Friday, September 7, 2012

CHADEMA wamtaka Kikwete awasimamishe vigogo Polisi

na Nasra Abdallah

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwasimamisha kazi vigogo wote wa Jeshi la Polisi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa tata kuhusu mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi, kujiuzulu nyadhifa zao na kupisha uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mahusiano na Habari wa chama hicho, John Mnyika, aliwataja vigogo hao wa polisi kuwa ni Kamanda wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja na RPC wa Iringa, Michael Kamhanda, ambao katika nyakati tofauti walidai kuwa Mwangosi alifikwa na mauti baada ya kuchoropoka kutoka kundi la wafuasi wa CHADEMA na kukimbilia mikononi mwa polisi na ghafla kulitokea mlipuko wa bomu la machozi uliosababisha kifo cha mwandishi huyo jambo ambalo sio la kweli.

Mnyika alisema maneno hayo yanatofautiana na ukweli na kuyaita kuwa ni ya uongo, ikizingatiwa kwamba picha mbalimbali zimeonesha kilichotokea, ikiwemo waandishi waliokuwemo eneo la tukio kutoa ushuhuda wao.

Kutokana na hali hiyo, Mnyika alisema ipo haja ya vigogo hao kung’oka na kupisha uchunguzi ili uweze kufanyika kwa haki.

Aliongeza kuwa rais atumie madaraka yake, askari saba wanaoonekana katika picha wakamatwe haraka na kuhojiwa ni nani alifyatua bunduki kwa namna gani na vigogo gani walitoa amri.

Kwa mujibu wa Mnyika, polisi imekuwa na tabia ya kukamata raia wanaokuwa eneo la tukio pindi kunapotokea mauaji kama hayo, hivyo ni wakati sasa wa polisi wanaoonekana katika picha wakimshambulia marehemu Mwangosi nao kukamatwa.

Aidha, alilitaka Jeshi la Polisi lisitumie vibaya fedha za walipa kodi kwa kuchunguza nani alihusika na mauaji hayo, wakati wauaji wanaonekana wazi kwenye picha, hivyo kinachotakiwa na wao kuhojiwa nani aliwaamuru kufanya mauaji hayo ya kinyama.

Alisema uchunguzi huo hauwezi kufanywa na polisi na badala yake unatakiwa kufanywa na chombo huru cha mahakama ambapo rais anapaswa kutumia sheria ya vifo kifungu cha tatu na kuwezesha kuundwa kwa chombo cha kimahakama ili kuweze kufanyika uchunguzi huru wa nyuma ya pazia mambo yote yaliyotokea na ukweli kuweza kudhihirika.

Pia Mnyika alitumia fursa hiyo kukanusha kuwa chama chao kimekuwa kikikaidi utawala wa sheria.

“Kuna ushahidi tosha wa matukio ya CHADEMA kuwa katika mikutano ya ndani ya chama ambapo polisi ndio walifika na kufyatua mabomu… hata pale watu walipoamua kutawanyika waliendelea kufyatua mabomu hayo hadi ndani ya ofisi zao,” alisema na kuongeza kuwa polisi wanaonesha wazi kuwa ndio wenye vurugu.

Alisema kama kweli polisi ilikuwa na dhamira ya kweli ya kuzuia maandamano ya CHADEMA kwa kisingizio cha sensa, ingemkamata Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Khalid Mohamed Bilal, akiwa amezindua mkutano wa hadhara Bububu ambao wala haukutawanywa na polisi kama ilivyokuwa kwa chama chao ambao wao walikuwa katika mkutano wa ndani.

Katika hatua nyingine, Mnyika amewataka wanachama wao kuchukua tahadhari hasa baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa kutoa taarifa kuwa Chama Cha Mapinduzi kinahusika na kuingiza silaha za kivita na kuwafundisha vijana mafunzo ya kivita kwenye makambi, ambapo wanataka kuigeuzia kibao CHADEMA na kupandikiza watu wao kwenye operesheni za chama hicho ili waonekane ndio wakorofi.

Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi na wanachama watakaokuwa kwenye operesheni hizo kuchukua hatua pale watakapowatilia shaka watu hao.

Pamoja na hilo, Mnyika alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amesitisha ziara yake nchini Marekani na alikuwa akitarajiwa kuwasili jana ili kusimamia na kuendeleza mashauriano na baadae kuja na tamko la hatua gani wameamua kuzichukua endapo serikali haitaweza kushughulikia maagizo ambayo wameyatoa awali.

Kauli ya mwisho ya marehemu

Mnyika alisema anakumbuka kauli ya mwisho ya Marehemu Mwangosi, aliyoongea muda mfupi baada ya kutoka katika mkutano wa waandishi na Jeshi la Polisi mkoani Iringa akiwemo ofisa habari wa chama hicho, kwamba polisi walianza kuwatahadharisha waandishi wa habari na kuwaambia kuna mambo yatawakuta siku hiyo.

“Baada ya tamko hilo, marehemu aliwajibu polisi na kuwaambia kwamba kama ameahidiwa kuishi milele ataogopa kufa, lakini kwa kuwa hajaahidiwa kuishi milele hataogopa kufa kwa kuwa akifa ataishi milelele kaburini… na hatimaye baaada ya muda mfupi akauawa kinyama,” alisema.

Mnyika alisema kwa kauli hiyo pamoja na kazi zake nyingine alizozifanya za kihabari, marehemu alionesha ni mwandishi aliyesimamia ukweli na hata wakati mwingine kuhatarisha maisha yake.
Katika mazingira hayo, alisema pamoja na marehemu kutangulia mbele ya haki, ipo haja ya kupewa tuzo kwani kuna watu kama yeye ambao wameshatangulia hadi leo na kuna tuzo zinazotolewa kwa ajili yao kama njia mojawapo ya kuwaenzi.


Mnyika ametoa wito kwa wanahabari kutoa tuzo hiyo yenye jina la marehemu, na kuongeza kuwa kwa kuwa aliacha watoto na mjane, ipo haja ya kuhakikisha wanapata huduma ikiwemo watoto wake kuendelea kusoma na kama chama wapo tayari kusaidia kwa hali na mali ili kuweza kutimiza ndoto zao na kuthamini mchango wake.

Chanzo:
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=40201

No comments: