Saturday, July 30, 2011

Salam za Mshikamano kwa Mdahalo wa Katiba

Nikiwa bungeni Dodoma nimefuatilia kupitia vyombo vya habari mdahalo wa katiba ambao umefanyika Ubungo Plaza. Natoa salamu za mshikamano na pongezi kwa waandaaji, watoa mada na washiriki wa mdahalo huu wenye kuchangia katika mjadala wa katiba mpya.

Kupitia kongamano hilo maoni mbalimbali ya maudhui hususani masuala ya muafaka wa kitaifa, ardhi na rasilimali za nchi, jinsia, muungano, haki za binadamu ikiwemo za makundi mbalimbali katika jamii, mgombea binafsi, bunge, mahakama, wananchi kuwa na mamlaka juu ya dola, maadili ya taifa nk

Kongamano pia limejadili masuala mbalimbali kuhusu mchakato wa katiba ikiwemo kasoro katika muswada wa kuandikwa kwa katiba mpya, muundo wa vyombo vitavyoratibu mchakato wa katiba mpya, haja ya kuwa na mkutano mkuu wa katiba, nafasi ya bunge katika mchakato wa katiba na umuhimu wa kupunguza mamlaka ya Rais katika mchakato wa katiba nk.

Hata hivyo, imezungumzwa katika mdahalo kuwa muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba utawasilishwa katika mkutano wa nne wa bunge unaoendelea hivi sasa. Natoa tahadhari kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuzingatia kuwa muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba umeondolewa kinyemela katika ratiba ya mkutano wa nne wa bunge, kilichobakishwa kwenye ratiba ni semina tu ya wabunge kuhusu muswada husika.

Hivyo, pamoja na kujadili kuhusu maudhui ni vizuri katika hatua ya sasa mkazo ukawekwa katika kujadili mchakato wa katiba mpya hususani kuhusu hatma ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba. Hii ni kwa sababu maoni kuhusu maudhui hayatazingatiwa kikamilifu ikiwa sheria ya kusimamia mchakato wa katiba mpya itacheleweshwa na itatungwa sheria mbovu.

Ikumbukwe kwamba hati ya dharura kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ilipoondolewa katika mkutano tatu wa Bunge mwezi Aprili serikali iliahidi muswada huo utajadiliwa katika mkutano wa nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa baada ya kupata maoni ya wananchi. Serikali haikutimiza ahadi ya kuwashirikisha wananchi kwa upana na uwazi kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba wala ahadi ya muswada huo kujadiliwa katika mkutano wa nne wa Bunge kama ilivyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Aidha wakati wa mkutano wa nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani akijibu maswali alieleza kwamba serikali imeshawasilisha kwa bunge marekebisho ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na Spika wa Bunge Anne Makinda akaongezea majibu kuwa sasa muswada huo uko kwa bunge ambalo ndilo litakaloamua hatma ya muswada husika.

Marekebisho ambayo serikali imeyawasilisha mpaka hivi sasa pamoja na kuyatafsiri kwa lugha ya Kiswahili (sio kuutunga upya) hayajazingatia hoja za msingi zilizotolewa na wananchi na wadau mbalimbali wakati walipoukataa muswada wa awali wa sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011 (The Constitutional Review Act 2011) uliochapwa katika gazeti la serikali toleo No. 1 Vol. 92 la tarehe 11 Machi 2011 na kuwasilishwa bungeni mwezi Aprili 2011.

Natoa mwito wa Kituo Cha Sheria za Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuelekeza nguvu katika hatua ya sasa kutaka muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba ulioandikwa upya kuwekwa hadharani hivi sasa. Pia kuitaka Serikali na Bunge kuzingatia kwa ukamilifu hatua zinazohusika kwa mujibu vifungu vya 80, 83 na 84 vya Kanuni za Kudumu za Bunge baada ya kuondolewa kwa hati ya dharura ikiwemo kutoa ufafanuzi kuhusu utata uliopo hivi sasa kuhusu muswada husika. Muswada mbovu wa sheria ya mabadiliko ya katiba utatuletea katiba bomu isiyo na uhalali wa kukubaliwa na umma na kuongeza mpasuko katika nchi badala ya kuwa na muafaka wa kitaifa na misingi muhimu ya uwajibikaji kwa ustawi wa wote.

John Mnyika (Mb)
29/07/2011

1 comment:

Helen Kijo -bisimba said...

Ndugu Mnyika Asante san kwa mawazo muhimu uliyoyaelekeza kwa Kituo cha sheria na wadau wote wa masuala ya Katiba Mpya nchini. Ni kweli kabisa kama tukishindwa kuhakikisha kuwa sheria inayoelekeza njia ya kufikia katiba mpya inakua nzuri tutaishia kukutnana na katiba Bomu. Ninachoshindwa kuelewa hasa nini kinachogomba kw jambo ambalo ni wazi kabisa. Hebu tujifunze kwa wenzetu nchi za Jirani tuikianzia na Afriaka Kusini ambao walitoka mahali pa kugumu sana lakini walipokubaliana wote na nikinukuu maneno ya Aliyekua Raisi wakati huo Ndugu Nelson Mandela alisema katiba mpya ya Afrika kusini imeandikwa kutoka kwenye viwanja vya michezo,makazini,mashambani, kwenye vyuo vya elimu,waliko watoto na vijana,na pia waliko wanawake wa nchi wanaodai kwa dhati usawa, na pia waliko wasio na ajira, na watu wenye ulemavu wakitafuta haki zao katika jamii(Nelson Mandela's Speeches2003:76).Hii inaonyesha mchakato uliotumika si suala la watu wachache ni suala la kila mtu na hii itawezekamna tu iwapo Sheria husika itaweka huo uwezekano. Huko Uganda ilikua vivyo na Wenzetu Kenya ilibidi wachukue miaka ishirini kwa vile msingi haukua mzuri mwanzoni .Yote haya yangekua mafundisho mema kwetu sote na tungeweza kuanza mchalkato vizuri kwa vile nia ni kuboresha hali namaisha ya Watanzania wote. Kial la heri wote na hakika mshikamano ni muhimu.