Nawatakia heri katika Maulid an-Nabi, ni siku ya
kukumbuka kuzaliwa na maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W)! Ifuatayo ni barua ya wazi kwa tume ya mabadiliko ya Katiba;
BARUA YA WAZI KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mwenyekiti,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam
Mheshimiwa,
YAH: KUPANUA WIGO WA KUKUSANYA MAONI YA WANANCHI BINAFSI KWA SIMU ZA MKONONI NA MAKUNDI YA WANANCHI KATIKA MABARAZA YA KATIBA
Nakuandikia nikirejea maelezo yako kwenye mkutano wako na waandishi wa habari tarehe 5 Januari 2013 kuhusu mchakato wa ukusanyaji maoni ya mabadiliko ya katiba.
Maelezo uliyotoa yanadhihirisha upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi unaoelezwa kukamilika kwa kuwa na idadi ndogo ya watu waliotoa maoni mpaka sasa ambapo mpaka awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni; kwa tafsiri yangu hii ni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9.
Upungufu huo uko zaidi katika utoaji maoni kwa simu za mkononi ambapo kwa mujibu wa maelezo yako wananchi waliotoa maoni kwa njia hiyo ni 16,261 tu; kwangu mimi hii ni sawa na asilimia 0.08 ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers).