Sunday, September 16, 2012

MAJARIBIO YA USAFIRI WA TRENI DAR ES SALAAM NI HATUA MUHIMU, TRL NA RAHCO WANAPASWA KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA ZAIDI KWA KUSHIRIKIANA NA HALMASHAURI KAMA NILIVYOZIELEZA BUNGENI AGOSTI 2012 KUHUSU MAENEO YA MABIBO NA UBUNGO

Tarehe 10 Septemba 2012 majaribio ya usafiri wa treni katika jiji la Dar es salaam yalifanywa kuanzia Stesheni mpaka Ubungo Maziwa. Kufuatia majaribio hayo kauli kuhusu changamoto zilizopo ilitolewa na Naibu Waziri Dkt Charles Tizeba na maoni mbalimbali yametolewa na wadau wengine kwenye vyombo vya habari tarehe 11 na 12 Septemba 2012.

Kwa nafasi yangu ya Mbunge wa Ubungo katika Jiji la Dar es salaam natambua kuwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika suala ambalo tangu mwaka 2010 kwa nyakati mbalimbali nimeihoji Serikali kutaka utekelezaji wa haraka kwa kuzingatia kuwa suala hilo lilikuwa kwenye mipango zaidi ya miaka 10 iliyopita hata hivyo hatua zaidi na za haraka zinahitajika kwa huduma ya usafiri wa reli kuanza tarehe 1 Oktoba 2012 na kuweka mazingira bora ya usafiri huo kupunguza msongamano.

Natoa mwito kwa Waziri na Naibu Waziri wa Uchukuzi kuzingatia mchango wangu nilioutoa bungeni mwezi Agosti 2012 ili kuhakikisha kwamba TRL na RAHCO zinashirikiana kwa karibu na Halmashauri za Jiji la Dar es salaam kushughulikia changamoto zinazohusu uvamizi wa maeneo ya hifadhi za njia za reli na ufinyu wa eneo la kugeuzia vichwa vya treni sehemu ya Ubungo Maziwa.


Aidha, Wizara ya Uchukuzi iharakishe mchakato wa kushirikiana na sekta binafsi kuhusu uwekezaji katika mradi wa maegesho ya magari eneo Ubungo ikiwemo katika eneo lililotengwa la ekari nne katika Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji ili wenye magari wanaokwenda Stesheni kuweza kuegesha magari yao na kupunguza msongamano wa magari kuelekea katika ya Jiji.

Pia, kwa kiwango cha fedha kiasi cha shilingi bilioni 4.75 zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 zitolewe zote mapema ikiwa ni sehemu ya matumizi vipaumbele na zielekezwe katika pamoja na mambo mengine kuboresha hali na hadhi ya mabehewa pamoja kurekebisha mataruma ya reli yakae pembe mraba na reli (squaring) ili kuongeza kasi ya treni hiyo kuwezesha muda wa safari kati ya stesheni ya Dar es salaam na Ubungo Maziwa kuweza kuwa dakika 35 tofauti na kasi ndogo iliyodhihirika tarehe 10 Septemba 2012 wakati wa majaribio.

Ikumbukwe kuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kati ya masuala ambayo niliwaahidi wananchi kuwa nitayaunga mkono na kuisimamia Serikali kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari ni pamoja na kuanzishwa kwa usafiri wa treni kuelekea katika ya jiji.

Mara baada ya kuchaguliwa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi mwaka 2011 niliitaka Serikali kuchukua kutoka katika fedha zilizotengwa kwenye usafiri na uchukuzi wa reli kufanya tathmini na kuanza ukarabati wa njia ya reli ya kutoka stesheni hadi Ubungo Maziwa.

Wizara ya Uchukuzi ilijibu mwaka 2011 kuwa imekubaliana na mchango huo na kuahidi kupitia Shirika la Reli (TRL), Kampuni ya Miliki ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kuwa imefanya tathmini ya gharama za kuanzisha huduma za reli na kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Izingatiwe kuwa bajeti ya utekelezaji imeongezwa zaidi katika mwaka wa fedha 2012/2013 ambayo inapaswa kufuatilia kwa karibu na mamlaka zote zinazohusika pamoja na wadau wote muhimu ili kuhakikisha ubora na ufanisi.

John Mnyika (Mb)
13/09/2012


No comments: