Wednesday, October 10, 2012

KIJANA AU MDAU WA MASUALA YA VIJANA WIKI YA VIJANA IMEANZA LEO; UMEPANGA KUFANYA KAZI GANI MOJA KWA MUSTAKABALI WA VIJANA NA TAIFA?


Kuanzia leo Oktoba 8 mpaka 14 vijana bila kujali itikadi tunapaswa kuungana kote nchini kuadhimisha wiki ya taifa ya vijana. Hata hivyo, toka wiki hii ilipoanzishwa na Serikali mwaka 2003 imekuwa ikiadhimishwa bila mwitikio wa kiasi cha kutosha katika ngazi mbalimbali isipokuwa katika maeneo ambayo wiki hii imekuwa ikiadhimishwa kitaifa kwa kufanya maonyesho ya namna mbalimbali. Hivyo, nia ya taarifa hii ni kuhimiza vijana, serikali na wadau mbalimbali ili maadhimisho ya mwaka huu yawe na hamasa na maana zaidi kwa maisha ya vijana wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.

Aidha, maadhimisho ya kila mwaka ya wiki ya vijana yamekuwa yakichanganywa pamoja na kilele cha mbio za Mwenge na Maadhimisho ya siku ya Mwalimu Nyerere kitaifa. Matokeo yake wiki ya vijana imekuwa ikifunikwa na shamrashamra za mbio za Mwenge na hatimaye kupoteza malengo ya msingi ya kushughulikia masuala yanayowagusa vijana moja kwa moja.

Pia zaidi ya maadhimisho yanafanyika kitaifa Shinyanga ni vyema mkazo ukawekwa katika kufanya maadhimisho katika ngazi mbalimbali hususani wilayani. Hivyo maafisa maendeleo wa vijana wa wilaya walau mwaka huu wajitokeze kutembelea vikundi vya vijana, kuratibu matukio ya asasi za vijana na kuhamasisha mijadala ya vijana kuhusu mustakabali wao na taifa kwa ujumla.

Natoa mwito kwa vijana nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya wiki ya taifa ya vijana ya mwaka huu iliyoanza  Oktoba 8 ambayo kilele chake kitafikia Oktoba 14. Kila kijana wa Tanzania afanye walau kitu kimoja katika wiki hii kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya jamii-kama ni kusaidia wasiojiweza, kufanya usafi wa mazingira, kufanya majadiliano kuhusu mustakabali wa vijana na taifa, kuonana na viongozi kuzungumza nao kuhusu maendeleo katika maeneo yao kuhusu masuala ya elimu, ajira, afya, ukuzaji wa vipaji vya vijana, michezo, ushiriki wa vijana katika uongozi na mengineyo.

Wiki hii ni muhimu kwa sababu kwa upande mmoja, vijana ndio kundi linaloathirika zaidi na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojiri nchini kwetu na duniani kwa ujumla. Kwa upande mwingine vijana ndio chachu ya mabadiliko katika taifa lolote duniani kutokana na nguvu, ubunifu, na uwingi wetu.

NB: Maelezo haya kwa sehemu kubwa yalikuwa sehemu ya Taarifa kwa Umma niliyoitoa tarehe 5 Oktoba, nayasambaza leo kuwakumbusha kwa ajili ya hatua kila mmoja kwa nafsi na nafasi yake.

Maslahi ya umma kwanza.

1 comment:

Unknown said...

je Hii ni kweli, watoto wa vigogo waliopita UVCCM ngazi ya taifa ni DICKSON MEMBE, FREDY LOWASA, RIDHIWANI KIKWETE, ASHURA HUSSEN MWINYI, BENY SAMWEL SITA, DEBORA MWANDOSYA, IREN PINDA, FELSTER NDUGAI, CHRISTOFER NDEJEMBI, SHARIFER BILALY, HAWA KIGODA, JUDITH MUKAMA NA JALOME MSEKWA.Kama ni kweli basi Nchi hii imekwisha. Inatia hasira, wacha watoto wa maskin tupambane kupitia mlango mwingine "CHADEMA" ili kute tea maskin wenzetu, wazaz na wadogo Zetu! Vita Hii Inaanza Sasa!