Thursday, March 26, 2015

Kufuatia Kumbukizi UDSM Tutangaze #AjaliBarabaraniJangalaTaifa Tuwajibike kuzipunguza










Kumbukizi maalum ya tarehe 20 Machi 2015 ya wanafunzi watano wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani imetukumbusha msiba mkubwa wa watu 50 katika ajali moja ya basi na lori ya tarehe 11 Machi 2015.

Wakati tukiendelea kuwaombea marehemu na majeruhi na kutoa pole kwa wafiwa na wahanga wakati umefika sasa tutangaze #AjaliBarabaraniJangalaTaifa tuwajibike kuzipunguza.

Kumbukizi katika ukumbi wa Nkurumah ilihusisha ibada, nyimbo maalum na kusomwa kwa wasifu wa wanafunzi walioaga dunia wakiwa wadogo familia zao na taifa likiwahitaji na hatimaye salamu kutoka makundi mbalimbali.

Niliguswa na salamu za Chuo cha Fani za Jamii zilizosomwa na Mkuu wa Chuo cha Fani za Jamii aliyeeleza kwamba mabasi sasa yanaua kuliko magonjwa mengi. Alipendekeza utafiti ufanyike UDSM kuchangia kupunguza hali hiyo kwa kuzingatia kwamba Chuo Kikuu hicho kina fani mbalimbali (multi disciplinary).

Alieleza kwamba kwa upande wa uhandisi waangalie iwapo teknolojia ya mabasi yenye spidi inawiana na barabara zetu kuu ambazo nyingi ni za njia moja. Huku fani ya jamii iangalie masuala ya maadili kufanya madereva wa mabasi kujifunza kwamba wanabeba binadamu sio wanyama.

Nakubali kwamba kuna umuhimu wa kuendelea na utafiti lakini tujiulize ni wananchi wangapi wataendelea kupoteza maisha wakati tukisubiri matokeo ya utafiti mpya.

Hivyo, kuna haja ya UDSM kuitisha Kongamano Maalum kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili matokeo ya tafiti zilizofanyika tayari yajadiliwe na mapendekezo ya hatua za dharura yatolewe.

Pamoja na tafiti zilizofanywa na wasomi, Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta awasilishe matokeo ya Ripoti ya kamati iliyoundwa kutathmini na kutoa mapendekezo ya hatua ya kuchukua ili kupunguza ajali za barabarani ambayo ripoti yake ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison Mwakyembe Novemba 2014.

 

UDSM iende mbele zaidi ya kufanya utafiti kwa kuzingatia dhima iwezeshe msukumo wa kisomi na kimkakati katika huduma kwa umma.

Natambua pia katika salamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar Es Salaam (DUCE) zilizosomwa kwa niaba ya Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Fani na Sayansi Jamii (DUCE) Serikali iliombwa kuongeza juhudi za kupunguza ajali.

Lakini maombi pekee hayatoshi kuna haja ya kutaka utekelezaji na uwajibikaji na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salam isibaki nyuma katika kukabiliana na  #AjaliBarabaraniJangalaTaifa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amenukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba chanzo cha ajali ya basi la Majinja Express na lori ni ubovu wa barabara katika eneo la ajali na mwendo kasi.

 

Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha kulikuwepo na shimo kubwa la muda mrefu katika barabara kuu. Lakini pamoja na hali hiyo hakuna kiongozi yoyote wa Wakala wa Barabara (TANROADS) au mamlaka zingine zinazohusika aliyewajibika au kuwajibishwa mpaka hivi sasa.

 

Baada ya Ikulu kusambaza taarifa ya salamu za rambirambi za Rais ni vyema sasa ikasambaza tena taarifa nyingine ya kueleza umma hatua ambazo Rais ameelekeza kuchukuliwa kwa waliosababisha hali hiyo.

 

Aidha, Waziri wa Uchukuzi atakiwe kuwasilisha kupitia Mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea hivi sasa kauli ya Serikali kuhusu mkakati wa kushughulikia kukithiri kwa ajali za barabarani nchini.

 

John Mnyika (Mb)

25 Machi 2015

No comments: