Friday, October 31, 2014

WAZIRI MUHONGO, WAZIRI MKUU PINDA NA SPIKA MAKINDA WAJITOKEZE KUTOA MAELEZO JUU YA HATUA WALIZOCHUKUA KUHUSU UFISADI NA UDHAIFU KATIKA WIZARA YA NISHATI NA MADINI; WASIPOFANYA HIVYO NITAUREJESHA MJADALA BUNGENI NOVEMBA 2014

Itakumbukwa kwamba tarehe 29 Aprili 2014 kupitia Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini (nimeambatisha nakala)  juu ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara tajwa kwa mwaka 2014/2015 nilieleza ufisadi na udhaifu uliopo katika Wizara hiyo na mashirika yaliyo chini yake.

Kutokana na kukithiri kwa ufisadi na udhaifu huo nilipendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa katika Mkutano wa 15 wa Bunge uliokuwa ukiendelea wakati huo, nanukuu:

Mosi, Spika aruhusu kabla ya mjadala huu kuendelea ziwekwe mezani nakala ya ripoti zote za kamati za uchunguzi kwenye Sekta ya Nishati na Madini zilizoundwa na matokeo yake kutowasilishwa bungeni mpaka sasa.

Thursday, October 23, 2014

Pata hapa nakala ya muswada wa Baraza la Vijana la Taifa; boresha tupate baraza bora

Katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.

Narudia tena kuwashukuru vijana na wadau tulioshirikiana kuandaa muswada huo na naomba kuendelea kupata ushirikiano wenu wa karibu katika hatua zinazoendelea.

Kuanzia tarehe 21 Oktoba 2014 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeanza vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada huo. Nakala tete ya muswada huo inapatikana hapa, tafadhali pakua pitia na wasilisha maoni yako sasa.

Unaweza kuandika maoni yako kwenye mtandao wa http://mnyika.blogspot.com au kutuma kwa barua pepe kwenda mbungeubungo@gmail.com na nakala kwa Kamati husika ya Bunge kupitia tanzparl@parliament.go.tz.

Ikiwa unataka kutumia njia nyingine kuwasilisha maoni yako tafadhali wasiliana na Gaston Garubimbi 0715/0767-825025 kwa maelezo zaidi. Mdau wa masuala ya vijana zingatia kwamba  zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa baraza  la Vijana la Taifa zimekuwa zikitolewa bila utekelezaji kamili na wa haraka.

Wednesday, October 8, 2014

Maharamia wamepitisha Katiba haramu: wameanzisha mgogoro chanya na mwanya wa mabadiliko

Dira ni kuwa na katiba bora itakayojenga Tanzania yenye demokrasia ya kweli, uhuru wa kweli na maendeleo endelevu kwa watu wake wote. Lakini uharamia katika mchakato wa katiba mpya umelipasua taifa. Mpasuko huu unaweza kuwa mgogoro hasi wenye madhara kwa wananchi au mgogoro chanya utakaoleta mabadiliko nchini. 

Maharamia wanashangilia kilevi katika Bunge Maalum baada ya kukamilisha uharamia dhidi ya rasimu ya katiba ya wananchi kwa kupata theluthi mbili kwa njia kiharamia. Katiba iliyopendekezwa kiharamia ni katiba haramu.

Katiba haramu, katiba ya maharamia, katiba ya mafisadi, katiba ya CCM wahafidhiana na mawakala wake inapaswa kupingwa mtaani na mahakamani kwa mbinu mbalimbali. 

Iwe ni kwa mikutano, migomo, maandamano, mashtaka au katika sanduku la kura. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba mchakato huu wa mabadiliko ya katiba ni mwanya wa mabadiliko katika taifa letu.