Thursday, July 7, 2011

Kuhusu uwajibikaji na bajeti ya ofisi ya Rais

Niliyozungumza bungeni tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala bora na Uhusiano na Uratibu)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Ninaomba Mwenyezi Mungu aniongoze na kunilinda, nitakapotoa mchango huu kwa siku ya leo. La kwanza, niseme kwamba, siungi mkono hoja iliyoko mbele yetu. Jana Hotuba iliposomwa wakati wa mapumziko nilipigiwa simu na baadhi ya Wananchi kutoka kwenye Jimbo langu; wazee, akina mama na vijana, wakanieleza kwamba, nisiunge mkono hoja hii iliyoko mbele yetu. Kwa sababu moja; Watumishi wa Umma wamepewa ahadi hewa, tafsiri inayojaribu kujengwa ni kama vile mishahara itaongezeka kwa asilimia 40, kitu ambacho sicho.

Mheshimiwa Spika, fungu lililozungumzwa la takriban shilingi trilioni 1.2 na kadhalika, limehusisha vitu vingi sana; wafanyakazi wapya, uhamisho wa wafanyakazi na mambo mengi sana, si kwa ajili ya mishahara peke yake. Kwa hiyo; ni vizuri kwanza wakati wa kuhitimisha hoja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), awaeleze Watanzania hali halisi ilivyo. Pamoja na majadiliano yanayoendelea, uzoefu wa nchi mbalimbali umeonesha kuwa, kima cha chini cha mshahara na kima cha juu cha mshahara siyo siri. Kwa hiyo, isemwe wazi kabisa ili pengo lijulikane na hali halisi ijulikane.

La pili, Bajeti hii inahusu ofisi nyeti kuliko zote katika nchi yetu, Ofisi ya Rais. Ofisi ya Rais kwa mujibu wa Katiba pamoja na kasoro zake, ibara ya 33 mpaka ibara ya 50, imeeleza ukuu wa Taasisi ya Rais, mamlaka makubwa aliyonayo Rais kama Amiri Jeshi Mkuu, kama Mkuu wa Shughuli zote na Kiongozi Mkuu wa Serikali, kama Mwajiri na Mwajiriwa Mkuu; ni mamlaka makubwa sana. Kwa hiyo, utumishi wote wa umma; iwe Watumishi wa Kawaida, Mawaziri au waziri mkuu, wote wanafanya kazi tu kwa niaba ya kumsaidia Rais; tafsiri yake ni nini?

Upungufu wowote ule tunaoweza kuuzungumza wa utekelezaji wa bajeti iliyopita, wa kuwajibika kwanza kabisa ni Ofisi ya Rais. Iwe ni upungufu wa TAKUKURU, mgao wa umeme na kadhalika, ndiyo Ofisi Kuu. Siungi mkono kwa sababu taarifa ya utekelezaji ya mwaka mzima, lakini ikiwa ni miezi sita toka Serikali iingie madarakani, haileti matumaini ya Ofisi hii kusimama ipasavyo kushughulikia kero za msingi za Wananchi.

Mheshimiwa Spika, sababu ya tatu, halafu nitajielekeza kwenye vifungu vya bajeti iliyoko mbele yetu; nimepitia Hotuba ya Waziri, ukurasa 61, linazungumzwa jambo linalogusa Wananchi wa Jimbo ambalo wamenituma kuwawakilisha. Kifungu cha (4) pale kinasema: “Mpango wa Urasimishaji katika miji imetajwa vilevile eneo la Kimara Baruti, Dar es Salaam, kwenye Mradi wa MKURABITA. Sasa kama Chombo cha Serikali kinaweza kuzungumza kwa mwaka mzima wa bajeti kufanya urasimishaji kwenye mtaa mmoja tu, Dar es Salaam, Kimara Baruti, mtaa tu siyo Kata wala siyo Jimbo; tupo kwenye hali mbaya kama Taifa na tupo kwenye hali hii kwa sababu ya kukosa vipaumbele.

Mheshimiwa Spika, ukiingia kwenye Kitabu cha Bajeti ya Maendeleo, Fungu 30, ukurasa wa 33, MKURABITA imetengewa shilingi bilioni tatu peke yake mwaka huu wa fedha wakati mwaka uliopita wa fedha ilitengewa shilingi bilioni sita. Tafsiri yake ni kwamba, tunarudi nyuma kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Sasa ningependa kupata ufafanuzi kuhusu hili suala la MKURABITA, urasimishaji eneo la Kimara Baruti. Kwa sababu nina ushahidi wa barua ambayo ipo Ofisi ya Rais (Ikulu), ya Kampuni inayoitwa Twiga Chemical Industry Limited, ikisema kwamba, Wananchi wa Kimara Baruti, eneo la ekari nane waondolewe. Sasa hili jambo kwa sababu tunajadili kuhusu TAKUKURU na Usalama wa Taifa, hapa ndiyo nafasi yao sasa. Hili jambo ni ufisadi mkubwa, Kampuni hii imelipwa shilingi bilioni tatu au milioni 3,000 fedha za umma kama fidia kwenye mazingira yasiyoeleweka kuhusiana na ardhi hii hii kinyume na agizo la Kamati ya Deni la Taifa katika kikao chake cha mwaka 2006 na inakusudiwa kulipa pesa nyingine shilingi bilioni 4.5. Sasa kama tuna pesa nyingi za namna hii za kulipa; kwa nini hatuzipeleki MKURABITA wakafanya urasimishaji wa Jiji zima la Dar es Salaam?

Ningeomba TAKUKURU na Usalama wa Taifa wachunguze mazingira ya malipo kwa Kampuni hii ya Twiga na tuelezwe ni kigogo gani ndani ya Serikali yuko nyuma ya Kampuni hii ya Twiga Chemical Industry. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaomba sasa nijielekeze kwenye vifungu vya bajeti hii, ambayo tunayo hapa na tunaipitia. Nimezungumza kuhusiana na Fungu la 30 - Ofisi ya Rais. Sasa ukilinganisha Kitabu cha Maendeleo na Kitabu cha Matumizi ya Kawaida, Ofisi ya Rais kwenye Matumizi ya Kawaida, imetengewa pesa nyingi kweli kweli, yatakuja kwenye takwimu kuliko matumizi ya maendeleo. Sasa kitu ambacho kinanifanya nisiunge mkono Bajeti hii mpaka nipewe maelezo ya kina sana ni kasma mojawapo, kasma ndogo inayoitwa Matumizi ya Kitaifa. Kwanza, ninaomba wakati Waziri atakapohitimisha hoja, alieleze Bunge kwa nini baada ya kuwasilisha Randama ya Wizara yake, hatujapewa nakala, kwa sababu tungepewa nakala, tungeingia ndani ya vifungu? Mimi ninafahamu kwenye kasma hii, shilingi bilioni 135 hazina mchanganuo, zinaitwa tu Matumizi ya Kitaifa. Halafu Bunge tunatakiwa tupitishe Matumizi ya Kitaifa Ikulu, shilingi bilioni 135.

Mheshimiwa Spika, ninataka atueleze fedha za bajeti iliyopita zilitumikaje kwa sababu tunaelewa fungu hili ndilo ambalo linatumika ukisikia safari nyingi sana za Rais nje ya nchi? Msafara mmoja wa Rais kwenda nje unagharimu kidogo sana ni shilingi milioni 50 na wakati mwingine msafara unakwenda mpaka shilingi milioni 200 na safari ni nyingi kweli kweli. Hatukatai Rais kusafiri; Mwalimu Nyerere, alikuwa anasafiri, wazee wangu walioko hapa wanajua kwamba, Mwalimu alikuwa anakwenda Marekani kipindi chote cha Urais wake, alikuwa akienda Marekani basi anakwenda kwenye Kikao cha Umoja wa Mataifa (UN). Kama amekwenda kwa shughuli za kawaida, State Visit Marekani, Mwalimu Nyerere alikwenda Marekani mara mbili au tatu kipindi chote. Safari nyingine ni za kwenda Umoja Mataifa.

Mheshimiwa Spika, tungekuwa na muda tungeingia ndani zaidi Zambia, nina kabrasha hapa la Bajeti ya Zambia.

(Hapa Mheshimiwa Mbunge alionesha kabrasha la Bajeti ya Zambia)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Zambia, Bajeti inaonesha kwa kina mpaka Rais anakwenda safari ngapi? Ninachosema, kupanga ni kuchagua, tupunguze kwenye fungu la shilingi bilioni 135 tuongeze pesa kwenye MKURABITA, tuwasaidie Watanzania waweze kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumza kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa na TAKUKURU. Ningeomba pamoja na kukimbizana na mambo mengine haya, Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya TAKUKURU, watusaidie maeneo ambayo yana kero zaidi kwa Wananchi. Kule ninapotoka, Jimbo la Ubungo, kero kubwa ni maji; sasa mtu atashangaa Usalama wa Taifa na TAKUKURU wanahusika vipi na maji? Kule kuna kero ya maji, kwa sababu kuna rushwa kwenye mtandao mzima wa maji na Mradi wa Maji uliopo pale wa mabomba ya Wachina, uliwekwa ovyo ovyo; rushwa; wizi.

Mimi ninatarajia kwamba, Vyombo vya Dola, pamoja na kazi za kawaida za Mawaziri, TAKUKURU ikachunguze mambo haya ya maji. Kule tunakerwa kweli na migogoro ya ardhi, wengine wanasema sasa TAKUKURU inahusika na Usalama wa Taifa wanahusika vipi na ardhi?

Mheshimiwa Spika, Usalama wa Taifa ulikuwa na mwakilishi ndani ya Kamati iliyoundwa ya Kuchunguza Migogoro ya Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam. Kulikuwa na Mjumbe wa Usalama wa Taifa. Ninataka kujua, baada ya hapo, pamoja na kwamba Ripoti imekuwa ni ya siri na inapaswa kuwa wazi; mapendekezo yaliyokuwa mle ndani ya Ripoti ni pamoja na hatua ambazo Usalama wa Taifa na TAKUKURU wanapaswa kuzichukua. Ninataka kujua kwenye mwaka wa fedha uliopita, Idara hizi zimefanya nini kushughulikia kero hizi za Wananchi wa kawaida sana.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba; ninaamini kwamba, ili tuendelee, pamoja na yale aliyoyazungumza Mwalimu, tunahitaji misingi mikubwa miwili, kwa maana ya kuwa na maono (Vision) na kuwa na maadili (Values). Sasa hii inatutaka tutoke kama Taifa kuwa na utamaduni wa haya mazoea ya ufisadi na tuanze kuwa na utamaduni wa uwajibikaji. Binafsi, nilisema na nirudie kusema hapo kwamba; kwa hali iliyofikia ya mgao wa umeme hivi sasa; ni wazi kwamba, Waziri wa Nishati na Naibu wake kimsingi nilisema mwezi Februari na ninarudia tena leo, wanapaswa kujiuzulu.

Kujiuzulu kwao hakutatoa tija zaidi ya tija ya uwajibikaji kwa Taifa kama Ofisi ya Rais, haitafanya maamuzi magumu. Tarehe 15 Februari, 2011, Baraza la Mawaziri lilikaa likapitisha maamuzi wakati ule, mimi nikatahadharisha kwamba, haya maamuzi yasiposimamiwa vizuri, tutakuwa na mgao; na Rais tarehe 1 Aprili 2011; na ndiyo maana nimesema Rais aanze kwanza kusafisha Ikulu. Kuna watu wanamshauri Rais vibaya, Rais akatoa Hotuba kwa Taifa kwamba, Julai, megawati 260 zitafanya kazi. Hii ni Julai; kuna mgao na kuna mgao mkubwa zaidi unakuja kwa sababu ya ufisadi kwenye Sekta ya Umeme na kwenye sekta ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasema hapa panahitaji uwajibikaji wa pamoja, siyo Wizara ya Nishati tu. Nimesoma kauli ya leo ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda na nilitarajia kauli ile ingetolewa Bungeni; Waziri Mkuu, hajatoa kauli Bungeni kuhusu mgao wa umeme. Kauli aliyoitoa Dar es Salaam kwenye matembezi ya Maonyesho Saba Saba siyo ya Wizara ya Nishati, siyo TANESCO, inalipotosha Taifa vilevile. Katika hatua tuliyofikia hivi sasa, ninahitaji kwenye majumuisho hayo ya Hotuba ya Rais, tupate kauli kutoka Ofisi ya Rais, kuhusu mgao wa umeme.

1 comment:

william said...

Serikali ya Tz ina kichwa cha kuku ndo maana wanasahau mapema mambo wanayosema kwa wananchi.Kuku ndo anasahu mara moja unapokuwa umemfukuza kutoka eneo hili, atarudia saa ileile.
Hii ni ishara tosha kwamba AHADI ZA JK zote ni uongo mtupu.Hawa wanaomshauri raisi wasilaumiwe sana kwani hali halisi ya umeme Kikwete anaifahamu na hahitaji kushauriwa bali kuchukua hatua za dhati.haiingii akilini kwamba Kikwete haoni mateso ya wananchi wanayoyapata juu ya mgao wa umeme.