Tarehe 4 Aprili 2014 Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Said Meck Sadiq amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba hawezi kusitisha kwa muda agizo lake la kukataza pikipiki/bodaboda na bajaj kuingia katikati ya Jiji. Mkuu wa Mkoa amenukuliwa akisema kwamba hawezi kufanya hivyo kwa kuwa agizo hilo si la kwake bali la sheria ambayo ameamua kuisimamia.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo kufuatia taarifa yangu ya tarehe 2 Aprili 2014 niliyoeleza kuwa nimemwandikia ujumbe kutaka asitishe kwa muda utekelezaji wa tamko alilotoa tarehe 3 Machi 2014 ili kupisha mazungumzo baina ya Serikali, wahusika wa Bodaboda na Bajaji na wadau wengine muhimu ili kupata ufumbuzi.
Kufuatia kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa nimeipitia kwa mara nyingine tena kifungu kwa kifungu Sheria inayohusika ambayo ni The Surface and Marine Transport Regulatory Authority Act; sheria namba 9 ya mwaka 2001. Hakuna kifungu chochote katika sheria hiyo kinachokataza pikipiki/bodaboda au bajaj kuingia katika maeneo ya katikakati ya jiji. Hivyo Mkuu wa Mkoa anapaswa kutoa ufafanuzi kwa umma ni sheria ipi hiyo ambayo anaitumia na kifungu kipi hicho cha sheria ambazo kinamzuia kutengua agizo lake.
Mkuu wa Mkoa anapaswa kuzingatia kwamba eneo linaloitwa katikati ya Jiji ambalo pikipiki/bodaboda na bajaj zimepigwa marufuku mipaka yake kwa barabara ya Morogoro ni Ubungo, barabara ya Uhuru ni Buguruni, Barabara ya Nyerere ni Tazara na Barabara ya Kilwa ni Chuo cha Uhasibu; na hivyo kuleta mgogoro na kuwakosesha wananchi huduma.
Mkuu wa Mkoa anapaswa kuzingatia kwamba sheria hiyo kifungu cha 5 kimetamka kwamba wajibu wa SUMATRA ni pamoja na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma na kuhamasisha upatikanaji wa huduma ikiwemo kwa wateja wa kipato cha chini.
Usafiri wa pikipiki/bodaboda na bajaj sio tu umetoa fursa ya ajira kwa vijana bali pia unasaidia wananchi wa kipato cha chini na pia unasaidia katika mazingira ya foleni katika Jiji la Dar Es Salaam. Hivyo, agizo la kutaka usafiri huo uishie Buguruni, Ubungo, Tazara na Chuo cha Uhasibu ni suala ambalo limeibua mgogoro unaostahili ufumbuzi wa haraka.
Natambua kwamba vifungu cha 6, 38 na 39 vya Sheria hiyo vimetoa fursa ya mamlaka zinazohusika kuweza kutunga Kanuni mbalimbali; hata hivyo ieleweke kwamba Kanuni hizo sio Sheria pamoja na kutungwa kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, kauli ya Mkuu wa Mkoa kwamba hawezi kusitisha sheria sio sahihi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa anatumia nguvu kubwa kusimamia kamata kamata ya pikipiki/bodaboda na bajaj kwa madai ya kwamba anasimamia Sheria wakati suala hilo likiwa halijatajwa kwenye Sheria lakini wakati huo huo akishindwa kuisimamia sheria nyingine nyingi kwenye masuala ambayo yapo chini ya mamlaka yake.
Hali hii inaleta hisia miongoni watumiaji, waendeshaji na wamiliki wa pikipiki/bodaboda na bajaj kwamba pengine zipo sababu nyingine za ziada ambazo Mkuu wa Mkoa anapaswa kuzieleza wazi badala ya kusingizia sheria.
Nafahamu kwamba katika kutekeleza matakwa ya Sheria no. 9 ya mwaka 2001 mwaka 2010 kulitungwa Kanuni za Transport Licensing (Motor Cycles and Tricycles) ambazo zilichapwa katika gazeti la Serikali namba 144 la tarehe 2 Aprili 2010.
Kanuni hizo katika vipengele cha 13 na 14 zimetoa mamlaka kwa Halmashauri za Serikali za Mitaa kuweza kutenga maeneo ya vituo vya pikipiki/bodaboda na bajaj na pia mipaka ya maeneo ambayo vyombo hivyo vya usafiri vinaweza kutoa huduma.
Tangu nimekuwa mbunge na hivyo kuwa mjumbe wa vikao vya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Jiji la Dar Es Salaam hakuna kikao ambacho nimewahi kushiriki kilichoidhinisha kwamba kuanzia sasa ni marufuku kwa pikipiki/bodaboda na bajaj kuvuka zaidi ya Ubungo, Buguruni, Tazara na Chuo cha Uhasibu (Temeke) kwa madai ya kwamba maeneo ya zaidi ya mipaka hiyo ni katikati ya Jiji (Central Business District- CBD).
Katika muktadha huo na kwa kuwa kwa sasa niko Dodoma katika Bunge Maalum, ndio maana nimemwandikia ujumbe Mkuu wa Mkoa ambao nakala nilimtumia pia Katibu Tawala wa Mkoa kutaka utekelezaji wa agizo hilo usitishwe kwa muda mpaka pale pande zote zinazohusika zitakapokutana kupata ufumbuzi wa mgogoro unaoendelea.
Kwa kuwa Mkuu wa Mkoa amekataa kusitisha agizo lake nakusudia kumwandikia barua rasmi kutaka kuitishwe kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa (Regional Consultative Council-RCC) ambalo litakutanisha pamoja Sekretariati ya Mkoa, Halmashauri ya Jiji, Halmashauri za Manispaa zote za Jiji la Dar Es Salaam, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na mamlaka zingine zinazohusika ili kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro huu kupatikana.
Aidha, ili fedha za umma ziweze kutumika vizuri, katika barua yangu ya kupendekeza ajenda nitapanua wigo wa mjadala wa matatizo ya usafiri katika Jiji la Dar Es Salaam ili masuala yote ya Kisheria ambayo Mkuu wa Mkoa na watendaji wengine walipaswa kuyasimamia lakini hawayasimii yaweze kujadiliwa na maazimio ya utekelezaji kuweza kupangwa.
Tayari nimeshawaandikia ujumbe wabunge wenzangu wa Mkoa wa Dar Es Salaam waweze kuunga mkono ajenda hii kujadiliwa na ufumbuzi uweze kupatikana kwa maslahi ya vijana na wasafiri katika Jiji Letu.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika
06/04/2014
2 comments:
mwanzo mzuri, nadhani mkuu wa mkoa kapitiwa kwa bahati mbaya katika hili, matatizo ya usafiri Dar ni janga linalohitaji majadiliano ya pamoja kufikia unafuu wake. ukiangalia route za usafili wa umma na jiografia ya katikati ya jiji ilivyo utagunduua ni jinsi gani usafiri wa bodaboda na bajaji ulivyomuhimu kwa wananchi walio wengi.
Mwendesha Pikipiki Binafsi: Juzi nimekutana na kundi kubwa la askari wakiwa wamebeba bunduki eneo la kituo cha polisi Oystabay umbali mdogo kutoka Moroco walinikamata na nikakuta pikipiki nyingi zimekamatwa cha kushangaza askari walikuwa wanatutukana sana hadi nikapata hofu nikagundua pia askari walikuwa wanabishana nilimskia mmoja wa askari akisema "Jamani kuweni makini naskia RPC anakuja huku..isije ikawa balaa" niliitwa katika chumba fulani na nikaambiwa unatakiwa kulipa faini sh.30,000/- nikalipa nikapewa NOTIFICATION OF TRAFFIC OFFENSES lakini cjapewa risiti ya malipo. Nikawa na wasiwasi sana na hii operation invyoendeshwa, Ni kweli vijana wa nchi hii tunaonewa sana na jeshi la Polisi naishauli mamlaka husika kuangalia kwa makini kabla hawajaamua kutekeleza jambo dhidi ya jamii.
Post a Comment