Viongozi wa BAWACHA Taifa,
Waheshimiwa Wabunge wa viti maalum,
Viongozi wa CHADEMA Jimbo la Ubungo,
Viongozi wa BAWACHA Jimbo la Ubungo,
Waheshimiwa Madiwani wa kata na viti maalum,
Viongozi wa BAWACHA toka kata zote za Jimbo la Ubungo.
Niungane nanyi katika kumshukuru Mungu kwa kutupa uzima na kuendelea na kazi katika mwaka mpya wa 2013. Kwa wale ambao hatujakutana mwezi huu wa Januari, nitumie fursa hii kuwatakia mwaka mpya mwema wenye upendo na uwajibikaji.
Nawashukuru kwa kunialika kuzungumza machache kwenye Mkutano huu wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Jimbo la Ubungo na niwapongeze waandaaji kwa kuweza kuwakutanisha pamoja viongozi kutoka kata zote na wawakilishi wa wanachama kutoka katika matawi na misingi na BAWACHA katika mitaa mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.
Mwezi Disemba 2012, CHADEMA taifa kiliutangaza 2013 kuwa ni mwaka wa ‘nguvu ya umma’. Kufuatia tamko hilo la Kamati Kuu, viongozi mbalimbali wa CCM walianza propaganda chafu kupitia vyombo vya habari kuwa CHADEMA imetangaza mwaka wa ‘vurugu’.
Propaganda hizo zinalenga kutisha umma, hususan wanawake wasiunge mkono vuguvugu la mabadiliko (M4C), kujiunga kwenu kwa wingi katika Jimbo la Ubungo kunadhihirisha kuwa wanawake hamko tayari kudanganywa kwa siasa chafu na mnaendelea kuiunga mkono CHADEMA; asanteni sana.
Nawaomba mkitoka hapa mkawaelimishe na wengine kuhusu maana halisi ya falsafa ya CHADEMA ya “Nguvu ya Umma” (People’Power) ambayo imeelezwa katika katiba ya chama ibara ya 3.A, kwamba wananchi ndio msingi na chimbuko la kuundwa kwa dola ya nchi, na kuwa umma ndiyo wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatma ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa.
Miaka ya CCM kudanganya na kughilibu umma imefika ukomo. Badala ya kusubiri mpaka mwaka 2015 ama kuwaachia viongozi walio madarakani ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao; mwaka 2013 ni wakati muafaka wa kutumia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ kuwezesha wananchi kuendeleza maamuzi na mawazo kuhusu rasilimali, uchumi na siasa za nchi yetu.
Maandamano ni moja kati ya mbinu nyingi halali za kidemokrasia za kusimamia uwajibikaji kwa “nguvu ya umma’ ; naamini wanawake nanyi mtajadili mbinu nyingine wakati mkisubiri ratiba itakayotolewa na chama taifa kuhusu kazi za mwaka huu wa 2013.
Nimeelezwa kwamba katika mkutano huu mada mbalimbali zitatolewa, nitoe rai kwenu kwamba katika kuzijadili mada hizo na masuala yatayojitokeza mzingatie kauli mbiu ya BAWACHA kwamba ‘wanawake; chimbuko la maendeleo”.
Mrejee pia maudhumuni ya BAWACHA yanayotajwa kwenye Mwongozo wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA kifungu cha 3 ya kutambua, kusimamia, kuendeleza na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa chama na wa taifa kwa ujumla.
Kwa kuwa mwaka 2013 ni kipindi cha kukamilisha uchaguzi wa ndani ya chama na kuendelea na maandalizi ya chaguzi za vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2014; mtumie pia nafasi hii kuhamasishana kugombea uongozi katika chaguzi za ndani ya chama na chaguzi za kiserikali.
Pamoja na ajenda zingine mlizojipangia katika mkutano wenu, napendekeza pia muingize ajenda ya “Ukuzaji wa Ajira” hususan kwa wanawake na vijana.
Zingatieni kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 3.B, CHADEMA ni chama cha mrengo wa kati ambacho pamoja na mambo mengine kinaamini katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa taifa na kuhakikisha umma kwa ujumla unanufaika na rasilimali hizo.
CHADEMA inaamini kumiliki rasilimali na mali miongoni mwa wananchi kunawapa uhuru zaidi hivyo kwa itikadi hiyo ya mrengo wa kati tunataka kujenga chama na tukishika uongozi wa nchi; tutajenga taifa lenye kutoa fursa, ambapo kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake.
Nchi yetu inakabiliwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa ajira hususan kwa wanawake na vijana; CCM na Serikali yake wanaelekea kutotambua uzito wa matatizo hayo, ndio maana Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka tarehe 21 Machi 2012 aliitaja hali hiyo kama ‘changamoto’ tu na kutoa ufafanuzi usiokidhi haja.
Mwezi Novemba 2012 wakati wabunge wengine tukiwa bungeni Dodoma tukitekeleza kazi ya kuwawakilisha wananchi, Waziri Kabaka alikuja jimboni Ubungo kwenye mahafali ya shule binafsi inayomilikiwa na mbunge mwenzake wa CCM na kutoa kauli mbalimbali kuhusu mimi.
Kiu ya wazazi na wanafunzi siku hiyo ilikuwa kumsikia akizungumzia kuhusu ukuzaji wa ajira kwa vijana ikiwemo wahitimu, badala yake katika suala hilo linalohusu Wizara yake Waziri akatoa majibu ya ujumla tu ya kuwataka vijana kujiajiri bila kueleza mazingira ambayo serikali imeyaweka ya kuwezesha ukuzaji na upatikanaji wa fursa za ajira nchini.
Nawashukuru Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Jimbo la Ubungo mlimjibu kwa kumweleza ukweli kuhusu masuala mengine ya maendeleo; wakati nikiwa naendelea na kazi ya kuwawakilisha wananchi wote wa Jimbo la Ubungo bungeni.
Mwezi huu wa Januari 2013 viongozi wa CCM makao makuu, mkoa na wilaya wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wao Mwigulu Nchemba walikuja kwa mara nyingine tena jimboni Ubungo kama ilivyokuwa 2012 na kuendeleza propaganda. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba ili nchi iendelee inahitaji siasa, lakini siasa safi.
CCM iliyoshindwa kuwezesha maendeleo ya nchi, sasa imehamia kwenye siasa chafu, mfano hai ni Nchemba na wenzake walivyodanganya wananchi katika mkutano wa hadhara Manzese tarehe 14 Januari 2012 kuwa Katibu Mwenezi wa Kata hii ya Saranga amehamia chama hicho, wakati katibu mwenezi wetu tunaye mpaka leo.
Proganda chafu hizo zimesambaa katika CCM mpaka kwenye taasisi zake na sasa zimefikia kwa kiwango ambacho hata viongozi wanawake wa CCM nao wanajiingiza katika siasa chafu za kusema uongo.
Siku chache baada ya mkutano huo wa Manzese, Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) nao ukafanya ziara katika katika kata hii ya Saranga na kuendeleza uzushi huo pamoja na kuanza kuwapotosha wanawake kwamba CCM sasa inaanzisha mikopo isiyo na riba kwa wanawake watakaojiunga na chama hicho.
Siasa hizo chafu za uzushi zimefanyika mbele ya Katibu wa UWT Taifa, Amina Makilagi mwaka huu wa 2013; na ni mwendelezo wa propaganda zingine ambazo ziliwahi kutolewa mbele ya Mwenyekiti wake Sophia Simba alipokuja jimbo la Ubungo miaka iliyopita.
Kwa kuwa mwishoni mwa mwaka 2012 nilifanya mikutano katika kata zote za Jimbo la Ubungo kwenye mitaa mbalimbali, sikuona ulazima wa kujibu uongo na uzushi kwa wananchi wenye kuulewa ukweli na wanaotarajia vyama vya siasa vifanye siasa safi za maendeleo ya nchi.
Nashukuru viongozi wa chama na BAWACHA kata ya Saranga kwa kuamua kufanya mkutano wa hadhara jana tarehe 19 Januari 2013 kwa kushirikiana na viongozi wa Jimbo na kuendeleza vuguvugu la mabadiliko na kusimamia siasa safi.
Nilitarajia Mawaziri wa Serikali kama Kabaka na Sophia Simba wanapokuja kukutana na wananchi badala ya kufanya propaganda watumie nafasi hiyo kuwaeleza wananchi ahadi za toka mwaka 2005 zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete ya kwamba “wanawake watawezeshwa” na ‘vijana watapata ajira”.
Mwaka huu wa 2013 nitaendeleza kutoka kazi nilizofanya kwa mwaka 2011 na 2012 nikiweka mkazo pia katika kutimiza wajibu wa kuisimamia Serikali bungeni ieleze hatua zilizofikiwa katika kutekeleza ahadi hizo.
Kwa upande wenu BAWACHA mtakapojadiliana kuhusu ajenda ya ‘ukuzaji wa ajira’ katika mkutano huu, pamoja na kazi mtakazojipangia ikiwa ni sehemu yakutekeleza dhumuni la kubuni mafunzo ya wanawake kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kukabiliana na changamoto mbalimbali; mpange pia mikakati ya kukabiliana na propaganda za UWT.
Muwaeleze wazi wanawake wenzenu Gaudencia Kabaka, Sophia Simba na Amina Makilagi ambao wote ni wabunge wenzangu badala ya kufanya propaganda kwamba CCM itatoa mikopo isiyokuwa na riba au ya riba ndogo kwa wanawake waunge mkono michango tunayotoa bungeni ya kutaka kutungwa kwa sheria ya usimamizi na udhibiti wa mikopo midogo midogo na taasisi ndogo za fedha, kuepushawanawake kunyonywa na wengine kuongezewa umaskini.
Aidha, muitake Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Benki kuu iweke mifumo ya dhamana ambavyo itawezesha riba kupungua katika mabenki na taasisi zingine za fedha na kujengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara wadogo ikiwemo wanawake na vijana kuweza kukopesheka kwa urahisi.
Mwaka 2013 umetangazwa kuwa ni mwaka wa “Nguvu ya Umma” pamoja na kutumia falsafa hii katika ushiriki wenu kwenye kuboresha mchakato wa katiba mpya na kutaka hatua za serikali dhidi ya kuongezeka kwa mauaji ya raia ikiwemo yenye mwelekeo wa kisiasa;
Ni wakati pia wa wanawake na vijana kuunganisha nguvu kutaka uwajibikaji wa Serikali kutekeleza Mpango uliokwama miaka mingi wa Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya kote nchini kutakiwa kutenga asilimia 10 ya Mapato yake ya Ndani kwa ajili ya mikopo ya masharti nafuu kwa wanawake na vijana kwa ajiri ya kujiajiri na kuchangia katika kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi.
Hatua hii iende sambamba na kuongeza mtaji kwa Benki ya Wanawake (TWB) kuiwezesha kufikia wanawake wengi zaidi ikiwemo wa mitaani na kuanzisha Benki ya Vijana (TYB).
BAWACHA mtumie kila nafasi kuwashauri wote mtakaokutana nao walio katika sekta ya umma, sekta binafsi na sekta ya kiraia kwamba kuongezeka kwa mfumuko wa bei na gharama za maisha kukichanganyika na ukosefu wa ajira ni hatari kwa uchumi na usalama.
Hivyo, badala ya vyombo vya ulinzi na usalama kutumia nguvu nyingi dhidi ya CHADEMA na M4C, Serikali na CCM kujikita katika propaganda chafu na mikakati ya hujuma; nguvu za sekta zote muhimu nchini zielekezwe katika kupambana na ufisadi, kutumia vizuri rasilimali za taifa na kuchangia katika ‘ukuzaji wa ajira’.
Wanawake; Chimbuko la Maendeleo. Nawatakia mafanikio katika mkutano na asanteni kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment