwekewe bajeti na menejimenti iliridhia kazi hiyo kwa kutoa barua kwa wanafunzi tarehe 3 Januari 2011 na kuandaa bajeti kupitia kikao cha bodi kilichoketi tarehe 26 Januari 2011.

Hata hivyo, baadhi ya watendaji wa serikali walichochea mgogoro katika Chuo hicho kutokana na barua ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwamba haijatoa idhini na mafunzo kwa vitendo na hivyo Seneti ya UDOM ilikaa tarehe 8 Juni 2011 na wanachuo kuelezwa kwamba hakuna fedha zitazoombwa Hazina kwa ajili ya wanafunzi kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kama serikali ilivyoahidi awali kupitia mawaziri na taarifa kufika kwa Waziri Mkuu.

Hali hiyo iliwachochea wanavyuo kutaka kuja Bungeni kukutana na Mawaziri husika ili kuwelezwa hatma yao lakini polisi wa kutuliza ghasia (FFU) waliwavamia njiani na kutumia nguvu kubwa kuwazuia kwa kupiga mabomu ya machozi, kuwapiga kwa vitako vya bunduki na kuwaumiza vibaya mathalani Malambo Ngata aliyevunjwa mguu wa kushoto. Pia, polisi ilikamata viongozi wa Serikali ya Wanafunzi na wanachuo wengine na kuwaweka rumande kuanzia tarehe 10 Juni 2011 hali iliyochochea wanafunzi wengine kuanza mgomo mpaka uongozi wa Chuo ulipofunga Chuo tarehe 16 Juni 2011.

Uamuzi huu ulitolewa kwa ghafla huku wanafunzi wakipewa muda mchache wa kuondoka chini ya ulinzi wa vyombo vya dola hali ambayo imesababisha wengi ikiwemo vijana wa kike kukwama Dodoma. Katika majumuisho ya Bajeti ya Wizara yake, Waziri Mkuu Pinda atoe tamko la kutekeleza ahadi ya Serikali ya kutoa fedha kwa wanafunzi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na pia kuwarejesha wanafunzi kuendelea na masomo bila masharti magumu ikiwemo kufuatilia hatma ya wanafunzi waliofukuzwa bila taratibu zinazohitajika kufuatwa.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
30 Juni 2011; Bungeni, Dodoma