Wednesday, October 17, 2012

MUSWADA KWA HATI YA DHARURA NA WAZIRI KUTAKIWA KUTOA MAELEZO KUHUSU FAO LA KUJITOA


Mwanzoni mwa wiki tarehe 15 Oktoba 2012 niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa kauli kwa umma ya ratiba ya kupata mapendekezo toka kwa wadau wa hifadhi ya jamii pamoja na kamati husika ya kudumu ya Bunge kwa kuzingatia kuwa vikao vya kamati za kudumu za bunge vimeanza tarehe 15 Oktoba 2012 bila suala hilo kuzingatiwa.

Nimefikia uamuzi huo kwa kuwa mpaka sasa ikiwa zimebaki siku chache Mkutano wa Tisa wa Bunge kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 ambao Serikali iliahidi kuwa italeta marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii, mpaka sasa Serikali haijaitisha mkutano na wafanyakazi pamoja na wadau wa jamii kupokea mapendekezo hali ambayo inaashiria upo uwezekano muswada huo usiwasilishwe kwa wakati.

Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuboresha mfumo wa utoaji wa mafao nchini ikiwemo kuwezesha kutolewa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) na mafao mengine muhimu ambayo hayatolewi katika utaratibu wa sasa wa mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii.

Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.

Hivyo, Waziri wa Kazi na Ajira kutoa kauli kwa umma kuhusu maelekezo aliyoyatoa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) baada ya mkutano wa nane wa Bunge kufuatia mapendekezo niliyotoa bungeni ya kuitaka Wizara husika kutoa muongozo wa kisera wa kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi:

John Mnyika (Mb)
15/10/2012

No comments: