Friday, January 25, 2013

Salamu za Maulid na Barua ya wazi kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Nawatakia heri katika Maulid an-Nabi, ni siku ya kukumbuka kuzaliwa na maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W)! Ifuatayo ni barua ya wazi kwa tume ya mabadiliko ya Katiba;


BARUA YA WAZI KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA 

Mwenyekiti, 

Tume ya Mabadiliko ya Katiba, 

Dar es Salaam 

Mheshimiwa, 

YAH: KUPANUA WIGO WA KUKUSANYA MAONI YA WANANCHI BINAFSI KWA SIMU ZA MKONONI NA MAKUNDI YA WANANCHI KATIKA MABARAZA YA KATIBA 

Nakuandikia nikirejea maelezo yako kwenye mkutano wako na waandishi wa habari tarehe 5 Januari 2013 kuhusu mchakato wa ukusanyaji maoni ya mabadiliko ya katiba. 

Maelezo uliyotoa yanadhihirisha upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi unaoelezwa kukamilika kwa kuwa na idadi ndogo ya watu waliotoa maoni mpaka sasa ambapo mpaka awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni; kwa tafsiri yangu hii ni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9. 

Upungufu huo uko zaidi katika utoaji maoni kwa simu za mkononi ambapo kwa mujibu wa maelezo yako wananchi waliotoa maoni kwa njia hiyo ni 16,261 tu; kwangu mimi hii ni sawa na asilimia 0.08 ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers).

Ili kuchangia katika kurekebisha hali hiyo, naomba tume ishirikiane na makampuni ya simu kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye simu kumpa dondoo za msingi za elimu ya katiba na kumpa namba anazoweza kutuma maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe wa bure wa maoni yake. 

Hii itafanya wananchi wengi kuweza kushiriki kutoa maoni. Aidha, pawepo na uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na mitandao mingine ya internet ili ufuatiliaji uweze kufanyika kwa ufanisi. 

Kwa upande mwingine, ili kurekebisha upungufu uliojitokeza kwenye awamu nne za ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi marekebisho na maboresho ya haraka ya ratiba na utaratibu yanapaswa kufanyika kwenye awamu ya ukusanyaji wa maoni ya makundi mbalimbali na hatua inayofuata ya kuunda mabaraza ya katiba. 

Kabla ya kutangaza na kusambaza utaratibu iliouita kwenye maelezo yako kuwa ni ‘namna bora ya kidemokrasia ya kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba kwa kuchaguliwa na wananchi wa maeneo husika’; naomba tume iweke wazi kwa umma mapendekezo na kutumia mikutano yake na makundi mbalimbali inayoendelea hivi sasa ipate maoni pia kuhusu muundo na utaratibu wa mabaraza ya katiba. 

Aidha, kwa kuzingatia upungufu uliojitokeza wa tume mikutano 1776 tu na wananchi wachache kutoa maoni kutokana na sababu mbalimbali, mabaraza ya katiba yanapaswa kuundwa kuanzia katika ngazi ya kata badala ya utaratibu unaondaliwa na tume wa kuunda mabaraza hayo katika ngazi ya wilaya. 

Tume ya Mabadiliko ya Katiba izingatie kwamba kifungu cha 18 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinatamka wazi kwamba “Mabaraza ya Katiba yataundwa na Tume kwa muda maalum kwa kuzingatia mgawanyiko wa jiographia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yatashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi toka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii”; hivyo kukubalika kwa muundo na utaratibu ni hatua muhimu katika kuwezesha kupatikana kwa maoni ya rasimu bora ya katiba mpya yenye muafaka wa kitaifa. 

Natanguliza shukrani nikitarajia kwamba mtachukua hatua zinazostahili katika kuboresha mchakato wa kukusanya maoni ili nchi yetu ipate katiba mpya na bora. 

Wenu katika uwakilishi wa wananchi, 


John Mnyika (Mb)
24 Januari 2013

1 comment:

Isakwisa Kanyelela said...

KAka tunashukuru kwa data, na barua yako ipo sahihi kabisa kwani watu walosomea elimu ya sheria ya katiba nadhani ndo wanaochangia ipasavyo lakini sisi wengine bado tupo gizani