Saturday, March 24, 2012

Kampeni Vijibweni Kigamboni na Migogoro ya Ardhi DSM

Leo jumamosi 24/03 niliweka kambi Kata ya Vijibweni, nawashukuru wananchi wa Kigamboni kwa kuunganisha nguvu ya umma. Asubuhi tulianza kwa maandamano mpaka Soweto, mchana nikaendesha mafunzo ya awali ya mawakala wa kampeni ya mtu kwa mtu pamoja na ulinzi wa kura katika uchaguzi. Jioni nikahutubia mkutano wa hadhara Kisiwani na usiku nimefanya kikao na makamanda kuwapa mikakati ya ziada ya ushindi. Askari wakiwa vitani walio nyumbani wajibu wao ni kuwapelekea mahitaji, endeleeni kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya M4C. Nimemsikiliza Isaya Mwita Chalres Diwani Mtarajiwa wa Kata ya Vijibweni kupitia CHADEMA, kijana msomi wa shahada ya uchumi mwenye uwezo wa kuwakilisha na kuisimamia serikali kwenye ngazi ya serikali za mitaa katika baraza la madiwani; anahitaji kuungwa mkono zaidi kwa kuwasiliana na timu ya kampeni kupitia 0714225960 au 0756091748 kwa ajili ya maelezo na maelekezo na mnipe mrejesho kupitia mnyika@chadema.or.tz. Hakuna Kulala Mpaka Kieleweke.


Nimezungumza na wananchi wa Kata ya Vijibweni bila kujali tofauti za vyama, dini, kabila, jinsia na hali zingine wako tayari kwa mabadiliko ya kweli. Matatizo ya mipango miji na migogoro ya ardhi yanawaunganisha. Serikali imevamia katika maeneo yao na kutaka kutwaa ardhi ya ekari zaidi ya 200 bila kuwashirikisha wala kufuata taratibu za kisheria. Aidha, wana mgogoro baina yao na wawekezaji wakubwa wengine yakiwa na makampuni ya kigeni yaliyotwaa ardhi, huku serikali ikishindwa kuwashirikisha na kufanya usimamizi bora wa rasilimali hii muhimu. Wapigakura wanaiamini CHADEMA kuwa ni chama chenye kuweza kuwawakilisha wananchi, kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa. Nimewaomba watupe Diwani Isaya Mwita Chalres awe kiungo kati ya CHADEMA na wananchi wa Vijibweni katika Jimbo la Kigamboni ambalo kwa sasa halina mwakilishi wa kuchaguliwa na wananchi katika ngazi ya kata yoyote kupitia CHADEMA. Nimewapa fursa ya kuuliza maswali, tukawajibu na hatimaye wakapiga kura za wazi za kuchagua mabadiliko na kuwa tayari kuunganisha nguvu ya umma kuhakikisha ushindi; M4C, kwa pamoja tutashinda.

Nimeguswa na wananchi waliotoka maeneo mengine ya jirani na Kata ya Vijibweni ya Pembamnazi, Kisota na Kibada waliokuja baada ya kusikia ningehutubia na kunieleza kuhusu migogoro katika maeneo yao na mashaka yao kuhusu mwelekeo wa mji mpya wa Kigamboni. Maelezo yao yamenirejesha kwenye migogoro ya miaka mingi niliyoikuta ya ardhi katika jimbo la Ubungo mathalani ya Kata ya Kwembe, Kata ya Kibamba na mingine ambayo nimeiwasilisha kwa mamlaka husika na naendelea kuisimamia serikali ipatiwe ufumbuzi. Hivyo, nitaendelea kufuatilia kupata kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni lini atakutana nasi kuhusu migogoro ya ardhi Dar es salaam kwa ujumla na pia kauli ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka ni lini atatembelea jimboni Ubungo kuipatia ufumbuzi migogoro tajwa kwa walivyoniahidi katika Mkutano wa nne wa Bunge mwezi Agosti mwaka 2011. Kukithiri kwa migogoro ya ardhi jijini Dar es salaam ambapo kunachangiwa pamoja na mambo mengine udhaifu katika mipango miji na kukithiri kwa ufisadi katika sekta ya ardhi ni bomu la wakati linalohitaji hatua za haraka. Maslahi ya Umma Kwanza.

No comments: